RIPOTI YA KAMATI TEULE
YA KURATIBU MJADALA WA NAMNA BORA YA
KUSIMAMIA HAKIMILIKI NCHINI TANZANIA
AGOSTI, 2022
1.0 Utangulizi
Hakimiliki
na Hakishiriki ni maeneo muhimu zaidi popote ubunifu unapotajwa. Hakimiliki na
Hakishiriki ni muhimu kwa kuwa ni msingi wa kuhakikisha kwamba wabunifu (wa
kazi sanaa na maandishi) wananufaika na matumizi ya kazi zao. Sheria imeweka wazi kwamba ni wabunifu
pekee ndio wenye uwezo wa kuruhusu matumizi ya kazi zao katika maeneo
mbalimbali. Hata hivyo, kwa kuwa kuna
baadhi ya haki ambazo wabunifu hawawezi kuzisimamia wenyewe, serikali nyingi
duniani zimekuwa zikianzisha taasisi mbalimbali kusimamia haki hizo. Kwa upande
wa Tanzania, kwa muda mrefu wajibu huu umekuwa ukifanywa na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA). Mnamo mwezi
Julai, 2022 Serikali ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Hakimiliki na
Hakishiriki ambapo mbali na mambo mengine imeifanya COSOTA kuwa Ofisi ya
Hakimiliki Tanzania na kuruhusu uanzishwaji wa makampuni au taasisi binafsi
(CMOs) zitakazokusanya na kugawa mirabaha kwa niaba ya wabunifu. Kwa mujibu wa
Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, CMOs zinatakiwa kuwa taasisi
zilizoidhinishwa kisheria chini ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, kufanya
shughuli za usimamizi wa Hakimiliki bila kuwa katika misingi ya kutengeneza
faida. Usimamizi wa taasisi hizi unatazamiwa kuwanufaisha moja kwa moja na kwa
njia rahisi waandishi, wabunifu na wamiliki wengine halali wa kazi za Sanaa.
Kwa kuzingatia usuli huo na kwa kuzingatia umuhimu wa usimamizi bora wa
Hakimiliki na Hakishiriki nchini Tanzania, mnamo tarehe 01.07.2022 Waziri wa
Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa aliteua kamati maalumu ya wajumbe 11 kwa lengo la
kuratibu namna bora ya usimamizi wa hakimiliki nchini Tanzania. Wajumbe hao ni
hawa wafuatao:
1.
Bw. Victor Michael
Tesha – Mwenyekiti
2.
Dkt. Saudin Mwakaje –
Makamu Mwenyekiti
3.
Bw. Dimesh S Mawj
– Katibu
4.
Mhe. Hamis Mwinjuma
– Mjumbe
5. Dkt. Omary
Mohamed – Mjumbe
6. Bw. Paul Mattysse – Mjumbe
7. Bi. Safina Kimbokota – Mjumbe
8. Bw. Torriano
Salamba – Mjumbe
9. Bw. Gabriel
Kitua – Mjumbe
10. Bw. Twiza Mbarouk
– Mjumbe
11. Dkt. Asha S
Mshana – Mjumbe
Wajumbe
wa kamati hii wana taaluma na uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwamo wataalamu
wa masuala ya fedha, wanasheria na wabunifu wa kada ya Sanaa na Maandishi.
2.0 Hadidu za rejea
Kamati ilipewa hadidu
za rejea zifuatazo:
1.
Kupendekeza mifumo bora zaidi ya kukusanya na kugawa mirabaha
inayoshabihiana na mifumo mingine duniani.
2.
Kupendekeza njia bora zaidi ya
kupambana na uharamia wa kazi za sanaa
nchini.
3.
Kupendekeza mfumo bora zaidi wa uendeshaji wa Taasisi ya Hakimiliki
Tanzania.
4.
Kuratibu kikao cha wadau wa
Hakimiliki cha kujadili mapendekezo ya kamati na
5. Kuwasilisha taarifa
ya kamati kwa Mhe. Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
3.0
Methodolojia
Ili
kufanya kazi kwa mujibu wa hadidu rejea, methodolojia iliyotumika katika kupata
taarifa ni upitiaji wa nyaraka mbalimbali zinazohusu hakimiliki, mahojiano,
hojaji na mikutano ya ana kwa ana ambayo ilishirikisha wadau mbalimbali muhimu
katika kupata taarifa kwa lengo la kukamilisha jukumu la Kamati. Mikutano hii
ilifanyika katika kanda sita kama ifuatavyo:
Mosi, kanda ya Kaskazini- Mkutano ulifanyika Mkoani Arusha katika
Hoteli ya Golden Rose, na kuhudhuriwa
na wabunifu pamoja na wadau 216.
Mkutano
huu pia ulihudhuriwa na Mhe. Pauline Gekul Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na
Michezo.
Pili, kanda ya
Kati – Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa
Dear Mama, mjini Dodoma na
kuhudhuriwa na wabunifu pamoja na wadau 126.
Tatu,
kanda ya Ziwa – Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya jijini
Mwanza na kuhudhuriwa na wabunifu 87.
