YOUTUBE PLAYLIST

Monday, August 29, 2022

UZURI NA UBAYA WA TEKNOLOJIA ZA KISASA ZA KUREKODI MUZIKI

 

Tape recorder ya studio miaka ya 90 kurudi nyuma


Kwa manamuziki ambaye uliewahi kurekodi miaka ya 90 na kurudi nyuma, hakika studio za siku hizi ni tofauti sana. Teknolojia inayotumika kurekodi siku hizi  inarahisisha sana kurekodi. Mwanamuziki mmoja mmoja anarekodi kipande chake, akikosea kuna uwezekano wa kurudia peke yake na wala si kazi ngumu. Waimbaji pia wanaimba mmoja mmoja na kuna uwezekanao hata muimbaji mmoja akaimba mara nyingi kipande kimoja na hatimae ikasikika kama ni kwaya nzima ilikuwa inaimba. Teknolojia inawezesha hata mtu asiyejua kuimba vizuri akarekebishwa na kusikika akiimba kwa sauti tamu ya kuvutia, pia kwa utaratibu huu wimbo mmoja unaweza hata ukachukua mwezi mzima kukamilisha kuurekodi. Kwa kweli kuna tofauti kubwa sana.
Teknolojia imebadili taratibu zote za utengenezaji wa muziki.  Ngoja nirudi nyuma miaka ya 80, nielezea taratibu za kurekodi nyimbo ambazo siku hizi zinaitwa zilipendwa. Kurekodi haikuwa kazi rahisi, hakukuwa na kompyuta ya kutengeneza mapigo na kutoa sauti mbalimbali za muziki na hata kuelekeza mwendo wa wimbo, ililazimika waweko watu halisi wapige muziki na kurekodiwa kwenye kanda zilizoitwa tape. Mashine za kurekodia zilizoitwa ‘tape recorders’ zilikuwa na uwezo wa kurekodi njia mbili  (two track), hebu linganisha hilo na zama hizi ambazo  hata kompyuta ya kawaida ikiwa na program sahihi inaweza kurekodi mamia ya ‘tracks’ bila tatizo lolote.  Hivyo basi teknolojia hii ya two track ililazimisha kundi linalotaka kurekodi liupige wimbo wao wote bila kukosea ‘live’ na akikosea mtu mmoja tu, lazima kufuta wimbo wote na kuanza upya. Hii ilikuwa na maana kuwa kila kundi lililotaka kwenda kurekodi, ilikuwa lazima kufanya mazoezi magumu ya muda mrefu ili kila mwanamuziki awe anauhakika na vipande vyake atakavyovipiga.

Studio kubwa za kurekodi muziki zilikuwa mbili, studio ya Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na studio za Tanzania Film Company (TFC). Zote zilikuwa na masharti yaliyofanya kazi ya kurekodi kuwa ngumu zaidi. Studio ya RTD ilikuwa inaipa kila bendi siku mbili za kurekodi. Siku ya kwanza kurekodi nyimbo mpya za bendi na siku ya pili kurekodi kipindi cha Club Raha Leo. Kila bendi ilikuwa inahitajika kuja na vyombo vyake. Mapema siku ya kwanza ya ratiba, bendi iliingiza vyombo studio na kazi ya kuvifunga na kuvitayarisha kwa kurekodi ilichukua muda wote wa asubuhi ya siku ya kwanza. Mchana baada ya kula ndipo wanamuziki walipoingia kurekodi nyimbo zao. Kulikuwa na sheria kuwa watu wote ambao si wafanyakazi wa RTD walitakiwa kuwa wameondoka eneo la RTD kabla ya kushushwa bendera saa 12 jioni. Hivyo basi bendi kama ilikuwa na nyimbo 4 au 10 ililazimika kukamilisha kazi ya kuzirekodi zote hizo kati ya saa 8 mchana mpaka saa kumi na mbili jioni. Kama nilivyosema awali, nyimbo zilitakiwa kupigwa na kuimbwa  bila kukosea, kwa kweli kazi iliyokuwa ikifanywa na wanamuziki wa enzi ile ni ya kusifika. Ukisikiliza kwa makini kuna nyimbo nyingi maarufu zilizopendwa huwa zinakuwa na makosa madogo madogo, lakini mara nyingi ilikuwa ni  kutokana na hali niliyoitaja hapo juu. Kuna wimbo mmoja wa African Fiesta ambao alikuwa anaimba Tabu Ley unaitwa Ndaya, wakati wa chorus unamsikia Tabu Ley akijichanganya maneno , lakini nadhani ilionekana upite, hii ilikuwa ikitokea pale wimbo umesharudiwa mara nyingi na wanamuziki wamekwisha choka.
Fundi mitambo alikuwa akitupigia wimbo tusikie baada ya kurekodi na alikuwa akiuliza' Vipi huu?' wenyewe tukiwa tumeridhika tulijibu 'Upite'.

TFC hawakuwa na masharti ya muda wa kuondoka studio, TFC ilikuwa shirika la umma na hivyo  lilikuwa likiendeshwa kibiashara na malipo ya studio yalikuwa kwa  siku. Kwa kuwa bendi hazikuwa na fedha, mara nyingi zililipa malipo ya kutumia studio siku mbili zikizidi sana tatu. Hapo ilikuwa wanamuziki wenyewe wanakuwa makini ili kutumia vizuri muda wao, ili usije ukaisha na fedha za kuongeza muda zisiweko. Nikiwa Vijana Jazz tulitumia studio za TFC kurekodi album iliyokuwa na nyimbo maarufu kama Thereza, VIP na Mfitini. Tulikesha siku mbili kukamilisha album ile.

