Nilipokuwa
mdogo nilikuwa naona vibabu vya mtaani kwetu viko vya aina mbili, aina ya
kwanza ilikuwa vibabu ambavyo vilikuwa havicheki kila saa vimenuna na kwa
ujumla, watoto wote tuliviogopa, na tulianza hata kutunga hadithi kuwa vitakuwa
vichawi, au vilipata matatizo makubwa wakati wa ujana na kadhalika. Kundi la
pili la vibabu ilikuwa vile vibabu ambavyo huvikuti vimenuna, ukiviamkia
vinakujibu kwa furaha na kuanza kuulizia wazazi wako, mambo yako ya shule na
kadhalika. Vibabu hivi hata kama una shida ilikuwa rahisi kukusikiliza na
kukupa ushauri hata msaada. Na pia kulikuwa na vibibi vya aina hiyohiyo pia,
tulikuwa na rafiki yetu bibi yake alikuwa anauza maji, kila baada ya siku
chache tulikuwa tukimtembelea bibi kwa kuwa lazima atatugawia senti kumi kumi kutokana na biashara yake ndogo ya
maji, kwa hesabu za harakaharaka alikuwa akitugawia pato lake la siku nzima
bila hata kusita, na wala hatukuwa wajukuu zake wa moja kwa moja. Sasa
yamenikuta siku hizi mimi ndie sasa nimekuwa babu, na polepole naanza kupata
picha kwanini wale babu na bibi zangu walikuwa vile.
Wahenga walikuwa na msemo, nyani mkongwe kakwepa mishale mingi, na ndio ilivyo
katika maisha, wakongwe wamekwepa mengi, wameona mengi, kwa asili ya mila na
tamaduni zetu, wazee walikuwa na nafasi muhimu katika kutoa ushauri wa mambo
kadhaa, lakini hili linapotea taratibu, na hasa ukichukua dhana ya siku hizi
isemayo ‘wazee wamepitwa na wakati’.
Wasanii ni sehemu ya jamii, hivyo hata kwenye tasnia hii dhana ya ‘wazee
wamepitwa na wakati’ inatumika sana.
Ukongwe katika fani unakupa elimu ya mambo mengi, mengine unafundishwa na
wakongwe uliowakuta, mengine unajifunza kazini, hatimae kichwa kinakuwa na
majibu ya mambo mengi ambayo kwa utamaduni wa zamani unatakiwa kuyarithisha kwa
wanaochipukia katika fani. Lakini hili linakuwa gumu pale inapokuja dhana kuwa
‘wazee wamepitwa na wakati’. Ukisha kutana na hali ya kuonekana umepitwa na
wakati kuna mambo mawili unaweza ukaamua, moja unaweza ukawa mtu wa kukasirika
kila wakati, kiasi cha kwamba mtaani ukaonekana ni babu moja mwenye hasira
zisizo na sababu, watoto wakaanza kuhadithiana kuwa utakuwa mchawi au ulipata
matatizo ya akili ulipokuwa kijana. Jambo la pili linaloweza kutokea ni kuamua
kuwa mchangamfu na kubaki unacheka na kila mtu, ili usisumbue kichwa chako, na
hatimae kuondoka duniani na elimu yako kwa furaha.
Kwa kicheko na furaha sana nakumbuka enzi kabla hakujawa na Baraza la Sanaa la
Taifa. Enzi hizo kulikuwa na taasisi
inaitwa Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), chombo kilichoanzishwa mwaka 1974.