Nne, kanda ya Nyanda za Juu Kusini- Mkutano
uliafanyika katika ukumbi
wa BEACO jijini Mbeya na
kuhudhuriwa na wabunifu 138
Tano,
Kanda ya kusini- mkutano huu ulifanyika mkoa wa Mtwara katika ukumbi wa
Halmashauri na ulihudhuriwa na wadau 181.
Sita,
kanda ya Mashariki, ambapo mkutano wa wabunifu na wadau wa sekta ya ubunifu 171 ulifanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam na
kuhudhuriwa na wajumbe wote wa kamati wakiongozwa na Mwenyekiti. Ripoti za
mikutano ya ukusanyaji maoni zimeambatishwa kama viambatisho Na. 4.2.
Wadau
wa jinsi zote, wakiwamo wenye mahitaji maalumu walishiriki. Kwa wastani 22% ya
wasanii na wadau waliohudhuria walikuwa wa jinsi ya kike na 78% walikuwa wa
jinsi ya kiume. Tasnia ya Sanaa ya Maonesho na Sanaa ya Ufundi zilikuwa na
uwiano mzuri zaidi wa uwakilishi kati ya jinsi ya kike na ile ya kiume. Katika
watoa maoni, uwiano wa wasanii wa kike ulikuwa mdogo zaidi kwa wasanii wa
muziki.
Aidha, kamati hii iliangalia uzoefu wa nchi nyingine kwenye usimamizi
wa Hakimiliki na kuchambua takwimu za wabunifu na wadau. Nchi zilizoangaliwa
kwa ajili ya uzoefu ni pamoja na Nigeria, Algeria, Afrika Kusini na Kenya.
4.0
Mapitio ya Mabadiliko ya Mfumo wa Sheria
Katika
kujenga usuli mzuri wa mapendekezo ya Kamati kwa mujibu wa hadidu za rejea
katika ripoti hii, na kwa lengo la kujenga welewa wa pamoja, kumetolewa usuli
wa mabadiliko ya mfumo wa sheria wa hakimiliki nchini Tanzania. Mabadiliko
yaliyojadiliwa katika ripoti hii ni:
Mosi,
mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ya mwaka 1999 ambayo
yalifanywa kwa lengo la kuziba baadhi ya mianya ya kiusimamizi iliyoonekana
kuwapo kwa wakati huo. Sheria hii ilibadilisha maeneo manne ambayo
ni
kifungu cha 4, Kifungu cha 9, kifungu cha 15 na kifungu cha 42. Vifungu hivi
vilifanyiwa uboreshaji ili kuendana na hali ya sasa kuhusiana na masuala ya
Hakimiliki na Hakishiriki.
Pili
ni mabadiliko ya sheria ya Machi, 2022 kufuatia mabadiliko ya sheria Na.1 ya mwaka 2022, ambapo kifungu
cha 3 kilibadilishwa kuongezewa tafsiri
na kifungu cha 12 kilibadilishwa na kuongezewa
vifungu vya 12A na 12B ili kuwezesha utekelezaji wa mkataba huo. Baadhi ya
marekebisho hayo ni:
a)
Kuweka utaratibu unaoruhusu
kunakili machapisho na kuyageuza katika muundo
(format) ya maandishi kwa ajili ya watu wasiiona au wenye matatizo ya kusoma
maandishi ya kawaida bila kupata idhini ya mwenye chapisho.
b)
Kuweka utaratibu wa kuruhusu
taasisi husika kuweza kurudufu machapisho na kuwayaweka katika mfumo wa kuweza
kusomwa na watu wenye matatizo ya kuona na taasisi hizo kuruhusiwa kusambaza
kwa wahusika kwa kutoza gharama za uchapishaji na si kwa ajili ya kupata faida.
Tatu,
ni mabadiliko yaliyofanywa na Sheria
ya Fedha ya Mwezi Julai, 2022 ambayo mbali na mambo mengine yamelenga
katika kuanzisha mfumo mpya wa usimamizi wa hakimiliki hapa Tanzania kwa
kuruhusu uanzishwaji wa makampuni binafsi ya ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha
nchini Tanzania. Pia mabadiliko haya yameanzisha tozo mpya kwa vibebeo vya kazi
za ubunifu vinavyotumika katika kudurufu, kusambaza, kuhifadhia na kuzalisha
kazi hizo. Aidha, mabadiliko yamefanyika katika kifungu cha 4 kwa kuongeza
tafsiri pamoja na kufuta neno chama
na kuweka neno ofisi. Pia vifungu vya 46, 47 na 48 vimerekebishwa ambapo baadhi
ya majukumu yaliyokuwa yakifanywa na COSOTA yameondolewa ili kuruhusu
uanzishwaji wa kampuni hizo na uazishwaji wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania.
