YOUTUBE PLAYLIST

Tuesday, August 23, 2022

SEHEMU YA RIPOTI YA TAMASHA LA BENDI LA TANZANIA LIVE MUSIC FESTIVAL 2012



Baada ya matayarisho mbalimbali yaliyochukua miezi mitatu hatimae tarehe 28 September 2012, bendi ziliweza kuanza kupanda jukwaani kufanya maonyesho katika viwanja vya Leaders Club.  Bendi zilizopanda jukwaani karibu zote zilikuwa na makubaliano ya kulipwa na zililipwa fedha ya awali wiki 2 kabla ya onyesho na fedha iliyobaki ilikamilishwa siku ambapo bendi zilipanda jukwaani. Hakuna bendi yoyote iliyokuwa ikiwadai watayarishaji.

Watayarishaji walijipanga kwa kuhakikisha kuna jukwaa la Kimataifa lililopambwa na taa za rangi za kiwango cha juu, na vifaa vya muziki ambavyo vilihakikisha kila bendi inapopiga muziki, muziki wake ulisikika kwa kiwango cha hali ya juu. Hakukusikika mpaka leo malalamiko kuhusu upande huo wa matayarisho.


MC BEN KINYAIA

Tamasha lilianza tarehe 28 September 2012, saa kumi na mbili jioni,  kwa bendi kuanza kufanya maonyesho, bendi ya kwanza kupanda jukwaani ilikuwa ni Msondo Ngoma Music Band na kufuatiwa na bendi ya Fm Academia, na baadae bendi za Akudo Impact, Mashujaa Band, kundi la Taarab la Mashauzi Classic na baadae vijana wa Orynx Band. Bendi zote zilifanya vizuri sana, bendi zilipanda  kwa zamu kama ratiba ilivyokuwa imewaelekeza na mshereheshaji  alikuwa ni Ben Kinyaiya alifanya kazi kwa umakini wa hali ya juu .

 

Tamasha liliendelea siku ya pili  kama ratiba ilivyokuwa imepangwa kwa bendi za Mlimani Park, Skylight band, B Band, Oryx Band, Bi. Khadija Kopa  kupanda jukwaani, na kama ilivyokuwa jana yake wakiongozwa na mshereheshaji  Ben Kinyaiya.





MAFANIKIO

Mafanikio yaliyopatikana ni uzoefu mkubwa wa namna ya kutayarisha tamasha la muziki wa bendi. Mawasiliano yaliweza kufunguliwa kati ya watayarishaji na wanamuziki wa bendi mbalimbali. Kumekuweko na mafanikio ya kujua namna ya kupata vyombo na mafundi bora wa sauti, upambaji wa jukwaa na matayarisho yote ya awali ya kuwezesha tamasha kufanyika. Kumepatikana uzoefu wa kuitisha press conference na kufanya mikutano na wadau mbalimbali wa matamasha, serikalini, katika kampuni binafsi na watu binafsi.



WADAU TAMASHA.

Tamasha hili liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Edge Entertaiment na Chama Cha Muziki  wa Dansi Tanzania(CHAMUDATA) baada ya makubaliano, ambayo yalifikiwa kukiweko na malengo ya kupata fedha kwa ajili ya kusaidia miradi ya CHAMUDATA na kutoa mchango kwa BASATA. Kampuni ya Edge Entertaiment iliingia  mkataba na Times Fm Radio ambao uliwezesha  Times Fm kulitangaza Tamasha  pia kutoa gharama za matumizi yote ya maandalizi ya tamasha  kwa makubaliano ya fedha zitakazotumika kurudishwa kutokana na mapato ya tamasha.



KAMATI.

Kamati ya pamoja ya Edge Entertaiment  na Times Fm Radio iliundwa na ikapewa majukumu ya kuhakikisha  tamasha linafanikiwa, kamati ilifanya kazi chini ya uangalizi wa upande zote mbili zilizokubaliana na kamati  iliomba kampuni ya Edge Entertaiment iajiri mtu wa PR atakayehakikisha mpangilio  mzuri wa Tamasha na Edge Entertainment ilifanya hivyo.



VYOMBO VYA HABARI.

Katika kuhakikisha tamasha linafanikiwa kamati ilitumia vyombo vya habari vifuatavyo Magazeti, Tv, Blogs, Radio

Magazeti yaliyotumika;

  (a)Mwananchi

  (b)Jambo leo

  (c)Mtanzania

  (d) Magazeti ya Global Publishers

Tv zilizotumika;

 (a) TBC - Mahojiano

 (b) Chanel Ten- Mahojiano

Blogs zilizotumika;

(a) Michuzi

(b) Full shangwe

(c) Dar blog

(d) www.musiciansintanzania.blogspot

Radio;

Radio iliyotumika ni Times Fm Radio hii ilitokana na udhamini ambao redio hii ilikuwa imetoa

 


MATATIZO.

Kulikuweko na matatizo kadha wa kadha, mengine ni kutokana na maamuzi yaliyofanyika, mengine ni kutokana na wadau mbalimbali wa Tamasha, na machache ambayo yalikuwa njee ya uwezo wa  Kamati ya tamasha

* Tamasha lilifanyika siku ya Ijumaa na Jumamosi, huu ulikuwa uamuzi ambao ulionekana kuwa ni mzuri, lakini kwa mawazo ya wadau waliohudhuria wengi waliona ingekuwa bora tamasha lingeanza Jumamosi na hatimae kufikia kilele Jumapili kwa maonyesho ambayo yangeanza Jumapili kuanzia saa nne asubuhi hadi kati ya saa4 na saa 6 usiku siku hiyo

* Pamoja na bendi kulipwa si chini ya shilingi laki saba kila bendi bendi ziliendelea kupanga ratiba zao na hata kutangaza kuwa wako katika sehemu nyingine kwa siku na wakati uleule ambapo bendi zilitegemewa kuwa jukwaani katika tamasha. Msondo Ngoma walipiga wimbo mmoja tu kwa malipo ya shilingi milioni 1.

* CHAMUDATA  kilikuwa mdau muhimu katika tamasha hili, kwanza kwa kuwa sehemu ya mapato yalikuwa yaiingie katika mfuko wa chama hicho, na pili hili lilikuwa tamasha la muziki wa bendi, hivyo kuwa linafanya kile ambacho chama hiki kinasimamia, lakini hakukuweko hata afisa mmoja wa  CHAMUDATA katika kipindi chote cha tamasha, ambapo ingetegemewa chama kiwe chombo kimojawapo cha kupigia debe mafanikio ya tamasha hili.

* Kulikuweko na matatizo ya matangazo ambapo palikuweko na matukio ya kubandua mabango, na wakati fulani kuchanganya taarifa katika matangazo ya magazeti.

* Pamoja na kuwa eneo la Leaders lilikuwa limelipiwa, bado uongozi wa bar ya Leaders ulikaidi na kuendelea kukiuka masharti kwa kuendelea kufanya mauzo ya vinywaji kinyume na utaratibu na makubaliano na wadhamini wakuu wa tamasha. Hili limepelekea wadhamini kugoma kulipa baki ya ada ya udhamini ambayo ni shilingi 10,000,000.

* Mgeni rasmi aliwasili kwa muda aliopangiwa ambao ulikuwa ni saa moja, hili lilikuwa kosa kwani muda huo ndio ratiba inaanza na si muda mzuri kwa mgeni rasmi kuwa ndio anawasili, pia hakukuweko na protokali za kumpokea mgeni rasmi jambo ambalo lilitia doa ujio wake. Na hivyo alishindwa hata kufanya shughuli ya kufungua rasmi tamasha

 


HITIMISHO.

Kwa ujumla Tamasha lilikuwa na mengi sana mazuri kiutendaji, vyombo vizuri na vya kisasa, stage kubwa ya kisasa, na  liliweza kufanyika  kwa bendi zaidi ya kumi kushiriki. Ni wazi ni muhimu utamaduni huu wa kuwa natamasha kila mwaka kuendelea japo matayarisho yanatakiwa kuanza sasa.
Wanamuziki wa mabendi walikatisha tamaa kwani wamekuwa wakilalamikia kukosekana kwa Tamasha lao,  lakini ni wazi walithamini zaidi kazi zao za kawaid kuliko Tamasha lililokuja kukidhi kiu yao.
 Kwa upande wa mapato hayakuwa mazuri waandaji  waliingia hasara  kubwa na  hivyo kushindwa kutimiza malengo yake likiwemo la kukisaidia Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA). Waandaji wataendelea na elimu na mafunzo mbalimbali kwa wanamuziki wa muziki wa dansi wakishirikiana na BASATA na CHAMUDATA ili kuweza kuleta mafanikio katika muziki wa dansi Tanzania.

