YOUTUBE PLAYLIST

Sunday, February 28, 2010

Kina nani hawa?


Leo natoa picha 3 za wanamuziki maarufu wakati wakiwa bado makinda, swali ni akina nani hawa?


Saturday, February 27, 2010

Mzee Hamisi Kitambi Hatunae Tena


Mzee Hamisi Kitambi hatunae tena. Amefariki tarehe 26 Feruary 2010, na kuzikwa tarehe 27 February 2010. Mzee Hamisi Kitambi kwa mara ya mwisho alikuwa bendi ya Msondo Group. Mungu Amlaze pema peponi.(Picha kwa hisani ya ya www.issamichuzi.blogspot.com)

Friday, February 26, 2010

Wana Bantu Ngoma wanakula miziki

Bantu Group chini ya Komandoo Hamza Kalala imekwisha toa wakali wengi katika anga la muziki hapa Tanzania. Komandoo mwenyewe ana historia ndefu ikiwemo ya kuwa moja wa waanzilishi wa Bendi ya Vijana chini ya mkongwe John Ondolo Chacha. Amekwishapitia bendi kama Matimila na kushiriki vibao vikali kama Alimasi, amepitia UDA na ikawa katika anga za juu kimuziki Tanzania wakati wake. Komandoo hatasahauliwa na vibao alivyopiga Vijana kama Mary Maria , mpini wake wakati wa Pambamoto Awamu ya pili haujarudiwa tena. Kibao chake Nimekusamehe lakini sitakusahau cha Washirika Stars ni picha tosha ya kazi za Hamza. Pichani ni Juni 1, mwaka 1996. Kwenye onyesho kubwa la Siku ya Mazingira ambalo ndilo lilikuwa onyesho la kwanza la muziki 'live' kuonyeshwa na ITV. Na lilirushwa kwa muda wa masaa kama 6 wananchi wakipiga simu lilendelee hewani!!!!. Wasanii kama MR2 walipata umaarufu mkubwa baada ya tamasha hili pale Mnazi Mmoja. Tamasha liliendeshwa na CHAMUDATA chini ya Mwenyekiti John Kitime.
Picha ya chini tunamwona watatu toka kushoto Eddy Sheggy, na mwishoni ni Rogart Hegga ambaye kwa sasa yuko Twanga Pepeta.

Vumbi





Kwa wapenzi wa Maquis Original jina la "Vumbi" ni la kutia kumbukumbu nyingi sana, na kwa wale ambao wamekuwa wakiusikia ule wimbo wa Chatanda Ngalula walisikia tena na tena Tchimanga Assossa akilitaja jina hilo wakati Vumbi anacharaza gitaa tamu la solo kwenye wimbo huo. Vumbi kwa sasa anaendelea na muziki huko Sweden na maelezo ya maisha yake kimuziki ni haya. Jina lake kamili ni Alain Kahanga Dekula , alizaliwa katika jimbo la Kivu katika Jamhuri ya Kongo. Baada ya kumaliza High School alianza kupiga gitaa katika bendi ya Bavy National iliyokuweko Uvira Kusini mwa Kivu. Baadae akiwa na kaka yake Rachid King wakajiunga katika bendi ya Grand's Mike Jazz Band wakati huo ikiwa na wanamuziki kama Remmy Ongala,Kasaloo Kyanga,na Kawele Mutimanwa. Akaja Tanzania na kujiunga na Orch.Maquis Original na kati ya nyimbo ambazo anajulikana nazo sana ni Ngalula and Makumbele.Wakiwa na mtindo wa Zembwela-Sendema,alikuwa jukwaa moja na miamba wa magitaa wakati huo akina Nguza Viking "Big Sound" na marehemu Ilunga Lubaba. Vumbi kwa sasa yuko Sweden akiwa na yule mwanamuziki maarufu toka Uganda Sammy Kasule wakiwa na bendi ya Ba makonde wamekwisha toa album CD mbili- Bamakonde na Asante. Akiwa na bendi ya kaka yake Rachid King Orch Grand’s Mike wametoa album ya CD Bolingo Ekeseni


