YOUTUBE PLAYLIST

Wednesday, February 17, 2010

Wanamuziki wanawake



Muziki wa dansi uliweza kupambwa na wanawake wengi waliopata sana umaarufu kutokana na umahiri wao enzi hizo. Wanamuziki wa dansi wanawake walichelewa sana kukubalika kwa wanamuziki wanaume tofauti na ilivyokuwa kwenye muziki wa aina nyingine kama taarab, na kwaya. Lakini wengi walijitokeza na kuzoa umaaruf mkubwa labda niwataje wachache na baadhi ya nyimbo zilizowapa umaarufu. Nianze na mama lao Tabia Mwanjelwa, huyu dada wa kinyakyusa alikuwa na sauti nzito ya kukwaruza lakini akiimba mwili utakusisimka. Pamoja na kuwa alikuwa akipanda katika majukwaa ya bendi mbalimbali ni bendi ya Maquis ndiyo iliyofanya hatua ya ziada na kumruhusu arekodi jambo ambalo lilikuwa gumu kwa wanawake katika bendi kabla ya hapo, wimbo uliompa umaaruf sana ni Jane..Jane mi nahangaika juu yako kwa maisha yako..... Pichani Tabia Mwanjelwa akiwa na gitaa, unaweza kupata mengineyo na kuwasiliana nae kupitia
Rahma Shally mwimbaji mwingine mahiri aliyepitia bendi nyingi na kurekodi kwanza na Mwenge Jazz nyimbo nyingi tu maarufu, akapitia MK Group Ngulupa tupa tupa akasikika katika kibao kile Jua asubuhi lapendeza, Sambulumaa akarekodi Sitaki sitaki visa vyako, akatua Vijana Jazz na kurekodi wimbo Sadi Badili mawazo. Alikuwa mwanamama shupavu jukwaani. Nana Njige binti mzuri aliyepitia Orchestra Mambo Bado ambapo alitamba na ule wimbo Lilikuwa jambo dogo tu, akapitia bendi kadhaa ikiwemo Vijana jazz , Tancut Almasi, Legho Stars. Bibie Emma Mkello ambaye hukumbukwa katika ule wimbo alioimba akiwa na Eddy Sheggy wakiwa Super Rainbow..Milima ya kwetu. Kida Waziri akionekana hapa katika picha aliopiga 1991 kwenye ukumbi wa Vijana Kinondoni, kwa sasa yuko Arusha atakumbukwa kwa nyimbo kama Shingo Feni,Penzi Haligawanyiki na Wifi Zangu ambazo zote alirekodi akiwa Vijana Jazz. Pia alipitia kundi la Roots and Culture lililoongozwa na Jah Kimbuteh.
Wapenzi wa Maquis watamkumbuka Rose Mwape ambae nae aliimbia Maquis kwa muda mrefu baada ya kuondoka Tabia Mwanjelwa.Jemsina Msuya pia alikuwa kati ya magwiji alikuwa Legho na akarekodi na Assossa nyimbo ya Mzazi mwenzangu. Wako wengine kama Karola Kinasha ambao bado wako katika muziki. Karola yuko Shada, Ana Mwaole yuko na Mzee King Kiki, Nuru Mhina baada ya kuondoka Police Jazz ametua Vijana Jazz mpaka leo. Nyota Waziri ambaye baada ya kuondoka Bicco Stars ametua Kilimanjaro Band akiwa bado na heshima yake katika wimbo Tupendane na Gere. Ni muhimu kumgusia Asia Darwesh ambay licha ya kuimba alikuwa pia mpiga Keyboards mahiri sana kama alivyoonyesha katika nyimbo alizorekodi MK Group na bendi yake Zanzibar Sounds. Nakaribisha kumbukumbu nyingine

16 comments:

  1. Hapa nafikiri umenikumbusha mbali sana Kitime, wimbo ambao alioimba Tabia mwanjelwa ninaoukumbuka una maneno yasemayo " kweli maisha ni safari ndefu ambayo haina mwisho, mwisho wake ni kifo" Hali kadhalika umenikumbusha mbali ulipomzungumzia Kida Waziri maana hata mimi nilikuwa shabaiki mkubwa wa Vijana jazz, wakati huo Kida alikuwa kwenye safu ya mbele ya Waimbaji. Alipata umaarufu sana alipoimba wimbo wa "Wifi Zangu Mna Mambo"

    ReplyDelete
  2. Asante kwa kutukumbusha ya kale ambayo tuliyasikia tangu tukiwa migongoni mwa mama zetu.