Teknolojia ya sasa inaruhusu mtu mmoja kama unauwezo wa kupiga vyombo mbalimbali na kuimba,ukaweza hata kutengeneza nyimbo ambazo zitasikika kama vile ni bendi nzima ilikuwa kazini. Kwa mfano kati ya album za kwanza za wanamuziki wa Tanzania ambazo zilitoka kwa kutumia teknolojia hii ya sasa  ya ‘multi track’ ni album ya Dhiki ya Patrick Balisidya. Katika album hii Patrick alipiga vyombo karibu vyote na pia kuimba sauti zote, ukisikia nyimbo hizo utadhani zilipigwa na bendi nzima.

Pamoja na ubora wote wa teknolojia hii, kurekodi kwa mtu mmoja mmoja kunaondoa sehemu kubwa ya utamu katika nyimbo zilizorekodiwa. Hebu fikiria ngoma yoyote ya kiasili, irekodiwe kwa mpigaji ngoma moja moja kuingia studio na kurekodi mapigo yake, utamu ule wa wapigaji kupeana hamasa wakati wa kupiga wote utaondoka. Pengine ndio sababu nyimbo za sasa zinarekodiwa na kusikika vizuri lakini zinakosa uhai fulani wa wapigaji kupiga kwa pamoja, na kuhamasishana, kupata ile 'feeling ya live'. Nyimbo za bendi zamani zilikuwa kwanza tayari zimeshapigwa mara nyingi katika kumbi mbalimbali hivyo kuwa na aina ya uhai ambao huwezi kuupata katika wimbo ambao ni mpya kabisa. Utaratibu huu uliwezesha bendi kuboresha wimbo hatimae siku ya kurekodi wimbo unakuwa umeiva.

Wednesday, August 24, 2022

NIMEPITWA NA WAKATI NGOJA NIKAPUMZIKE

 


Nilipokuwa mdogo nilikuwa naona vibabu vya mtaani kwetu viko vya aina mbili, aina ya kwanza ilikuwa vibabu ambavyo vilikuwa havicheki kila saa vimenuna na kwa ujumla, watoto wote tuliviogopa, na tulianza hata kutunga hadithi kuwa vitakuwa vichawi, au vilipata matatizo makubwa wakati wa ujana na kadhalika. Kundi la pili la vibabu ilikuwa vile vibabu ambavyo huvikuti vimenuna, ukiviamkia vinakujibu kwa furaha na kuanza kuulizia wazazi wako, mambo yako ya shule na kadhalika. Vibabu hivi hata kama una shida ilikuwa rahisi kukusikiliza na kukupa ushauri hata msaada. Na pia kulikuwa na vibibi vya aina hiyohiyo pia, tulikuwa na rafiki yetu bibi yake alikuwa anauza maji, kila baada ya siku chache tulikuwa tukimtembelea bibi kwa kuwa lazima atatugawia senti  kumi kumi kutokana na biashara yake ndogo ya maji, kwa hesabu za harakaharaka alikuwa akitugawia pato lake la siku nzima bila hata kusita, na wala hatukuwa wajukuu zake wa moja kwa moja. Sasa yamenikuta siku hizi mimi ndie sasa nimekuwa babu, na polepole naanza kupata picha kwanini wale babu na bibi zangu walikuwa vile.
Wahenga walikuwa na msemo, nyani mkongwe kakwepa mishale mingi, na ndio ilivyo katika maisha, wakongwe wamekwepa mengi, wameona mengi, kwa asili ya mila na tamaduni zetu, wazee walikuwa na nafasi muhimu katika kutoa ushauri wa mambo kadhaa, lakini hili linapotea taratibu, na hasa ukichukua dhana ya siku hizi isemayo ‘wazee wamepitwa na wakati’.
Wasanii ni sehemu ya jamii, hivyo hata kwenye tasnia hii dhana ya ‘wazee wamepitwa na wakati’ inatumika sana.
Ukongwe katika fani unakupa elimu ya mambo mengi, mengine unafundishwa na wakongwe uliowakuta, mengine unajifunza kazini, hatimae kichwa kinakuwa na majibu ya mambo mengi ambayo kwa utamaduni wa zamani unatakiwa kuyarithisha kwa wanaochipukia katika fani. Lakini hili linakuwa gumu pale inapokuja dhana kuwa ‘wazee wamepitwa na wakati’. Ukisha kutana na hali ya kuonekana umepitwa na wakati kuna mambo mawili unaweza ukaamua, moja unaweza ukawa mtu wa kukasirika kila wakati, kiasi cha kwamba mtaani ukaonekana ni babu moja mwenye hasira zisizo na sababu, watoto wakaanza kuhadithiana kuwa utakuwa mchawi au ulipata matatizo ya akili ulipokuwa kijana. Jambo la pili linaloweza kutokea ni kuamua kuwa mchangamfu na kubaki unacheka na kila mtu, ili usisumbue kichwa chako, na hatimae kuondoka duniani na elimu yako kwa furaha.
Kwa kicheko na furaha sana nakumbuka enzi kabla hakujawa na Baraza la Sanaa la Taifa. Enzi hizo  kulikuwa na taasisi inaitwa Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), chombo kilichoanzishwa mwaka 1974. Kazi ya BAMUTA ilikuwa kuratibu shughuli za muziki na muziki wa aina zote. BAMUTA iliuangalia muziki kwa mapana yake yote, elimu, vifaa, masoko, maadili, BAMUTA pia ilikuwa na kazi ya kuandaa sera za Taifa za muziki. Katika kipindi cha BAMUTA bendi zilisaidiwa vyombo vya muziki na serikali, BAMUTA ilitungwa vitabu kadhaa vilivyohusu muziki, ukiwemo muziki wa asili. Mitaala ya muziki ilitayarishwa na muziki ukawa somo mojawapo linalofundishika mashuleni, waalimu wake walitayarishwa katika vyuo vya waalimu wa sanaa kama vile Chuo cha Butimba, na wakaenezwa katika vyuo na mashule nchini kote, wengine wakawa maafisa utamaduni na wengine kuwa katika ngazi mbalimbali za wizara ya Utamaduni na sanaa. Kila mkoa ulikuwa na japo bendi moja iliyokuwa na umaarufu, kulikuwa na kwaya nyingi, madisco mengi,  japo wakati huo uwekezaji katika muziki haukuwa mkubwa kama ulivyo sasa. Mazingira yakawekwa yaliyoruhusu wapenzi wa muziki waweze kusikiliza aina mbalimbali za muziki hata muziki ule ambao si wa kibiashara lakini ni mzuri kwa ubora wake au kwa ujumbe wake. Mazingira hayo yaliwapa wanamuziki maktaba pana ya kuweza kutohoa aina mpya za muziki. Wajumbe wa BAMUTA walitoka kila kona ya nchi na hivyo kuipa BAMUTA sura ya Kitaifa, angalia orodha ya wajumbe wa Baraza la Muziki Tanzania;