Monday, February 22, 2010

Historia fupi ya muziki wa dansi

Ukitaka kuongea muziki wa dansi uliingiaje nchini ni muhimu kujua historia ya mji wa Tanga. Tanga ndipo muziki wa dansi ulipoingilia nchini. Wajerumani waliusambaratisha mji wa Tanga kwa mizinga kati mwaka 1888 na 89. Na baada ya hapo kuujenga upya kwa kufuata mpangilio uliosababisha Tanga kuwa na mitaa maarufu kama barabara ya kwanza ya pili na kuendelea. Wajerumani walianzisha shule ya kwanza ya serikali Tanga 1892 na hapohapo wakanzisha bendi ya shule ya kwanza, pamoja na kuwa Wajerumani hawakutawala muda mrefu baada ya hapo lakini Waingereza waliiendeleza sana bendi hiyo iliyokuwa ikipiga aina mbalimbali za muziki wa kigeni. Dansi ilianza kwanza kama klabu ambapo watu walialikana kuja kucheza aina mbalimbali za muziki wa kizungu mtindo maarufu unaojulikana kama ballroom dancing. Aina hizi za klabu zilianzia Mombasa na kuingia nchini kupitia Tanga na kisha kuletwa Dar Es Salaam na klab iliyokuwa maarufu Tanga iliyoitwa Tanga Young Comrades Club, klabu nyingine ilianzishwa ikaitwa New Generation Club ambayo ilianzisha matawi miji mbalimbali. Klabu hizi ndizo zilizozaa bendi za dansi. Inaonekana Dar Es Salaam ndio ilikuwa ya kwanza kuwa na bendi yake African Association Jazz Band, ambapo wanamuziki wengine waliihama na kuanzisha Dar Es Salaam Jazz Band, hiki kilikuwa kipindi kati ya miaka 1930 na 1940, kwenye 1950 kulikuwa na bendi maarufu Bagamoyo iliyoitwa Lucky Star jazz band ambayo ilikuwa na urafiki na Dar Jazz. Baada ya hapo kulianza bendi ambazo wanamuziki na wanachama wake walipatikana kutokana na wanakotoka, kulikuweko na Ulanga Jazz band ya Wapogolo, Rufiji Jazz Band iliyoanzishwa na Wandengeleko, Western Jazz iliyoanzishwa kwanza na Wanyamwezi. Bendi zote hizi baadae zilikuja kuwa na wanachama mchanganyiko bila kujali uzawa. Na kulikuweko na Skokian Jazz Band hii ilikuwa ni bendi na klabu ya watu mchanganyiko. Mwaka 1958 wanamuziki kutoka Kilwa walianzisha Kilwa Jazz Band wanamuziki hawa walitoka bendi iliyoitwa Tanganyika Jazz. Ilipofika 1966 bendi ilikuwa na wanamuziki takribani 26, 15 wakiwa Kilwa A na 11 Kilwa B. Zamani bendi zilikuwa na mtindo wa kuwa na bendi B ambayo ni ya Vijana. Patrick Balisdya aliwahi kuwa Dar Jazz B. Kilwa Jazz ilikuwa na wanachama kama 50 wengine wakiwa viongozi wa juu serikalini. Waliolipa ada ya uanachama na hivyo kuweza kuingia madansi ya bendi bila kulipa. Wakati huo makao makuu ya Kilwa Jazz yalikuwa katika ukumbi ambao kwa sasa unaitwa Kwa Madobi maeneo yaa Jangwani…itaendelea.

Friday, February 19, 2010

Jerry Nashon aka Dudumizi


Nimeweza kumpata mtu ambae ndiye aliyemlea Jerry Nashon kimuziki na haya ndo aliyoniambia kuhusu Jerry. Nae si mwingine bali ni Bwana Ruyembe ambae kwa sasa ni kiongozi pale Baraza la Sanaa la Taifa

Jerry alikulia Musoma Mjini kijiji kiitwacho Kigera kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Musoma jirani na shule ya Sekondari Mara. Nilikutana naye mara ya kwanza akiwa Musoma Catholic Mission club ambayo leo ni Mwembeni secondary School akiwa anajifunza kupiga gitaa. Alikuwa ana mazoea ya kwenda kwenye hiyo social club ya kanisa iliyowaunganisha vijana wanamichezo mbalimbali. Nilimchukua katika Bendi yangu niliyokuwa nimeiunda muda huo 1980s ikiitwa Special Baruti Band. Nilimuunganisha na Mpiga rhythm wangu akiitwa Charles Koya ambaye hivi sasa anapiga na Bendi ya Mwanza Hotel (solo guitar), ili amwendeleze na akiwa pia mwana Bendi wetu. Alikuwa mwanafunzi mzuri alikuwa na bidii na akaweza baada ya muda mfupi kupiga programu yetu kubwa! Mimi nilikuwa mtunzi na mwimbaji licha ya kumiliki Bendi hiyo. Tulirekodi naye mara ya kwanza TFC pia RTD na baadaye tulirekodi Kenya katika studios mbalimbali na producers mbalimbali na tumepiga muziki clubs mbalimbali Nairobi ikiwa kama vile Bombax Hotel, Kaka Night Club, Rwadhia Night Club na nje ya Jiji katika mikoa takribani yote ya Kenya kasoro Mombasa na Kisumu! Hapa tulishirikiana na mwanamuziki hodari Joseph Kamaru. Muda huo yeye akipiga gitaa la rythm na Bendi yetu wakisaidiana na Koya. Jerry alivutiwa na uimbaji pia utunzi baada ya kuona nafasi niliyokuwa nayo na umaarufu nilioupata enzi hizo Nairobi. Alijifunza nikampa mwanga na kipaji chake kikajitokeza katika kuimba na utunzi pia!.Hatimaye Jeshi la Magereza Musoma walimchukua kwa nia ya kumleta Dar ajiunge na Bendi yao ya Magereza. Alipitia mafunzo na aliondoka baada ya kuwa na Special Baruti kwa miaka miwili na nusu hivi au mitatu. Muda huo Musoma kulikuwa na Musoma Jazz Band(segese) ambayo mimi na wanamuziki wengi wa Special Baruti tulipigia baadaye tukahama na kuiacha hali mbaya! Ilikuwepo pia Mara Jazz Band(Sensera) hizi ndizo zilikuwa Band maarufu mjini hapo wakati huo. Aidha ilikuwapo bendi iliyomilikiwa na Parokia ya Catholic Mission Makoko Seminary ikiitwa Juja Jazz Band lakini ilikuwa ndogo sana na haikuwa kwa misingi ya kibiashara zaidi!. jerry Baadae alijiunga na Bima Orchestra na kisha Vijana Jazz mpaka mauti yake.


