TANCUT ALMASI ORCHESTRA wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma |
Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki
nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika maisha yangu ya muziki, hakukuwa na wilaya hata moja, kati ya
wilaya zilizokuweko Tanzania Bara kati
ya mwaka 1982 na 1992 ambayo sikufika na kufanya onyesho la muziki.
Leo nimekumbuka safari ya kuzunguka Kanda ya Ziwa nikiwa mmoja wa wanamuziki wa Tancut Almasi
Orchestra iliyokuwa na masikani yake Iringa, ikimilikiwa na wafanyakazi wa
kampuni ya Tanzania Diamond Cutting Company (kiwanda cha kuchonga almasi).
Wakala wa mfanya biashara maarufu wa Mwanza
alikuja Iringa kufanya mpango ili bendi ikafanye ziara Kanda ya Ziwa. Bendi
ilikuwa tayari kwa ziara hiyo lakini ilikuwa na mkataba wa kwenda kufanya
onyesho moja kwenye mahafali ya Chuo cha IDM Morogoro, baada ya hapo bendi ingeweza
kuelekea Mwanza kuanza ziara ya Kanda ya Ziwa.
Baada ya onyesho la IDM, usiku uleule tulienda kituo cha treni Morogoro kujaribu
kupata nafasi katika treni iliyokuwa iktoka Dar es Salaam na kuelekea Mwanza,
bahati mbaya tulichelewa treni. Wakala akisaidiana na viongozi wa bendi
waliweza kutafuta ‘Fuso’ usiku uleule, wanamuziki na vyombo tukajazana kwenye
‘Fuso’. Nia ilikuwa tusafiri usiku ule mpaka Dodoma na kuiwahi treni
iliyotupita Morogoro. Hilo lilishindikana kwani uzito wa vyombo na watu
ulisababisha ‘Fuso’ yetu ipate pancha mara nne, hivyo badala ya kuingia Dodoma
alfajiri, tuliingia Dodoma saa nane mchana. Mara baada ya kufika Dodoma, wanamuziki
walitafutiwa sehemu ya kula na kulala kwa siku hiyo na pia kutafutiwa tiketi za kwenda Mwanza na treni
kesho yake. Mimi na Katibu Msaidizi wa bendi tukapewa jukumu la kuhakikisha
kuwa tunafanya mipango ya kusafirisha vyombo vya muziki. Tulienda kituo cha
treni na kuweza kukamilisha taratibu zote za kusafirisha vyombo kutumia
mabehewa ya mizigo, vyombo viliingizwa katika behewa moja tayari kwa safari.
Uongozi wa Shirika la reli ukatuhakikishia kuwa vyombo vitasafirishwa na treni
ya mizigo siku ileile. Kwa vile treni za
mizigo hazikuwa na ratiba maalumu tulilazimika kuweko palepale ili tuhakikishe
vyombo vyetu kweli vimeanza safari. Treni za mizigo kadhaa zilifika na kuondoka na mabehewa
kadhaa ya mizigo yaliyokuwepo pale yaliunganishwa na kuondoka, lakini behewa
letu likawa haliunganishwi, tulipouliza sababu tukaambiwa kuwa kulikuwa na
tatizo la mipira ya breki. Tulishinda pale mchana ule na usiku ukaingia tukiwa
pale pale na tukakesha pale tukiumwa na mbu na kuteswa na baridi kali. Kesho
yake wanamuziki wenzetu walipata nafasi katika treni la abiria na kuanza safari
ya kuelekea Mwanza, sisi wawili na behewa letu la vyombo tukaingia siku ya pili
pale kituoni. Hatimae mtu mmoja akatushtua kuwa tusipoangalia tutafikisha hata
wiki moja pale, tumtafute muhusika na kumpa fedha kidogo mipira breki
itapatikana, tukafanya hivyo na mipira kweli ikapatikana kimiujiza. Behewa letu
