Imani ya uchawi ni utamaduni ambao umekuweko katika historia ya jamii zote za binadamu. Maandiko ya dini mbalimbali yanatuhakikishia kuwa jambo hilo lipo na hulilaani. Mara nyingi hudhaniwa kuwa kadri maendeleo na elimu yanavyoongezeka ndio imani ya ushirikina inavyopungua na kupotea, lakini ni wazi dhana hiyo si ya kweli, safari ya kuachana na uchawi bado ni ndefu sana, kwani ukipita katika mitaa mingi utaona vibao vikiashiria waganga wanaoweza kutibu matatizo mbalimbali kama ‘kusafisha nyota’, ‘kuondoa majini’, ‘kurudisha mpenzi aliyekimbia’ na kadhalika, wasomi wenye milolongo ya shahada na stashahada si ajabu kabisa nao kuwakuta kwenye vibanda vya waganga wakitafuta kusaidiwa kwenye mambo ambayo mtu mwingine ungetegemea yanawezekana kwa juhudi tu za kibinadamu.
Muziki haujakwepa kuguswa na dhana ya ushirikina. Muziki unatumika unatumika
katika kufanikisha dhana ya uchawi na wanamuziki wengi wanaamini na kushiriki
katika shughuli mbalimbali za uchawi.
Tuanze na dhana ya muziki iliyopewa jina la Kiingereza ‘ healing music’. Duniani kote waganga na wachawi hutumia muziki wa aina
yake kupandisha mashetani au kuita mizimu na kadhalika, muziki huu ndio huitwa healing music, huku kwetu mara nyingine huitwa muziki wa kupandisha mashetani.
Katika
maisha yangu ya muziki niliona na kusikia vituko vingi vilivyohusishwa na
imani ya uchawi. Mara ya kwanza kuanza kuona vitimbi hivi ‘live’ ni
nilipojiunga bado mdogo na kuwa mwanamuziki katika bendi yetu ndogo huko
Iringa. Tualianza kupiga muziki wenyewe wachache bila kuwa na wazo lolote la
kuhusisha muziki wetu na imani yoyote ya kishirikina. Siku moja akaja mzee
mmoja akatukaribisha kufanya mazoezi kwenye sehemu yake ya biashara, na kwa
vile tulikuwa hatuna sehemu maalumu tuliona huu ni ufadhili mkubwa. Tulihamishia vyombo vyetu vichache kwake, na
haikuchukua muda mrefu tukagundua kuwa biashara yake ni uganga wa
kienyeji.
Siku moja akatueleza kuwa hatutaweza weza kuwa bendui kubwa bila ‘kusafishwa
nyota’. Tulipewa dawa za kuoga na tukaendelea na mazoezi makali tukijua muda
wetu wa kuwa bendi kubwa umewadia. Tulikubaliana kuwa tungepunguza deni la kazi
yake ya kutusafisha nyota kwa kumlipa kidogo kidogo kila tulipofanya onyesho, kweli tukaanza kumlipa kila tulipopiga.
Sikumbuki ni muda gani tuliendelea kumlipa yule mganga, japo kuwa hakuna
chochote kilichobadilika katika hadhi ya bendi yetu.
Siku moja mganga yule
alienda disco na akamtishia msichana mmoja kwa nyoka aliyekuwa nae mfukoni,
hapo ndipo alipokamatwa na polisi na hatukumuona tena deni likayeyuka.
Miaka mingi baadae
nilikuja kujiunga na bendi moja kubwa jijini Dar es Salaam, hapo ndipo
nilipoona tena shughuli za ushirikina. Ilikuwa ni siku chache baada ya kurekodi
nyimbo mpya za bendi yetu katika studio za Radio Tanzania. Kulikuwa na kipindi
kilichoitwa Misakato , kipindi ambacho kilitambulisha nyimbo mpya
zilizorekodiwa na studio za redio hiyo, tulikuwa tumekubaliana kuwa wanamuziki
wote tukusanyike nyumbani kwa kiongozi wetu ili wote tuzisikilize nyimbo zetu
zikirushwa kwa mara ya kwanza hewani.
Zilipoanza kupigwa nyimbo zetu nikashuhudia mmoja wa viongozi wetu akiwa
anaifukiza redio kwa moshi kutoka dawa zilizokuwa zimechomwa kwenye kifuu cha nazi, hii ilikuwa kwa imani kuwa kwa kufanya hivyo, vibaovyetu vipya vikisikika vitatikisa roho za wasikilizaji wake. Katika kundi hili vituko vingi
viliendelea hatimae tulizoea kuwa uongozi wa bendi yetu unaamini sana uchawi.