5. Matokeo ya Utafiti
Baada
ya majadiliano na wadau na kwa kuzingatia hojaji zilizotolewa mapendekezo
yafuatayo yalizingatiwa:
5.1
Elimu kwa umma
Wadau
wote waliohudhuria katika mikutano ya kukusanya maoni walijibu maswali kuhusu elimu
ya hakimiliki, usimamizi wa maslahi ya wasanii na uharamia wa kazi za
sanaa. Wadau wengi walionesha uhitaji wa elimu zaidi kwa umma kuhusu hakimiliki
na masuala kadhaa yanayoambatana na hakimiliki. Aidha, washiriki wengi
walionesha kuelewa zaidi kuhusu Taasisi ya Hakimiliki nchini kuliko mambo
muhimu kama umiliki wa hakimiliki za sanaa; anayestahili malipo kutokana na
kazi za sanaa na kuhusu uharamia wa kazi za sanaa.
Vilevile, ufahamu wa washiriki kuhusu uharamia wa kazi za wasanii
ulikuwa mdogo zaidi ukifuatiwa na uelewa kuhusu umiliki wa hakimiliki na
stahiki za mapato yatokanayo na hakimiliki
5.2 Umuhimu wa kuwa na Chombo kimpya cha kusimamia masuala ya hakimiliki nchini
Maeneo
mengine yaliyotolewa maoni ni iwapo kuna mahitaji ya chombo kipya cha kusimamia
mashauri ya hakimiliki nchini.
Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba tasnia ya Sanaa ya Ufundi
ikifuatiwa na tasnia ya Muziki na Filamu zilipendekeza kwa asilimia zaidi ya 50% kuwe na chombo
kipya wakati tasnia hizo za Sanaa uelewa wao kuhusu hakimiliki ya kazi za sanaa
zao ulikuwa chini ya asilimia 50%. Wakati huohuo tasnia hizo tatu uelewa wao
kuhusu Ofisi ya Hakimiliki ulikuwa 63%, 77% na 72% kwa Sanaa ya Ufundi, Sanaa
ya Muziki na Sanaa ya filamu katika mpangilio huo.
Matokeo ya Utafiti huu yanaonesha umuhimu wa Kamati kuzingatia mambo
mawili: Mosi, kupendekeza mkakati
na mfumo utakaowezesha uwekezaji na jitihada
za dhati kuhusu elimu kwa
wasanii wa tasnia zote na umma kuhusu mambo ya hakimiliki na uharamia wa kazi
za sanaa.
Pili, kupendekeza kanuni na taratibu ambazo zimeakisi kanuni
bora zaidi kutoka nchi zenye mazingira sawa na
Tanzania.
6.0
Mapendekezo ya Kamati
Kutokana
na mabadilko ya Sheria ya mwezi Julai 2022 ambayo yameanzisha utaratbu mpya wa
usimamizi wa hakimiliki ambapo kazi za usimamizi wa hakimiliki na ukusanyaji wa
mirabaha zitafanywa na CMOs, na pia kwa kuzingatia maoni na mapendekezo
mbalimbali yaliyotolewa na wadau, Kamati inapendekeza masuala ya kisera na
kisheria katika maeneo manne: (1)
mfumo bora wa kukusanya na kugawa mirabaha, (2) njia bora ya kupambana na
uharamia, (3) mfumo bora wa uendeshaji wa taasisi ya hakimiliki, na (4)
mapendekezo mengine ya jumla.
6.1
Mfumo Bora wa Kukusanya
na Kugawa Mirabaha
Katika sehemu
hii kuna mambo
mawili ya msingi
ambayo ni kanuni za usimamizi wa ukusanyaji wa mirabaha na ushirikiano na Taasisi mbalimbali
za serikali
6.1.1
Kanuni za Usimamizi wa Ukusanyaji Mirabaha
Ili
kutekeleza mfumo mpya wa usimamizi wa hakimiliki hapa Tanzania, Kamati
inapendelkeza kanuni zitungwe kwa kuzingatia mambo yafuatayo:
i.
Kabla ya kufanyiwa usajili au
kupewa leseni ya kukusanya mirahaba, CMOs zifanyiwe tathmini ya uwezo wao wa
kiutawala, wawasilishe mpango wa biashara wakibainisha mbinu watakazotumia
kutambua wasanii wa eneo hilo na namna ukusanyaji wa mirabaha utakavyofanyika,
ziwe na mfumo unaokubalika wa kihasibu, waajiri watalaamu wenye sifa, katika
bodi ya wakurugenzi kuwa na wawakilishi wa tasnia husika ya sanaa (wamiliki).
ii.
Kwa kuanzia, makampuni yatakayopewa
dhamana ya kukusanya mirabaha yapewe aina moja ya sanaa kwa kazi zote.
Utaratibu huu utazifanya kampuni hizi zitakazopewa leseni ya kukusanya mirabaha
kufanya kazi kwa ufanisi kwa kulenga
aina moja tu ya kazi.
iii.
Kila mwaka utendaji wa kampuni hizi
ufanyiwe tathmini ili kujua kama zina ufanisi au la. Vigezo viwekwe
vitakavyoongoza Ofisi ya Hakimiliki kuamua kuhuisha au kutohuisha leseni ya
kampuni. Kiwekwe kiwango cha alama za chini cha utendaji katika ukusanyaji
mapato.
iv.