Thursday, February 18, 2010

Wednesday, February 17, 2010

Wanamuziki wanawake



Muziki wa dansi uliweza kupambwa na wanawake wengi waliopata sana umaarufu kutokana na umahiri wao enzi hizo. Wanamuziki wa dansi wanawake walichelewa sana kukubalika kwa wanamuziki wanaume tofauti na ilivyokuwa kwenye muziki wa aina nyingine kama taarab, na kwaya. Lakini wengi walijitokeza na kuzoa umaaruf mkubwa labda niwataje wachache na baadhi ya nyimbo zilizowapa umaarufu. Nianze na mama lao Tabia Mwanjelwa, huyu dada wa kinyakyusa alikuwa na sauti nzito ya kukwaruza lakini akiimba mwili utakusisimka. Pamoja na kuwa alikuwa akipanda katika majukwaa ya bendi mbalimbali ni bendi ya Maquis ndiyo iliyofanya hatua ya ziada na kumruhusu arekodi jambo ambalo lilikuwa gumu kwa wanawake katika bendi kabla ya hapo, wimbo uliompa umaaruf sana ni Jane..Jane mi nahangaika juu yako kwa maisha yako..... Pichani Tabia Mwanjelwa akiwa na gitaa, unaweza kupata mengineyo na kuwasiliana nae kupitia
Rahma Shally mwimbaji mwingine mahiri aliyepitia bendi nyingi na kurekodi kwanza na Mwenge Jazz nyimbo nyingi tu maarufu, akapitia MK Group Ngulupa tupa tupa akasikika katika kibao kile Jua asubuhi lapendeza, Sambulumaa akarekodi Sitaki sitaki visa vyako, akatua Vijana Jazz na kurekodi wimbo Sadi Badili mawazo. Alikuwa mwanamama shupavu jukwaani. Nana Njige binti mzuri aliyepitia Orchestra Mambo Bado ambapo alitamba na ule wimbo Lilikuwa jambo dogo tu, akapitia bendi kadhaa ikiwemo Vijana jazz , Tancut Almasi, Legho Stars. Bibie Emma Mkello ambaye hukumbukwa katika ule wimbo alioimba akiwa na Eddy Sheggy wakiwa Super Rainbow..Milima ya kwetu. Kida Waziri akionekana hapa katika picha aliopiga 1991 kwenye ukumbi wa Vijana Kinondoni, kwa sasa yuko Arusha atakumbukwa kwa nyimbo kama Shingo Feni,Penzi Haligawanyiki na Wifi Zangu ambazo zote alirekodi akiwa Vijana Jazz. Pia alipitia kundi la Roots and Culture lililoongozwa na Jah Kimbuteh.
Wapenzi wa Maquis watamkumbuka Rose Mwape ambae nae aliimbia Maquis kwa muda mrefu baada ya kuondoka Tabia Mwanjelwa.Jemsina Msuya pia alikuwa kati ya magwiji alikuwa Legho na akarekodi na Assossa nyimbo ya Mzazi mwenzangu. Wako wengine kama Karola Kinasha ambao bado wako katika muziki. Karola yuko Shada, Ana Mwaole yuko na Mzee King Kiki, Nuru Mhina baada ya kuondoka Police Jazz ametua Vijana Jazz mpaka leo. Nyota Waziri ambaye baada ya kuondoka Bicco Stars ametua Kilimanjaro Band akiwa bado na heshima yake katika wimbo Tupendane na Gere. Ni muhimu kumgusia Asia Darwesh ambay licha ya kuimba alikuwa pia mpiga Keyboards mahiri sana kama alivyoonyesha katika nyimbo alizorekodi MK Group na bendi yake Zanzibar Sounds. Nakaribisha kumbukumbu nyingine

Vijana Jazz Vs Maquis

Katika kipindi cha mwisho cha miaka ya 80, Kinondoni ilkuwa inawaka moto kwa Vijana siku ya Jumapili. Lang'ata ambayo baadae ilikuja kuwa Club ASET na sasa kanisa, palikuwa ndo ukumbi wa Dansi za kuanzia mchana kwa Bendi ya Maquis. Ukija hapa mbele Vijana Jazz Pambamoto awamu ya pili chini ya uongozi wa Hemed Maneti walikuwa nao kila Jumapili mchana wanaporomosha Dansi, na siku hiyo ilipewa jina Vijana Day. Kwa kweli Maquis walikuwa wanajaa watu na Vijana wanajaa watu. Kulikuweko na wapenzi wa kudumu wa Vijana kama ilivyokuwa Maquis. Wakati huo nyimbo kama Ngalula, Makumbele zilikuwa zinalia Lang'ata huku Vijana wanateremsha Shingo feni, Ngapulila, Azda. Ushindani huu ulilazimisha bendi kujitahidi kupiga vizuri na kwa displine au la wapenzi wanahamia bendi jirani. Kuna wakati Vijana Jazz walikuwa wanaanza muziki saa kumi na moja jioni na kupumzika saa tatu na nusu usiku kisha kumaliza dansi saa nne. Maquis wakawa wanaanza saa kumi na kumaliza saa tano usiku. Na wakaanza kuruhusu mtu yeyote atakayekuwa kapigwa muhuri wa kuruhusu kutoka nje ya ukumbi Vijana Jazz,aliruhusiwa kuingia Maquis bure. Vijana wakabadili ratiba na kuanza kupiga saa 9 mchana, kwa mtindo wa bandika bandua, yaani muziki nonstop. Na kufuta kupumzika hadi saa tano. Hiyo ndo ilikuwa raha kwa wapenzi. Vijana haikuwa na show wakati wa Maneti, Lakini show ilikuja baadae katika kukabili show ya Maquis ambayo ilikuwq nzuri sana chini ya mwalimu wao Wabangoi. Majina makubwa yalitawala madansi hayo Maquis kulikuwa na Dekula Vumbi kwenye solo,second solo Mbwana Cox (aliyetoka Vijana Jazz), banza Mchafu Bass, Nguza Viking, Adios, Tshimanga Assossa,Parashi Lukumbule Vijana Jazz kulikwa Shaaban Wanted, Hemed Maneti, Eddy Sheggy, Adam Bakari, Kida Waziri, Abou Semhando, Rashid Pembe na wengine wengi, basi raha kila jumapili ilikuwa kama tamasha