Katibu

 


Monday, August 22, 2022

KUWA MWANAMUZIKI ZAMANI HAIKUWA LELEMAMA

 

Vijana Jazz Band tukielekea Ifakara

Kuwa mwanamuziki katika miaka ya tisini na kurudi nyuma haikuwa lelemama, ilikuwa kazi ngumu, iliyokuwa yakujitolea haswa. Kati mambo magumu miaka hiyo ilikuwa kusafiri kwenda kufanya maonyesho. Katika zama hizi mwanamuziki anapata mualiko, anatajiwa na fungu atakalolipwa, anachagua aina ya hoteli ya kulala na hata usafiri kama ni wa ndege au gari la abiria  au hata gari binafsi, fursa hizo hazikuweko miaka hiyo.
Kwanza kabisa kulikuwa na taratibu za kiserikali, ili bendi au kikundi cha muziki kitoke katika mkoa ambako ni masikani taratibu zilikuwa ngumu. Kikundi kilianza kwa kuandika barua kwa Afisa Utamaduni wa mkoa kuomba ruksa ya kutoka nje ya mkoa. Afisa Utamaduni akisha kutoa kibali kile, muwakilishi wa bendi hutangulia kwenda kuwakilisha kibali kwa Afisa Utamaduni wa mkoa ambao kundi linaenda ili kupata kibali cha kufanya kazi katika mkoa husika, Afisa Utamaduni Mkoa akisha toa kibali kuingia mkoa wake, ndipo nakala ya kibali hupelekwa kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya ili nae atoe kibali cha kuruhusu kundi kufanya maonyesho katika wilaya yake. Kutokana na uchache wa magazeti, vikundi vingi vilianza safari bila matangazo yoyote, kwani kuna wilaya nyingine, magazeti hayakuwa yanafika kabisa au magazeti yalifika machache na hata hayo yaliweza kuchelewa hata siku nne.  Mwakilishi wa kikundi akishafika kwenye mji ambao bendi au kundi lingefanya maonyesho, alishirikiana na Afisa Utamaduni kupata kumbi na kufanya booking ya mahala pa kulala. Matangazo ilikuwa ni karatasi za kuandika kwa mkono na kisha kubandika katika kuta na nguzo mbalimbali. Baada ya hapo alitafutwa mwenyeji ambaye ni mtangazaji naye alipita katika mitaa mbalimbali akitangaza kupitia kipaza sauti cha mkononi. Nakumbuka mwaka mmoja mapema miaka ya 80, nikiwa na Orchestra Mambo Bado, tulifika Mpanda na kuelekezwa kuwa mtu maalumu ambaye hutangaza mambo yote pale, alikuwa bwana mmoja aliyepewa jina la utani la Mshindo Mkeyenge. Huyu alikuwa akipita mitaa mbalimbali na ngoma yake na hiyo hugonga  ili watu wamsikilize na ndipo hapo hutangaza kuwa kuna dansi linakuja na litakuwa wapi na kiingilio chake.

Usafiri wa bendi ulikuwa wa basi za abiria na mara nyingi malori ambamo wanamuziki walijazana humo wakiwa na vyombo vyao. Kati ya safari za aina hii nilizowahi kusafiri kwa roli ni toka Mbeya hadi Chunya na kurudi, kutoka Mtwara na kuzunguka miji ya kusini mingi kama Masasi , Nachingwea, Lindi kutumia lori la aina ya Isuzu Long base. Na nikiwa na bendi ya Tancut kwa ujumla usafiri wetu ulikuwa ni loti aina ya ‘canter’, humo tulizunguka miji kuanzia Makambako, Njombe, Songea, Mbeya, Tunduma na miji mingine mingi, tuliwahi pia kuzunguka miji mingi kanda ya ziwa kutumia  lori aina ya Leylan Albion. Huo ndio ulikuwa usafiri wa masupastaa wa mika hiyo.

 Malazi kwa kawaida hayakuwa ya kifahari, kwa kawaida vyumba vilivyokodishwa vilikuwa ni dabo ili kupunguza gharama, na gesti zenyewe zilikuwa ni zile ambazo gharama zake zikuwa chini. Kulala njaa halikuwa jambo la ajabu, hasa mkipiga dansi na kukosa wateja, hapo ndipo mnaweza kujikuta mmelala ukumbini ili pesa itoshe gharama za kuwasafirisha kwenda mji unaofuata. Miji mingi haikuwa na umeme hivyo bendi nyingine zilikuwa zikizunguka na jenereta, au kukodi kwa ajili ya kila onyesho.

Kama ilivyo katika biashara nyingine uongo nao ulikuwa mwingi sana, utasikia , ‘Bwana bendi ikienda Nyarugusu kule fedha nje nje, wachimba migodi wana pesa sana lazima mtarudi na pesa za kutosha kununua vyombo vipya’ . Hapo harakati za kwenda Nyarugusu zitaanza. Miaka hiyo Nyarugusu ilikuwa mji mmoja maarufu kwa wachimba dhahabu wadogowadogo, lakini sijawahi kuona bendi ikipata fedha za ajabu baada ya kwenda Nyarugusu. Kuna wakati  Bendi tatu tulikutana Mwanza kila moja ikiwa ina mpango wa kwenda Nyarugusu. Vijana Jazz Band,  Maquis  na Ngorongoro Heroes wote tukawa Mwanza. Hali ilikuwa mbaya sana kwa Maquis ambayo ilikuwa safarini huku  kwa zaidi ya miezi mitatu, ilifikia kiasi cha wanamuziki kuanza kurudi Dar es Salam mmoja mmoja.
Lakini ilikuwa ni baada ya safari hii walipojipanga upya na kurekodi vile vibao vyao vikali, Makumbele, Tipwa tipwa na Ngalula na kurudisha heshima yao mjini.

Kifupi hayo ndiyo yalikuwa maisha ya mwanamuziki wakati huo, ujana ulisababisha watu wafurahie kuzunguka huko na huku nchi nzima, wakipata mikasa na kuitungia nyimbo ambazo nyingine bado zinapendwa mpaka leo. Hakika sitaweza kukumbuka sehemu zote ambazo binafsi nimewahi kupiga muziki, kwani pamoja na miji mikubwa tulikuwa pia tunapiga katika vijiji ili mradi tupate pesa za kuendelea na safari.  Najaribu kupata picha vijana wa zama hizi kukubali kusafiri kwa lori kwenye barabara zilizokuwa duni na za vumbi. Nina uhakika madansi mengi yasingelia kwa supastaa kugom kupiga.

Sunday, August 21, 2022

KUJIBRAND SIO DHANA MPYA

 


Katika zama hizi ni kawaida kabisa kusikia wanamuziki wa kizazi kipya wakisema wanaji‘brand’. Kujibrand ni kujitengeneza kwa aina fulani ili uwe tofauti na watu wengine na huo kuwa utambulisho wako kibiashara. Katika mazungumzo ya wasanii wengi wa kiazi kipya, huwa wanaamini wao ndio wamegundua dhana ya kujibrand, niliwahi hata kumsikia msanii mmoja akisema tatizo la wana muziki wa dansi ni kuwa hawajibrand, kuna ukweli kiasi katika sentensi hiyo lakini msanii huyu alisema hivi kwa kudhani wasanii wa bendi hawajawahi kuelewa dhana ya kujibrand.

Kujibrand kumekuwa sehemu ya muziki wa dansi kwa muda mwingi wa historia ya muziki huo. Hebu turudi nyuma kuanzia miaka ya sitini. Bendi zilijitambulisha kwa majina mbalimbali, jina ni kipengele kimoja cha kujibrand. Kulikuwa na majina yaliyotokana na matukio mbalimbali ya kihistoria na bendi nyingine zilikuwa na majina yaliyotokana na masikani ya bendi na mara nyingine jina ambalo lilikuwa ni la ubunifu tu wasanii wahusika.