Kila mwaka wa fedha unapoanza,
kampuni hizi ziwasilishe makadirio ya makusanyo kwa mwaka ambayo yatafanyiwa
tathimini na kuidhinishwa na Ofisi ya Hakimiliki. Endapo kampuni itakusanya
chini ya asilimia 50 ya makadirio bila kutoa sababu za msingi, Kanuni zitoe mamlaka
kwa Ofisi ya
Hakimili
kukataa maombi ya kuhuisha leseni ya kukusanya mirabaha kwa kampuni husika.
v.
CMOs iweke mfumo wa kielektroniki
ambao utaruhusu taarifa za muda mfupi za makusanyo ya mirahaba kuonwa na Ofisi ya Hakimiliki na wamiliki wa haki.
vi.
Kwa kuwa kampuni za ukusanyaji
zitakuwa zikikusanya na kubaki na fedha za
wamiliki, ni vyema kanuni zikaweka ukomo wa matumizi ya uendeshaji ili kulinda
maslahi ya wamiliki.
vii.
Katika maombi ya leseni (mpya au
kuhuisha), kanuni ziweke sharti kwa kampuni za ukusanyaji wa mirabaha
kuwasilisha dhamana ya fedha kutoka benki kwa kiwango kisichopungua asilimia 50
ya matarajio ya makusanyo katika mwaka unaofuata.
viii.
Katika kipindi cha mpito kabla ya
Kanuni za utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria kutungwa, Ofisi ya Hakilimili
Tanzania iendekee kutambulika kama ina majukumu ya kukusanya mirabaha
na kuendelea kukusanya
mirabaha mpaka hapo makampuni
yatakayopewa leseni ya kukusanya yatakapoanza kazi kikamili na kujisajili
katika mashirika ya kimataifa ya ukusanyaji wa mirabaha.
6.1.2
Ushirikiano wa Taasisi Mbalimbali za Serikali
Masuala
yanayohusu usimamizi wa hakimiliki ni mtambuka na yanahusisha taasisi nyingi za
serikali na nyakati fulani zenye maslahi pingani. Hivyo Kamati inapendekeza
yafuatayo:
i.
Kuundwa kisheria kwa Kamati ya
Kiuratibu ya Wizarani kwa ajili ya usimamizi wa masuala ya hakimiliki
ikihusisha Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, BASATA, Bodi ya Filamu, TRA,TCRA,
BRELA,TCU, na TAMISEMI. Taasisi hizi zinasimamia wazalishaji na watumiaji wa
kazi za sanaa. Ni vyema kukawa na wajibu wa kisheria kwa taasisi hizi kushirikiana ili kuwa na mkakati wa pamoja katika kushughulikia uharamia
wa kazi za wasanii na ukusanywaji wa mirabaha.
ii.
Katika utoaji wa leseni za biashara
kwa taasisi zinazotumia kazi za sanaa, kwa mfano redio, televisheni, baa na
shule kuwepo na matakwa ya mwombaji
kuwasilisha cheti cha utambuzi kutoka Ofisi ya Hakimiliki ya Tanzania. Hii
itasaidia kuwabana wahusika kama hawatoi ushirikiano katika kuwasilisha malipo
ya mirabaha kutokana na matumizi ya kazi za sanaa.
6.1.3 Njia Bora ya Kupambana na Uharamia wa kazi za sanaa
Katika
sehemu hii, Kamati inapendekeza mambo mawili ya msingi ambapo kila moja
limefafanuliwa katika vipengele vidogovidogo kadhaa: Mambo hayo ni kuongeza
adhabu kwa makosa ya uharamia wa kazi za hakimiliki pamoja na kusajili mikataba
ya wasanii. Ufafanuzi wa mapendekezo haya ni kama unavyoonekana hapa chini:
a)
Kuongeza Adhabu kwa Makosa ya Uharamia wa kazi za sanaa
Mojawapo
ya njia ya kuboresha usimamizi wa hakimiliki ni kufanyia marekebisho kwa adhabu zinazotolewa. Kwa mfumo wa sasa
wa adhabu, ambao unatoa adhabu ya faini au kifungo cha jela bila kuzingatia
uzito wa kosa. Hapa Kamati inatoa mapendekezo yafuatayo:
i.
Adhabu zitolewe kwa kuzingatia uzito wa kosa,
ii.
Mahakama au Ofisi ya Hakimiliki
iwekewe kiwango cha chini cha faini au kifungo, lakini iachiwe uhuru wa kuamua
kiwango cha juu cha adhabu kwa kuzingatia muktadha na uzito wa kosa
lililofanyika;
iii.
Adhabu ihusishe kufutiwa leseni ya
biashara endapo itathibitika kuwa mkosaji alifanya kosa hilo kwa kukusudia;
iv.
Adhabu ihusishe kutaifishwa na
kuharibiwa kwa vifaa vinavyotumika katika kufanya uharamia
v.