Kazi ya BAMUTA ilikuwa kuratibu shughuli za muziki na muziki wa aina zote. BAMUTA
iliuangalia muziki kwa mapana yake yote, elimu, vifaa, masoko, maadili, BAMUTA
pia ilikuwa na kazi ya kuandaa sera za Taifa za muziki. Katika kipindi cha
BAMUTA bendi zilisaidiwa vyombo vya muziki na serikali, BAMUTA ilitungwa vitabu
kadhaa vilivyohusu muziki, ukiwemo muziki wa asili. Mitaala ya muziki
ilitayarishwa na muziki ukawa somo mojawapo linalofundishika mashuleni, waalimu
wake walitayarishwa katika vyuo vya waalimu wa sanaa kama vile Chuo cha Butimba,
na wakaenezwa katika vyuo na mashule nchini kote, wengine wakawa maafisa
utamaduni na wengine kuwa katika ngazi mbalimbali za wizara ya Utamaduni na
sanaa. Kila mkoa ulikuwa na japo bendi moja iliyokuwa na umaarufu, kulikuwa na
kwaya nyingi, madisco mengi, japo wakati
huo uwekezaji katika muziki haukuwa mkubwa kama ulivyo sasa. Mazingira
yakawekwa yaliyoruhusu wapenzi wa muziki waweze kusikiliza aina mbalimbali za
muziki hata muziki ule ambao si wa kibiashara lakini ni mzuri kwa ubora wake au
kwa ujumbe wake. Mazingira hayo yaliwapa wanamuziki maktaba pana ya kuweza
kutohoa aina mpya za muziki. Wajumbe wa BAMUTA walitoka kila kona ya nchi na
hivyo kuipa BAMUTA sura ya Kitaifa, angalia orodha ya wajumbe wa Baraza la
Muziki Tanzania;
1. Boniface Musiba (Mwenyekiti wa
BAMUTA)
2. D. R. Mbilinyi (Mwenyekiti Msaidizi wa BAMUTA)
3. S. Chidumizi (Mjumbe wa BAMUTA-Dodoma)
4. J.Y. Sapali (Mjumbe wa BAMUTA-lringa)
5. Padre J.M. Buluma (Mjumbe wa BAMUTA-Mwanza)
6. A. Kosana (Mjumbe wa BAMUTA-Shinyanga)
7. R. Singano (Mjumbe wa BAMUTA-Tanga)
8. Mbaraka Mwishehe (Mjumbe wa BAMUTA-Morogoro)
9. Padre Kayatto (Mjumbe wa BAMUTA-Mbeya)
10. Gwabukoba (Mjumbe wa BAMUTA-Kigoma)
11. P. Balisidya (Mjumbe wa BAMUTA-Dar es Salaam)
12. R. Mselewa (Katibu Mtendaji wa BAMUTA)
13. E. Kavalambi (Mkufunzi wa Muziki-Marangu CE.T.)
14. K. J. Nsibu (Aflsa Utamaduni-Korogwe)
15. E. Lameck (Mwanakwaya-Mwatex)
16. G. Kanyabwoya (Mwalimu-Kigoma)
17. T. Busyanya (Mkufunzi wa Muziki-DSM CE.T.)
18. G. Daudi (Afisa Sanaa za Maonyesho-Rukwa)
19. John Mgandu (Mwalimu wa Muziki-Tabora Shule ya Seko-ndari ya Wavulana)
20. E. G. Makala (Wizara ya Utamaduni)
21. F.E. Nkwera (Mkufunzi wa Muziki-Songea CE.T.)
22. T. Nkera (Mkufunzi wa Muziki-Ndwika CE.T.)
Wakati ufanisi wa Baraza hili ukiendelea, akatokea mtu mmoja akaanzisha wazo la
kuwa na Baraza moja kwa ajili ya Sanaa zote, na ndipo likazaliwa Baraza la
Sanaa la Taifa. muziki ukashushwa na kuwa ni Idara tu katika katika Baraza hili,
tena hata hiyuo idara ilisha uwawa .
Lakini nisijichoshe, ngoja nikacheze na watoto, si unajua wazee tumepitwa
na wakati.
Ha ha ha hakika uendeshaji wa masuala ya muziki kwa hivi sasa nchini yamebadilika sana. Hoja yako nimeielewa ila wakati, tekinolojia na utandawazi vimebadilisha kabisa namna yetu ya kuendesha shughuli na biashara nzima ya muziki hapa nchini Tanzania.
ReplyDelete