Kati ya Bendi ambazo Mzee J Mwendapole aliziendesha kwa muda mrefu ni Afriso ngoma. Hiyo ilikuwa bendi yake, ikawa na wanamuziki kama Maida na Belly Kankonde, iliweza kurekodi nyimbo kadhaa, lakini bendi hii iliongezeka umaarufu alipoingia marehemu Lovy Longomba, wakati huo akiwa na akina Kinguti system, Anania Ngoliga, Toffy Mvambe, Salim Shaaban Malik Nduka Masengo(Maliky Star) hao wakiwa waimbaji, Solo Gitaa- John Maida, Peter Kazadi, Robert Tumaini Mabrish, Rythm- Mjusi Shemboza, Bass-George na Kasongo, Drum -Ayub Karume, Abdul, Tumba- Magoma Sony, Trumpet-Juma Urungu, Ramadhani, Mbaraka Othman. wengi kati niliowataja wametangulia mbele ya haki. Baada ya hapo aliwahi pia kuwa na bendi ambayo ilikuwa na wanamuziki kadhaa kutoka sikinde ikawa inaitwa Sikinde Academia, ambayo haikudumu sana. Baada ya hapo amekuwa msaada mkubwa wa kuwasaidia wanamuziki wengi vyombo wakati wananzisha bendi zao.
Pichani ni Marehemu Lovy Longomba

Tuesday, February 16, 2010

Kwa heri Juma Mwendapole

Kwa masikitiko makubwa nimepata taarifa ya kifo cha mdau muhimu wa muziki wa dansi Juma Mwendapole. Amefariki Ijumaa tarehe 12 February 2010 na kuzikwa kesho yake. Mwendapole ndiye aliyekuwa mmiliki wa Bendi ya Afriso Ngoma iliyokuwa na wanamuziki maarufu kama Lovy Longomba. Kwa miaka ya karibuni wanamuziki wengi wamekuwa wakimtegemea kwa kukodi vyombo vya muziki toka kwake. Bendi nyingi zisingekuweko kama si msaada wa Juma Mwendapole.
Mungu Amlaze pema peponi Amin

Saturday, February 13, 2010

Historia za mfumo wa Bendi

Utaratibu wa bendi hapa nchini ulifuata sana utaratibu wa bendi za nje kutokana na muziki wa bendi kuwa ni wa mapokeo. Hapa naongelea aina ya vyombo vilivyotumika stejini. Katika rekodi za kwanza zaidi za bendi kama vile zile za Cuban Marimba bendi zilipiga bila chombo chochote kilichotumia umeme kwa kuiga staili ya Cuba, na pia teknolojiaa ya vifaa vya umeme ilikuwa bado kuingia. Hivyo kulikuwa na gitaa moja na ngoma za kizungu (drums), bongoz, na vyombo vya kupuliza, filimbi, trumpet, saxaphone. Nyimbo za zamani za Salum Abdallah na Dar es Salaam Jazz Band zinatoa picha za vyombo hivyo. Mwanzoni mwa miaka ya 60, vifaa vya umeme vilianza kutumika na bendi kwa kawaida zilikuwa na Gitaa la bezi, rithim na solo,tarumbeta na saksafon. Halafu kulikuwa na bongoz. Baadae tumba zilichukua nafasi ya bongoz. Baadae bendi ziliingiza gitaa jingine ambalo liliitwa second solo. Hili lilikuwa gitaa ambalo lilipigwa katikati ya rithm na solo. Cuban Marimba katika kipindi fulani cha Mzee Kilaza aliweza kuongeza gitaa jingine waliloliita chord gitaa.
Kuingia kwa vinanda kuliliondoa gitaa la second solo katika bendi, japo kwenye bendi kama Tancut almasi na Vijana Jazz gitaa hilo liliendelea sambamba na kinanda. Kinanda pia kikachukua nafasi ya tarumbeta na saxaphone katika bendi nyingi. Kwa bendi zile ambazo zilikuwa zikifuata muziki wa magharibi mpangilio wao haukuwa na mfumo maalumu kutokana nani aina gani ya muziki wanafuatia. Mpaka sasa bendi kama The Kilimanjaro kwa kawaida hupiga gitaa moja,vinanda vitatu, gitaa la bezi, drums na conga au maarufu tumba. Wakati bendi kama Shada ni wana kinanda magitaa mawili na ngoma ya kiasili. Tatizo kubwa sana sasa ni bendi zinaigana katika mfumo katika kila kitu ubunifu ziro. Franko Makiadi aliondoka kwenye mfumo wa second solo akawa na solo gitaa 2, yeye mwenyewe akipiga solo na akawa na mpiga solo mwingine katika wimbo uleule. Ni wakati sasa wanamuziki kuangalia nyuma na kuona ni nini wanaweza kujifunza kitakachofanya muziki wao uwe tofauti na wa wengine.

Friday, February 12, 2010


Mwaka 1982/83 Tchimanga Kalala Assossa alianzisha na kuongoza bendi iliyoweza kutia changa moto katika ulimwengu wa muziki wakati huo. Bendi hiyo iliitwa Orchestra Mambo Bado na mtindo wake wa Bomoa Tutajenga Kesho. Wanamuziki katika bendi hiyo walikuwa Tchimanga Assossa, Kiongozi na muimbaji, Kazembe wa Kazembe mpiga solo (pamoja na jina hilo alikuwa Msukuma), William Maselenge, rythm guitar, Huluka Uvuruge second solo guitar, Sadi Mnala drums, Mzee Albert Milonge second solo, Lucas Faustin muimbaji, John Kitime muimbaji na rythm guitar, George Mzee muimbaji, Athuman Cholilo muimbaji, Likisi Matola Bass na keyboards, Jenipher Ndesile muimbaji, selemani Nyanga Drums. Album ya kwanza ya bendi hii ilikuwa na nyimbo zilizotamba kama vile Kutokuelewana, Bomoa Tutajenga Kesho , hii ilipigwa marufuku. Picha ya Assossa iliyotoka kwenye tangazo la kwanza la bendi, hapa akiwa amevaa shati la ndege ambalo kwa siku hizo walikuwa wanavaa wajanja tu.