Baadhi ya bendi ambazo zilikuwa na majina kutokana na masikani ya bendi hizo ni  Morogoro Jazz, Tabora Jazz, Mbeya Jazz, Dodoma Jazz, Dar es Salaam Jazz Band, Super Matimila Orchestra, Mara Jazz na kadhalika. Butiama Jazz Band ilipata jina hilo kwa historia tofauti kidogo, bendi hiyo haikuwa na maskani Butiama, lakini ilijipatia hilo jina kama heshima kwa kijiji alikozaliwa Mwalimu  Nyerere,  ambaye ndie aliyewanunulia vyombo vyao vya muziki. Western Jazz Band ilijipa jina hilo kutokana na waanzilishi kuwa wanatoka jimbo la Magharibi la Tanganyika. Wakati wa ukoloni nchi iligawanywa katika majimbo yakiwemo Northern Province, southern Highlands Province, Western Province, Lake Province na majimbo mengine. Kilwa Jazz Band ilijibrand hivyo kutokana na muanzilishi wa bendi hiyo, Ahmed Kipande kutokea Kilwa.
 Kulikuwa na bendi zenye majina ya matukio kama Jamhuri Jazz, Ujamaa Jazz, Kilimo Jazz na kadhalika. Halafu kulikuweko na majina ya ubunifu kama Highland Stars, Mitonga Jazz, Kochoko Jazz, Makondeko Six, Cobash Brothers, jina lililotokana na muunganiko wa majina ya mwanamuziki waliokuwemo kwenye bendi hii, Orchestra Safari Sound, Kyauri Voice, Orchestra Toma Toma jina lililotokana na mwenye bendi aliyeitwa Timmy Thomas, kulikuweko na Super Rainbow, Rainbow Connection, Afro 70, Safari Trippers, Atomic Jazz Band, Super Volcano Orchestra, Orchestra Zela Zela,  Orchestra Super Veya, Zaire Success, orchestra Ban Africa Kituli na kadhalika.
Halafu kulikuweko na bendi ambazo zilijipa majina kutokana na kuwa chini ya kampuni au jumuiya ya kijamii. Kulikuweko na Vijana Jazz iliyokuwa chini ya Jumuiya ya Vijana wa CCM, Bima Lee iliyokuwa mali ya kampuni ya Taifa ya Bima, Tancut Almasi Orchestra iliyokuwa mali ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi cha Iringa, Mwenge Jazz mali ya brigedi ya Mwenge na kadhalika. Kule Kilombelo kulikuwa na  Sukari Jazz Band, iliyokuwa ni mali ya kiwanda cha sukari cha Kilombelo, UDA Jazz Band iliyokuwa mali ya kampuni ya mabasi ya usafiri Dar es Salaam, kulikuweko na BAT Jazz iliyokuwa mali ya kiwanda cha sigara cha BAT,  na kadhalika.  Majina haya hakika yalikuwa njia mojawapo ya kujibrand.
Bendi hizi zilianzisha mitindo yao ya kupiga na kucheza na kuipa majina kama njia nyingine ya kujibrand. Katika kumbukumbu hizi lazima tuanze na ‘brand’ kongwe kuliko zote nayo ni mtindo wa  Msondo uliyoanzishwa na NUTA Jazz Band kati ya mwaka 1964 na 1965 na mpaka leo bado uko hai na una nguvu. Kumepita mitindo mingine kama Sikinde, Ndekule, Bayankata, Kiweke, Sensera, Dondola, Afrosa, Koka Koka, Ambianse, Sululu, Saboso, Paselepa, Segere Matata, Vangavanga, Sokomoko, Fimbo Lugoda, King’ita Ngoma, Disco Agwaya, Super Mnayanyuo, Washawasha,  Super Bomboka na mitindo mingine mingi sana,  itachukua kurasa kadhaa kuitaja yote.   
Bendi pia zilikuwa na mavazi mbalimbali, mashati na suruali zishonwa kwa rangi mbalimbali na mitindo ya kupendeza ilyofanya  wanamuziki wapendeze wanapokuwa jukwaani, tena wakicheza kwa utaratibu maalum wa mtindo wao. Kati ya mafundi maarufu na wabunifu wa nguo hizo walikuwa ni mtuma salam maarufu Loboko Lobi Papaa na Mzee Kitenge ambaye kwa sasa yupo soko la Machinga Ilala.
 Kulikuwa na kujibrand kwa mtu mmoja mmoja ambapo wasanii walijipa majina mbali mbali ya kuvutia. Kulikuwa na majina kama Sauti ya Zege, Stereo Voice, Electronic voice, Computer, Golden Fingers, Dudumizi, King Michael na  King Kiki, akina mama hawakuwa nyuma kulikuwa na Stone Lady, Super Mama na wengineo. Kuna wanamuziki waliojikuta wanapata majina kutokana na nyimbo zao, Mzee Zacharia Daniel alijulikana zaidi kama Zacharia Tendawema kutokana na wimbo aliouimba akiwa Shinyanga Jazz Band ulioitwa Tenda Wema Uende zako, Mabrouk Khamis alijulikana zaidi kwa jina la Babu Njenje kutokana na wimbo aliokuwa akiuimba ulioitwa Njenje. Eddy Sheggy nae alianza kuitwa Chaurembo kutokana wimbo alioutunga uliokuwa na jina hilo.

Kwa mifano michache hii, kujibrand si dhana ngeni, bali kutokana na teknolojia imechukua sura mpya na pana zaidi.  Ikihusisha kusambaza picha mnato na video kwenye mitandao, siku hizi hata kutumia mikasa ya uongo kama vile kujitangaza kufa, au kujitangaza kukutwa na jambo la aibu kama kufumaniwa kunatajwa kama kujibrand, hata kuimba nyimbo zisizo kubalika na wengi ili tu zilete mtafaruku  inachukuliwa kama njia ya kuji brand.

Friday, August 19, 2022

KIINGILIO KINYWAJI NINI HATIMA?

 


Ni kawaida kabisa siku hizi kukuta bango likitangaza onyesho la kundi la muziki, na chini kukawa na maneno, kiingilio kinywaji au hata mara nyingine kiingilio bure.  Ni wazi wanamuziki magwiji marehemu kama wangeweza kurudi wangeshangaa na kuuliza hii inawezekana vipi?

Binafsi nimekulia katika utamaduni wa maonyesho kuwa na viingilio, tofauti ilikuwa ni kiwango cha viingilio, makundi maarufu yalikuwa na viingilio vikubwa na makundi machanga yalikuwa na viingilio vidogo. Wenye kumbi walikuwa wakizifuata bendi kubembeleza ziwe zinapiga katika kumbi zao na bendi zikawa na nguvu ya kutoa masharti, kwa mfano mwenye ukumbi angeambiwa atalipwa gharama ya umeme tu, fedha zote za kiingilio ni za bendi, au pengine kukubaliana kuwa baa itapata gawio la asilimia kumi ya mapato ya kiingilio baada ya kuondoa gharama, na makubaliano mengine ya namna hiyo. Hivyo bendi ziliuza muziki mlangoni na mwenye baa akawa anauza vinywaji na chakula chake. Kulikuwa hakuna muingiliano kiasi cha kwamba ilikuwa kawaida saa sita kasoro dakika chache usiku, kulikuwa kunatolewa tangazo kuwa, ‘Ikifika saa sita kaunta inafungwa’,  Hii ilitokana na sheria iliyohusu mauzo ya pombe, watu walinunua vinywaji vya ziada na saa sita biashara ya pombe ilifungwa biashara ya muziki iliendelea mpaka saa nane au tisa usiku.
Lakini kwa zama hizi ni jambo ambalo la kawaida kukuta kiongozi wa bendi anazunguka kutafuta ukumbi kwa kazi za ‘kiingilio bure’. Bendi inaahidiwa kiasi malipo, ambayo mara nyingi ni madogo sana, na kuanza kupiga muziki ili watu wapate burudani wakati wakinywa.
Utamaduni huu umeanza lini? Turudi nyuma miaka ya tisini mwishoni mwishoni. Kulikuwa na kampuni mbili kubwa za bia zilizokuwa na ushindani mkubwa. Kampuni moja ikabuni kitu kilichokuja kufahamika kama ‘promosheni’. Kampuni hii ikaanza kukusanya wasanii wa Sanaa za maigizo na kuwazungusha kwenye kumbi mbalimbali kunapouzwa pombe, huko wasanii walifanya maonyesho na kisha kulipwa na kampuni. Haukupita muda mrefu bendi ndogondogo zikaanza kugombea kujiunga katika katika biashara hiyo, na kwa kweli kulikuwa na bendi ambazo zingetangaza kuwa zinafanya maonyesho hakika hazingepata kiwango ambacho kilikuwa kikitolewa na kampuni ile ya bia, hivyo ilikuwa ni jambo la faida kwa bendi hizi. Pia wakati huohuo kukaanzisha kitu kilichopewa jina la bonanza, hasa ziku za mwisho wa wiki, huko nako bendi na wasanii wa Sanaa za maonyesho hasa wasanii wachekeshaji wakapata kazi na kulipwa  wakati wapenzi wa Sanaa wakifaidi bila kulipa. Miaka ikaenda bendi  za kupiga kwa kiingilio taratibu zikaanza kupungua. Wakati utaratibu huu unakolea, kukatokea tatizo moja kubwa, moja ya hizo kampuni za mbili za bia, ikapotea kwenye soko. Ushindani wa makampuni ukawa haupo, kwa hiyo umuhimu wa ‘promosheni’ ukapungua, kazi zikafifia, wasanii wengi wakapotea moja kwa moja, ikiwemo bendi kadhaa ambazo zilijua ingekuwa vigumu kuanza kutangaza kuwa sasa zimeanza kupiga kwa kiingilio, baya zaidi kukawa kumetengenezwa jamii ambayo imelelewa kutokulipia maonyesho ya Sanaa. Wasanii walikuwa wameshiriki wenyewe  kutengeneza wateja wa ‘maonyesho ya bure’.
Lakini pia kukawa kumezaliwa utamaduni wa wanywaji kuzoea kinywaji na maonyesho ya Sanaa, hili likwafanya wenye kumbi kulazimika kuanza kubeba jukumu la kutafuta wasanii wa kufanya maonyesho kwenye kumbi zao. Lakini uwezo wa wenye kumbi kulipia ‘promosheni’ ukawa mdogo, hivyo basi bendi zimekuwa zikipiga kwa ujira mdogo sana.
Malipo madogo yanafanya ishindikane kuendesha bendi kwa misingi inayotakiwa. Bendi zinashindwa kununua vyombo vizuri, zinashindwa kufanya mazoezi, au hata kurekodi nyimbo mpya. Na baya zaidi mtizamo wa wanamuziki katika utunzi unakuwa mfinyu sana, tungo zinalenga kufurahisha wanywaji tu, hivyo kiwango cha utunzi nacho kinashuka sana. Na si ajabu ukisikia siku hizi kuwa kiwango cha muziki wa bendi kimeshuka, mfumo wa muziki unafanya aina ya utunzi ufanye bendi zionekane zimeshuka kiwango.