Kuna wakati aliletwa mganga ambaye alidaiwa aliwahi kuifanya timu moja maarufu
ya soka, ishinde kombe na kuwa bingwa wa
Taifa, hata jina lake aliitwa Bingwa, kutokana na sifa hizo bendi ilimchukua
kwa mkataba na kazi yake ikawa ni kukaa mlangoni akijifanya ni muuza machungwa,
hapo alitakiwa afanye vimbwanga vyake ili wateja wengi waingie kwenye muziki.
Yeye alidai kila anapomenya chungwa kwa kuunganisha maganda kama mkanda, basi
na wateja nao wataingia katika ukumbi kwa kuunganika kwa foleni ndefu, huyu alikaa nasi kiasi
cha kuweza kuwa katika misafara
mbalimbali ya bendi tulipoenda ziara za mikoani. Harakati za bendi kutafuta
umaarufu kwa uchawi ilifikia mpaka bendi ikasafiri hadi kwenda Mpanda, ambako
viongozi wa bendi walikwenda kwa mganga na kufanya mambo yao ambayo yalihusisha
na hata kumchinja mbuzi. Baadae walirudi na nyama ya mbuzi huyu mpaka
tulipokuwa tumefikia, nadhani masharti yalikuwa ni sisi wanamuziki wote tule
kipande cha mbuzi yule wa kafala. Sijajua mpaka leo viongozi walifanya nini na
nyama ya mbuzi yule maana wanamuziki walifanya mgomo wa kumla yule mbuzi.
Ushirikina una matatizo ya kufanya watu
wasiaminiane hata kwenye bendi yenyewe, haikuchukua muda mrefu bendi ilipoanza
kupoteza umaarufu, Kiongozi wa bendi akaaitisha mkutano na kutuambia kuwa
kuanguka kwa bendi kunatokana na mmoja wetu kuiloga bendi, hapo ikatolewa
tishio kuwa mtuhumiwa asipojitaja mwenyewe na kuomba msamaha mganga aliyeagua
hilo aliahidi atamfanya awe kichaa. Jambo ambalo liliungwa mkono na wote kuwa
kama ni kweli kuna mtu namna hiyo basi apate uchizi. Hakuna aliyekumbwa na
tatizo hilo mpaka leo.
Miezi michache baadae, wanamuziki wawili walioamua kuacha bendi walirudisha sare
za bendi kama ilivyokuwa kawaida zama zile. Shati zilikuwa zimechanywa kwenye
kwapa na suruali kuchanywa kwenye maungio ya miguu kwa imani kuwa hizo ndizo
sehemu zenye jasho kwa hiyo kama wangerudisha sare zao bila kuondoa sehemu hizo
wangeweza kurogwa kirahisi na kuharibiwa maisha.
Mpiga tumba mmoja tuliyekuwa nae bendi moja alinichekesha aliponihadithia kuwa kiongozi wa bendi yao moja aliyopitia, aliwahi kuwapeleka kwa mganga aliyewataka waende na vyombo vyao vya muziki. Kisha akawa ana chanja chombo na kukipaka dawa,na baada ya hapo kumchanja mwenye chombo matakoni na kumpaka dawa!!!!
Katika mizunguko kwenye bendi mbalimbali, siku moja bendi yetu ilikuwa na mpambano
wa kupiga bendi zaidi ya moja katika ukumbi mmoja. Hili lilichukuliwa kuwa ni
jambo kubwa na la hatari linalohitaji matayarisho, mganga maalumu lazima atafutwe ili kuilinda
bendi isimalizwe na wapinzani. Ilikuwa inaaminika kuwa katika mpambano wa
bendi, uchawi hutumika kuimaliza bendi ambayo itakuwa haina kinga, siku moja
kabla ya pambano, maboksi ya spika yalifunguliwa na ndani yake kuliwekwa tunguli na hirizi mbalimbali tayari
kwa mpambano. Nakumbuka siku hiyo bendi pinzani nayo iligoma kupanga vyombo kwenye jukwaa
kuu kwa madai kuwa kuna mbuzi alifukiwa katika jukwaa lile.
Kwa ukweli
kabisa hata wanamuziki kutembeleana mara nyingine ilikuwa ni vigumu, kwani
ukionekana mwanamuziki wa bendi nyingine katika ukumbi, basi bendi iliyo
jukwaani haina raha, anaweza hata akatumwa mtu kufuatilia kila utakachofanya.