1.   Boniface Musiba (Mwenyekiti wa BAMUTA)
2. D. R. Mbilinyi (Mwenyekiti Msaidizi wa BAMUTA)
3. S. Chidumizi (Mjumbe wa BAMUTA-Dodoma)
4. J.Y. Sapali (Mjumbe wa BAMUTA-lringa)
5. Padre J.M. Buluma (Mjumbe wa BAMUTA-Mwanza)
6. A. Kosana (Mjumbe wa BAMUTA-Shinyanga)
7. R. Singano (Mjumbe wa BAMUTA-Tanga)
8. Mbaraka Mwishehe (Mjumbe wa BAMUTA-Morogoro)
9. Padre Kayatto (Mjumbe wa BAMUTA-Mbeya)
10. Gwabukoba (Mjumbe wa BAMUTA-Kigoma)
11. P. Balisidya (Mjumbe wa BAMUTA-Dar es Salaam)
12. R. Mselewa (Katibu Mtendaji wa BAMUTA)
13. E. Kavalambi (Mkufunzi wa Muziki-Marangu CE.T.)
14. K. J. Nsibu (Aflsa Utamaduni-Korogwe)
15. E. Lameck (Mwanakwaya-Mwatex)
16. G. Kanyabwoya (Mwalimu-Kigoma)
17. T. Busyanya (Mkufunzi wa Muziki-DSM CE.T.)
18. G. Daudi (Afisa Sanaa za Maonyesho-Rukwa)
19. John Mgandu (Mwalimu wa Muziki-Tabora Shule ya Seko-ndari ya Wavulana)
20. E. G. Makala (Wizara ya Utamaduni)
21. F.E. Nkwera (Mkufunzi wa Muziki-Songea CE.T.)
22. T. Nkera (Mkufunzi wa Muziki-Ndwika CE.T.)
Wakati ufanisi wa Baraza hili ukiendelea, akatokea mtu mmoja akaanzisha wazo la kuwa na Baraza moja kwa ajili ya Sanaa zote, na ndipo likazaliwa Baraza la Sanaa la Taifa. muziki ukashushwa na kuwa ni Idara tu katika katika Baraza hili, tena hata hiyuo idara ilisha uwawa .

Lakini nisijichoshe, ngoja nikacheze na watoto, si unajua wazee tumepitwa na wakati.

 

Tuesday, August 23, 2022

SEHEMU YA RIPOTI YA TAMASHA LA BENDI LA TANZANIA LIVE MUSIC FESTIVAL 2012



Baada ya matayarisho mbalimbali yaliyochukua miezi mitatu hatimae tarehe 28 September 2012, bendi ziliweza kuanza kupanda jukwaani kufanya maonyesho katika viwanja vya Leaders Club.  Bendi zilizopanda jukwaani karibu zote zilikuwa na makubaliano ya kulipwa na zililipwa fedha ya awali wiki 2 kabla ya onyesho na fedha iliyobaki ilikamilishwa siku ambapo bendi zilipanda jukwaani. Hakuna bendi yoyote iliyokuwa ikiwadai watayarishaji.

Watayarishaji walijipanga kwa kuhakikisha kuna jukwaa la Kimataifa lililopambwa na taa za rangi za kiwango cha juu, na vifaa vya muziki ambavyo vilihakikisha kila bendi inapopiga muziki, muziki wake ulisikika kwa kiwango cha hali ya juu. Hakukusikika mpaka leo malalamiko kuhusu upande huo wa matayarisho.


MC BEN KINYAIA

Tamasha lilianza tarehe 28 September 2012, saa kumi na mbili jioni,  kwa bendi kuanza kufanya maonyesho, bendi ya kwanza kupanda jukwaani ilikuwa ni Msondo Ngoma Music Band na kufuatiwa na bendi ya Fm Academia, na baadae bendi za Akudo Impact, Mashujaa Band, kundi la Taarab la Mashauzi Classic na baadae vijana wa Orynx Band. Bendi zote zilifanya vizuri sana, bendi zilipanda  kwa zamu kama ratiba ilivyokuwa imewaelekeza na mshereheshaji  alikuwa ni Ben Kinyaiya alifanya kazi kwa umakini wa hali ya juu .