Thursday, February 11, 2010

Hemed Maneti


Hemed Maneti mwanamuziki muimbaji aliyetokea Cuban Marimba na kutua Vijana Jazz mpaka kifo chake. Wimbo wa mwisho aliyorekodi uliitwa Nelson Mandela uliyotungwa na John Kitime. Wimbo huo ulitungwa ili kupigwa radioni wakati Mzee Mandela alipokuwa anatembelea Tanzania mara baada ya kuachiwa toka gerezani. Hakupanda tena jukwaani baada ya kurekodi wimbo huo.

Tuesday, February 9, 2010

Muziki wa soul

Kila zama na vitabu vyake ni msemo unaoeleza kuhusu mambo ambayo hutokea katika kipindi fulani. Kila wakati kuna kizazi kipya, jambo ambalo kila kiza kipya kilichopo hudhani wao ndo wa kwanza. Katika miaka ya sitini kulikuwa na kizazi kipya cha wakati huo na moja ya muziki uliopendwa na kupigwa na vijana wakati huo ni muziki aina ya soul. Vijana walivaa kama wanamuziki wa soul wa wakati huo, walipiga muziki wao na bendi zilijipa majina ya bendi za soul. Ntataja baadhi ya wanamuziki ambao walipendwa na vijana wakati huo, najua kizazi kipya wa enzi hizo watakuwa na mengi ya kusema.

OTIS REDDING alileta raha kwa vibao kama Mr Pitiful, Fa-fa-fa-fa ambao Papa Wemba aliuimba tena miaka michache iliyopita. Sitting on the dock of the Bay, Respect, na wimbo ambao kila bendi ya soul iliupiga Direct Me. Otis alifariki katika ajali ya ndege ya kukodi na wanamuziki wenzake wane wa kundi lake la Barkays


Wilson Pickett alizaliwa March 18 1941, na kufariki kwa ugonjwa wa moyo Alhamisi 19 January 2006 alipendwa na nyimbo zake kama In the Midnight Hour, Don’t Fight It, Ninety-Nine and a Half (Won’t Do), She’s So Good to Me, Land of a 1,000 Dances,
Mustang Sally, na Funky Broadway nakuigwa sana na bendi za vijana wakati ule

James Brown huyu alikuwa ni mzee wao, alipewa majina mbalimbali kama Soul Brother Number One, the Godfather of Soul, the Hardest Working Man in Show Business, Mr. Dynamite, the Original Disco Man. Na mzee huyu ndo alikuwa kinara wa soul music miaka ya sitini, alikuwa mwanzilishi wa funk katika miaka ya 70, na alitoa mchango katika rap music miaka ya themanini. Pia alijua kucheza, Michael Jackson alikiri kuwa ile moonwalk aliipata toka kwa James Brown. JB alikuwa na nyimbo nyingi sana nitaje chache tu, The Popcorn, Mother Popcorn, Papas got a brand new bag, I am black and proud, Sex machine, James alifariki 25 Disemba 2006. Muhimu kutaja kundi lake the Famous Flames aliloanza nalo toka 1955.

Clarence Carter mwimbaji kipofu ambaye aliwakamata vijana kwa nyimbo kama too weak to fight, getting the bills ,slip away, patches

Aretha Franklin- mwanamke wa shoka huyu alipendwa sana kwa nyimbo zake kama respect, save me na think,

Sunday, February 7, 2010

Wanamuziki kutoka Kongo


Huwezi kuongea kuhusu muziki wa bendi Tanzania bila kutaja wanamuziki kutoka Kongo. Kuna sababu kadha wa kadha. Kwanza historia. 1945 kwa sababu za kipropaganda Wamarikani walianzisha kituo cha radio kikubwa katika mji unaoitwa sasa Kinshasa hii iliwezesha muziki wa Wakongo kusikika katika eneo kubwa la Afrika ya kati na mashariki, 1947 ndugu wawili wa Kigiriki walianzisha record company katika mji unaoitwa sasa Kinshasa na santuri za wanamuziki kama Wendo Kolosay na nyimbo kama Akili ya bibi sawasawa mtoto mdogo zilisambazwa chini ya label ya Ngoma na Loningisa na kusambaa sana nchini kwetu, mambo haya mawili yaliweza kuusambaza muziki wa Kikongo katika maeneo yaliyoizunguka na kufanya wanamuziki kuanza kuiga mipigo ya Wakongo. Vita ya wenyewe kwa wenyewe ilianzisha kuhama kwa wanamuziki kutoka Kongo na kuja Afrika Mashariki. Kati ya wanamuziki wa kwanza kuja huku ni Paschal Onema. Lakini baada ya hapo zilikuja Bendi nyingi. Nakumbuka Super Bocca na wimbo wao Suzana mwana Tanzanie, Maquiz du Zaire, Fauvette haya jamani karibu tuendelee .........Pichani ni Mzee Makassy mara tu baada ya kuingia nchini kutoka Uganda

Enzi za Buggy

Katika miaka ya 60 hadi katikati ya 70 kulikuwa na bendi nyingi za vijana ambazo unaweza kulinganisha na wanamuziki wa sasa wanaojulikana kama kizazi kipya. Katika jiji la Dar es Salaam, kulikuweko na bendi nyingi kama vile The Sparks, The Comets, The Flames, The Jets, Crimson Rage, The Lovebugs, Trippers Imagination, Safari Trippers, Afro 70. je unakumbuka nyingine ?

