YOUTUBE PLAYLIST

Monday, September 12, 2022

MITINDO ILITAMBULISHA BENDI NA MUZIKI WAKE

 



Katika miaka ya karibuni, utamaduni wa kila bendi kuwa na mtindo wake umefifia sana. Lakini ulikuwa utamaduni uliokuwa maarufu sana kuanzia miaka ya sitini. Kila bendi ilipoanza, ilijinasibu kwa kuja na mtindo wake, ingekuwa siku hizi ingetambulika kama kuji ‘brand’.
Ni vigumu kutaja mitindo yote iliyowahi kugunduliwa kwani kuna mingi ambayo haikuwahi kupata nafasi kutambuliwa katika vyombo vya utangazaji au kuwekwa  katika kumbukumbu za aina yoyote. Majina ya mitindo mingine ilikuwa na sababu au historia na maana maalumu, lakini majina mengine yalikuwa ya kutunga tu na kwa kweli hata waliokuwa waliokuwa wakiyatumia hawakuwa na maelezo ya maana ya maneno hayo. Nakumbuka nikiwa bado mwanamuziki mdogo huko Iringa tulikuwa na bendi ambayo mtindo wake ulikuwa ni Chikwala chikwala, namkumbuka aliyetunga jina hili, alikuwa mpiga gitaa la rhythm ambaye pia alikuwa fundi saa. Hata yeye hakuwa na maelezo ya maana kuhusu jina lile, ila kwa wakati ule, ilikuwa ni staili kwa majina ya mitindo  ya bendi kuwa na jina linalojirudia rudia, hii ilitokana na bendi kadhaa Kongo kuwa na majina yaliyojirudia rudia mfano Orchestra Lipua Lipua, Orchestra Bella Bella na Orchestra Shama Shama.
Baadhi ya majina ya mitindo ya bendi yalikuwa Mundo, Saboso,  Msondo, Sokomoko, Dondola, Toyota, Kiweke, Segere matata, Super mnyanyuo, Vangavanga, Libeneke, Chakachua, Sululu, Ambianse, Takatuka, Afrosa na majina mengineyo mengi. Bendi nyingi zilibuni hata aina ya uchezaji wa mitindo yao, na uchezaji mwingine ulibuniwa hata na wapenzi wa bendi hizi. Kila bendi ilikuwa ikijitahidi kuwa tofauti na bendi nyingine. Kwa mfano katika mji wa Tanga ulikuwa na bendi kubwa mbili, Jamhuri Jazz Band na Atomic Jazz Band, kuna wakati bendi ya Jamhuri ilikuwa na mtindo wa Toyota, na baadae Dondola, wakati  Atomic walikuwa na mtindo wa Kiweke, muziki wao ulikuwa tofauti, hivyo Jamhuri ikawa na wapenzi wake na Atomic ikawa na wapenzi wake, na mpaka leo, wazee waliokuwa wapenzi wa bendi hizi mbili hubaki kusifia ubora wa bendi zao, wazee wa Jamhuri husifu mtindo wa upigaji wa gitaa la rythm la Harrison Siwale(Satchmo), huku wapenzi wa Atomic watakwambia hakuna kama Kiweke, kwani upigaji wa gitaa la solo wa John Kijiko, au bass la Mwanyiro haukuwa na mpinzani. Kule Morogoro kulikuwa na Morogoro Jazz Band na Cuban Marimba, bendi hizi zilikuwa na mitindo mbalimbali kwa nyakati mbalimbali, na wapenzi wao walikuwa tayari kutetea ubora wa mitindo ya bendi zao. Cuban Marimba wakisifia mtindo wa Ambianse, Morogoro wakisifia Likembe, au sululu. Na hakika kulikuwa na tofauti kubwa ya mitindo hii miwili japo ilipigwa na bendi zilizotoka mji mmoja.
Nimeanza kwanza kwa kutaja bendi zilizokuwa katika mji mmoja, tena huko mikoani ambako kwanza miji ilikuwa bado na watu wachache kulinganisha na sasa, wanamuziki walikuwa wanajuana na kuishi jirani, hali hiyo ndio iliyokuwa Tabora, ambako pamoja na Tabora Jazz, kulikuweko na Nyanyembe Jazz, Kiko Kids, lakini muziki wa kila bendi ulikuwa tofauti na mwingine. Dar es salaam kulikuwa na bendi nyingi na hivyo mitindo mingi, na pia kulikuwa na bendi za watu wa mataifa kutoka nje ya Tanzania. Kulikuwa na bendi za Magoa, kulikuwa na bendi za Wakongo, nao pia wakawa na mitindo yao.  Hakuna aliyeweza kuchanganya mtindo wa Ogelea piga mbizi ya  Maquis na mtindo wa Chunusi wa  Orchestra Safari Sound, hata pale ambapo wanamuziki wa kutoka bendi moja walipohamia bendi pinzani kila bendi ilibaki na staili yake na kuilinda kwa kuongeza ubora kila mara. Hivyo haikuwezekana ukasema  Sikinde na Msondo zilipiga muziki uliofanana au mitindo ya Sokomoko na Afrosa ilikuwa na ukaribu. Kikubwa ninachotaka kueleza ni kuwa bendi kuwa na mtindo ilikuwa si jina tu bali kulikuweko na kazi ilifanyika ili kupata, kulinda na kuendeleza mtindo ambao bendi iliamua kuwa nao. Nakumbuka wakati wa mazoezi enzi hizo unaweza ukatunga wimbo ukianza kuimba wenzio watakwambia mbona unafanana na bendi fulani na hapo utakarabatiwa mpaka uwe katika mtindo wa bendi husika.

Wiki chache zilizopita nilipata bahati ya kuhudhuria onyesho moja la bendi iliyoko Mbeya, baridi ndio ilinilazimisha kukumbuka kuwa niko Mbeya, upigaji, uchezaji, uimbaji wa bendi hii ulikuwa kama bendi nyingi zilizopo Dar es Salaam. Bendi zimekuwa kama vile zimepewa amri kuwa lazima zipige muziki unaofanana. Toka umeingia mtindo wa ‘sebene’ mwanzoni mwaka 2000, basi ni kama kila ubunifu umesimamishwa. Hata zile bendi ambazo hupiga nyimbo za bendi ya zamani, hulazimisha kuingiza sebene, kwenye nyimbo hizo. Juzijuzi kwenye onyesho moja kubwa la muziki, bendi moja ilikuwa ikipiga wimbo wa Super Volcano unaoitwa Shida, ghafla ukabadilika kwa kuongezewa sebene.  Kipindi aina ya muziki wa sebene ulipokuwa ukiingia nchini, kulikuwa na aina ya muziki wa hapa nyumbani uliokuwa unaitwa Mchiriku. Sasa toka wakati huo,Mchiriku umeweza kujiongeza na kubadilika mpaka sasa unaitwa singeli, tena hata hiyo singeli imeanza kuota matawi, lakini wanamuziki wa dansi wamekwama palepale kwenye sebene. Hili linanikumbusha enzi za teknolojia ya santuri, santuri zilikuwa zinaweza kupata mchubuko na hivyo sindano ikakwama sehemu moja, ikawa inarudia kupiga muziki sehemu ileile haiendi mbele wala hairudi nyuma mpaka betri itakapoisha.

No comments:

Post a Comment

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...