Kuna haja ya wanamuziki hasa wa dansi kukaa na kutafakari namna ya kuondoka kwenye hili shimo ambalo ni baya sana. Bendi ikiwa inaamka na kulala kwa kujipanga kwenda kupigia wanywaji tuu, haitakuwa na mawazo ya kushindana katika ulimwengu wa muziki, ni wazi mtu mwenye safari ya kutoka mtaa mmoja hadi mwingine kamwe hawezi kuhangaika kutafuta passport kwani haimuhusu.  Bendi nyingi sasa hazina hata tungo zake binafsi, bendi zinategemea kurudia tungo za wanamuziki wengine. Karibuni tumeanza kusikia viongozi wa vikundi wakilalamika kuwa kuna vikundi vipya vinaundwa vikitegemea nyimbo za kuiga tu kwenye maonyesho yao, hiyo ni changamoto kubwa kwenye muziki wa ‘live’. Pia muda umefika kwa wenye kumbi kuelewa kuwa kama watahitaji muziki bora utakaoleta wateja wengi kwenye kumbi zao ni vizuri wachangie katika swala la kulipa vizuri zaidi. 

Japo swali la wahenga litakuja. Nini kilianza kuku au yai? Malipo mazuri au muziki mzuri?

Saturday, August 13, 2022

NGOMA AFRICA BAND KUTIKISA KWENYE TAMASHA LA KIMATAIFA LA AFRIKA EXPO, TUBINGEN,GERMANY 2022


BENDI  maarufu ya  Ngoma Africa band itashiriki katika burudani za kukata na shoka zitakazotumbuiza wahudhuriaji wa tamasha  la  15 la International African EXPO  Festival  litakalofanyikaTübingen, Ujerumani. Tamasha litakuwa kati ya tarehe 01September - 04th September 2022  Fest Platz,  Tübingen, Ujerumani.
Ngoma africa band watakuwa jukwaani Jumamosi 03 September 2022
Ngoma Africa, ni bendi yenye makao yake Ujerumani na ilianzishwa mwaka  1993 na kiongozi wa bendi hiyo Ebrahim Makunja anaejulikana pia kama Kamanda Ras Makunja. Bendi hii ina wanamuziki wakali kama soloist Christian Bakotessa aka Chris-B, wengine ni Jo Souza, Matondo Benda, Aj Nbongo, Flora William, Jessicha Ouyah, Vially Nbongo, na wengio. Bendi hii ina mamilioni ya wapenzi na inajulikana kwa kupagawisha kwa midundo yake yenye uasili wa Afrika ya Mashariki.

Ngoma Africa imeshaachia CD kadhaa ikiwemo CD yake mpya inayoitwa “BONGO TAMBARARE” , nyimbo mbili hizi  "Mapenzi ya Pesa" na "Supu Ya Mawe" unaweza kuzisikiliza ukiingia hapa www.reverbnation.com/ngomaafricaband

RIPOTI YA KAMATI TEULE YA KURATIBU MJADALA WA NAMNA BORA YA KUSIMAMIA HAKIMILIKI NCHINI TANZANIA AGOSTI, 2022

 




RIPOTI YA KAMATI TEULE YA KURATIBU MJADALA WA NAMNA BORA YA KUSIMAMIA HAKIMILIKI NCHINI TANZANIA

AGOSTI, 2022

 

 

1.0 Utangulizi

Hakimiliki na Hakishiriki ni maeneo muhimu zaidi popote ubunifu unapotajwa. Hakimiliki na Hakishiriki ni muhimu kwa kuwa ni msingi wa kuhakikisha kwamba wabunifu (wa kazi sanaa na maandishi) wananufaika na matumizi ya kazi zao. Sheria imeweka wazi kwamba ni wabunifu pekee ndio wenye uwezo wa kuruhusu matumizi ya kazi zao katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, kwa kuwa kuna baadhi ya haki ambazo wabunifu hawawezi kuzisimamia wenyewe, serikali nyingi duniani zimekuwa zikianzisha taasisi mbalimbali kusimamia haki hizo. Kwa upande wa Tanzania, kwa muda mrefu wajibu huu umekuwa ukifanywa na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA). Mnamo mwezi Julai, 2022 Serikali ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ambapo mbali na mambo mengine imeifanya COSOTA kuwa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania na kuruhusu uanzishwaji wa makampuni au taasisi binafsi (CMOs) zitakazokusanya na kugawa mirabaha kwa niaba ya wabunifu. Kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, CMOs zinatakiwa kuwa taasisi zilizoidhinishwa kisheria chini ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, kufanya shughuli za usimamizi wa Hakimiliki bila kuwa katika misingi ya kutengeneza faida. Usimamizi wa taasisi hizi unatazamiwa kuwanufaisha moja kwa moja na kwa njia rahisi waandishi, wabunifu na wamiliki wengine halali wa kazi za Sanaa.

 

Kwa kuzingatia usuli huo na kwa kuzingatia umuhimu wa usimamizi bora wa Hakimiliki na Hakishiriki nchini Tanzania, mnamo tarehe 01.07.2022 Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa aliteua kamati maalumu ya wajumbe 11 kwa lengo la kuratibu namna bora ya usimamizi wa hakimiliki nchini Tanzania. Wajumbe hao ni hawa wafuatao:

1.    Bw. Victor Michael Tesha Mwenyekiti

2.    Dkt. Saudin Mwakaje – Makamu Mwenyekiti

3.    Bw. Dimesh S Mawj Katibu

4.    Mhe. Hamis Mwinjuma Mjumbe


5.    Dkt. Omary Mohamed – Mjumbe

6.    Bw. Paul Mattysse Mjumbe

7.    Bi. Safina Kimbokota Mjumbe

8.    Bw. Torriano Salamba Mjumbe

9.    Bw. Gabriel Kitua Mjumbe

10. Bw. Twiza Mbarouk – Mjumbe

11. Dkt. Asha S Mshana Mjumbe

 

 

Wajumbe wa kamati hii wana taaluma na uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwamo wataalamu wa masuala ya fedha, wanasheria na wabunifu wa kada ya Sanaa na Maandishi.

 

2.0 Hadidu za rejea

Kamati ilipewa hadidu za rejea zifuatazo:

1.    Kupendekeza mifumo bora zaidi ya kukusanya na kugawa mirabaha inayoshabihiana na mifumo mingine duniani.

2.    Kupendekeza njia bora zaidi ya kupambana na uharamia wa kazi za sanaa nchini.

3.    Kupendekeza mfumo bora zaidi wa uendeshaji wa Taasisi ya Hakimiliki Tanzania.

4.    Kuratibu kikao cha wadau wa Hakimiliki cha kujadili mapendekezo ya kamati na

5.    Kuwasilisha taarifa ya kamati kwa Mhe. Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

 

3.0    Methodolojia

Ili kufanya kazi kwa mujibu wa hadidu rejea, methodolojia iliyotumika katika kupata taarifa ni upitiaji wa nyaraka mbalimbali zinazohusu hakimiliki, mahojiano, hojaji na mikutano ya ana kwa ana ambayo ilishirikisha wadau mbalimbali muhimu katika kupata taarifa kwa lengo la kukamilisha jukumu la Kamati. Mikutano hii ilifanyika katika kanda sita kama ifuatavyo:

Mosi, kanda ya Kaskazini- Mkutano ulifanyika Mkoani Arusha katika Hoteli ya Golden Rose, na kuhudhuriwa na wabunifu pamoja na wadau 216.


