Baada ya matayarisho mbalimbali yaliyochukua miezi mitatu hatimae tarehe 28 September 2012, bendi ziliweza kuanza kupanda jukwaani kufanya maonyesho katika viwanja vya Leaders Club. Bendi zilizopanda jukwaani karibu zote zilikuwa na makubaliano ya kulipwa na zililipwa fedha ya awali wiki 2 kabla ya onyesho na fedha iliyobaki ilikamilishwa siku ambapo bendi zilipanda jukwaani. Hakuna bendi yoyote iliyokuwa ikiwadai watayarishaji.
Watayarishaji
walijipanga kwa kuhakikisha kuna jukwaa la Kimataifa lililopambwa na taa za
rangi za kiwango cha juu, na vifaa vya muziki ambavyo vilihakikisha kila bendi
inapopiga muziki, muziki wake ulisikika kwa kiwango cha hali ya juu.
Hakukusikika mpaka leo malalamiko kuhusu upande huo wa matayarisho.
Tamasha lilianza tarehe 28 September 2012, saa kumi na mbili
jioni, kwa bendi kuanza kufanya
maonyesho, bendi ya kwanza kupanda jukwaani ilikuwa ni Msondo Ngoma Music Band
na kufuatiwa na bendi ya Fm Academia, na baadae bendi za Akudo Impact, Mashujaa
Band, kundi la Taarab la Mashauzi Classic na baadae vijana wa Orynx Band. Bendi
zote zilifanya vizuri sana, bendi zilipanda
kwa zamu kama ratiba ilivyokuwa imewaelekeza na mshereheshaji alikuwa ni Ben Kinyaiya alifanya kazi kwa
umakini wa hali ya juu .
Tamasha liliendelea siku ya pili kama ratiba ilivyokuwa imepangwa kwa bendi za
Mlimani Park, Skylight band, B Band, Oryx Band, Bi. Khadija Kopa kupanda jukwaani, na kama ilivyokuwa jana
yake wakiongozwa na mshereheshaji Ben
Kinyaiya.
MAFANIKIO
Mafanikio yaliyopatikana
ni uzoefu mkubwa wa namna ya kutayarisha tamasha la muziki wa bendi.
Mawasiliano yaliweza kufunguliwa kati ya watayarishaji na wanamuziki wa bendi
mbalimbali. Kumekuweko na mafanikio ya kujua namna ya kupata vyombo na mafundi
bora wa sauti, upambaji wa jukwaa na matayarisho yote ya awali ya kuwezesha
tamasha kufanyika. Kumepatikana uzoefu wa kuitisha press conference na kufanya
mikutano na wadau mbalimbali wa matamasha, serikalini, katika kampuni binafsi
na watu binafsi.
WADAU TAMASHA.
Tamasha hili
liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Edge Entertaiment na Chama Cha Muziki wa Dansi Tanzania(CHAMUDATA) baada ya
makubaliano, ambayo yalifikiwa kukiweko na malengo ya kupata fedha kwa ajili ya
kusaidia miradi ya CHAMUDATA na kutoa mchango kwa BASATA. Kampuni ya Edge
Entertaiment iliingia mkataba na Times
Fm Radio ambao uliwezesha Times Fm
kulitangaza Tamasha pia kutoa gharama za
matumizi yote ya maandalizi ya tamasha
kwa makubaliano ya fedha zitakazotumika kurudishwa kutokana na mapato ya
tamasha.
KAMATI.
Kamati ya
pamoja ya Edge Entertaiment na Times Fm
Radio iliundwa na ikapewa majukumu ya kuhakikisha tamasha linafanikiwa, kamati ilifanya kazi chini
ya uangalizi wa upande zote mbili zilizokubaliana na kamati iliomba kampuni ya Edge Entertaiment iajiri
mtu wa PR atakayehakikisha mpangilio mzuri
wa Tamasha na Edge Entertainment ilifanya hivyo.
VYOMBO VYA HABARI.
Katika
kuhakikisha tamasha linafanikiwa kamati ilitumia vyombo vya habari vifuatavyo
Magazeti, Tv, Blogs, Radio
Magazeti
yaliyotumika;
(a)Mwananchi
(b)Jambo leo
(c)Mtanzania
(d) Magazeti ya Global Publishers
Tv
zilizotumika;
(a) TBC - Mahojiano
(b) Chanel Ten- Mahojiano
Blogs
zilizotumika;
(a) Michuzi
(b) Full
shangwe
(c) Dar blog
(d)
www.musiciansintanzania.blogspot
Radio;
Radio
iliyotumika ni Times Fm Radio hii ilitokana na udhamini ambao redio hii ilikuwa
imetoa
MATATIZO.