Adhabu ziwaguse waliofanya makosa
na waliowasaidia kutekeleza uharamia. Kutanua wigo wa wahusika kutasaidia
katika kuimarisha usimamizi na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa
hakimiliki nchini.
b)
Kusajili Mikataba ya Wasanii
Mojawapo
ya malalamiko makubwa na yanayojirudia ni kuwa wasanii wengi wanahisi wanaonewa kimaslahi katika kazi
wanazofanya chini wa mwavuli wa makampuni au wasanii wakubwa. Ili kushughulikia
suala hilo, tunapendekeza:
i.
Katika kanuni zitakazotungwa,
kiongezwe kipengele ambacho kitatoa motisha kwa makampuni na wasanii wakubwa
kusajili mikataba yao katika Ofisi ya Hakimiliki. Vivutio hivi vinaweza
kujumuisha kuruhusu nafuu za kikodi kwa makampuni yatakayosajili mikataba ya
wasanii. Kanuni ziweke wajibu kuwa mikataba ya wasanii wanaochipukia isajiliwe
katika Ofisi ya Hakimiliki.
ii.
Pia, sheria itoe mamlaka kwa Ofisi
ya Hakimiliki kupitia vifungu vya mikataba inayosajiliwa na endapo
itajiridhisha kuwa kuna vifungu kandamizi Ofisi iwe na mamlaka ya kushauri mamlaka husika kufanya marekebisho.
6.1.4 Mapendekezo Kuhusu Mfumo wa
Kisheria
Katika sehemu
hii Kamati inatoa
mapendekezo katika maeneo saba
kama ifuatavyo:
a) Marekebisho ya Sheria
ya Hakimiliki na Hakishiriki ya 1999
Kwa
kuzingatia maendeleo ya kiteknolojia ambayo yamebadili mfumo mzima wa jinsi
kazi za sanaa zinarudufiwa na maharamia, tunapendekeza:
i.
Orodha ya vifaa vitakavyotozwa kodi
(blanket levy) katika mabadiliko ya sheria ya hakimiliki ya mwezi Julai 2022
iboreshwe kwa kuongezea vifaa ambavyo kwa teknolojia ya sasa vinatumika katika
kuridifu na kuhifadhi kazi za sanaa. Vifaa vilivyo katika orodha ya sasa ni vya
zamani na havitumiki sana.
ii.
Wigo wa mfumo au njia za utambuzi
wa matukio ya uharamia na ulinzi wa kazi za sanaa uboreshwe kwa kuzingatia na
kutumia mifumo ya kiteknolojia iliyopo sasa. Hii itaendana na hatua ambazo
mashirika ya kimataifa kama vile WIPO yamechukua kwa kupitisha na kutumia
Mkataba maalumu wa kimataifa wa hakimiliki ambao umejikita
zaidi katika masuala
ya kiteknolojia (WIPO Copyight
Treaty of 1996)
b) Kuanzisha Mfumo wa Mahakama Tembezi
Ili
kushughulikia tatizo linaloongezeka la uharamia wa kazi za wasanii, ni vyema
mfumo wa utoaji haki uboreshwe ili uweze kushughulikia makosa yanayojitokeza
kulingana na uhalisia na mazingira ya utendaji wa makosa ya kiuharamia. Katika
mazingira ya Tanzania ambapo makosa ya kiuharamia hufanyika kwa kiwango kikubwa
na kidogo ikihusisha sehemu ambazo ni rahisi kuharibu ushahidi endapo ukamataji
utachelewa, inapendekezwa kuanzishwa kwa mahakama zinazotembea ambazo zitakuwa
na mamlaka ya kutoa maamuzi papohapo endapo ushahidi utakuwa umejitosheleza.
c) Kuongeza Mamlaka ya Kiusimamizi kwa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania
Ili
kuboresha usimamizi wa masuala ya hakimiliki hapa Tanzania, inashauriwa kuwa
Ofisi ya Hakimiliki ipewe mamlaka
ya kisheria ili kushughulikia utatuzi wa migogoro
na
makosa ya uharamia na kutoa adhabu kwa wahusika watakopatikana na hatia.
Mamlaka hiyo inapaswa kutumia nguvu ya kisheria kuagiza vifaa vinanvotumika
kufanya kazi za uharamia kukamatwa mara tu vinapogundulika mahali vilipo,
watuhumiwa wa uharamia kukamatwa, kutoa amri ya kuviharibu vifaa
vitakavyothibitika ni zao la uharamia au vinatumika kufanya uharamia. Kwa kuchukua hatua hii, itawezesha Ofisi ya
Usimamizi wa Hakimiliki kuwa na nguvu ya kisheria ya kutoa maamuzi ya haraka na
yenye nguvu za kisheria. Pia, hatua hii itapunguza kwa kiwango kikubwa
ucheleweshaji wa kesi za uharamia wa kazi za sanaa na kupunguza gharama za
kuendesha kesi kwa walalamikaji.
d)
Ofisi ya Hakimiliki Iongeze
Wigo wa kazi Inazosimamia
Kwa
ujumla, katika utendaji wake, COSOTA imekuwa ikijikita zaidi katika kazi za
Sanaa ya muziki. Wakati umefika sasa wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania kujipambanua na kuweka mkakati wa kutumia
rasilimali na nguvu ileile katika kusimamia kazi zote za sanaa. Inapendekezwaza
kuwa Ofisi ya Hakimiliki kuzigawa aina mbalimbali za sanaa na kuanzisha vitengo
vya ndani vitakavyosimamia maeneo hayo ya sanaa.