Na ilikuwa vigumu kuruhusiwa kugusa vyombo vya bendi nyingine kwa wasiwasi wa
kuwa unaweza ukaloga kile chombo. Niliwahi kuona bendi ikisimamisha muziki
katikati ya onyesho na kudai shabiki mmoja wa bendi pinzani, tena alikuwa mwanamke,
atolewe ukumbini kwani alikuwa ametumwa kufanya ushirikina, na hakika alitolewa nje.
Kulikuwa na
hadithi nyingi zilizoonyesha ni kiasi gani cha ushirikina bendi ziliweza kufanya ili
kupata wateja. Kuna bendi ambayo ilisifika kuwa kila wakimaliza kupiga muziki walipita
katika kumbi mzima na kuokota vizibo vya
chupa za bia na soda, mifupa na mabaki ya nyama zilizotupwa na wateja, na hata
kupata maji toka vyoo vya ukumbi na kwenda kuloga ili wale walioingia wasiingie
bendi nyingine yoyote kasoro yao. Bendi nyingine zilidaiwa kuwa ziliweka mkataba ambapo
zililazimika kutoa kafala ya mtu mmoja kila mwaka, hivyo viongozi wa bendi
kufiwa na watoto, ndugu na hata wanamuziki wageni waliojiunga katika bendi hizo kukutwa na mauti
ambayo habari za chini chini zilidai ni katika kutoa kafala.
Bendi mbili
ambazo zilikuwa na upinzani mkubwa katika jiji la Dar es Salaam zilidaiwa hata
kutaka kuweka uchawi katika chanzo cha maji Dar es Salaam , na kujikuta
wakitaka kuumbuana hadharani kuhusu hilo.
Kuna wanamuziki wapiga magitaa wa
zamani waliowahi kupatwa na matatizo ya akili na wazee wengi mpaka leo hudai
matatizo yao yalitokana na ushindani wa uchawi katika bendi zao. Kama
nilivyosema imani ya uchawi huleta kutokuaminiana na hata madhara makubwa ya
kutuhumiana mambo ambayo mara nyingi hayana ukweli wowote. Kuna mwanamuziki
niliyejaribu kumshawishi aingie katika bendi niliyokuwa nikipigia , alikataa
katakata kwa kuwa alidai mmoja wa wanamuziki katika bendi hiyo ni mchawi.
Mwanamuziki mmoja mpiga gitaa mahiri aliwahi kunihadithia jinsi alivyopita uchochoro wa nyumba ya
mwanamuziki mwenzake akashangaa kusikia jina lake likitajwa na mwenzie
aliyekuwa chumbani kwake na kusema,’ Nyota ya …….(jina la mwanamuziki huyo) izimike kama kaa hili’, akadai
alichungulia katika ufa na akakuta mwenzie anatumbukiza kaa la moto kwenye
maji.
Ugonjwa wa ukimwi ulipoanza kuuwa wanamuziki kwa mara ya kwanza mara nyingi
ulihusishwa na uchawi. Rafiki yangu mmoja nilipomtembelea wakati akiwa hoi
kitandani akanambia,’Nikupe siri? Mi ntakufa lakini nauawa na wanamuziki
wenzangu kwenye bendi. Nimepata mganga kanitajia na majina kabisa’. Miezi
michache baadae mwanamuziki huyu kabla hajafariki alinambia,’Mjomba sijalogwa
wala nini, udude huu, unaniua udude’. Alifariki siku chache baada ya kunambia
haya.
Kama nilivyosema awali, elimu na teknolojia hazijaondoa kabisa dhana ya uchawi.
Siku moja nilimsikia producer maarufu akiwakanya wasanii wa muziki wa
Bongofleva wanaoingia studioni mwake, wasifanye mambo ya ushirikina kwenye
studio yake.
Na siku
chache baada ya hapo tena mwanamuziki mwingine wa muziki huo kawataja ambao
aliwaita wabaya wake wanaomloga.!!!!!!! Nikaona loh kumbe shughuli bado
inaendelea, wanamuziki hawa wenye umri mdogo tayari wamekwisha jenga imani ya
kulogana katika enzi hizi za dijitali, safari bado ndefu sana, USHIRIKAINA BADO
UKO HAI KATIKA SANAA YA MUZIKI
Ushirikina ni sumu Kubwa sana
ReplyDeleteAisee, Mimi ni mmoja wa watu wasioamini mambo hayo ya ushirikina, ninachoamini ni juhudi ya kazi, Kwa upande wa Muziki na Wanamuziki kikubwa ni ubunifu wa Kazi zao, ubunifu ndiyo hasa mlango wa mafanikio kwa kazi zao
ReplyDelete