YOUTUBE PLAYLIST

Thursday, November 3, 2022

MKOANI PIA KUNA WANAMUZIKI WAKALI, KWANINI WANATENGWA?

 

Kila jamii ina muziki, kuna aina mbalimbali za muziki na zenye matumizi mbalimbali, kadri ya utamaduni wa jamii husika.
Katika zama hizi hasa mijini, muziki huonekana hasa kazi yake ni kwa kuleta burudani. Lakini kwa asili katika jamii zetu mbalimbali muziki ulikuwa na matumizi ya aina nyingi na hata kupewa majina kutokana na shughuli husika.
Kati ya shughuli ambazo muziki ulitumika na sehemu  nyingine bado unatumika ni kwenye  matambiko, tiba,  misiba, sherehe mbalimbali kama mavuno, harusi na kadhalika.
Leo niongelee muziki na siasa za nchi yetu.
Kabla ya Uhuru, katika maeneo mbalimbali nchini, wanamuziki kama marehemu Mzee Moses Nnauye walianzisha vikundi vya muziki kuhamasisha kudai Uhuru, vikundi vya kwaya, ngoma za asili, na muziki wa taarab na muziki wa dansi, vilitunga nyimbo zenye ujumbe  ambao uliwafikia vizuri wananchi wengi na hivyo  kuwahamasisha kuwa wana haki ya kujitawala na kuanza kudai Uhuru.
Mara baada ya kupata Uhuru,Disemba 9 1961, vikundi vya muziki  vilitunga nyimbo zilizoongelea furaha ya kupata Uhuru na pia kuanza kuelezea ndoto za  wananchi baada ya uhuru. Mahusiano ya muziki na siasa yaliongezeka sana, na baada ya Tanzania kuamua kuwa nchi ya Kijamaa, serikali iliwekeza sana katika sanaa, kwani ilitambua kuwa hiyo ilikuwa njia muhimu ya kufikisha taarifa ya malengo ya serikali. Pamoja na kuweko majengo yalikuwa maalumu kwa ajili ya maonyesho ya muziki, pia yalihamasishwa mashindano, matamasha na maonyesho ya aina mbalimbali ya muziki kila kona ya nchi.

Watu waliokuwa vijana na watoto katika miaka ya 60, 70, na 80 wanaweza kukueleza hadithi ndefu jinsi walivyokuwa wakishiriki kwa namna moja au nyingine katika nyimbo mbalimbali zilizohusu mambo ya nchi yao. Kulikuwa na shughuli za muziki kuanzia ngazi ya vijiji, mada mbalimbali zilitungiwa muziki kwa kutumia muziki wa asili, kwaya na muziki wa kisasa. Kwa njia hiyo taarifa za mambo mbalimbali zilieneka kila kona ya nchi japokuwa mawasiliano ya umma  yalikuwa hafifu mno kulinganisha na zama hizi.
 Kulikuweko na Maafisa Utamaduni wa Wilaya na Mkoa nchi nzima, na maafisa hawa wakahamasisha kuanzishwa vikundi vya muziki wa aina mbalimbali kwenye sehemu za kazi, shuleni, vijijini na kadhalika.  Taasisi za serikali na mashirika ya umma vilihamasishwa kuanzisha vikundi vya sanaa, na ndipo kukawepo kundi la sanaa la Taifa, vikundi vya sanaa majeshini ambapo huko pia kukawa na vikundi vya taarab na dansi, mashirika kama Bima, DDC, URAFIKI, TANCUT na mengine mengi yakawa na vikundi vya sanaa vizuri sana, Kurugenzi za mikoa Dodoma na Arusha nazo zikaanzisha vikundi, Umoja wa Vijana wa TANU nao ukawa na vikundi ikiwemo bendi yake maarufu Vijana Jazz band. Vikundi vyote hivyo vilishiriki sana katika kuimba nyimbo mbalimbali za maisha katika jamii na pia siasa, na maendeleo na nchi. Katika mfumo huo walikuja kupatikana akina Mzee makongoro , Mzee Mwinamila, John Komba na kadhalika.  
Viongozi wa ngazi mbalimbali walivitembelea vikundi vilivyo chini ya himaya yao kuvikagua navyo viljitayarisha kuonyesha umahiri wao, hivyo nchi nzima ilichangamka kwa ubunifu katika muziki wake.

Katika ziara ambazo zilichukuliwa kwa uzito mkubwa na  vikundi vyote, zilikuwa ziara za viongozi wakuu wa  nchi. Mazoezi yalikuwa makubwa, kwaya zilitunga nyimbo mpya, ngoma zilitunga nyimbo mpya, bendi na vikundi vya taarab vilitunga nyimbo mpya, kila moja ilijitahidi kwa umahiri ili tu kupata nafasi kuonyesha kazi mbele ya umma na viongozi hao wakuu. Na hakika kabla ya kiongozi kuanza shughuli au  hotuba, wanamuziki waliburudisha umma kwa kazi zao. Ni katika mfumo huo ambapo wanamuziki kama Bi Shakila walipogunduliwa. Ilikuwa ni siku Mwalimu Nyerere alipotembelea Pangani na Shakila akawa mmoja wa wanamuziki wa pale Pangani walioweza kutumbuiza mbele ya Mwalimu Nyerere, na umahiri wake kugunduliwa. Na hali kadhalika wasanii wengi waliokuja kuwa maarufu walionekana kwanza katika maonyesho mbele ya viongozi wakuu.
Machifu wengi wa zamani walitumia wasanii kupata taarifa za hali ya utawala wao. Wasanii wachekeshaji na wanamuziki waliweza kutunga vichekesho au nyimbo zilizokuwa zikielezea ukweli wa jinsi wananchi walivyokuwa wakijihisi wakiwa chini ya Chifu wao, nae alichukua ujumbe huo uliokuwa ukionekana kama utani au wimbo mzuri na kuufanyia kazi.
Zama hizi za dot com mambo ni tofauti sana, ni jambo la kawaida kabisa viongozi wa juu wakiwa katika ziara zao nchini,  kusindikizana na wanamuziki ‘maarufu’ Kitaifa.  Hali hii ya kuletewa msanii ‘maarufu’ kutumbuiza ‘nyumbani kwao’  na kuwadharau wasanii wenyeji ina waacha wasanii wenyeji wakijiuliza maswali kuhusu thamani yao mbele ya kiongozi huyo mkuu. Taratibu hii mpya pia inamyima kiongozi mkuu fursa ya kuona sura nyingine ya sanaa za wananchi anaowaongoza,  na muhimu zaidi anakosa kusikia ujumbe mpya kutoka kwa wananchi wa sehemu anayozuru.
Nina imani kabisa kabisa kuwa wasanii wote wana haki sawa mbele ya viongozi wakuu, hivyo si haki kudharauliwa kwa kipimo cha umaarufu wa kibiashara.

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...