Bendi Zetu

Tanzania tuna bahati mbaya ya kutokuweka kumbukumbu nyingi sana. Kati ya hizo ni kumbukumbu za bendi gani au vikundi gani vya muziki viliwahi kuweko. Labda tusaidiane kila mmoja wetu ajaribu kukumbuka ni kikundi gani kilikuweko wilayani kwake nianzae na mifano michache
******
Iringa-
Highland Stars
Tancut Almasi Orchestra
Chikwala chikwala
Ruaha International
Vico Stars
Mkwawa Orchestra
******

Morogoro
La Paloma Jazz
Cuban Marimba
Morogoro Jazz
Les Cubano
Vina vina Orchestra
******

Ifakara
Sukari Jazz
Kilombelo Jazz
Malinyi Jazz
Kwiro Jazz
Mahenge Jazz
******

Tanga
New Star Jazz
Jamuhuri Jazz
Atomic Jazz
Tanga International
Amboni Jazz
******

Tabora
Tabora Jazz
Nyanyembe Jazz
Kiko Kids haya tuendelee
******

Mwanza
Orchestra Super Veya
******

Moshi
Orchestra Zaire Success
Bana Africa Kituli
********

Mpwapwa
Mpwapwa Jazz
******

Dodoma Jazz
Dodoma International
Materu Stars
Saki Band
Super Melody
*****

Songea
Tembo Jazz
Orchestra Sere sere
******

Lindi
Mitonga Jazz
******

Masasi
Kochoko Jazz

Saturday, February 6, 2010

Mzee Humplick aliwahi kupigwa marufuku

Je unajua kuwa Mzee Frank Humplick ambaye ndiye mtunzi wa nyimbo kama Chaupele Mpenzi, Embe dodo imelala mchangani, aliwahi kutunga nyimbo iliyopigwa marufuku na kusakwa nyumba hadi nyumba ili kusibakie hata nakala ya wimbo huo? Maneno ya wimbo huo yalisema hivi:
Uganda
nayo iende

Tanganyika ikichangaruka, Kenya na Nyasa zitaumana

Nasikia fununu wanavyoichanachana China, Kitisho!

I am a democrat, I don't want communism, English, Yes, No I don't know, Kizungu sikijui

Wanyika msishindane na Watanganyika

Wimbo huo ukaanza kutumika kabla ya mikutano ya Mwalimu Nyerere na kuanza kuwa maarufu kama wimbo wa kudai uhuru, wakoloni haraka sana wakaona wimbo huu utaweza kusababisha vurugu kama ambazo zilikuwa zinaendelea Kenya chini ya Maumau. Serikali ikaupiga marufuku na kuanza kuusaka nyumba hadi nyumba

Friday, February 5, 2010

Young Audiences Music Award

2 February 2010, Jeunesses Musicales International (JMI) launches a call for nominations for the Young Audiences Music Award 2010, an international prize that will celebrate top musical productions for children and youth.

"Looking at the quality of productions presented in schools and within education and audience development programs today, it's obvious that a new standard has been set" said JMI Secretary General Blasko Smilevski "What we see are productions nothing short of spectacular - in terms of artistry but also in terms of message. The once common ‘What instrument is this? lesson' is being fast replaced by subtle teachings on social, environmental, and intercultural issues through music."

Do you know a young audiences production with impact? Visit the all-new www.yama-award.com to apply today! Deadline for submissions is May 1st 2010, thereafter an international panel of experts will select 5 finalists to be presented online and open for public vote. The best productions, one selected by the expert panel and the other by public vote, will win €2,500 each, towards a future production for young people and children. The winners will be revealed at the Young Audiences Music Award ceremony to take place in Skanderborg, Denmark in October 2010.

The Young Audiences Music Award aims to identify and support cutting-edge productions that impact young people with both social and artistic value, targeting and engaging vulnerable/at-risk groups of youth from marginalized communities and deprived areas, addressing issues of vital concern (eg. violence, poverty, discrimination, abuse, HIV/AIDS) and that use music as a tool to promote intercultural dialogue and understanding. All of JMI's work with young audiences is based on the underlying principal that all children and youth should receive access to music/culture as a fundamental human right. Thus, although in many nations we now celebrate an improvement in the music programs of education institutions, the YAMA serves as a beacon of hope to those still facing less than desirable circumstances, to continue the fight for this crucial sector of human development.

YAMA is a JMI Young Audiences Working Group Initiative

More info:

Matt Clark
Communications Officer
Jeunesses Musicales International
matt@jmi.net

T. +32 2 513 97 74

Jeunesses Musicales International (JMI) is the world's largest youth-music NGO. With a mission "to enable young people to develop through music across all boundaries," JMI reaches over 5 million young people aged 13-30 annually through 36,000 activities and is the leading organization in the field of young audiences.


Thursday, February 4, 2010

Mara nyingine mtu unaweza kuanza kupata picha kama vile wanamuziki wako Dar es Salaam tu, jambo ambalo si kweli. Japo ukweli ni kuwa zamani kulikuweko na Bendi karibu kila wilaya nchini. Hapa ni bendi 2 kutoka Dodoma. Super Melody na Saki Stars.
Mwenye gitaa na jaketi la rangi mbili ni Mzee Ikunji, huyu pamoja na kupigia bendi kama Tabora Jazz pia alikuweko Tancut Almasi Orchestra na ndie aliyepiga second solo kwenye nyimbo kama Masafa Marefu, Nimemkaribisha nyoka, na Kashasha

Hii ni Bendi inayoitwa Karafuu Band,moja ya bendi kadha wa kadha zilizo na masikani Zanzibar. Mwenye miwani ya jua ndio kiongozi wa bendi anaitwa Anania Ngoliga, ni mwanamuziki mwenye ulemavu wa macho lakini kati ya wanamuziki mahiri Tanzania. Anania ambaye kwa wakati huu yuko Marekani katika tour ambayo anasindikizana na mwanamuziki Bela Fleck. Fleck amepata grammy awards 3 mwaka huu. Na katika album iliyopata awards kuna nyimbo 2 ambazo zimetungwa na Anania. Anania kisha kuwa mwanamuziki katika bendi ya Legho Stars, Afrisongoma, Tango Stars, Tacosode Band. Amesharekodi na wanamuziki wengi mahiri wakimataifa akiwemo Kriss Kristoffeson, na Zapmama


Hapa kuna wakubwa wawili katika ulimwengu wa soka, Sylersaid Mziray, kocha anaeheshimika sana, na Mzee Hassan Dalali mwenyekiti wa Simba Sports Club enzi hizo akiwa Kiongozi na mpigaji solo wa bendi ya Vijana Jazz.Mziray alikuwa katembelea Kilimanjaro Band wananjenje.