Maeneo haya yanaweza kujumuisha tasnia nne za
sanaa ambazo ni
(1)
Sanaa za ufundi (2) Sanaa za maonesho
(3) sanaa za muziki na (4) Sanaa za filamu. Ili
kutilia mkazo, tunapendekeza maeneo hayo yabainishwe na kutengewa rasilimali
kwa ajili ya utekelezaji katika mpango mkakati wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania.
Hatua hii itaongeza tija katika tansinia ya sanaa na kuongeza wigo wa mapato
kwa serikali na wasanii.
e)
Kutungwa Sera ya Taifa ya Miliki Dhihini (National Intellectual Property Policy)
Ili kuyashughulikia masuala ya hakimiliki kwa upana wake, maeneo
mengine ya miliki ya ubunifu na
taasisi nyingine zinazoshughulikia miliki ya ubunifu kama vile BRELA, FCC,
BASATA, COSTECH zinahusika. Hivyo, tunapendekeza kuwa mchakato unaondelea wa
kutunga na kupitisha sera ya kitaifa ya miliki ya ubunifu uharakishwe ili
Tanzania iwe na sera inayotoa dira ya jumla ya jinsi masuala haya yanavyopaswa
kushughulikiwa.
f)
Elimu ya Hakimiliki
Kutokana
na umuhimu wa tasnia yab sanaa na masuala yote ya ubunifu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
kiutamaduni na sayansi hapa Tanzania, tunapendekeza mitaaala ya elimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi ijumuishe moduli zinazofundisha masuala ya miliki
za ubunifu na umuhimu wa kuheshimu
na kuzilinda haki za wabunifu kupitia sheria zilizopo. Mbali na mitaala ya shuleni, Wizara ianzishe mpango kabambe wa kuandaa
vipindi vya kuelimisha jamii kupitia television, radio, mitandao ya kijamii na
njia nyinginezo zitakazosaidia kufikisha elimu kwa walengwa na wadau
mbalimbali.
g)
Kuridhia Mikataba ya Kimataifa Inayohusu Hakimiliki
Ili
kuboresha usimamizi wa hakimiliki ni muhimu kwa Tanzania kuanzisha mchakato wa
kuridhia mikataba ya kimataifa inayohusu hakimiliki na kuimarisha zaidi
ushirikiano na mashirika ya kimataifa na kikanda. Miongoni mwa mashirika hayo
ni:
i.
Shirika la Kimataifa la Miliki ya
Ubunifu (World Intellectual Property Organization (WIPO))
ii.
Shirika la Biashara
la Kimataifa (World
Trade Organization (WTO)
iii.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (United Nation
Educational Scientific and Cultural Organization (UNESCO)
iv.
Shirika la Kikanda
la Miliki ya Ubunifu Africa
(ARIPO)
6.1.5
Muundo wa kiuongozi unaopendekezwa kwa ajili ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania
Kwa
kuwa ofisi hii imepunguziwa kazi ya kuandikisha wanachama, kukusanya na kugawa
mirahaba, idadi wa wafanyakazi inapaswa kuanza
kwa kiwango kinacholingana na uhalisia wa shughuli lengwa na pia ili
kuwezesha wafanyakazi watakaokuwapo a) kuwa na kazi ya kutosha na b) kulipwa
stahiki zao ipasavyo na kuwezesha mchango wa rasilimali fedha kwa CMOs mpya.
Inapendekezwa kuhakikisha wanaajiriwa wafanyakazi wenye weledi, mahiri na
wanaostahili.
6.1.6
Mchanganuo wa kina wa idadi ya wafanyakazi
kwa kila idara
Bodi
ya Wakurugenzi inapaswa kuandaa mpango mkakati, kwa kuanzia wa miaka mitatu kisha wa miaka mitano mitano ili kuongoza
shughuli za Ofisi ya Hakimiliki.
Mpango mkakati
unaweza kuzingatia mapendekezo ya idadi ya wafanyakazi kuanzia ngazi ya maofisa kwenda juu kama
ifuatavyo:
a) Idara ya Usimamizi
wa Sheria na Kuzuia Uharamia
(watu 5 - 8)
Idara
hii ni moja ya idara muhimili kwa kuwa inahusu majukumu ya kisheria ya Ofisi ya
Hakimiliki Tanzania. Meneja ataripoti kwa Msajili wa Hakimiliki na atawajibika
pia kuwasilisha katika bodi ripoti
za hali ya utekelezwaji wa sheria za hakimiliki nchini na mapambano dhidi ya
uharamia. Idara hii pamoja na idara ya Utafiti, Elimu na TEHAMA vitachukua
sehemu kubwa ya bajeti ya matumizi ya uendeshaji wa Ofisi ya Hakimiliki
Tanzania.
