Ni kawaida kabisa siku hizi kukuta bango likitangaza onyesho la kundi la muziki, na chini kukawa na maneno, kiingilio kinywaji au hata mara nyingine kiingilio bure. Ni wazi wanamuziki magwiji marehemu kama wangeweza kurudi wangeshangaa na kuuliza hii inawezekana vipi?
Binafsi
nimekulia katika utamaduni wa maonyesho kuwa na viingilio, tofauti ilikuwa ni
kiwango cha viingilio, makundi maarufu yalikuwa na viingilio vikubwa na makundi
machanga yalikuwa na viingilio vidogo. Wenye kumbi walikuwa wakizifuata bendi
kubembeleza ziwe zinapiga katika kumbi zao na bendi zikawa na nguvu ya kutoa
masharti, kwa mfano mwenye ukumbi angeambiwa atalipwa gharama ya umeme tu,
fedha zote za kiingilio ni za bendi, au pengine kukubaliana kuwa baa itapata
gawio la asilimia kumi ya mapato ya kiingilio baada ya kuondoa gharama, na
makubaliano mengine ya namna hiyo. Hivyo bendi ziliuza muziki mlangoni na
mwenye baa akawa anauza vinywaji na chakula chake. Kulikuwa hakuna muingiliano
kiasi cha kwamba ilikuwa kawaida saa sita kasoro dakika chache usiku, kulikuwa
kunatolewa tangazo kuwa, ‘Ikifika saa sita kaunta inafungwa’, Hii ilitokana na sheria iliyohusu mauzo ya
pombe, watu walinunua vinywaji vya ziada na saa sita biashara ya pombe
ilifungwa biashara ya muziki iliendelea mpaka saa nane au tisa usiku.
Lakini kwa zama hizi ni jambo ambalo la kawaida kukuta kiongozi wa bendi anazunguka
kutafuta ukumbi kwa kazi za ‘kiingilio bure’. Bendi inaahidiwa kiasi malipo,
ambayo mara nyingi ni madogo sana, na kuanza kupiga muziki ili watu wapate
burudani wakati wakinywa.
Utamaduni huu umeanza lini? Turudi nyuma miaka ya tisini mwishoni mwishoni.
Kulikuwa na kampuni mbili kubwa za bia zilizokuwa na ushindani mkubwa. Kampuni
moja ikabuni kitu kilichokuja kufahamika kama ‘promosheni’. Kampuni hii ikaanza
kukusanya wasanii wa Sanaa za maigizo na kuwazungusha kwenye kumbi mbalimbali
kunapouzwa pombe, huko wasanii walifanya maonyesho na kisha kulipwa na kampuni.
Haukupita muda mrefu bendi ndogondogo zikaanza kugombea kujiunga katika katika
biashara hiyo, na kwa kweli kulikuwa na bendi ambazo zingetangaza kuwa
zinafanya maonyesho hakika hazingepata kiwango ambacho kilikuwa kikitolewa na
kampuni ile ya bia, hivyo ilikuwa ni jambo la faida kwa bendi hizi. Pia wakati
huohuo kukaanzisha kitu kilichopewa jina la bonanza, hasa ziku za mwisho wa
wiki, huko nako bendi na wasanii wa Sanaa za maonyesho hasa wasanii wachekeshaji
wakapata kazi na kulipwa wakati wapenzi
wa Sanaa wakifaidi bila kulipa. Miaka ikaenda bendi za kupiga kwa kiingilio taratibu zikaanza
kupungua. Wakati utaratibu huu unakolea, kukatokea tatizo moja kubwa, moja ya
hizo kampuni za mbili za bia, ikapotea kwenye soko. Ushindani wa makampuni
ukawa haupo, kwa hiyo umuhimu wa ‘promosheni’ ukapungua, kazi zikafifia,
wasanii wengi wakapotea moja kwa moja, ikiwemo bendi kadhaa ambazo zilijua ingekuwa
vigumu kuanza kutangaza kuwa sasa zimeanza kupiga kwa kiingilio, baya zaidi
kukawa kumetengenezwa jamii ambayo imelelewa kutokulipia maonyesho ya Sanaa.
Wasanii walikuwa wameshiriki wenyewe
kutengeneza wateja wa ‘maonyesho ya bure’.
Lakini pia kukawa kumezaliwa utamaduni wa wanywaji kuzoea kinywaji na maonyesho
ya Sanaa, hili likwafanya wenye kumbi kulazimika kuanza kubeba jukumu la kutafuta
wasanii wa kufanya maonyesho kwenye kumbi zao. Lakini uwezo wa wenye kumbi kulipia
‘promosheni’ ukawa mdogo, hivyo basi bendi zimekuwa zikipiga kwa ujira mdogo
sana.