    ReplyDelete
  3. Lo mtani ulikuwa unasikiliza nini wakati huo we mdogo uko mgongoni?

    ReplyDelete
  4. Dah Uncle.
    Leo tumewaza moja. Nilikuwa nataka kukuuliza kuhusu wanamama Asia Darwesh na Rahma Shally. Nakumbuka saana walivyokuja kujenga HESHIMA katika muziki wa Dansi. Lakini hapa nimepata zaidi ya nilivyotaka. Hasa huyo Emma Mkello ambaye aliimba na Eddy Sheggy katika wimbo wa Milima ya kwetu.
    Nimefarijika na kufurahi kusikia kuhusu wengine.
    SWALI:
    Huo wimbo ambao umeuita SHINGO FENI ni tofauti na PENZI HALIGAWANYIKI II (Part two)?
    Nimekuwa nao kwa jina la PENZI HALIGAWANYIKI II japo nakumbuka mdundiko wake uliitwa Shingo Feni(kwa sisi tuliokuwa Moro tunajua kuwa kila wimbo uliovuma ulitengenezewa mdundiko)

    Wanaopenda kujikumbusha basi wanaweza kusikiliza PENZI HALIGAWANYIKI (sehemu ya kwanza) kwenye link hiyo hapa chini
    (http://www.archive.org/details/PenziHaligawanyikiI) na pia PENZI HALIGAWANYIKI (sehemu ya pili) kwa kufuata link hii hapa chini
    (http://www.archive.org/details/PenziHaligawanyikiIi)

    ReplyDelete
  5. Anonymous03:04

    kwa kweli john hutukumbushi yazamani tuu, bali unatuacha na simanzi na majonzi huku tukijikaza machozi yasitutoke maana viumri navyo vimekwenda, kulia mbele ya watoto watauliza sana mama analia sababu ni nini? lakini nimepitia mengi humu ndani sina la kusema, nilidhani ni mimi mwenyewe ninaye ona mziki wa nyumbani unavyovurugwa, na watu wanachekelea, kumbe tuko wengi tunaoumia, tafadhali zidi kutukumbusha mengi ya zamani na mengine mengi tusiyofahamu kwani huwezi kujua unavyotupa faraja, sijaona ukimtaja dudumizi, vipi mzee mzima King kiki? sijui kwa sasa Kitime uko wapi lakini kama uko nyumbani huwezi kuandaa tamasha japo moja tu litakalounganisha wanamuziki wa zamani ambao kweli ni wanamuziki na si covers, bila kujali nana aliiimba na nani au alikua bendi gani ama alikua na chuki gani, mkaporomosha vibao vya zamani? japo mtutoe hamu ya miaka mingi, ikibidi mutengeneze hata cd na dvd ili walioko nje nao wafaidi? ni swali na ombi tu kama yawezekana. maana sijui hiyo siku itakuaje. all in all asante sana mzee Kitime kwa kutukumbus
    ha mbali.

    ReplyDelete
  6. Anonymous06:28

    Mh,labda nikuulize tu huyu kida Waziri huko Arusha anajishughurisha na nini....? na vipi kuhusu mziki tena au ndio Basi.....! kwakweli alinisababisha kuipenda sana Vijana Jazz enzi hizo,maana sauti yake na Hayati Hemmed Manety,,ya Man....umenikumbusha nilikuwa na redio yangu ya mbao National...la..!