Meneja
atasaidiwa na maofisa wawili wanasheria na maofisa wawili watakaochukuliwa
kutoka Jeshi la Polisi. Maofisa waliotoka jeshi la polisi kama itawezekana nao
wawe wanasheria ingawa si lazima. Maoni yametolewa kuhusu umuhimu wa kuwa na
wafanyakazi watakaoazimwa kutoka Jeshi la Polisi ili kuongeza ushirikiano na
uharaka wa uchukuaji hatua za kuzuia uharamia na kuhakikisha sheria inafanya
kazi nchini kote. Ili kutenda kwa ufanisi, idara hii itahitaji magari mawili ya
kuzunguka nchi nzima.
b) Idara ya Utafiti
Elimu na TEHAMA (watu
5)
Hii
ni moja ya idara mhimili za Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Idara hii itajikita
katika elimu kwa wasanii, wadau na umma kwa ujumla kuhusu hakimiliki, kazi za
usanii/ ubunifu na haki za wabunifu.
Ili kupangilia elimu stahiki na kwa maeneo stahiki, idara hii pia
inapaswa kutekeleza jukumu la utafiti. Kwa kuwa njia za kuwafikia wadau kwa
njia ya kielektroniki zinazidi kukua, pia idara hii itakuwa ndiyo ina ofisa
TEHAMA wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Vigezo vya ajira katika Ofisi ya
Hakimiliki Tanzania yapaswa kuzingatia uelewa wa msingi wa TEHAMA unazingatiwa
kwa kila mwajiriwa, katika kila
idara.
c) Idara ya Usimamizi
wa CMOs (watu 4
- 5)
Hii
nayo ni idara mhimili. Idara hii ndiyo itatoa leseni kwa CMOs, kupokea ripoti
za robo, nusu mwaka na za mwaka za CMOs na kukagua CMOs.
CMOs zitakaguliwa ili kuhakikisha kwamba zinaendesha shughuli zake kwa
kuzingatia kanuni zilizoidhinishwa na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania. Ukaguzi pia
utafanywa kuhakikisha
kwamba
juhudi stahiki za kukubaliana na taasisi zinazolipa mirabaha zinafanywa kwa kampuni zote, makusanyo na leseni kwa
watumiaji wa kazi za wasanii yanafuata
taratibu, haki na sheria na, gharama za uendeshaji CMOs haziathiri maslahi ya
wanachama wake (wamiliki wa hakimiliki). Idara hii itahakikisha kwamba mgawanyo
wa mirabaha ni wa haki kwa wasanii wote stahiki.
Idara itakuwa na afisa mmoja mwanasheria na maafisa wawili hadi watatu wa fani ya uhasibu. Maafisa wa kihasibu wanaweza kuongezwa kutoka
wawili hadi watatu na zaidi baada ya kuwepo kwa angalau CMOs mbili.
d) Idara ya Fedha na Utawala
(watu 6)
Idara
hii itaongozwa na meneja mmoja. Chini ya meneja kutakuwa na wahasibu wasiozidi
wawili, mtaalamu wa rasilimali watu mmoja na watunza kumbukumbu za kazi za
hakimiliki wawili. Imependekezwa watunza kumbukumbu wa hakimiliki wawe chini ya
idara hii kwa kuwa ndiyo itakayopokea fedha na hivyo itawajibika kupokea kazi
za wabunifu na kuzitunza pia.
Meneja
ataripoti kwa Msajili wa Hakimiliki. Atatoa taarifa katika kila kikao cha Bodi,
pamoja na mambo ya fedha na rasilimali watu, kuhusu takwimu sahihi na
kumbukumbu zilizohuishwa za hakimiliki katika daftari la kuorodhesha kazi
zilizosajiliwa. Inapendekezwa kuanza na nafasi mbili ili mtu mmoja akiwa na
udhuru mwingine aendelee kutoa huduma. Watunza
kumbukumbu za hakimiliki wanapaswa kuwa wanasheria. Hawa ni watu ambao wanapaswa pia kuelewa kazi ngeni – mfano hata za kutoka nje ya nchi au zilizolengwa kutumika
kupitia mifumo mipya.
e) Miiko na Maadili
ya Utendaji Kazi
Wafanyakazi
wote wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania watatakiwa kuzingatia weledi wa hali ya
juu. Hata hivyo, wafanyakazi wa idara ya usimamizi wa CMOs, wafanyakazi wa
idara ya Usimamizi wa Sheria na Kuzuia Uharamia, Msajili wa Hakimiliki na
Wakurugenzi wa Bodi wanapaswa kulinda haki katika maamuzi yote watakayofanya
kuhusiana na hakimiliki. Ofisi ya Hakimiliki Tanzania iweke kanuni za maadili
kulingana na ngazi ya maafisa husika katika maeneo tajwa katika aya hii.
f) Miundombinu
Ofisi
ya Hakimiliki Tanzania haina jengo la ofisi za kudumu. Imepewa ofisi katika
majengo ya Ofisi za Utumishi zilizopo Kivukoni, Dar es Salaam na Chumba kimoja
kilichopo Dodoma kwenye ofisi za Wizara zilizopo jengo la PSSSF lakini bado
ofisi hizo ni finyu haswa kwa majukumu mapya yaliyopendekezwa hapo juu yatakapoanza kutekelezwa.