Malipo madogo yanafanya ishindikane kuendesha bendi kwa misingi inayotakiwa. Bendi
zinashindwa kununua vyombo vizuri, zinashindwa kufanya mazoezi, au hata
kurekodi nyimbo mpya. Na baya zaidi mtizamo wa wanamuziki katika utunzi unakuwa
mfinyu sana, tungo zinalenga kufurahisha wanywaji tu, hivyo kiwango cha utunzi
nacho kinashuka sana. Na si ajabu ukisikia siku hizi kuwa kiwango cha muziki wa
bendi kimeshuka, mfumo wa muziki unafanya aina ya utunzi ufanye bendi zionekane
zimeshuka kiwango.
Kuna haja ya
wanamuziki hasa wa dansi kukaa na kutafakari namna ya kuondoka kwenye hili
shimo ambalo ni baya sana. Bendi ikiwa inaamka na kulala kwa kujipanga kwenda
kupigia wanywaji tuu, haitakuwa na mawazo ya kushindana katika ulimwengu wa
muziki, ni wazi mtu mwenye safari ya kutoka mtaa mmoja hadi mwingine kamwe
hawezi kuhangaika kutafuta passport kwani haimuhusu. Bendi nyingi sasa hazina hata tungo zake
binafsi, bendi zinategemea kurudia tungo za wanamuziki wengine. Karibuni tumeanza
kusikia viongozi wa vikundi wakilalamika kuwa kuna vikundi vipya vinaundwa
vikitegemea nyimbo za kuiga tu kwenye maonyesho yao, hiyo ni changamoto kubwa
kwenye muziki wa ‘live’. Pia muda umefika kwa wenye kumbi kuelewa kuwa kama
watahitaji muziki bora utakaoleta wateja wengi kwenye kumbi zao ni vizuri
wachangie katika swala la kulipa vizuri zaidi.
Japo swali
la wahenga litakuja. Nini kilianza kuku au yai? Malipo mazuri au muziki mzuri?
Dah umegusa maada muhimu sana.. Ni kweli hawa makampuni ama Corporates wamechangia kama sio kupandikiza desturi ya kutumia muziki kama chombo cha kutangaza bidhaa au huduma zao.
ReplyDeleteila angalau siku hizi naona taratibu watu wanakubali kulipa. nafikiri kwa kuwa muziki wa bure inakosa uhuru wa kupata kile anachohitaji mlaji.
Ikipigwa ile Amapiano yenye chorus *sisi ni walevi*😃 kuna baadhi yetu humu tuna sing along kwa sautibya kwanza.. hehehe.Ijumaa karim.
ReplyDeleteKwa kuleta live music kwenye bar kwa wateja, you are giving them a significant source of entertainment, and adding vibrancy and excitement to the atmosphere of the venue.
Hence Live music lifts the vibe and instantly draws a crowd. Whether it’s because the music wafts out to the street and attracts passersby, or it provides a fun and distracting reason for customers to prolong their stay past stopping for a pint of beer.
Vile vile kuna pub food business ambayo kwa kweli ni ngumu.
Pale wateja wanapo endelea kujichana makuku bila hatacya *kupay attention* msanii anaimba nini nakumbuka Case ya Nina Simon kuchoma mteja mwenye kelele kupita wote kisu cha mezani Huko Ufaransa wakati Nina ana perform, ambayo ilimpelekea Nina kupelekwa Rehabilitation... ila nilimuelewa.
Kule Zanzibar kwenye mahotel ya kitalii wanamuziki hulazimishwa kupiga back ground yaani wawepo kama hawapo.
La msingi ni kurejesha ustaarabu wa kumbi za starehe yaani Performance spaces maalum kwa Sanaa za maonyesho tuu.
Mfano Makumbusho yataifa.. ambapo kazi ni moja tuu Art.
Napenda kwapa tano Asedeva Ndugu Abeneko na wenzake kwa hilo
Muda Dance na Nafasi Art space kwa kutilia maanani Sanaa zaidi ya biashara ya pombe.
Mwakitime ngweliwe sana tena sana...
ReplyDeleteNikukaribishe tarehe 27 agust 2022 F2 florida, morogoro tukupe hata dakika 3 za kutusalimia
Naitwa kikoti mkurugenzi wa special one entertainment