Mkutano huu pia ulihudhuriwa na Mhe. Pauline Gekul Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

 

Pili, kanda ya Kati – Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Dear Mama, mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wabunifu pamoja na wadau 126.

Tatu, kanda ya Ziwa – Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya jijini Mwanza na kuhudhuriwa na wabunifu 87.

 

Nne, kanda ya Nyanda za Juu Kusini- Mkutano uliafanyika katika ukumbi wa BEACO jijini Mbeya na kuhudhuriwa na wabunifu 138

 

Tano, Kanda ya kusini- mkutano huu ulifanyika mkoa wa Mtwara katika ukumbi wa Halmashauri na ulihudhuriwa na wadau 181.

 

Sita, kanda ya Mashariki, ambapo mkutano wa wabunifu na wadau wa sekta ya ubunifu 171 ulifanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wote wa kamati wakiongozwa na Mwenyekiti. Ripoti za mikutano ya ukusanyaji maoni zimeambatishwa kama viambatisho Na. 4.2.

 

Wadau wa jinsi zote, wakiwamo wenye mahitaji maalumu walishiriki. Kwa wastani 22% ya wasanii na wadau waliohudhuria walikuwa wa jinsi ya kike na 78% walikuwa wa jinsi ya kiume. Tasnia ya Sanaa ya Maonesho na Sanaa ya Ufundi zilikuwa na uwiano mzuri zaidi wa uwakilishi kati ya jinsi ya kike na ile ya kiume. Katika watoa maoni, uwiano wa wasanii wa kike ulikuwa mdogo zaidi kwa wasanii wa muziki.

 

Aidha, kamati hii iliangalia uzoefu wa nchi nyingine kwenye usimamizi wa Hakimiliki na kuchambua takwimu za wabunifu na wadau. Nchi zilizoangaliwa kwa ajili ya uzoefu ni pamoja na Nigeria, Algeria, Afrika Kusini na Kenya.

 

4.0    Mapitio ya Mabadiliko ya Mfumo wa Sheria

Katika kujenga usuli mzuri wa mapendekezo ya Kamati kwa mujibu wa hadidu za rejea katika ripoti hii, na kwa lengo la kujenga welewa wa pamoja, kumetolewa usuli wa mabadiliko ya mfumo wa sheria wa hakimiliki nchini Tanzania. Mabadiliko yaliyojadiliwa katika ripoti hii ni:

 

Mosi, mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ya mwaka 1999 ambayo yalifanywa kwa lengo la kuziba baadhi ya mianya ya kiusimamizi iliyoonekana kuwapo kwa wakati huo. Sheria hii ilibadilisha maeneo manne ambayo


ni kifungu cha 4, Kifungu cha 9, kifungu cha 15 na kifungu cha 42. Vifungu hivi vilifanyiwa uboreshaji ili kuendana na hali ya sasa kuhusiana na masuala ya Hakimiliki na Hakishiriki.

 

Pili ni mabadiliko ya sheria ya Machi, 2022 kufuatia mabadiliko ya sheria Na.1 ya mwaka 2022, ambapo kifungu cha 3 kilibadilishwa kuongezewa tafsiri na kifungu cha 12 kilibadilishwa na kuongezewa vifungu vya 12A na 12B ili kuwezesha utekelezaji wa mkataba huo. Baadhi ya marekebisho hayo ni:

a)      Kuweka utaratibu unaoruhusu kunakili machapisho na kuyageuza katika muundo (format) ya maandishi kwa ajili ya watu wasiiona au wenye matatizo ya kusoma maandishi ya kawaida bila kupata idhini ya mwenye chapisho.

b)      Kuweka utaratibu wa kuruhusu taasisi husika kuweza kurudufu machapisho na kuwayaweka katika mfumo wa kuweza kusomwa na watu wenye matatizo ya kuona na taasisi hizo kuruhusiwa kusambaza kwa wahusika kwa kutoza gharama za uchapishaji na si kwa ajili ya kupata faida.

 

Tatu, ni mabadiliko yaliyofanywa na Sheria ya Fedha ya Mwezi Julai, 2022 ambayo mbali na mambo mengine yamelenga katika kuanzisha mfumo mpya wa usimamizi wa hakimiliki hapa Tanzania kwa kuruhusu uanzishwaji wa makampuni binafsi ya ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha nchini Tanzania. Pia mabadiliko haya yameanzisha tozo mpya kwa vibebeo vya kazi za ubunifu vinavyotumika katika kudurufu, kusambaza, kuhifadhia na kuzalisha kazi hizo. Aidha, mabadiliko yamefanyika katika kifungu cha 4 kwa kuongeza tafsiri pamoja na kufuta neno chama na kuweka neno ofisi. Pia vifungu vya 46, 47 na 48 vimerekebishwa ambapo baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakifanywa na COSOTA yameondolewa ili kuruhusu uanzishwaji wa kampuni hizo na uazishwaji wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania.

 

5.  Matokeo ya Utafiti

Baada ya majadiliano na wadau na kwa kuzingatia hojaji zilizotolewa mapendekezo yafuatayo yalizingatiwa:


5.1     Elimu kwa umma

Wadau wote waliohudhuria katika mikutano ya kukusanya maoni walijibu maswali kuhusu elimu ya hakimiliki, usimamizi wa maslahi ya wasanii na uharamia wa kazi za sanaa. Wadau wengi walionesha uhitaji wa elimu zaidi kwa umma kuhusu hakimiliki na masuala kadhaa yanayoambatana na hakimiliki. Aidha, washiriki wengi walionesha kuelewa zaidi kuhusu Taasisi ya Hakimiliki nchini kuliko mambo muhimu kama umiliki wa hakimiliki za sanaa; anayestahili malipo kutokana na kazi za sanaa na kuhusu uharamia wa kazi za sanaa.

 

Vilevile, ufahamu wa washiriki kuhusu uharamia wa kazi za wasanii ulikuwa mdogo zaidi ukifuatiwa na uelewa kuhusu umiliki wa hakimiliki na stahiki za mapato yatokanayo na hakimiliki

 

5.2    Umuhimu wa kuwa na Chombo kimpya cha kusimamia masuala ya hakimiliki nchini

Maeneo mengine yaliyotolewa maoni ni iwapo kuna mahitaji ya chombo kipya cha kusimamia mashauri ya hakimiliki nchini.

 

Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba tasnia ya Sanaa ya Ufundi ikifuatiwa na tasnia ya Muziki na Filamu zilipendekeza kwa asilimia zaidi ya 50% kuwe na chombo kipya wakati tasnia hizo za Sanaa uelewa wao kuhusu hakimiliki ya kazi za sanaa zao ulikuwa chini ya asilimia 50%. Wakati huohuo tasnia hizo tatu uelewa wao kuhusu Ofisi ya Hakimiliki ulikuwa 63%, 77% na 72% kwa Sanaa ya Ufundi, Sanaa ya Muziki na Sanaa ya filamu katika mpangilio huo.

 

Matokeo ya Utafiti huu yanaonesha umuhimu wa Kamati kuzingatia mambo mawili: Mosi, kupendekeza mkakati na mfumo utakaowezesha uwekezaji na jitihada za dhati kuhusu elimu kwa wasanii wa tasnia zote na umma kuhusu mambo ya hakimiliki na uharamia wa kazi za sanaa.

 

Pili, kupendekeza kanuni na taratibu ambazo zimeakisi kanuni bora zaidi kutoka nchi zenye mazingira sawa na Tanzania.


6.0    Mapendekezo ya Kamati

Kutokana na mabadilko ya Sheria ya mwezi Julai 2022 ambayo yameanzisha utaratbu mpya wa usimamizi wa hakimiliki ambapo kazi za usimamizi wa hakimiliki na ukusanyaji wa mirabaha zitafanywa na CMOs, na pia kwa kuzingatia maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na wadau, Kamati inapendekeza masuala ya kisera na kisheria katika maeneo manne: (1) mfumo bora wa kukusanya na kugawa mirabaha, (2) njia bora ya kupambana na uharamia, (3) mfumo bora wa uendeshaji wa taasisi ya hakimiliki, na (4) mapendekezo mengine ya jumla.