Kati ya mwanamuziki Mtanzania ambae historia hajamtendewa haki kutokana na kutothaminiwa kwa kazi zake ni marehemu Mzee Frank Humprik. Mzee Humprik anaeonekana hapa katika picha ya rangi ameishi kwa miaka mingi ya mwisho wa maisha yake Lushoto. Mzee huyu akiwa na dada zake wawili walitikisa anga za muziki wa Afrika ya Mashariki, na bado wanaendelea kufanya hivyo japo hawatambuliwi kabisa. Kundi lao lililoitwa Frank na dada zake waliuletea ulimwengu nyimbo kama Embe dodo imelala mchangani, Kolokolola, Chaupele Mpenzi na nyingine nyingi ambazo bendi bado zinapiga nyimbo hizo mpaka leo na baadhi ya wanamuziki wamekuwa wanazirekodi bila hata kutaja mtunzi wa nyimbo hizo. Mbaya zaidi mara nyingi nyimbo hizo zimekuwa zikitambulishwa kama nyimbo za mwanamuziki mwingine kutoka Kenya marehemu Fundi Konde.
Mzee Fundi Konde ambae hapa chini yuko na mwanamuziki mwingine maarufu wa Kenya Fadhili William aliyeimba Malaika, ndiye aliyetuachia nyimbo kama Ajali haikingi, Mama Leli, Wekundu si hoja, Mombasa siendi tena na kadhalika

Mzee Frank Humprick


Kati ya mwanamuziki ambae hajatendewa haki kutokana na kutothaminiwa kwa kazi zake ni marehemu Mzee Frank Humprick. Mzee huyu akiwa na dada zake walitunga nyimbo nyingi sana ambazo mpaka leo zinapigwa majukwaani na karibu kila bendi Afrika mashariki. Bendi nyingine zimediriki kurekodi upya nyimbo hizo tena bila hata kumtaarifu Mzee huyu au nduguze. Baya zaidi ni nyimbo zake nyingi kutambulishwa kuwa ni za Fundi Konde. Nyimbo zake kama Embe dodo imelala mchangani, Chaupele mpenzi,I am a democrat(uliopigwa marufuku wakati wa mkoloni),Kolokolola na nyingine nyingi. Mzee huyu Mtanzania aliyekuwa akiishi Lushoto mpaka kifo chake anastahili kuenziwa na wapenzi wote wa muziki Tanzania.

John Mwenda Bosco,ni kati ya wanamuziki ambao w alileta mabadiliko mengi katika muziki wa Afrika ya Mashariki. Muziki wake unapendwa sana mpaka leo. Je unajua alikuwa nani?

Peter Colmore ambaye alifanya kazi kwa karibu sana na Mzee Ally Sykes ambaye kwa bahati mbaya hajatunukiwa nafasi anayostahili katika historia ya muziki wa Tanzania ndie aliye mleta John Mwenda Bosco Afrika ya Mashariki. Bosco alitambulishwa kwa Colmore kupitia Edward Masengo,mwanamuziki mwingine toka Kongo ambae alikuwa maarufu sana na hasa kutokana na matangazo ya biashara yaliyokuwa yanafanywa na kampuni ya Colmore na Mzee Sykes, Colmore akalazimika kumfuata Bosco hadi Congo ambapo serikali ya Kibergiji wakati huo ilimlazimisha alipe Faranga 30,000 kama pesa ya kuhakikisha atamrudisha Bosco kwao. Bosco alikuwa tayari anajulikana sana Afrika ya Mashariki kupitia santuri zake. Kati ya nyimbo maarufu za Bosco ni ule wimbo wa ala tupu ambao hutumika na Radio Tanzania kuashiria kuanza kwa kipindi cha zilipendwa.

Taarab
Muziki wa Taarab unautata wa vyanzo viwili. Kuna wanaosema taarab iliingia nchini mwetu kupitia ikitokea Mombasa. Kuna tafiti nyingine ambazo zinaonyesha Sultan Barghash wa Zanzibar aliwapeleka wanamuzikiwawili Misri kujifunza upigaji wa Taarab,na hao waliporudi ndo walipanda mbegu ya Taarab nchini mwetu. Taarab imekuwa nahistoria ambayo ya kuwa na aina nyingi za taarab, na mpaka leo mabadiliko ya taarab yanaendelea. Imefikia sasa kuna hata vikundi vya taarab vina wacheza show. Taarab imekuwa pia ni ya kucheza na si kusikiliza ujumbe tu kama ilivyokuwa zamani

Wednesday, February 3, 2010

Extra Bongo ya Ally Choky kazini







Vijana Jazz Band wakisubiri kupiga muziki katika siku ya kumpokea Mzee Nelson Mandela mara baada ya kuachiwa kifungoni, hapa wakiwa stadium Morogoro. Toka kushoto waliosimama John Kitime kwa sasa yupo Kilimanjaro Band, Marehemu Agrey Ndumbalo, Mhasibu wa Bendi, Abou Semhando yupo African Stars (Twanga Pepeta),Marehemu Fred Benjamin, Said Mnyupe yuko Msondo,Said Mohamed Ndula, Rashid Pembe anendelea na muziki Mak Band, Hassan Show yupo Malasyia na Kinguti System wakipiga muziki huko. Waliokaa mpenzi wa bendi, marehemu Bakari Semhando, Juma Choka yupo sikinde.