 

Tamasha liliendelea siku ya pili  kama ratiba ilivyokuwa imepangwa kwa bendi za Mlimani Park, Skylight band, B Band, Oryx Band, Bi. Khadija Kopa  kupanda jukwaani, na kama ilivyokuwa jana yake wakiongozwa na mshereheshaji  Ben Kinyaiya.





MAFANIKIO

Mafanikio yaliyopatikana ni uzoefu mkubwa wa namna ya kutayarisha tamasha la muziki wa bendi. Mawasiliano yaliweza kufunguliwa kati ya watayarishaji na wanamuziki wa bendi mbalimbali. Kumekuweko na mafanikio ya kujua namna ya kupata vyombo na mafundi bora wa sauti, upambaji wa jukwaa na matayarisho yote ya awali ya kuwezesha tamasha kufanyika. Kumepatikana uzoefu wa kuitisha press conference na kufanya mikutano na wadau mbalimbali wa matamasha, serikalini, katika kampuni binafsi na watu binafsi.



WADAU TAMASHA.

Tamasha hili liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Edge Entertaiment na Chama Cha Muziki  wa Dansi Tanzania(CHAMUDATA) baada ya makubaliano, ambayo yalifikiwa kukiweko na malengo ya kupata fedha kwa ajili ya kusaidia miradi ya CHAMUDATA na kutoa mchango kwa BASATA. Kampuni ya Edge Entertaiment iliingia  mkataba na Times Fm Radio ambao uliwezesha  Times Fm kulitangaza Tamasha  pia kutoa gharama za matumizi yote ya maandalizi ya tamasha  kwa makubaliano ya fedha zitakazotumika kurudishwa kutokana na mapato ya tamasha.



KAMATI.

Kamati ya pamoja ya Edge Entertaiment  na Times Fm Radio iliundwa na ikapewa majukumu ya kuhakikisha  tamasha linafanikiwa, kamati ilifanya kazi chini ya uangalizi wa upande zote mbili zilizokubaliana na kamati  iliomba kampuni ya Edge Entertaiment iajiri mtu wa PR atakayehakikisha mpangilio  mzuri wa Tamasha na Edge Entertainment ilifanya hivyo.



VYOMBO VYA HABARI.

Katika kuhakikisha tamasha linafanikiwa kamati ilitumia vyombo vya habari vifuatavyo Magazeti, Tv, Blogs, Radio

Magazeti yaliyotumika;

  (a)Mwananchi

  (b)Jambo leo

  (c)Mtanzania

  (d) Magazeti ya Global Publishers

Tv zilizotumika;

 (a) TBC - Mahojiano

 (b) Chanel Ten- Mahojiano

Blogs zilizotumika;

(a) Michuzi

(b) Full shangwe

(c) Dar blog

(d) www.musiciansintanzania.blogspot

Radio;

Radio iliyotumika ni Times Fm Radio hii ilitokana na udhamini ambao redio hii ilikuwa imetoa

 


MATATIZO.

Kulikuweko na matatizo kadha wa kadha, mengine ni kutokana na maamuzi yaliyofanyika, mengine ni kutokana na wadau mbalimbali wa Tamasha, na machache ambayo yalikuwa njee ya uwezo wa  Kamati ya tamasha

* Tamasha lilifanyika siku ya Ijumaa na Jumamosi, huu ulikuwa uamuzi ambao ulionekana kuwa ni mzuri, lakini kwa mawazo ya wadau waliohudhuria wengi waliona ingekuwa bora tamasha lingeanza Jumamosi na hatimae kufikia kilele Jumapili kwa maonyesho ambayo yangeanza Jumapili kuanzia saa nne asubuhi hadi kati ya saa4 na saa 6 usiku siku hiyo

* Pamoja na bendi kulipwa si chini ya shilingi laki saba kila bendi bendi ziliendelea kupanga ratiba zao na hata kutangaza kuwa wako katika sehemu nyingine kwa siku na wakati uleule ambapo bendi zilitegemewa kuwa jukwaani katika tamasha. Msondo Ngoma walipiga wimbo mmoja tu kwa malipo ya shilingi milioni 1.

* CHAMUDATA  kilikuwa mdau muhimu katika tamasha hili, kwanza kwa kuwa sehemu ya mapato yalikuwa yaiingie katika mfuko wa chama hicho, na pili hili lilikuwa tamasha la muziki wa bendi, hivyo kuwa linafanya kile ambacho chama hiki kinasimamia, lakini hakukuweko hata afisa mmoja wa  CHAMUDATA katika kipindi chote cha tamasha, ambapo ingetegemewa chama kiwe chombo kimojawapo cha kupigia debe mafanikio ya tamasha hili.

* Kulikuweko na matatizo ya matangazo ambapo palikuweko na matukio ya kubandua mabango, na wakati fulani kuchanganya taarifa katika matangazo ya magazeti.

* Pamoja na kuwa eneo la Leaders lilikuwa limelipiwa, bado uongozi wa bar ya Leaders ulikaidi na kuendelea kukiuka masharti kwa kuendelea kufanya mauzo ya vinywaji kinyume na utaratibu na makubaliano na wadhamini wakuu wa tamasha. Hili limepelekea wadhamini kugoma kulipa baki ya ada ya udhamini ambayo ni shilingi 10,000,000.

