YOUTUBE PLAYLIST

Sunday, August 21, 2022

KUJIBRAND SIO DHANA MPYA

 


Katika zama hizi ni kawaida kabisa kusikia wanamuziki wa kizazi kipya wakisema wanaji‘brand’. Kujibrand ni kujitengeneza kwa aina fulani ili uwe tofauti na watu wengine na huo kuwa utambulisho wako kibiashara. Katika mazungumzo ya wasanii wengi wa kiazi kipya, huwa wanaamini wao ndio wamegundua dhana ya kujibrand, niliwahi hata kumsikia msanii mmoja akisema tatizo la wana muziki wa dansi ni kuwa hawajibrand, kuna ukweli kiasi katika sentensi hiyo lakini msanii huyu alisema hivi kwa kudhani wasanii wa bendi hawajawahi kuelewa dhana ya kujibrand.

Kujibrand kumekuwa sehemu ya muziki wa dansi kwa muda mwingi wa historia ya muziki huo. Hebu turudi nyuma kuanzia miaka ya sitini. Bendi zilijitambulisha kwa majina mbalimbali, jina ni kipengele kimoja cha kujibrand. Kulikuwa na majina yaliyotokana na matukio mbalimbali ya kihistoria na bendi nyingine zilikuwa na majina yaliyotokana na masikani ya bendi na mara nyingine jina ambalo lilikuwa ni la ubunifu tu wasanii wahusika.

