Ma ‘superstar’ ni watu ambao wametokea kujizolea
umaarufu mkubwa katika jamii. Superstar anaweza kuwa ametokea katika nafasi
mbalimbali katika jamii, anaweza akawa mwanasiasa, mwalimu, mkulima au mtu
yeyote katika jamii, hapa kwetu sifa hii zaidi huhusiana na wasanii. Sifa ya
‘usupastaa’ imejitokeza zaidi baada ya tasnia ya filamu kukua, jambo ambalo
limeenda sambamba na kuongezeka kwa vyombo vya utangazaji. Na kwa kweli katika zama hizi tunao watu
wengi ambao wanapewa sifa ya ‘u
superstar’ katika jamii. Hakuna chuo maalumu cha kufundisha usupastaa kwani
umaarufu wa mtu huweza kutokana na sababu mbalimbali.
Wasanii huingia katika sanaa kwa njia na sababu
mbalimbali, wengine huzaliwa na kipaji, wengine huingia katika fani hiyo kama
njia ya kutafuta maisha, wengine huingia kwa kuiga wenzao waliomo katika sanaa,
kuna hata waliolazimishwa na ndugu na jamaa kuingia katika fani ya sanaa, na
kadhalika. Kutokana na sababu hizi mbalimbali za kujiingiza kwenye sanaa,
waliomo humu nao wanakuwa na mategemeo mbalimbali yatakayopatikana katika fani
hiyo. Wengine nia yao ni kutengeneza sanaa nzuri, bila kujali sifa wala malipo,
wengine wanafanya sanaa ili wapate kipato kizuri na wengine wakitegemea sifa tu
kutokana na ubora wa kazi yao. Na wengine kutumia sanaa kama jukwaa la kufanyia
shughuli nyingine kabisa ambazo hazihusiani na sanaa. Wasanii waliomo katika
sanaa kutafuta kipato, hulazimika kutafuta mbinu mbalimbali ili sanaa yao
iuzike, na moja ya njia kubwa ya kuhakikisha sanaa inauzika ni kwa wao kuwa
maarufu. Watu wengi wanatabia ya kufuatilia maisha na kununua kazi za sanaa za
watu maarufu. Kutokana na sababu hii, msanii huanza mbinu mbalimbali za kupata
umaarufu. Msanii atajitokeza kwenye vyombo vya habari kutangaza kazi zake na
hata kuelezea maisha yake, picha zake nzuri kusambazwa,na hata kazi hizo
kusambazwa ili watu wengi wazifahamu.
Katika nchi ambazo tasnia imejengeneka vizuri, kuna
makampuni maalumu ambayo hutumia mamilioni ya fedha kujenga sifa za msanii
husika na kazi zake, kwa kutegemea faida kubwa baadae. Msanii huingia katika
mikataba ya muda mrefu na kampuni huwekeza katika kujenga sifa ya msanii ili
kupata wateja wengi wa kazi za msanii huyo.
Je unapataje ‘u super star’ hapa Tanzania? Kama ilivyo
duniani kote kuna wasanii ambao kazi zao zimepokelewa vizuri na jamii na
kuwafanya wasanii mbalimbali kuwa maarufu kwa urahisi sana. Lakini kuna mambo
mengi ambayo yanapita nyuma ya pazia katika kupata ‘u superstar’ hapa kwetu.
Rushwa ni moja ya jambo kubwa katika kujenga ‘ma superstar’ wa hapa kwetu. Na
hili halikuanza karibuni, kwa wanamuziki wa zamani wanaelewa hali ilivyokuwa
enzi kulipokuwa na redio moja tu, ilivyolazimika kutoa rushwa ili mashahiri ya
nyimbo walizotaka kurekodi yakubalike na nyimbo zirekodiwe, kisha kutoa rushwa
ili nyimbo zilizorekodiwa zipigwe kwenye vipindi mbalimbali huku sifa za
kujenga usupastar wa wasanii hao zikimiminika, hali hii haiko tofauti sana na
sasa japo kwa sasa kuna utititiri wa redio na luninga. Watangazaji wengi
wamefaidika na rushwa kutoka kwa wasanii waliokuwa na hamu ya ‘kutoka’. Kuna
wakati watangazi wa redio mbalimbali walitengeneza umoja, ambapo mwanamuziki
alikuwa akilipia ili kazi zake zirushwe hewani. Watangazaji wa vipindi vya
redio wengi waligeuka kuwa mameneja wa wasanii na hivyo kuhakikisha wanawatangaza
wasanii wao ili wawezekuwa ‘ma supersta’. Rushwa ya ngono sio siri katika
tasnia ya sanaa katika kutafuta ‘u superstar’ . Wasanii wa kike wengi wana
hadithi ya kupitia katika mtihani huu katika kutafuta ‘kutoka’. Kuna wakati
wasanii wawili wakubwa wa kike, walitangaza
mpango wa kuanza kuwajenga wenzao ili wasipitie adha ya kudaiwa rushwa hii.
Jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa rushwa hii bado iko hai.
Katika kutafuta ‘U superstar’, kuna wasanii ambao
wamefanya mambo mengi ya ajabu ikiwemo kutunga visa ambavyo vingewaweka katika
vichwa vya habari. Habari za msanii kufumaniwa, kupigwa, kulewa, kulazwa
hospitali, kupendana, kuachana na kadhalika vimekuwa vikitungwa na wasanii
mbalimbali ili kujiweka katika nafasi ya kutengeneza hadithi kwenye vyombo vya
habari kujiongezea umaarufu. Ujio wa mitandao ya kijamii umekuwa tena nafasi
nzuri za kutengeneza ‘U superstar’ wasichana ambao wamekuwa wanatumia sanaa
kama daraja la kupata ‘U superstar’, wamekuwa wakitumia kurasa zao kwa
kutundika picha wakiwa nusu utupu ili mradi kutafuta kujulikana na kupata
wateja wa shughuli isiyohusiana na sanaa.
Matokeo ya vurugu hizo zote ni kuwa msanii kuwa
‘superstar’ si lazima awe msanii bora. Wako wasanii wa aina hiyo wengi na ukiulizia
kazi zao za sanaa, hazionekani au hazijulikani. Na kwa kazi zao za kisanii
ambazo hutolewa hadharani, huishia kupotea baada ya muda mfupi, lakini sifa za
‘u supersta’ zinaendelea kujengwa kwa namna moja au nyingine. Jambo ambalo ni bahati
mbaya kwa tasnia nzima ya sanaa, nikuwa masupastaa hawa wajanja wajanja
huaminiwa sana hata na viongozi wa ngazi za juu nchini, na hutumika kama vigezo vya kukua kwa tasnia.
Na mara nyingine huombwa hata kutoa ushauri wa namna ya kuboresha tasnia ya
sanaa. Mungu isaidie tasnia ya sanaa Tanzania.
No comments:
Post a Comment