* Mgeni rasmi aliwasili kwa muda aliopangiwa ambao ulikuwa ni saa moja, hili lilikuwa kosa kwani muda huo ndio ratiba inaanza na si muda mzuri kwa mgeni rasmi kuwa ndio anawasili, pia hakukuweko na protokali za kumpokea mgeni rasmi jambo ambalo lilitia doa ujio wake. Na hivyo alishindwa hata kufanya shughuli ya kufungua rasmi tamasha

 


HITIMISHO.

Kwa ujumla Tamasha lilikuwa na mengi sana mazuri kiutendaji, vyombo vizuri na vya kisasa, stage kubwa ya kisasa, na  liliweza kufanyika  kwa bendi zaidi ya kumi kushiriki. Ni wazi ni muhimu utamaduni huu wa kuwa natamasha kila mwaka kuendelea japo matayarisho yanatakiwa kuanza sasa.
Wanamuziki wa mabendi walikatisha tamaa kwani wamekuwa wakilalamikia kukosekana kwa Tamasha lao,  lakini ni wazi walithamini zaidi kazi zao za kawaid kuliko Tamasha lililokuja kukidhi kiu yao.
 Kwa upande wa mapato hayakuwa mazuri waandaji  waliingia hasara  kubwa na  hivyo kushindwa kutimiza malengo yake likiwemo la kukisaidia Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA). Waandaji wataendelea na elimu na mafunzo mbalimbali kwa wanamuziki wa muziki wa dansi wakishirikiana na BASATA na CHAMUDATA ili kuweza kuleta mafanikio katika muziki wa dansi Tanzania.

Katibu

 


Monday, August 22, 2022

KUWA MWANAMUZIKI ZAMANI HAIKUWA LELEMAMA

 

Vijana Jazz Band tukielekea Ifakara

Kuwa mwanamuziki katika miaka ya tisini na kurudi nyuma haikuwa lelemama, ilikuwa kazi ngumu, iliyokuwa yakujitolea haswa. Kati mambo magumu miaka hiyo ilikuwa kusafiri kwenda kufanya maonyesho. Katika zama hizi mwanamuziki anapata mualiko, anatajiwa na fungu atakalolipwa, anachagua aina ya hoteli ya kulala na hata usafiri kama ni wa ndege au gari la abiria  au hata gari binafsi, fursa hizo hazikuweko miaka hiyo.
Kwanza kabisa kulikuwa na taratibu za kiserikali, ili bendi au kikundi cha muziki kitoke katika mkoa ambako ni masikani taratibu zilikuwa ngumu. Kikundi kilianza kwa kuandika barua kwa Afisa Utamaduni wa mkoa kuomba ruksa ya kutoka nje ya mkoa. Afisa Utamaduni akisha kutoa kibali kile, muwakilishi wa bendi hutangulia kwenda kuwakilisha kibali kwa Afisa Utamaduni wa mkoa ambao kundi linaenda ili kupata kibali cha kufanya kazi katika mkoa husika, Afisa Utamaduni Mkoa akisha toa kibali kuingia mkoa wake, ndipo nakala ya kibali hupelekwa kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya ili nae atoe kibali cha kuruhusu kundi kufanya maonyesho katika wilaya yake. Kutokana na uchache wa magazeti, vikundi vingi vilianza safari bila matangazo yoyote, kwani kuna wilaya nyingine, magazeti hayakuwa yanafika kabisa au magazeti yalifika machache na hata hayo yaliweza kuchelewa hata siku nne.  Mwakilishi wa kikundi akishafika kwenye mji ambao bendi au kundi lingefanya maonyesho, alishirikiana na Afisa Utamaduni kupata kumbi na kufanya booking ya mahala pa kulala. Matangazo ilikuwa ni karatasi za kuandika kwa mkono na kisha kubandika katika kuta na nguzo mbalimbali. Baada ya hapo alitafutwa mwenyeji ambaye ni mtangazaji naye alipita katika mitaa mbalimbali akitangaza kupitia kipaza sauti cha mkononi. Nakumbuka mwaka mmoja mapema miaka ya 80, nikiwa na Orchestra Mambo Bado, tulifika Mpanda na kuelekezwa kuwa mtu maalumu ambaye hutangaza mambo yote pale, alikuwa bwana mmoja aliyepewa jina la utani la Mshindo Mkeyenge. Huyu alikuwa akipita mitaa mbalimbali na ngoma yake na hiyo hugonga  ili watu wamsikilize na ndipo hapo hutangaza kuwa kuna dansi linakuja na litakuwa wapi na kiingilio chake.

Usafiri wa bendi ulikuwa wa basi za abiria na mara nyingi malori ambamo wanamuziki walijazana humo wakiwa na vyombo vyao. Kati ya safari za aina hii nilizowahi kusafiri kwa roli ni toka Mbeya hadi Chunya na kurudi, kutoka Mtwara na kuzunguka miji ya kusini mingi kama Masasi , Nachingwea, Lindi kutumia lori la aina ya Isuzu Long base. Na nikiwa na bendi ya Tancut kwa ujumla usafiri wetu ulikuwa ni loti aina ya ‘canter’, humo tulizunguka miji kuanzia Makambako, Njombe, Songea, Mbeya, Tunduma na miji mingine mingi, tuliwahi pia kuzunguka miji mingi kanda ya ziwa kutumia  lori aina ya Leylan Albion. Huo ndio ulikuwa usafiri wa masupastaa wa mika hiyo.