 

6.1    Mfumo Bora wa Kukusanya na Kugawa Mirabaha

Katika sehemu hii kuna mambo mawili ya msingi ambayo ni kanuni za usimamizi wa ukusanyaji wa mirabaha na ushirikiano na Taasisi mbalimbali za serikali

6.1.1        Kanuni za Usimamizi wa Ukusanyaji Mirabaha

Ili kutekeleza mfumo mpya wa usimamizi wa hakimiliki hapa Tanzania, Kamati inapendelkeza kanuni zitungwe kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

i.        Kabla ya kufanyiwa usajili au kupewa leseni ya kukusanya mirahaba, CMOs zifanyiwe tathmini ya uwezo wao wa kiutawala, wawasilishe mpango wa biashara wakibainisha mbinu watakazotumia kutambua wasanii wa eneo hilo na namna ukusanyaji wa mirabaha utakavyofanyika, ziwe na mfumo unaokubalika wa kihasibu, waajiri watalaamu wenye sifa, katika bodi ya wakurugenzi kuwa na wawakilishi wa tasnia husika ya sanaa (wamiliki).

ii.        Kwa kuanzia, makampuni yatakayopewa dhamana ya kukusanya mirabaha yapewe aina moja ya sanaa kwa kazi zote. Utaratibu huu utazifanya kampuni hizi zitakazopewa leseni ya kukusanya mirabaha kufanya kazi kwa ufanisi kwa kulenga aina moja tu ya kazi.

iii.        Kila mwaka utendaji wa kampuni hizi ufanyiwe tathmini ili kujua kama zina ufanisi au la. Vigezo viwekwe vitakavyoongoza Ofisi ya Hakimiliki kuamua kuhuisha au kutohuisha leseni ya kampuni. Kiwekwe kiwango cha alama za chini cha utendaji katika ukusanyaji mapato.

iv.        Kila mwaka wa fedha unapoanza, kampuni hizi ziwasilishe makadirio ya makusanyo kwa mwaka ambayo yatafanyiwa tathimini na kuidhinishwa na Ofisi ya Hakimiliki. Endapo kampuni itakusanya chini ya asilimia 50 ya makadirio bila kutoa sababu za msingi, Kanuni zitoe mamlaka kwa Ofisi ya


Hakimili kukataa maombi ya kuhuisha leseni ya kukusanya mirabaha kwa kampuni husika.

v.        CMOs iweke mfumo wa kielektroniki ambao utaruhusu taarifa za muda mfupi za makusanyo ya mirahaba kuonwa na Ofisi ya Hakimiliki na wamiliki wa haki.

vi.        Kwa kuwa kampuni za ukusanyaji zitakuwa zikikusanya na kubaki na fedha za wamiliki, ni vyema kanuni zikaweka ukomo wa matumizi ya uendeshaji ili kulinda maslahi ya wamiliki.

vii.        Katika maombi ya leseni (mpya au kuhuisha), kanuni ziweke sharti kwa kampuni za ukusanyaji wa mirabaha kuwasilisha dhamana ya fedha kutoka benki kwa kiwango kisichopungua asilimia 50 ya matarajio ya makusanyo katika mwaka unaofuata.

viii.        Katika kipindi cha mpito kabla ya Kanuni za utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria kutungwa, Ofisi ya Hakilimili Tanzania iendekee kutambulika kama ina majukumu ya kukusanya mirabaha na kuendelea kukusanya mirabaha mpaka hapo makampuni yatakayopewa leseni ya kukusanya yatakapoanza kazi kikamili na kujisajili katika mashirika ya kimataifa ya ukusanyaji wa mirabaha.

 

6.1.2        Ushirikiano wa Taasisi Mbalimbali za Serikali

Masuala yanayohusu usimamizi wa hakimiliki ni mtambuka na yanahusisha taasisi nyingi za serikali na nyakati fulani zenye maslahi pingani. Hivyo Kamati inapendekeza yafuatayo:

i.        Kuundwa kisheria kwa Kamati ya Kiuratibu ya Wizarani kwa ajili ya usimamizi wa masuala ya hakimiliki ikihusisha Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, BASATA, Bodi ya Filamu, TRA,TCRA, BRELA,TCU, na TAMISEMI. Taasisi hizi zinasimamia wazalishaji na watumiaji wa kazi za sanaa. Ni vyema kukawa na wajibu wa kisheria kwa taasisi hizi kushirikiana ili kuwa na mkakati wa pamoja katika kushughulikia uharamia wa kazi za wasanii na ukusanywaji wa mirabaha.

ii.        Katika utoaji wa leseni za biashara kwa taasisi zinazotumia kazi za sanaa, kwa mfano redio, televisheni, baa na shule kuwepo na matakwa ya mwombaji kuwasilisha cheti cha utambuzi kutoka Ofisi ya Hakimiliki ya Tanzania. Hii itasaidia kuwabana wahusika kama hawatoi ushirikiano katika kuwasilisha malipo ya mirabaha kutokana na matumizi ya kazi za sanaa.


6.1.3    Njia Bora ya Kupambana na Uharamia wa kazi za sanaa

Katika sehemu hii, Kamati inapendekeza mambo mawili ya msingi ambapo kila moja limefafanuliwa katika vipengele vidogovidogo kadhaa: Mambo hayo ni kuongeza adhabu kwa makosa ya uharamia wa kazi za hakimiliki pamoja na kusajili mikataba ya wasanii. Ufafanuzi wa mapendekezo haya ni kama unavyoonekana hapa chini:

a)        Kuongeza Adhabu kwa Makosa ya Uharamia wa kazi za sanaa

Mojawapo ya njia ya kuboresha usimamizi wa hakimiliki ni kufanyia marekebisho kwa adhabu zinazotolewa. Kwa mfumo wa sasa wa adhabu, ambao unatoa adhabu ya faini au kifungo cha jela bila kuzingatia uzito wa kosa. Hapa Kamati inatoa mapendekezo yafuatayo:

i.        Adhabu zitolewe kwa kuzingatia uzito wa kosa,

ii.        Mahakama au Ofisi ya Hakimiliki iwekewe kiwango cha chini cha faini au kifungo, lakini iachiwe uhuru wa kuamua kiwango cha juu cha adhabu kwa kuzingatia muktadha na uzito wa kosa lililofanyika;

iii.        Adhabu ihusishe kufutiwa leseni ya biashara endapo itathibitika kuwa mkosaji alifanya kosa hilo kwa kukusudia;

iv.        Adhabu ihusishe kutaifishwa na kuharibiwa kwa vifaa vinavyotumika katika kufanya uharamia

v.        Adhabu ziwaguse waliofanya makosa na waliowasaidia kutekeleza uharamia. Kutanua wigo wa wahusika kutasaidia katika kuimarisha usimamizi na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa hakimiliki nchini.

 

b)        Kusajili Mikataba ya Wasanii

Mojawapo ya malalamiko makubwa na yanayojirudia ni kuwa wasanii wengi wanahisi wanaonewa kimaslahi katika kazi wanazofanya chini wa mwavuli wa makampuni au wasanii wakubwa. Ili kushughulikia suala hilo, tunapendekeza:

i.        Katika kanuni zitakazotungwa, kiongezwe kipengele ambacho kitatoa motisha kwa makampuni na wasanii wakubwa kusajili mikataba yao katika Ofisi ya Hakimiliki. Vivutio hivi vinaweza kujumuisha kuruhusu nafuu za kikodi kwa makampuni yatakayosajili mikataba ya wasanii. Kanuni ziweke wajibu kuwa mikataba ya wasanii wanaochipukia isajiliwe katika Ofisi ya Hakimiliki.


ii.        Pia, sheria itoe mamlaka kwa Ofisi ya Hakimiliki kupitia vifungu vya mikataba inayosajiliwa na endapo itajiridhisha kuwa kuna vifungu kandamizi Ofisi iwe na mamlaka ya kushauri mamlaka husika kufanya marekebisho.