    ReplyDelete
  7. Anonymous06:30

    Mh,labda nikuulize tu huyu kida Waziri huko Arusha anajishughurisha na nini....? na vipi kuhusu mziki tena au ndio Basi.....! kwakweli alinisababisha kuipenda sana Vijana Jazz enzi hizo,maana sauti yake na Hayati Hemmed Manety,,ya Man....umenikumbusha nilikuwa na redio yangu ya mbao National...la..!

    ReplyDelete
  8. Anonymous08:55

    Bwana Kitime habari yako mzee mimi nilikuwa naomba na kama kweli unafatilia muziki na wanamuziki wa zamani basi tupe taarifa za mzee mwenzio Hamisi kitambi kwani toka alivyotelekezwa na msondo na chamudata hadi leo hii ametokea mfadhili kumsaidia maswala ya matibabu ya mguu wake alioumia ktk ajali akiwa na msongo ngoma miaaka takribani 5 iliopita. sasa tunaomba utueleze japo anaendeleaje kupitia blog hii ya wanamuziki haswa wa Tanzania.
    kama huna contact yake ni hii 0713576475 anaishi Magomeni mapipa
    Mdau
    Kisiju pwani

    ReplyDelete
  9. mzee kitime umemsikia anonymous wa kwanza. hebu kuna kichwa. inawezekana. mziki wa zamani una wenyewe na wenyewe ndio sisi. wadhamini wapo kibao tu kuanzia makampuni ya bia mpaka ya simu. wakati fulani hawana sehemu za kupeleka mipesa yao. ukifanikisha jambo hili binafsi nitasafiri kutoka mbeya kuja kuhudhuria.

    ReplyDelete
  10. Anonymous10:13

    John asante sana kwa yoote unayofanya. Hebu ukipata muda uzungumzie chombo kimoja "tumba" napata raha sana ninapokuja kwenye showz za wana njenje nakumkuta kijana akijituma kisanyansi. siku hizi vijana hawajui tumba na conga tofauti ni ipi nk

    ReplyDelete
  11. Anonymous14:20

    Mkuu,

    Vipi waimbaji wa kike waliokuwa wakiimbia bendi za maghorofani (sijui hii terminology ya bendi za mghorofani aliicoin nani nadhani Julius Nyaisanga)kama kina Amina Mbonde, Betty Enock and the Tanzanites, Lucy na Mionzi, Stella Lukumbuzya, Veronica Farasi, Frola Mkumbo, Diana Mshala na wengineo? Wao pia wana chachu yao katika muziki wa dansi wa mtindo wao! Au vipi?

    ReplyDelete
  12. Maabadi21:51

    John Kitime asante kwa kumbukumbu mahsusi ya muziki wa dansi. Nimekuwa mpenzi wa dansi la bongo tangu nilipoifahamu RTD na sikuwahi kuficha upenzi wangu kwa wana Saga Rhumba...Natamani sana kujua Shaaban Yohana "wanted" yu wapi siku hizi? huyu ni mpiga solo aliyenitia hamasa kujifunza gitaa.

    ReplyDelete
  13. Kwa kweli waimbaji wa kike walikuwa wengi na hawa waliokuwa wanaitwa wa hotelini kutokana na kuimbia bendi ambazo zilikuwa zimeamua kuwa zinapiga katika mahoteli tu. Na walikuwa wazuri sana na muhimu kuwaongelea kama ulivyowataja, lakini niliona nianze na wale ambao walianza kurekodi na bendi. Bendi ya magorofani ilikuwa ni jina ambalo bendi ya MK Group ilipewa kwa kuwa wakati ule ilikuwa ikipiga katika ghorofa la kwanza pale New Africa Hotel. Shaaban Wanted Yohana yuko Botswana anaendelea na muziki.

    ReplyDelete
  14. Anonymous19:18

    Mkuu,

    Tukimaliza wa zamani naomba tuwazungumzie wa sasa. Wapo wengi tena vere saksefuli!

    ReplyDelete
  15. Hakuna ubishi hebu tuongee tujue tulikotoka halafu tutajua tunakokwenda

    ReplyDelete
  16. Anonymous23:47

    Anko j kitime nashukuru sana kwa post hii nzuri sana ahsante

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...