 Malazi kwa kawaida hayakuwa ya kifahari, kwa kawaida vyumba vilivyokodishwa vilikuwa ni dabo ili kupunguza gharama, na gesti zenyewe zilikuwa ni zile ambazo gharama zake zikuwa chini. Kulala njaa halikuwa jambo la ajabu, hasa mkipiga dansi na kukosa wateja, hapo ndipo mnaweza kujikuta mmelala ukumbini ili pesa itoshe gharama za kuwasafirisha kwenda mji unaofuata. Miji mingi haikuwa na umeme hivyo bendi nyingine zilikuwa zikizunguka na jenereta, au kukodi kwa ajili ya kila onyesho.

Kama ilivyo katika biashara nyingine uongo nao ulikuwa mwingi sana, utasikia , ‘Bwana bendi ikienda Nyarugusu kule fedha nje nje, wachimba migodi wana pesa sana lazima mtarudi na pesa za kutosha kununua vyombo vipya’ . Hapo harakati za kwenda Nyarugusu zitaanza. Miaka hiyo Nyarugusu ilikuwa mji mmoja maarufu kwa wachimba dhahabu wadogowadogo, lakini sijawahi kuona bendi ikipata fedha za ajabu baada ya kwenda Nyarugusu. Kuna wakati  Bendi tatu tulikutana Mwanza kila moja ikiwa ina mpango wa kwenda Nyarugusu. Vijana Jazz Band,  Maquis  na Ngorongoro Heroes wote tukawa Mwanza. Hali ilikuwa mbaya sana kwa Maquis ambayo ilikuwa safarini huku  kwa zaidi ya miezi mitatu, ilifikia kiasi cha wanamuziki kuanza kurudi Dar es Salam mmoja mmoja.
Lakini ilikuwa ni baada ya safari hii walipojipanga upya na kurekodi vile vibao vyao vikali, Makumbele, Tipwa tipwa na Ngalula na kurudisha heshima yao mjini.

Kifupi hayo ndiyo yalikuwa maisha ya mwanamuziki wakati huo, ujana ulisababisha watu wafurahie kuzunguka huko na huku nchi nzima, wakipata mikasa na kuitungia nyimbo ambazo nyingine bado zinapendwa mpaka leo. Hakika sitaweza kukumbuka sehemu zote ambazo binafsi nimewahi kupiga muziki, kwani pamoja na miji mikubwa tulikuwa pia tunapiga katika vijiji ili mradi tupate pesa za kuendelea na safari.  Najaribu kupata picha vijana wa zama hizi kukubali kusafiri kwa lori kwenye barabara zilizokuwa duni na za vumbi. Nina uhakika madansi mengi yasingelia kwa supastaa kugom kupiga.

Sunday, August 21, 2022

KUJIBRAND SIO DHANA MPYA

 


Katika zama hizi ni kawaida kabisa kusikia wanamuziki wa kizazi kipya wakisema wanaji‘brand’. Kujibrand ni kujitengeneza kwa aina fulani ili uwe tofauti na watu wengine na huo kuwa utambulisho wako kibiashara. Katika mazungumzo ya wasanii wengi wa kiazi kipya, huwa wanaamini wao ndio wamegundua dhana ya kujibrand, niliwahi hata kumsikia msanii mmoja akisema tatizo la wana muziki wa dansi ni kuwa hawajibrand, kuna ukweli kiasi katika sentensi hiyo lakini msanii huyu alisema hivi kwa kudhani wasanii wa bendi hawajawahi kuelewa dhana ya kujibrand.

Kujibrand kumekuwa sehemu ya muziki wa dansi kwa muda mwingi wa historia ya muziki huo. Hebu turudi nyuma kuanzia miaka ya sitini. Bendi zilijitambulisha kwa majina mbalimbali, jina ni kipengele kimoja cha kujibrand. Kulikuwa na majina yaliyotokana na matukio mbalimbali ya kihistoria na bendi nyingine zilikuwa na majina yaliyotokana na masikani ya bendi na mara nyingine jina ambalo lilikuwa ni la ubunifu tu wasanii wahusika.