 

6.1.4    Mapendekezo Kuhusu Mfumo wa Kisheria

Katika sehemu hii Kamati inatoa mapendekezo katika maeneo saba kama ifuatavyo:

 

 

a)      Marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya 1999

Kwa kuzingatia maendeleo ya kiteknolojia ambayo yamebadili mfumo mzima wa jinsi kazi za sanaa zinarudufiwa na maharamia, tunapendekeza:

i.        Orodha ya vifaa vitakavyotozwa kodi (blanket levy) katika mabadiliko ya sheria ya hakimiliki ya mwezi Julai 2022 iboreshwe kwa kuongezea vifaa ambavyo kwa teknolojia ya sasa vinatumika katika kuridifu na kuhifadhi kazi za sanaa. Vifaa vilivyo katika orodha ya sasa ni vya zamani na havitumiki sana.

ii.        Wigo wa mfumo au njia za utambuzi wa matukio ya uharamia na ulinzi wa kazi za sanaa uboreshwe kwa kuzingatia na kutumia mifumo ya kiteknolojia iliyopo sasa. Hii itaendana na hatua ambazo mashirika ya kimataifa kama vile WIPO yamechukua kwa kupitisha na kutumia Mkataba maalumu wa kimataifa wa hakimiliki ambao umejikita zaidi katika masuala ya kiteknolojia (WIPO Copyight Treaty of 1996)

 

b)     Kuanzisha Mfumo wa Mahakama Tembezi

Ili kushughulikia tatizo linaloongezeka la uharamia wa kazi za wasanii, ni vyema mfumo wa utoaji haki uboreshwe ili uweze kushughulikia makosa yanayojitokeza kulingana na uhalisia na mazingira ya utendaji wa makosa ya kiuharamia. Katika mazingira ya Tanzania ambapo makosa ya kiuharamia hufanyika kwa kiwango kikubwa na kidogo ikihusisha sehemu ambazo ni rahisi kuharibu ushahidi endapo ukamataji utachelewa, inapendekezwa kuanzishwa kwa mahakama zinazotembea ambazo zitakuwa na mamlaka ya kutoa maamuzi papohapo endapo ushahidi utakuwa umejitosheleza.

 

c)      Kuongeza Mamlaka ya Kiusimamizi kwa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania

Ili kuboresha usimamizi wa masuala ya hakimiliki hapa Tanzania, inashauriwa kuwa Ofisi ya Hakimiliki ipewe mamlaka ya kisheria ili kushughulikia utatuzi wa migogoro


na makosa ya uharamia na kutoa adhabu kwa wahusika watakopatikana na hatia. Mamlaka hiyo inapaswa kutumia nguvu ya kisheria kuagiza vifaa vinanvotumika kufanya kazi za uharamia kukamatwa mara tu vinapogundulika mahali vilipo, watuhumiwa wa uharamia kukamatwa, kutoa amri ya kuviharibu vifaa vitakavyothibitika ni zao la uharamia au vinatumika kufanya uharamia. Kwa kuchukua hatua hii, itawezesha Ofisi ya Usimamizi wa Hakimiliki kuwa na nguvu ya kisheria ya kutoa maamuzi ya haraka na yenye nguvu za kisheria. Pia, hatua hii itapunguza kwa kiwango kikubwa ucheleweshaji wa kesi za uharamia wa kazi za sanaa na kupunguza gharama za kuendesha kesi kwa walalamikaji.

 

d)                 Ofisi ya Hakimiliki Iongeze Wigo wa kazi Inazosimamia

Kwa ujumla, katika utendaji wake, COSOTA imekuwa ikijikita zaidi katika kazi za Sanaa ya muziki. Wakati umefika sasa wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania kujipambanua na kuweka mkakati wa kutumia rasilimali na nguvu ileile katika kusimamia kazi zote za sanaa. Inapendekezwaza kuwa Ofisi ya Hakimiliki kuzigawa aina mbalimbali za sanaa na kuanzisha vitengo vya ndani vitakavyosimamia maeneo hayo ya sanaa. Maeneo haya yanaweza kujumuisha tasnia nne za sanaa ambazo ni

(1) Sanaa za ufundi (2) Sanaa za maonesho (3) sanaa za muziki na (4) Sanaa za filamu. Ili kutilia mkazo, tunapendekeza maeneo hayo yabainishwe na kutengewa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji katika mpango mkakati wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Hatua hii itaongeza tija katika tansinia ya sanaa na kuongeza wigo wa mapato kwa serikali na wasanii.

 

e)                  Kutungwa Sera ya Taifa ya Miliki Dhihini (National Intellectual Property Policy)

Ili kuyashughulikia masuala ya hakimiliki kwa upana wake, maeneo mengine ya miliki ya ubunifu na taasisi nyingine zinazoshughulikia miliki ya ubunifu kama vile BRELA, FCC, BASATA, COSTECH zinahusika. Hivyo, tunapendekeza kuwa mchakato unaondelea wa kutunga na kupitisha sera ya kitaifa ya miliki ya ubunifu uharakishwe ili Tanzania iwe na sera inayotoa dira ya jumla ya jinsi masuala haya yanavyopaswa kushughulikiwa.


f)                   Elimu ya Hakimiliki

Kutokana na umuhimu wa tasnia yab sanaa na masuala yote ya ubunifu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kiutamaduni na sayansi hapa Tanzania, tunapendekeza mitaaala ya elimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi ijumuishe moduli zinazofundisha masuala ya miliki za ubunifu na umuhimu wa kuheshimu na kuzilinda haki za wabunifu kupitia sheria zilizopo. Mbali na mitaala ya shuleni, Wizara ianzishe mpango kabambe wa kuandaa vipindi vya kuelimisha jamii kupitia television, radio, mitandao ya kijamii na njia nyinginezo zitakazosaidia kufikisha elimu kwa walengwa na wadau mbalimbali.

 

g)                 Kuridhia Mikataba ya Kimataifa Inayohusu Hakimiliki

Ili kuboresha usimamizi wa hakimiliki ni muhimu kwa Tanzania kuanzisha mchakato wa kuridhia mikataba ya kimataifa inayohusu hakimiliki na kuimarisha zaidi ushirikiano na mashirika ya kimataifa na kikanda. Miongoni mwa mashirika hayo ni:

i.        Shirika la Kimataifa la Miliki ya Ubunifu (World Intellectual Property Organization (WIPO))

ii.        Shirika la Biashara la Kimataifa (World Trade Organization (WTO)

iii.        Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (United Nation Educational Scientific and Cultural Organization (UNESCO)

iv.        Shirika la Kikanda la Miliki ya Ubunifu Africa (ARIPO)

 

 

6.1.5        Muundo wa kiuongozi unaopendekezwa kwa ajili ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania

Kwa kuwa ofisi hii imepunguziwa kazi ya kuandikisha wanachama, kukusanya na kugawa mirahaba, idadi wa wafanyakazi inapaswa kuanza kwa kiwango kinacholingana na uhalisia wa shughuli lengwa na pia ili kuwezesha wafanyakazi watakaokuwapo a) kuwa na kazi ya kutosha na b) kulipwa stahiki zao ipasavyo na kuwezesha mchango wa rasilimali fedha kwa CMOs mpya. Inapendekezwa kuhakikisha wanaajiriwa wafanyakazi wenye weledi, mahiri na wanaostahili.

 

6.1.6         Mchanganuo wa kina wa idadi ya wafanyakazi kwa kila idara

Bodi ya Wakurugenzi inapaswa kuandaa mpango mkakati, kwa kuanzia wa miaka mitatu kisha wa miaka mitano mitano ili kuongoza shughuli za Ofisi ya Hakimiliki.


Mpango mkakati unaweza kuzingatia mapendekezo ya idadi ya wafanyakazi kuanzia ngazi ya maofisa kwenda juu kama ifuatavyo:

 

a)      Idara ya Usimamizi wa Sheria na Kuzuia Uharamia (watu 5 - 8)

Idara hii ni moja ya idara muhimili kwa kuwa inahusu majukumu ya kisheria ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Meneja ataripoti kwa Msajili wa Hakimiliki na atawajibika pia kuwasilisha katika bodi ripoti za hali ya utekelezwaji wa sheria za hakimiliki nchini na mapambano dhidi ya uharamia. Idara hii pamoja na idara ya Utafiti, Elimu na TEHAMA vitachukua sehemu kubwa ya bajeti ya matumizi ya uendeshaji wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania.

 

Meneja atasaidiwa na maofisa wawili wanasheria na maofisa wawili watakaochukuliwa kutoka Jeshi la Polisi. Maofisa waliotoka jeshi la polisi kama itawezekana nao wawe wanasheria ingawa si lazima. Maoni yametolewa kuhusu umuhimu wa kuwa na wafanyakazi watakaoazimwa kutoka Jeshi la Polisi ili kuongeza ushirikiano na uharaka wa uchukuaji hatua za kuzuia uharamia na kuhakikisha sheria inafanya kazi nchini kote. Ili kutenda kwa ufanisi, idara hii itahitaji magari mawili ya kuzunguka nchi nzima.