liliunganishwa kwenye treni ya mizigo na safari ikaanza. Kwa vile ilikuwa ni
treni ya mizigo, mimi na mwenzangu tukaingia kwenye kichwa cha treni, nauli
tukamlipa dreva wa treni, kwa mara ya kwanza nikaweza kuona jinsi dreva wa
treni anavyoendesha treni. Safari ilikuwa nzuri, ila kila tulipokaribia katika
kituo, tulilazimika kuingia sehemu ya injini kujificha, kwani dreva hakuwa
anaruhusiwa kubeba abiria. Kwa kweli kule ndani kwenye sehemu ya injini kunatisha
mno. Tuliingia Mwanza kama saa tano mchana na siku hiyo ilikuwa siku ya sikukuu
ya Iddi. Bendi ilikuwa imeshatangaza
kuwa ingefanya onyesho la mchana katika Uwanja wa Kirumba na usiku bendi
ingepiga ukumbi wa Shinyanga Hotel. Onyesho la Kirumba lilifanyika vizuri
likaisha saa 12 jioni, vyombo vikahamishwa na kupelekwa kwenye ukumbi wa Shinyanga Hotel ambako
onyesho jingine lilianza saa tatu usiku mpaka usiku wa manane. Tulipoanza tu onyesho,
akaonekana mtu mmoja anapiga picha za video, onyesho likasimama na kukaweko
ugomvi mkubwa kumzuia mpiga video kwani alikuwa hajatuomba ruksa, hatimae aliruhusiwa kutupiga video baada ya
kutulipa shilingi alfu kumi na tatu. Wanamuziki tukagawana shilingi mia tano
kila mmoja na .
Baada ya kufanya
maonyesho kadhaa katika kumbi tofauti
pale Mwanza ukiwemo ukumbi wa Polisi na ukumbi maarufu wa Pamba House, bendi ikaendea kufanya
onyesho Tarime. Bendi ilisafirishwa na basi la tajiri aliyekodi bendi. Onyesho
la Tarime halikuwa na mafanikio sana,
mara baada ya kumaliza onyesho Tarime ilianza safari ya kurudi Mwanza.
Baadhi ya wanamuziki walikuwa wamejenga urafiki na wasaidizi wa tajiri
aliyekodi bendi, wasaidizi hao wakawaeleza rafiki zao kuwa mpango umesukwa wa kuitelekeza bendi stendi kuu ya Mwanza,
mara baada ya kufika Mwanza wakala angetangaza kuwa basi linaenda ‘service’
hivyo watu na mizigo yote ishushwe. Baada ya hapo basi lingeondoka na
lisingerudi tena. Baada ya taarifa hii kufahamika, uongozi wa bendi ukapanga
mkakati, kwanza wanamuziki wangegoma
kushuka kwenye basi, na kwa kuwa mkataba ulimtaka wakala kuirudisha bendi Iringa
baada ya ziara, bendi ilikuwa tayari kuachana na mkataba kama wanamuziki wangepelekwa kwenye mgodi wa almasi
wa Mwadui. Mgodi wa Mwadui ulikuwa chini ya shirika la STAMICO kama ilivyokuwa
kampuni ya Diamond Cutting Company, tulijua kuwa kama tungefika kule ingekuwa
kama kufika nyumbani.
Mimi nikaambiwa nishuke pale Mwanza kutafuta mfadhili ambaye angeweza kutukopesha shilingi alfu arobaini, fedha hizi ingekuwa ni mtaji tosha wa bendi kuweza kurudi Iringa kama mambo yasingefana Mwadui. Kweli tulipofika stendi Mwanza, wakala akatangaza kuwa watu wote na vifaa vyote vishushwe ili basi liende service tayari kwa safari ya kurudi Iringa. Akajibiwa kuwa hakuna haja ya kushusha vyombo kwani havitaingilia service, ugomvi mkubwa ukazuka, hatimae ndipo wakala akaambiwa akitaka aachane nasi basi basi lituache Mwadui, alikubali na basi likaelekea Mwadui……Itaendelea,