Baadhi ya bendi ambazo zilikuwa na majina kutokana na masikani ya bendi hizo ni  Morogoro Jazz, Tabora Jazz, Mbeya Jazz, Dodoma Jazz, Dar es Salaam Jazz Band, Super Matimila Orchestra, Mara Jazz na kadhalika. Butiama Jazz Band ilipata jina hilo kwa historia tofauti kidogo, bendi hiyo haikuwa na maskani Butiama, lakini ilijipatia hilo jina kama heshima kwa kijiji alikozaliwa Mwalimu  Nyerere,  ambaye ndie aliyewanunulia vyombo vyao vya muziki. Western Jazz Band ilijipa jina hilo kutokana na waanzilishi kuwa wanatoka jimbo la Magharibi la Tanganyika. Wakati wa ukoloni nchi iligawanywa katika majimbo yakiwemo Northern Province, southern Highlands Province, Western Province, Lake Province na majimbo mengine. Kilwa Jazz Band ilijibrand hivyo kutokana na muanzilishi wa bendi hiyo, Ahmed Kipande kutokea Kilwa.
 Kulikuwa na bendi zenye majina ya matukio kama Jamhuri Jazz, Ujamaa Jazz, Kilimo Jazz na kadhalika. Halafu kulikuweko na majina ya ubunifu kama Highland Stars, Mitonga Jazz, Kochoko Jazz, Makondeko Six, Cobash Brothers, jina lililotokana na muunganiko wa majina ya mwanamuziki waliokuwemo kwenye bendi hii, Orchestra Safari Sound, Kyauri Voice, Orchestra Toma Toma jina lililotokana na mwenye bendi aliyeitwa Timmy Thomas, kulikuweko na Super Rainbow, Rainbow Connection, Afro 70, Safari Trippers, Atomic Jazz Band, Super Volcano Orchestra, Orchestra Zela Zela,  Orchestra Super Veya, Zaire Success, orchestra Ban Africa Kituli na kadhalika.
Halafu kulikuweko na bendi ambazo zilijipa majina kutokana na kuwa chini ya kampuni au jumuiya ya kijamii. Kulikuweko na Vijana Jazz iliyokuwa chini ya Jumuiya ya Vijana wa CCM, Bima Lee iliyokuwa mali ya kampuni ya Taifa ya Bima, Tancut Almasi Orchestra iliyokuwa mali ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi cha Iringa, Mwenge Jazz mali ya brigedi ya Mwenge na kadhalika. Kule Kilombelo kulikuwa na  Sukari Jazz Band, iliyokuwa ni mali ya kiwanda cha sukari cha Kilombelo, UDA Jazz Band iliyokuwa mali ya kampuni ya mabasi ya usafiri Dar es Salaam, kulikuweko na BAT Jazz iliyokuwa mali ya kiwanda cha sigara cha BAT,  na kadhalika.  Majina haya hakika yalikuwa njia mojawapo ya kujibrand.
Bendi hizi zilianzisha mitindo yao ya kupiga na kucheza na kuipa majina kama njia nyingine ya kujibrand. Katika kumbukumbu hizi lazima tuanze na ‘brand’ kongwe kuliko zote nayo ni mtindo wa  Msondo uliyoanzishwa na NUTA Jazz Band kati ya mwaka 1964 na 1965 na mpaka leo bado uko hai na una nguvu. Kumepita mitindo mingine kama Sikinde, Ndekule, Bayankata, Kiweke, Sensera, Dondola, Afrosa, Koka Koka, Ambianse, Sululu, Saboso, Paselepa, Segere Matata, Vangavanga, Sokomoko, Fimbo Lugoda, King’ita Ngoma, Disco Agwaya, Super Mnayanyuo, Washawasha,  Super Bomboka na mitindo mingine mingi sana,  itachukua kurasa kadhaa kuitaja yote.   
Bendi pia zilikuwa na mavazi mbalimbali, mashati na suruali zishonwa kwa rangi mbalimbali na mitindo ya kupendeza ilyofanya  wanamuziki wapendeze wanapokuwa jukwaani, tena wakicheza kwa utaratibu maalum wa mtindo wao. Kati ya mafundi maarufu na wabunifu wa nguo hizo walikuwa ni mtuma salam maarufu Loboko Lobi Papaa na Mzee Kitenge ambaye kwa sasa yupo soko la Machinga Ilala.
 Kulikuwa na kujibrand kwa mtu mmoja mmoja ambapo wasanii walijipa majina mbali mbali ya kuvutia. Kulikuwa na majina kama Sauti ya Zege, Stereo Voice, Electronic voice, Computer, Golden Fingers, Dudumizi, King Michael na  King Kiki, akina mama hawakuwa nyuma kulikuwa na Stone Lady, Super Mama na wengineo. Kuna wanamuziki waliojikuta wanapata majina kutokana na nyimbo zao, Mzee Zacharia Daniel alijulikana zaidi kama Zacharia Tendawema kutokana na wimbo aliouimba akiwa Shinyanga Jazz Band ulioitwa Tenda Wema Uende zako, Mabrouk Khamis alijulikana zaidi kwa jina la Babu Njenje kutokana na wimbo aliokuwa akiuimba ulioitwa Njenje. Eddy Sheggy nae alianza kuitwa Chaurembo kutokana wimbo alioutunga uliokuwa na jina hilo.

Kwa mifano michache hii, kujibrand si dhana ngeni, bali kutokana na teknolojia imechukua sura mpya na pana zaidi.  Ikihusisha kusambaza picha mnato na video kwenye mitandao, siku hizi hata kutumia mikasa ya uongo kama vile kujitangaza kufa, au kujitangaza kukutwa na jambo la aibu kama kufumaniwa kunatajwa kama kujibrand, hata kuimba nyimbo zisizo kubalika na wengi ili tu zilete mtafaruku  inachukuliwa kama njia ya kuji brand.

Friday, August 19, 2022

KIINGILIO KINYWAJI NINI HATIMA?

 


Ni kawaida kabisa siku hizi kukuta bango likitangaza onyesho la kundi la muziki, na chini kukawa na maneno, kiingilio kinywaji au hata mara nyingine kiingilio bure.  Ni wazi wanamuziki magwiji marehemu kama wangeweza kurudi wangeshangaa na kuuliza hii inawezekana vipi?

