Tape recorder ya studio miaka ya 90 kurudi nyuma
Teknolojia imebadili taratibu zote za utengenezaji wa muziki. Ngoja nirudi nyuma miaka ya 80, nielezea taratibu za kurekodi nyimbo ambazo siku hizi zinaitwa zilipendwa. Kurekodi haikuwa kazi rahisi, hakukuwa na kompyuta ya kutengeneza mapigo na kutoa sauti mbalimbali za muziki na hata kuelekeza mwendo wa wimbo, ililazimika waweko watu halisi wapige muziki na kurekodiwa kwenye kanda zilizoitwa tape. Mashine za kurekodia zilizoitwa ‘tape recorders’ zilikuwa na uwezo wa kurekodi njia mbili (two track), hebu linganisha hilo na zama hizi ambazo hata kompyuta ya kawaida ikiwa na program sahihi inaweza kurekodi mamia ya ‘tracks’ bila tatizo lolote. Hivyo basi teknolojia hii ya two track ililazimisha kundi linalotaka kurekodi liupige wimbo wao wote bila kukosea ‘live’ na akikosea mtu mmoja tu, lazima kufuta wimbo wote na kuanza upya. Hii ilikuwa na maana kuwa kila kundi lililotaka kwenda kurekodi, ilikuwa lazima kufanya mazoezi magumu ya muda mrefu ili kila mwanamuziki awe anauhakika na vipande vyake atakavyovipiga.
Studio kubwa
za kurekodi muziki zilikuwa mbili, studio ya Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD)
na studio za Tanzania Film Company (TFC). Zote zilikuwa na masharti yaliyofanya
kazi ya kurekodi kuwa ngumu zaidi. Studio ya RTD ilikuwa inaipa kila bendi siku
mbili za kurekodi. Siku ya kwanza kurekodi nyimbo mpya za bendi na siku ya pili
kurekodi kipindi cha Club Raha Leo. Kila bendi ilikuwa inahitajika kuja na
vyombo vyake. Mapema siku ya kwanza ya ratiba, bendi iliingiza vyombo studio na
kazi ya kuvifunga na kuvitayarisha kwa kurekodi ilichukua muda wote wa asubuhi ya siku ya
kwanza. Mchana baada ya kula ndipo wanamuziki walipoingia kurekodi nyimbo zao.
Kulikuwa na sheria kuwa watu wote ambao si wafanyakazi wa RTD walitakiwa kuwa
wameondoka eneo la RTD kabla ya kushushwa bendera saa 12 jioni. Hivyo basi bendi kama ilikuwa na
nyimbo 4 au 10 ililazimika kukamilisha kazi ya kuzirekodi zote hizo kati ya saa 8
mchana mpaka saa kumi na mbili jioni. Kama nilivyosema awali, nyimbo zilitakiwa kupigwa
na kuimbwa bila kukosea, kwa kweli
kazi iliyokuwa ikifanywa na wanamuziki wa enzi ile ni ya kusifika. Ukisikiliza kwa makini kuna nyimbo nyingi maarufu zilizopendwa huwa zinakuwa na makosa madogo madogo, lakini mara nyingi ilikuwa ni kutokana na hali niliyoitaja hapo juu. Kuna wimbo mmoja wa African Fiesta ambao alikuwa anaimba Tabu Ley unaitwa Ndaya, wakati wa chorus unamsikia Tabu Ley akijichanganya maneno , lakini nadhani ilionekana upite, hii ilikuwa ikitokea pale wimbo umesharudiwa mara nyingi na wanamuziki wamekwisha choka.
Fundi mitambo alikuwa akitupigia wimbo tusikie baada ya kurekodi na alikuwa akiuliza' Vipi huu?' wenyewe tukiwa tumeridhika tulijibu 'Upite'.
TFC hawakuwa
na masharti ya muda wa kuondoka studio, TFC ilikuwa shirika la umma
na hivyo lilikuwa likiendeshwa
kibiashara na malipo ya studio yalikuwa kwa siku. Kwa kuwa bendi hazikuwa na
fedha, mara nyingi zililipa malipo ya kutumia studio siku mbili zikizidi sana tatu. Hapo
ilikuwa wanamuziki wenyewe wanakuwa makini ili kutumia vizuri muda wao, ili
usije ukaisha na fedha za kuongeza muda zisiweko. Nikiwa Vijana Jazz tulitumia
studio za TFC kurekodi album iliyokuwa na nyimbo maarufu kama Thereza, VIP na
Mfitini. Tulikesha siku mbili kukamilisha album ile.
Teknolojia
ya sasa inaruhusu mtu mmoja kama unauwezo wa kupiga vyombo mbalimbali na
kuimba,ukaweza hata kutengeneza nyimbo ambazo zitasikika kama vile ni bendi
nzima ilikuwa kazini. Kwa mfano kati ya album za kwanza za wanamuziki wa
Tanzania ambazo zilitoka kwa kutumia teknolojia hii ya sasa ya ‘multi track’ ni album ya Dhiki ya Patrick
Balisidya. Katika album hii Patrick alipiga vyombo karibu vyote na pia kuimba
sauti zote, ukisikia nyimbo hizo utadhani zilipigwa na bendi nzima.
Pamoja na
ubora wote wa teknolojia hii, kurekodi kwa mtu mmoja mmoja kunaondoa sehemu
kubwa ya utamu katika nyimbo zilizorekodiwa. Hebu fikiria ngoma yoyote ya
kiasili, irekodiwe kwa mpigaji ngoma moja moja kuingia studio na kurekodi
mapigo yake, utamu ule wa wapigaji kupeana hamasa wakati wa kupiga wote utaondoka.
Pengine ndio sababu nyimbo za sasa zinarekodiwa na kusikika vizuri lakini zinakosa
uhai fulani wa wapigaji kupiga kwa pamoja, na kuhamasishana, kupata ile 'feeling ya live'. Nyimbo za bendi zamani zilikuwa kwanza tayari zimeshapigwa mara nyingi katika kumbi mbalimbali hivyo kuwa na aina ya uhai ambao huwezi kuupata katika wimbo ambao ni mpya kabisa. Utaratibu huu uliwezesha bendi kuboresha wimbo hatimae siku ya kurekodi wimbo unakuwa umeiva.
No comments:
Post a Comment