7.0 MAKADIRIO YA MAKUSANYO YA SERIKALI
Makadirio ya makusanyo ya serikali yanatarajiwa
kufanywa kwa kuhusisha vyanzo vitatu ambavyo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania,
COSOTA, Mfuko wa Utamaduni na Malipo ya Mrabaha kama inavyofafanuliwa hapa
chini:
a.
Mamlaka ya mapato Tanzania
Endapo serikali ikikubali kupokea mapendekezo ya
kamati hii ya kurekebisha vifaa vitakavyotozwa tozo ya Kifaa kitupu,
inakadiriwa kuwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania itakusanya Tsh. 681,837,257,900
kutoka kwenye tozo hii mpya kwa mwaka wa kwanza wa fedha huku mwaka wa pili wakiweza
kukusanya Tsh. bilioni
712.5. Makadirio ya miaka kumi (10) ijayo ni
Mamlaka ya mapato Tanzania itaweza kukusanya mapato kiasi cha trilioni Tsh.
9.838.
b.
COSOTA
Kutokana na makadirio haya ya marekebisho ya tozo
hii, COSOTA itaweza kupata Tsh bilioni 2.05 kwa mwaka wa kwanza wa fedha wa
makusanyo haya, mwaka wa pili wataweza kupata bilioni Tsh. 2.14, mwaka wa tatu wataweza kupata Tsh. bilioni
2.24 huku katika kipindi cha miaka kumi (10) ijayo,
jumla ya Tsh. bilioni 29.5 zitatolewa kwa COSOTA kwa matumizi yake ya ndani.
c.
Mfuko wa
utamaduni
Mfuko wa Utamaduni unatarajiwa kupata Tsh. bilioni
1.02 kwa mwaka wa kwanza wa
makusanyo, Tsh. bilioni 1.07 kwa mwaka wa pili. Makadirio ya miaka kumi (10)
ijayo ni Tsh. bilioni 15.616 zitatolewa kwa mfuko huu kama gawio kutoka kwenye
tozo ya vifaa vitupu.
d.
Malipo ya Mrabaha
Kwa kuzingatia vyanzo viwili vya mirabaha
vilivyolengwa ambavyo ni mrabaha wa utendaji kazi (Performance royalties) na
mrabaha utokanao na kutoza ushuru wa vifaa vitupu, inaonekana kuwa serikali
itaweza kukusanya jumla ya Tsh. bilioni 15.59 kwa mwaka wa kwanza, Tsh. bilioni 19.14 kwa mwaka wa pili, Tsh. bilioni 23.59 kwa mwaka wa tatu na
jumla ya bilioni Tsh.419.67 kwa kipindi cha miaka kumi (10) ijayo.
Aidha,
kwa kuzingatia mapendekezo ya sasa ya utengano kati ya CMO’s yaani Muundo
Jumuishi wa Usimamizi Menejimenti na taasisi ya kusimamia Hakimiliki,
inatazamiwa kuwa vyama hivi vya usimamizi na ukusanyaji wa mirabaha, vitaweza
kukusanya takribani Tsh. Trilioni 3.76 kwa miaka 10 ijayo huku ulinganishi wa
takwimu za kihistoria za miaka 17 iliyopita (2004 mpaka 2021), inaonesha COSOTA
imeweza kufanya makusanyo ya Tsh. 3,114,778,220.
8.0 Shukrani
Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutuwezesha kukamilisha kazi hii muhimu kwa maslahi mapana ya taifa na
watu wake. Aidha, kwa namna ya kipekee tunakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa
imani uliyoionesha kwetu na kututetua kufanya kazi hii muhimu. Umeonesha imani
kubwa kwetu nasi tumejitahidi kufanya kazi kwa kuzingatia hadidu za rejea
tulizopewa.
Kukamilika
kwa kazi hii kumetokana na ushirikiano wa dhati uliooneshwa kutoka katika
makundi mbalimbali. Tunawashukuru wadau wote walioshirikiana nasi katika hatua
mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa zilizofanikisha kuandikwa kwa ripoti hii.
Tunatambua kuna wadau waliojaza hojaji, waliosaidia kupatikana kwa nyaraka
mbalimbali na wale walioshiriki katika mikutano iliyohusisha kanda sita kama
zilivyotajwa hapo juu. Kipekee kabisa tunatoa shukrani za dhati kwa Mhe.
Pauline Gekul (Mb.) Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye licha ya
majukumu mengi ya kitaifa aliyonayo, aliweza kutenga muda wake na kushiriki
nasi katika mkutano wa wadau wa kanda ya Kaskazini. Mkutano huu ulifanyika
Mkoani Arusha katika Hoteli ya Golden Rose, na kuhudhuriwa na takriban
washiriki 216.
No comments:
Post a Comment