Picha ya chini, Mohammed Gotagota, Freddy Benjamin,Mhando,Said Mohamed 'Ndula',Rashid Pembe,Aggrey Ndumbalo, hiyo ndo Vijana Jazz Saga Rhumba


Tancut Almasi Orchestra, bendi iliyokuwa namakazi yake Iringa kuanzia 1987, ilikuwa chini ya Kiwanda cha kuchonga almasi cha hapo Iringa, Diamond Cutting Company. Bahati mbaya wengi ni marehemu. Kutoka kushoto Buhero Bakari inasemekana ni mganga wa dawa za asili kwa sasa,marehemu Kyanga Songa, Kasaloo Kyanga yupo Dar anaendelea na muziki,Kabeya Badu, yuko na King Kiki na wazee sugu, Marehemu Kalala Mbwebwe, Abdul Mngatwa, yuko Iringa ameacha muziki, Akuliake Salehe aka King Maluu yupo Dar anaendelea na muziki

Tuesday, February 2, 2010

Hao si wengine bali ni wanamuziki wa The Revolutions, ambayo sasa inajulikana kama The Kilimanjaro Band aka Wananjenje. Pichani kutoka kushoto, Juma Omary(Drums/uimbaji),Mohammed Mrisho (Gitaa/uimbaji), Mabrouk Omary( Mwimbaji), Waziri Ally (Keyboards/ uimbaji), Marehemu Chuky,Keppy Kiombile(Bass /Uimbaji).Tangazo mojawapo la Kilimanjaro Band katika moja ya safari za Oman

UMUHIMU WA KULIPIA MATUMIZI YA MUZIKI

Ukitunga wimbo na ukiiweka katika hali ya kushikika mara hiyo unaanza kupata haki zote za wimbo hiyo. Wimbo ni mali itokananyo na ubunifu hivyo moja kwa moja unapata haki zinazostahili kutokana na mali hiyo na ni mali yako kama vile mali nyingine. Mara wimbo utakapokuwa tayari kutumika ni muhimu kusajili katika sehemu husika ili uweze kupata ulinzi na stahili zitakazopatikana kutokana na mali hiyo. Kuna haki za aina mbili, Performance Rights na Mechanical Rights.

Performance Rights ni zile haki zitokanazo na tungo ya muziki kutumika hadharani au kurushwa hewani. Hii inajumlisha pamoja na muziki kupigwa na Live Band na, au hata muziki uliokwisha rekodiwa kupigwa hadharani katika sehemu za hadhara kama restaurants, bar, klabu za usiku, kwenye maharusi, na kadhalika. Performance rights pia ni haki zinazoambatisha muziki kurushwa hewani kupitia radio na televisheni. Kutokana na kuweko kwa haki hizi, watu binafsi na makampuni ambayo yangependa kutumia kazi hizo ni lazima wapate ruksa kwa mwenye mali na hivyo mwenye wimbo kupata royalties kila wimbo wake unaporushwa hewani au kutumika hadharani.

Mechanical Rights ni zile haki zinazohusiana na kuweka tungo katika vinasa sauti kama vile kanda CD na DVD. Hivyo mtu au kampuni inapotaka kuweka kazi ya mtu katika kinasa sauti cha aina yoyote kutalazimika kuwepo na ruksa kutoka kwa mwenye mali au taasisi ambayo ina mamalaka ya Mechanical Rights za kazi hiyo. Watunzi hupata Mechanical Rights kwa nyimbo zinaposambazwa na wauzaji.

Ili kurahisisha ufuatiliaji na uratibu wa haki zilizotajwa hapo juu copyright collecting agency au copyright collecting society hutengenezwa ambapo aidha huwa ni chombo kilichobuniwa na watunzi au chombo kilichowekwa kisheria. Chombo hiki hupewa mamlaka na wanachama pia kutoa na kusimamia leseni mbalimbali kwa kazi walizozisajiri

Kwa hapa Tanzania Bara chombo ni COSOTA na Zanzibar COSOZA. Hivi ni vyombo vilichopewa mamlaka kisheria kushughulika kwa niaba ya watunzi kufuatilia haki zao, na kukusanya mafao yatokanayo na kazi hizo.

Ujio wa vinasa sauti bora na mtandao wa intanet unawezesha mamilioni ya watu kuweza kusikiliza wimbo kwa wakati mmoja katika maeneno mbalimbali ulimwenguni. Siyo siri kuwa matumizi kama ringtones ni biashara kubwa sana ambayo wasanii hawajapata manufaa stahili kutokana na mapato ya kazi zao.

Kuweko kwa taratibu za kukusanya mirabaha kuna wapatia fulsa wanamuziki wakongwe kuendelea kupata chochote na hata kutajirika japo nyimbo zao ni za zamani, napengine haziuziki tena. Mtunzi wa wimbo wa Red red wine alikwisha kata tama kimaisha uliporekodiwa upya wimbo huo ametajirika kutokana na wimbo huo.

Kuweko kwa vinasa sauti kumepunguza umuhimu wa kuweko kwa live music, hivyo malipo ya mirabaha inawezesha wanamuziki kupata mafao yao kwa kazi zao zilizotumika badala ya wao. Ni ukweli usiopingika kuwa kuna baadhi ya shughuli haziwezi kukamilika bila ya matumizi ya muziki. Kwa mfano biashara nyingi huongezea motisha kwa kupiga muziki. Mabaa, restaurant, magari ya kusafirisha abairia, na kadhalika. Haya ni matumizi makubwa tu ya muziki.

Shughuli mbali mbali za sherehe kama vile mikutano ya kisiasa, harusi birthday party hutawaliwa na muziki ambao matumizi yake huwa hayalipiwi kinyume kabisa cha haki za kimsingi za binadamu waliotunga nyimbo zinazotumika

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...