Baadhi ya bendi ambazo zilikuwa na majina kutokana na masikani ya bendi hizo ni  Morogoro Jazz, Tabora Jazz, Mbeya Jazz, Dodoma Jazz, Dar es Salaam Jazz Band, Super Matimila Orchestra, Mara Jazz na kadhalika. Butiama Jazz Band ilipata jina hilo kwa historia tofauti kidogo, bendi hiyo haikuwa na maskani Butiama, lakini ilijipatia hilo jina kama heshima kwa kijiji alikozaliwa Mwalimu  Nyerere,  ambaye ndie aliyewanunulia vyombo vyao vya muziki. Western Jazz Band ilijipa jina hilo kutokana na waanzilishi kuwa wanatoka jimbo la Magharibi la Tanganyika. Wakati wa ukoloni nchi iligawanywa katika majimbo yakiwemo Northern Province, southern Highlands Province, Western Province, Lake Province na majimbo mengine. Kilwa Jazz Band ilijibrand hivyo kutokana na muanzilishi wa bendi hiyo, Ahmed Kipande kutokea Kilwa.
 Kulikuwa na bendi zenye majina ya matukio kama Jamhuri Jazz, Ujamaa Jazz, Kilimo Jazz na kadhalika. Halafu kulikuweko na majina ya ubunifu kama Highland Stars, Mitonga Jazz, Kochoko Jazz, Makondeko Six, Cobash Brothers, jina lililotokana na muunganiko wa majina ya mwanamuziki waliokuwemo kwenye bendi hii, Orchestra Safari Sound, Kyauri Voice, Orchestra Toma Toma jina lililotokana na mwenye bendi aliyeitwa Timmy Thomas, kulikuweko na Super Rainbow, Rainbow Connection, Afro 70, Safari Trippers, Atomic Jazz Band, Super Volcano Orchestra, Orchestra Zela Zela,  Orchestra Super Veya, Zaire Success, orchestra Ban Africa Kituli na kadhalika.
Halafu kulikuweko na bendi ambazo zilijipa majina kutokana na kuwa chini ya kampuni au jumuiya ya kijamii. Kulikuweko na Vijana Jazz iliyokuwa chini ya Jumuiya ya Vijana wa CCM, Bima Lee iliyokuwa mali ya kampuni ya Taifa ya Bima, Tancut Almasi Orchestra iliyokuwa mali ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi cha Iringa, Mwenge Jazz mali ya brigedi ya Mwenge na kadhalika. Kule Kilombelo kulikuwa na  Sukari Jazz Band, iliyokuwa ni mali ya kiwanda cha sukari cha Kilombelo, UDA Jazz Band iliyokuwa mali ya kampuni ya mabasi ya usafiri Dar es Salaam, kulikuweko na BAT Jazz iliyokuwa mali ya kiwanda cha sigara cha BAT,  na kadhalika.  Majina haya hakika yalikuwa njia mojawapo ya kujibrand.
Bendi hizi zilianzisha mitindo yao ya kupiga na kucheza na kuipa majina kama njia nyingine ya kujibrand. Katika kumbukumbu hizi lazima tuanze na ‘brand’ kongwe kuliko zote nayo ni mtindo wa  Msondo uliyoanzishwa na NUTA Jazz Band kati ya mwaka 1964 na 1965 na mpaka leo bado uko hai na una nguvu. Kumepita mitindo mingine kama Sikinde, Ndekule, Bayankata, Kiweke, Sensera, Dondola, Afrosa, Koka Koka, Ambianse, Sululu, Saboso, Paselepa, Segere Matata, Vangavanga, Sokomoko, Fimbo Lugoda, King’ita Ngoma, Disco Agwaya, Super Mnayanyuo, Washawasha,  Super Bomboka na mitindo mingine mingi sana,  itachukua kurasa kadhaa kuitaja yote.   
Bendi pia zilikuwa na mavazi mbalimbali, mashati na suruali zishonwa kwa rangi mbalimbali na mitindo ya kupendeza ilyofanya  wanamuziki wapendeze wanapokuwa jukwaani, tena wakicheza kwa utaratibu maalum wa mtindo wao. Kati ya mafundi maarufu na wabunifu wa nguo hizo walikuwa ni mtuma salam maarufu Loboko Lobi Papaa na Mzee Kitenge ambaye kwa sasa yupo soko la Machinga Ilala.
 Kulikuwa na kujibrand kwa mtu mmoja mmoja ambapo wasanii walijipa majina mbali mbali ya kuvutia. Kulikuwa na majina kama Sauti ya Zege, Stereo Voice, Electronic voice, Computer, Golden Fingers, Dudumizi, King Michael na  King Kiki, akina mama hawakuwa nyuma kulikuwa na Stone Lady, Super Mama na wengineo. Kuna wanamuziki waliojikuta wanapata majina kutokana na nyimbo zao, Mzee Zacharia Daniel alijulikana zaidi kama Zacharia Tendawema kutokana na wimbo aliouimba akiwa Shinyanga Jazz Band ulioitwa Tenda Wema Uende zako, Mabrouk Khamis alijulikana zaidi kwa jina la Babu Njenje kutokana na wimbo aliokuwa akiuimba ulioitwa Njenje. Eddy Sheggy nae alianza kuitwa Chaurembo kutokana wimbo alioutunga uliokuwa na jina hilo.

Kwa mifano michache hii, kujibrand si dhana ngeni, bali kutokana na teknolojia imechukua sura mpya na pana zaidi.  Ikihusisha kusambaza picha mnato na video kwenye mitandao, siku hizi hata kutumia mikasa ya uongo kama vile kujitangaza kufa, au kujitangaza kukutwa na jambo la aibu kama kufumaniwa kunatajwa kama kujibrand, hata kuimba nyimbo zisizo kubalika na wengi ili tu zilete mtafaruku  inachukuliwa kama njia ya kuji brand.

1 comment:

  1. Anonymous23:00

    Endelea kutuelimisha mzee wangu mimi ni mpenzi wa miziki ya dance ndiyo maana huwa nafatilia sana nakala zako za ezi hizo. Pia kampuni yangu ikishilikiana na mama akuso tumeanda usiku wa hrumba morogoro tarehe 27/08/2022 na tutaitambulisha band mpya siku hiyo. Karibu sana mzee wangu.
    Naitwa kikoti - 0719 333 527

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...