Binafsi nimekulia katika utamaduni wa maonyesho kuwa na viingilio, tofauti ilikuwa ni kiwango cha viingilio, makundi maarufu yalikuwa na viingilio vikubwa na makundi machanga yalikuwa na viingilio vidogo. Wenye kumbi walikuwa wakizifuata bendi kubembeleza ziwe zinapiga katika kumbi zao na bendi zikawa na nguvu ya kutoa masharti, kwa mfano mwenye ukumbi angeambiwa atalipwa gharama ya umeme tu, fedha zote za kiingilio ni za bendi, au pengine kukubaliana kuwa baa itapata gawio la asilimia kumi ya mapato ya kiingilio baada ya kuondoa gharama, na makubaliano mengine ya namna hiyo. Hivyo bendi ziliuza muziki mlangoni na mwenye baa akawa anauza vinywaji na chakula chake. Kulikuwa hakuna muingiliano kiasi cha kwamba ilikuwa kawaida saa sita kasoro dakika chache usiku, kulikuwa kunatolewa tangazo kuwa, ‘Ikifika saa sita kaunta inafungwa’,  Hii ilitokana na sheria iliyohusu mauzo ya pombe, watu walinunua vinywaji vya ziada na saa sita biashara ya pombe ilifungwa biashara ya muziki iliendelea mpaka saa nane au tisa usiku.
Lakini kwa zama hizi ni jambo ambalo la kawaida kukuta kiongozi wa bendi anazunguka kutafuta ukumbi kwa kazi za ‘kiingilio bure’. Bendi inaahidiwa kiasi malipo, ambayo mara nyingi ni madogo sana, na kuanza kupiga muziki ili watu wapate burudani wakati wakinywa.
Utamaduni huu umeanza lini? Turudi nyuma miaka ya tisini mwishoni mwishoni. Kulikuwa na kampuni mbili kubwa za bia zilizokuwa na ushindani mkubwa. Kampuni moja ikabuni kitu kilichokuja kufahamika kama ‘promosheni’. Kampuni hii ikaanza kukusanya wasanii wa Sanaa za maigizo na kuwazungusha kwenye kumbi mbalimbali kunapouzwa pombe, huko wasanii walifanya maonyesho na kisha kulipwa na kampuni. Haukupita muda mrefu bendi ndogondogo zikaanza kugombea kujiunga katika katika biashara hiyo, na kwa kweli kulikuwa na bendi ambazo zingetangaza kuwa zinafanya maonyesho hakika hazingepata kiwango ambacho kilikuwa kikitolewa na kampuni ile ya bia, hivyo ilikuwa ni jambo la faida kwa bendi hizi. Pia wakati huohuo kukaanzisha kitu kilichopewa jina la bonanza, hasa ziku za mwisho wa wiki, huko nako bendi na wasanii wa Sanaa za maonyesho hasa wasanii wachekeshaji wakapata kazi na kulipwa  wakati wapenzi wa Sanaa wakifaidi bila kulipa. Miaka ikaenda bendi  za kupiga kwa kiingilio taratibu zikaanza kupungua. Wakati utaratibu huu unakolea, kukatokea tatizo moja kubwa, moja ya hizo kampuni za mbili za bia, ikapotea kwenye soko. Ushindani wa makampuni ukawa haupo, kwa hiyo umuhimu wa ‘promosheni’ ukapungua, kazi zikafifia, wasanii wengi wakapotea moja kwa moja, ikiwemo bendi kadhaa ambazo zilijua ingekuwa vigumu kuanza kutangaza kuwa sasa zimeanza kupiga kwa kiingilio, baya zaidi kukawa kumetengenezwa jamii ambayo imelelewa kutokulipia maonyesho ya Sanaa. Wasanii walikuwa wameshiriki wenyewe  kutengeneza wateja wa ‘maonyesho ya bure’.
Lakini pia kukawa kumezaliwa utamaduni wa wanywaji kuzoea kinywaji na maonyesho ya Sanaa, hili likwafanya wenye kumbi kulazimika kuanza kubeba jukumu la kutafuta wasanii wa kufanya maonyesho kwenye kumbi zao. Lakini uwezo wa wenye kumbi kulipia ‘promosheni’ ukawa mdogo, hivyo basi bendi zimekuwa zikipiga kwa ujira mdogo sana.
Malipo madogo yanafanya ishindikane kuendesha bendi kwa misingi inayotakiwa. Bendi zinashindwa kununua vyombo vizuri, zinashindwa kufanya mazoezi, au hata kurekodi nyimbo mpya. Na baya zaidi mtizamo wa wanamuziki katika utunzi unakuwa mfinyu sana, tungo zinalenga kufurahisha wanywaji tu, hivyo kiwango cha utunzi nacho kinashuka sana. Na si ajabu ukisikia siku hizi kuwa kiwango cha muziki wa bendi kimeshuka, mfumo wa muziki unafanya aina ya utunzi ufanye bendi zionekane zimeshuka kiwango.

Kuna haja ya wanamuziki hasa wa dansi kukaa na kutafakari namna ya kuondoka kwenye hili shimo ambalo ni baya sana. Bendi ikiwa inaamka na kulala kwa kujipanga kwenda kupigia wanywaji tuu, haitakuwa na mawazo ya kushindana katika ulimwengu wa muziki, ni wazi mtu mwenye safari ya kutoka mtaa mmoja hadi mwingine kamwe hawezi kuhangaika kutafuta passport kwani haimuhusu.  Bendi nyingi sasa hazina hata tungo zake binafsi, bendi zinategemea kurudia tungo za wanamuziki wengine. Karibuni tumeanza kusikia viongozi wa vikundi wakilalamika kuwa kuna vikundi vipya vinaundwa vikitegemea nyimbo za kuiga tu kwenye maonyesho yao, hiyo ni changamoto kubwa kwenye muziki wa ‘live’. Pia muda umefika kwa wenye kumbi kuelewa kuwa kama watahitaji muziki bora utakaoleta wateja wengi kwenye kumbi zao ni vizuri wachangie katika swala la kulipa vizuri zaidi. 

Japo swali la wahenga litakuja. Nini kilianza kuku au yai? Malipo mazuri au muziki mzuri?

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...