Vijana Jazz Band tukielekea Ifakara |
Kuwa
mwanamuziki katika miaka ya tisini na kurudi nyuma haikuwa lelemama, ilikuwa kazi ngumu,
iliyokuwa yakujitolea haswa. Kati mambo magumu miaka hiyo ilikuwa kusafiri
kwenda kufanya maonyesho. Katika zama hizi mwanamuziki anapata mualiko,
anatajiwa na fungu atakalolipwa, anachagua aina ya hoteli ya kulala na hata
usafiri kama ni wa ndege au gari la abiria
au hata gari binafsi, fursa hizo hazikuweko miaka hiyo.
Kwanza kabisa kulikuwa na taratibu za kiserikali, ili bendi au kikundi cha
muziki kitoke katika mkoa ambako ni masikani taratibu zilikuwa ngumu. Kikundi
kilianza kwa kuandika barua kwa Afisa Utamaduni wa mkoa kuomba ruksa ya kutoka
nje ya mkoa. Afisa Utamaduni akisha kutoa kibali kile, muwakilishi wa bendi
hutangulia kwenda kuwakilisha kibali kwa Afisa Utamaduni wa mkoa ambao kundi
linaenda ili kupata kibali cha kufanya kazi katika mkoa husika, Afisa Utamaduni
Mkoa akisha toa kibali kuingia mkoa wake, ndipo nakala ya kibali hupelekwa kwa
Afisa Utamaduni wa Wilaya ili nae atoe kibali cha kuruhusu kundi kufanya
maonyesho katika wilaya yake. Kutokana na uchache wa magazeti, vikundi vingi
vilianza safari bila matangazo yoyote, kwani kuna wilaya nyingine, magazeti
hayakuwa yanafika kabisa au magazeti yalifika machache na hata hayo yaliweza
kuchelewa hata siku nne. Mwakilishi wa
kikundi akishafika kwenye mji ambao bendi au kundi lingefanya maonyesho,
alishirikiana na Afisa Utamaduni kupata kumbi na kufanya booking ya mahala pa
kulala. Matangazo ilikuwa ni karatasi za kuandika kwa mkono na kisha kubandika
katika kuta na nguzo mbalimbali. Baada ya hapo alitafutwa mwenyeji ambaye ni
mtangazaji naye alipita katika mitaa mbalimbali akitangaza kupitia kipaza sauti
cha mkononi. Nakumbuka mwaka mmoja mapema miaka ya 80, nikiwa na Orchestra
Mambo Bado, tulifika Mpanda na kuelekezwa kuwa mtu maalumu ambaye hutangaza mambo
yote pale, alikuwa bwana mmoja aliyepewa jina la utani la Mshindo Mkeyenge.
Huyu alikuwa akipita mitaa mbalimbali na ngoma yake na hiyo hugonga ili watu wamsikilize na ndipo hapo hutangaza
kuwa kuna dansi linakuja na litakuwa wapi na kiingilio chake.
Usafiri wa
bendi ulikuwa wa basi za abiria na mara nyingi malori ambamo wanamuziki
walijazana humo wakiwa na vyombo vyao. Kati ya safari za aina hii nilizowahi
kusafiri kwa roli ni toka Mbeya hadi Chunya na kurudi, kutoka Mtwara na
kuzunguka miji ya kusini mingi kama Masasi , Nachingwea, Lindi kutumia lori la
aina ya Isuzu Long base. Na nikiwa na bendi ya Tancut kwa ujumla usafiri wetu
ulikuwa ni loti aina ya ‘canter’, humo tulizunguka miji kuanzia Makambako,
Njombe, Songea, Mbeya, Tunduma na miji mingine mingi, tuliwahi pia kuzunguka
miji mingi kanda ya ziwa kutumia lori
aina ya Leylan Albion. Huo ndio ulikuwa usafiri wa masupastaa wa mika hiyo.
Malazi kwa kawaida hayakuwa ya kifahari, kwa
kawaida vyumba vilivyokodishwa vilikuwa ni dabo ili kupunguza gharama, na gesti
zenyewe zilikuwa ni zile ambazo gharama zake zikuwa chini. Kulala njaa halikuwa
jambo la ajabu, hasa mkipiga dansi na kukosa wateja, hapo ndipo mnaweza
kujikuta mmelala ukumbini ili pesa itoshe gharama za kuwasafirisha kwenda mji
unaofuata. Miji mingi haikuwa na umeme hivyo bendi nyingine zilikuwa
zikizunguka na jenereta, au kukodi kwa ajili ya kila onyesho.
Kama ilivyo
katika biashara nyingine uongo nao ulikuwa mwingi sana, utasikia , ‘Bwana bendi
ikienda Nyarugusu kule fedha nje nje, wachimba migodi wana pesa sana lazima
mtarudi na pesa za kutosha kununua vyombo vipya’ . Hapo harakati za kwenda
Nyarugusu zitaanza. Miaka hiyo Nyarugusu ilikuwa mji mmoja maarufu kwa wachimba
dhahabu wadogowadogo, lakini sijawahi kuona bendi ikipata fedha za ajabu baada
ya kwenda Nyarugusu. Kuna wakati Bendi
tatu tulikutana Mwanza kila moja ikiwa ina mpango wa kwenda Nyarugusu. Vijana
Jazz Band, Maquis na Ngorongoro Heroes wote tukawa Mwanza. Hali
ilikuwa mbaya sana kwa Maquis ambayo ilikuwa safarini huku kwa zaidi ya miezi mitatu, ilifikia kiasi cha
wanamuziki kuanza kurudi Dar es Salam mmoja mmoja.
Lakini ilikuwa ni baada ya safari hii walipojipanga upya na kurekodi vile vibao
vyao vikali, Makumbele, Tipwa tipwa na Ngalula na kurudisha heshima yao mjini.
Kifupi hayo
ndiyo yalikuwa maisha ya mwanamuziki wakati huo, ujana ulisababisha watu
wafurahie kuzunguka huko na huku nchi nzima, wakipata mikasa na kuitungia
nyimbo ambazo nyingine bado zinapendwa mpaka leo. Hakika sitaweza kukumbuka
sehemu zote ambazo binafsi nimewahi kupiga muziki, kwani pamoja na miji mikubwa
tulikuwa pia tunapiga katika vijiji ili mradi tupate pesa za kuendelea na
safari. Najaribu kupata picha vijana wa
zama hizi kukubali kusafiri kwa lori kwenye barabara zilizokuwa duni na za
vumbi. Nina uhakika madansi mengi yasingelia kwa supastaa kugom kupiga.
Dah! Ilikua shughuli kweli kweli. Kwa safari hizo ngumu za kimuziki ndio maana muziki wa enzi hizo utadumu daima. Nakumbuka leo asubuhi kabla sijasoma article hii nilikua najiimbia taratibu wimbo wa Dar Jazz uliokuwa unasema "ninawaachia wenzangu mie, wenye asili ya kupendwa...." mara tena nikakumbuka wimbo wa NUTA jazz enzi hizo baada ya chorus ulikua unaenda hivi "Mpenzi tafadhali njoo jioni tuyazungumze, nakusubiri kwa hamu kubwa sanaaa " nilipoona picha hii ya Vijana Jazz nikakumbuka wimbo "Matapeli" sasa hivi nikisikia Bongo fleva wanamuziki ambao muziki wao hauna kichwa wala miguu wananunua ndege huwa pumzi zinaruka.
ReplyDelete