 

b)     Idara ya Utafiti Elimu na TEHAMA (watu 5)

Hii ni moja ya idara mhimili za Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Idara hii itajikita katika elimu kwa wasanii, wadau na umma kwa ujumla kuhusu hakimiliki, kazi za usanii/ ubunifu na haki za wabunifu. Ili kupangilia elimu stahiki na kwa maeneo stahiki, idara hii pia inapaswa kutekeleza jukumu la utafiti. Kwa kuwa njia za kuwafikia wadau kwa njia ya kielektroniki zinazidi kukua, pia idara hii itakuwa ndiyo ina ofisa TEHAMA wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Vigezo vya ajira katika Ofisi ya Hakimiliki Tanzania yapaswa kuzingatia uelewa wa msingi wa TEHAMA unazingatiwa kwa kila mwajiriwa, katika kila idara.

 

c)      Idara ya Usimamizi wa CMOs (watu 4 - 5)

Hii nayo ni idara mhimili. Idara hii ndiyo itatoa leseni kwa CMOs, kupokea ripoti za robo, nusu mwaka na za mwaka za CMOs na kukagua CMOs. CMOs zitakaguliwa ili kuhakikisha kwamba zinaendesha shughuli zake kwa kuzingatia kanuni zilizoidhinishwa na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Ukaguzi pia utafanywa kuhakikisha


kwamba juhudi stahiki za kukubaliana na taasisi zinazolipa mirabaha zinafanywa kwa kampuni zote, makusanyo na leseni kwa watumiaji wa kazi za wasanii yanafuata taratibu, haki na sheria na, gharama za uendeshaji CMOs haziathiri maslahi ya wanachama wake (wamiliki wa hakimiliki). Idara hii itahakikisha kwamba mgawanyo wa mirabaha ni wa haki kwa wasanii wote stahiki.

 

Idara itakuwa na afisa mmoja mwanasheria na maafisa wawili hadi watatu wa fani ya uhasibu. Maafisa wa kihasibu wanaweza kuongezwa kutoka wawili hadi watatu na zaidi baada ya kuwepo kwa angalau CMOs mbili.

 

d)     Idara ya Fedha na Utawala (watu 6)

Idara hii itaongozwa na meneja mmoja. Chini ya meneja kutakuwa na wahasibu wasiozidi wawili, mtaalamu wa rasilimali watu mmoja na watunza kumbukumbu za kazi za hakimiliki wawili. Imependekezwa watunza kumbukumbu wa hakimiliki wawe chini ya idara hii kwa kuwa ndiyo itakayopokea fedha na hivyo itawajibika kupokea kazi za wabunifu na kuzitunza pia.

 

Meneja ataripoti kwa Msajili wa Hakimiliki. Atatoa taarifa katika kila kikao cha Bodi, pamoja na mambo ya fedha na rasilimali watu, kuhusu takwimu sahihi na kumbukumbu zilizohuishwa za hakimiliki katika daftari la kuorodhesha kazi zilizosajiliwa. Inapendekezwa kuanza na nafasi mbili ili mtu mmoja akiwa na udhuru mwingine aendelee kutoa huduma. Watunza kumbukumbu za hakimiliki wanapaswa kuwa wanasheria. Hawa ni watu ambao wanapaswa pia kuelewa kazi ngeni – mfano hata za kutoka nje ya nchi au zilizolengwa kutumika kupitia mifumo mipya.

 

e)      Miiko na Maadili ya Utendaji Kazi

Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania watatakiwa kuzingatia weledi wa hali ya juu. Hata hivyo, wafanyakazi wa idara ya usimamizi wa CMOs, wafanyakazi wa idara ya Usimamizi wa Sheria na Kuzuia Uharamia, Msajili wa Hakimiliki na Wakurugenzi wa Bodi wanapaswa kulinda haki katika maamuzi yote watakayofanya kuhusiana na hakimiliki. Ofisi ya Hakimiliki Tanzania iweke kanuni za maadili kulingana na ngazi ya maafisa husika katika maeneo tajwa katika aya hii.


f)       Miundombinu

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania haina jengo la ofisi za kudumu. Imepewa ofisi katika majengo ya Ofisi za Utumishi zilizopo Kivukoni, Dar es Salaam na Chumba kimoja kilichopo Dodoma kwenye ofisi za Wizara zilizopo jengo la PSSSF lakini bado ofisi hizo ni finyu haswa kwa majukumu mapya yaliyopendekezwa hapo juu yatakapoanza kutekelezwa.

 

7.0       MAKADIRIO YA MAKUSANYO YA SERIKALI

Makadirio ya makusanyo ya serikali yanatarajiwa kufanywa kwa kuhusisha vyanzo vitatu ambavyo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania, COSOTA, Mfuko wa Utamaduni na Malipo ya Mrabaha kama inavyofafanuliwa hapa chini:

a.   Mamlaka ya mapato Tanzania

 

Endapo serikali ikikubali kupokea mapendekezo ya kamati hii ya kurekebisha vifaa vitakavyotozwa tozo ya Kifaa kitupu, inakadiriwa kuwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania itakusanya Tsh. 681,837,257,900 kutoka kwenye tozo hii mpya kwa mwaka wa kwanza wa fedha huku mwaka wa pili wakiweza kukusanya Tsh. bilioni

712.5. Makadirio ya miaka kumi (10) ijayo ni Mamlaka ya mapato Tanzania itaweza kukusanya mapato kiasi cha trilioni Tsh. 9.838.

 

b.   COSOTA

 

Kutokana na makadirio haya ya marekebisho ya tozo hii, COSOTA itaweza kupata Tsh bilioni 2.05 kwa mwaka wa kwanza wa fedha wa makusanyo haya, mwaka wa pili wataweza kupata bilioni Tsh. 2.14, mwaka wa tatu wataweza kupata Tsh. bilioni

2.24 huku katika kipindi cha miaka kumi (10) ijayo, jumla ya Tsh. bilioni 29.5 zitatolewa kwa COSOTA kwa matumizi yake ya ndani.

 

c.    Mfuko wa utamaduni

 

Mfuko wa Utamaduni unatarajiwa kupata Tsh. bilioni 1.02 kwa mwaka wa kwanza wa makusanyo, Tsh. bilioni 1.07 kwa mwaka wa pili. Makadirio ya miaka kumi (10) ijayo ni Tsh. bilioni 15.616 zitatolewa kwa mfuko huu kama gawio kutoka kwenye tozo ya vifaa vitupu.


d.   Malipo ya Mrabaha

 

Kwa kuzingatia vyanzo viwili vya mirabaha vilivyolengwa ambavyo ni mrabaha wa utendaji kazi (Performance royalties) na mrabaha utokanao na kutoza ushuru wa vifaa vitupu, inaonekana kuwa serikali itaweza kukusanya jumla ya Tsh. bilioni 15.59 kwa mwaka wa kwanza, Tsh. bilioni 19.14 kwa mwaka wa pili, Tsh. bilioni 23.59 kwa mwaka wa tatu na jumla ya bilioni Tsh.419.67 kwa kipindi cha miaka kumi (10) ijayo.

 

Aidha, kwa kuzingatia mapendekezo ya sasa ya utengano kati ya CMO’s yaani Muundo Jumuishi wa Usimamizi Menejimenti na taasisi ya kusimamia Hakimiliki, inatazamiwa kuwa vyama hivi vya usimamizi na ukusanyaji wa mirabaha, vitaweza kukusanya takribani Tsh. Trilioni 3.76 kwa miaka 10 ijayo huku ulinganishi wa takwimu za kihistoria za miaka 17 iliyopita (2004 mpaka 2021), inaonesha COSOTA imeweza kufanya makusanyo ya Tsh. 3,114,778,220.

 

8.0 Shukrani

Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukamilisha kazi hii muhimu kwa maslahi mapana ya taifa na watu wake. Aidha, kwa namna ya kipekee tunakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa imani uliyoionesha kwetu na kututetua kufanya kazi hii muhimu. Umeonesha imani kubwa kwetu nasi tumejitahidi kufanya kazi kwa kuzingatia hadidu za rejea tulizopewa.

Kukamilika kwa kazi hii kumetokana na ushirikiano wa dhati uliooneshwa kutoka katika makundi mbalimbali. Tunawashukuru wadau wote walioshirikiana nasi katika hatua mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa zilizofanikisha kuandikwa kwa ripoti hii. Tunatambua kuna wadau waliojaza hojaji, waliosaidia kupatikana kwa nyaraka mbalimbali na wale walioshiriki katika mikutano iliyohusisha kanda sita kama zilivyotajwa hapo juu. Kipekee kabisa tunatoa shukrani za dhati kwa Mhe. Pauline Gekul (Mb.) Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye licha ya majukumu mengi ya kitaifa aliyonayo, aliweza kutenga muda wake na kushiriki nasi katika mkutano wa wadau wa kanda ya Kaskazini. Mkutano huu ulifanyika Mkoani Arusha katika Hoteli ya Golden Rose, na kuhudhuriwa na takriban washiriki 216.

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...