Kulikuweko
na matatizo kadha wa kadha, mengine ni kutokana na maamuzi yaliyofanyika,
mengine ni kutokana na wadau mbalimbali wa Tamasha, na machache ambayo yalikuwa
njee ya uwezo wa Kamati ya tamasha
* Tamasha lilifanyika
siku ya Ijumaa na Jumamosi, huu ulikuwa uamuzi ambao ulionekana kuwa ni mzuri,
lakini kwa mawazo ya wadau waliohudhuria wengi waliona ingekuwa bora tamasha
lingeanza Jumamosi na hatimae kufikia kilele Jumapili kwa maonyesho ambayo
yangeanza Jumapili kuanzia saa nne asubuhi hadi kati ya saa4 na saa 6 usiku
siku hiyo
* Pamoja na
bendi kulipwa si chini ya shilingi laki saba kila bendi bendi ziliendelea
kupanga ratiba zao na hata kutangaza kuwa wako katika sehemu nyingine kwa siku
na wakati uleule ambapo bendi zilitegemewa kuwa jukwaani katika tamasha. Msondo
Ngoma walipiga wimbo mmoja tu kwa malipo ya shilingi milioni 1.
* CHAMUDATA kilikuwa mdau muhimu katika tamasha hili,
kwanza kwa kuwa sehemu ya mapato yalikuwa yaiingie katika mfuko wa chama hicho,
na pili hili lilikuwa tamasha la muziki wa bendi, hivyo kuwa linafanya kile
ambacho chama hiki kinasimamia, lakini hakukuweko hata afisa mmoja wa CHAMUDATA katika kipindi chote cha tamasha,
ambapo ingetegemewa chama kiwe chombo kimojawapo cha kupigia debe mafanikio ya
tamasha hili.
* Kulikuweko
na matatizo ya matangazo ambapo palikuweko na matukio ya kubandua mabango, na
wakati fulani kuchanganya taarifa katika matangazo ya magazeti.
* Pamoja na
kuwa eneo la Leaders lilikuwa limelipiwa, bado uongozi wa bar ya Leaders
ulikaidi na kuendelea kukiuka masharti kwa kuendelea kufanya mauzo ya vinywaji
kinyume na utaratibu na makubaliano na wadhamini wakuu wa tamasha. Hili
limepelekea wadhamini kugoma kulipa baki ya ada ya udhamini ambayo ni shilingi 10,000,000.
* Mgeni
rasmi aliwasili kwa muda aliopangiwa ambao ulikuwa ni saa moja, hili lilikuwa
kosa kwani muda huo ndio ratiba inaanza na si muda mzuri kwa mgeni rasmi kuwa
ndio anawasili, pia hakukuweko na protokali za kumpokea mgeni rasmi jambo
ambalo lilitia doa ujio wake. Na hivyo alishindwa hata kufanya shughuli ya
kufungua rasmi tamasha
HITIMISHO.
Kwa ujumla
Tamasha lilikuwa na mengi sana mazuri kiutendaji, vyombo vizuri na vya kisasa, stage
kubwa ya kisasa, na liliweza kufanyika kwa bendi zaidi ya kumi kushiriki. Ni wazi ni
muhimu utamaduni huu wa kuwa natamasha kila mwaka kuendelea japo matayarisho
yanatakiwa kuanza sasa.
Wanamuziki wa mabendi walikatisha tamaa kwani wamekuwa wakilalamikia kukosekana
kwa Tamasha lao, lakini ni wazi
walithamini zaidi kazi zao za kawaid kuliko Tamasha lililokuja kukidhi kiu yao.
Kwa upande wa mapato hayakuwa mazuri waandaji waliingia hasara kubwa na hivyo kushindwa kutimiza malengo yake likiwemo
la kukisaidia Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA). Waandaji
wataendelea na elimu na mafunzo mbalimbali kwa wanamuziki wa muziki wa dansi
wakishirikiana na BASATA na CHAMUDATA ili kuweza kuleta mafanikio katika muziki
wa dansi Tanzania.
Katibu
No comments:
Post a Comment