YOUTUBE PLAYLIST

Thursday, March 9, 2023

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

 

TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma


 Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika maisha yangu ya muziki,  hakukuwa na wilaya hata moja, kati ya wilaya  zilizokuweko Tanzania Bara kati ya mwaka 1982 na 1992 ambayo sikufika na kufanya onyesho la muziki.
Leo nimekumbuka safari ya kuzunguka Kanda ya Ziwa  nikiwa mmoja wa wanamuziki wa Tancut Almasi Orchestra iliyokuwa na masikani yake Iringa, ikimilikiwa na wafanyakazi wa kampuni ya Tanzania Diamond Cutting Company (kiwanda cha kuchonga almasi).
 Wakala wa mfanya biashara maarufu wa Mwanza alikuja Iringa kufanya mpango ili bendi ikafanye ziara Kanda ya Ziwa. Bendi ilikuwa tayari kwa ziara hiyo lakini ilikuwa na mkataba wa kwenda kufanya onyesho moja kwenye mahafali ya Chuo cha IDM Morogoro, baada ya hapo bendi ingeweza kuelekea Mwanza kuanza ziara ya Kanda ya Ziwa. 
Baada ya onyesho la IDM, usiku uleule tulienda kituo cha treni Morogoro kujaribu kupata nafasi katika treni iliyokuwa iktoka Dar es Salaam na kuelekea Mwanza, bahati mbaya tulichelewa treni. Wakala akisaidiana na viongozi wa bendi waliweza kutafuta ‘Fuso’ usiku uleule, wanamuziki na vyombo tukajazana kwenye ‘Fuso’. Nia ilikuwa tusafiri usiku ule mpaka Dodoma na kuiwahi treni iliyotupita Morogoro. Hilo lilishindikana kwani uzito wa vyombo na watu ulisababisha ‘Fuso’ yetu ipate pancha mara nne, hivyo badala ya kuingia Dodoma alfajiri, tuliingia Dodoma saa nane mchana. Mara baada ya kufika Dodoma, wanamuziki walitafutiwa sehemu ya kula na kulala kwa siku hiyo na pia  kutafutiwa tiketi za kwenda Mwanza na treni kesho yake. Mimi na Katibu Msaidizi wa bendi tukapewa jukumu la kuhakikisha kuwa tunafanya mipango ya kusafirisha vyombo vya muziki. Tulienda kituo cha treni na kuweza kukamilisha taratibu zote za kusafirisha vyombo kutumia mabehewa ya mizigo, vyombo viliingizwa katika behewa moja tayari kwa safari. Uongozi wa Shirika la reli ukatuhakikishia kuwa vyombo vitasafirishwa na treni ya mizigo siku ileile.  Kwa vile treni za mizigo hazikuwa na ratiba maalumu tulilazimika kuweko palepale ili tuhakikishe vyombo vyetu kweli vimeanza safari. Treni za mizigo  kadhaa zilifika na kuondoka na mabehewa kadhaa ya mizigo yaliyokuwepo pale yaliunganishwa na kuondoka, lakini behewa letu likawa haliunganishwi, tulipouliza sababu tukaambiwa kuwa kulikuwa na tatizo la mipira ya breki. Tulishinda pale mchana ule na usiku ukaingia tukiwa pale pale na tukakesha pale tukiumwa na mbu na kuteswa na baridi kali. Kesho yake wanamuziki wenzetu walipata nafasi katika treni la abiria na kuanza safari ya kuelekea Mwanza, sisi wawili na behewa letu la vyombo tukaingia siku ya pili pale kituoni. Hatimae mtu mmoja akatushtua kuwa tusipoangalia tutafikisha hata wiki moja pale, tumtafute muhusika na kumpa fedha kidogo mipira breki itapatikana, tukafanya hivyo na mipira kweli ikapatikana kimiujiza. Behewa letu liliunganishwa kwenye treni ya mizigo na safari ikaanza. Kwa vile ilikuwa ni treni ya mizigo, mimi na mwenzangu tukaingia kwenye kichwa cha treni, nauli tukamlipa dreva wa treni, kwa mara ya kwanza nikaweza kuona jinsi dreva wa treni anavyoendesha treni. Safari ilikuwa nzuri, ila kila tulipokaribia katika kituo, tulilazimika kuingia sehemu ya injini kujificha, kwani dreva hakuwa anaruhusiwa kubeba abiria. Kwa kweli kule ndani kwenye sehemu ya injini kunatisha mno. Tuliingia Mwanza kama saa tano mchana na siku hiyo ilikuwa siku ya sikukuu ya Iddi.  Bendi ilikuwa imeshatangaza kuwa ingefanya onyesho la mchana katika Uwanja wa Kirumba na usiku bendi ingepiga ukumbi wa Shinyanga Hotel. Onyesho la Kirumba lilifanyika vizuri likaisha saa 12 jioni, vyombo vikahamishwa na kupelekwa  kwenye ukumbi wa Shinyanga Hotel ambako onyesho jingine lilianza saa tatu usiku mpaka usiku wa manane. Tulipoanza tu onyesho, akaonekana mtu mmoja anapiga picha za video, onyesho likasimama na kukaweko ugomvi mkubwa kumzuia mpiga video kwani alikuwa hajatuomba ruksa,  hatimae aliruhusiwa kutupiga video baada ya kutulipa shilingi alfu kumi na tatu. Wanamuziki tukagawana shilingi mia tano kila mmoja na .

Baada ya kufanya maonyesho kadhaa  katika kumbi tofauti pale Mwanza ukiwemo ukumbi wa Polisi na ukumbi maarufu  wa Pamba House, bendi ikaendea kufanya onyesho Tarime. Bendi ilisafirishwa na basi la tajiri aliyekodi bendi. Onyesho la Tarime halikuwa na mafanikio sana,  mara baada ya kumaliza onyesho Tarime ilianza safari ya kurudi Mwanza. Baadhi ya wanamuziki walikuwa wamejenga urafiki na wasaidizi wa tajiri aliyekodi bendi, wasaidizi hao wakawaeleza rafiki zao kuwa mpango umesukwa  wa kuitelekeza bendi stendi kuu ya Mwanza, mara baada ya kufika Mwanza wakala angetangaza kuwa basi linaenda ‘service’ hivyo watu na mizigo yote ishushwe. Baada ya hapo basi lingeondoka na lisingerudi tena. Baada ya taarifa hii kufahamika, uongozi wa bendi ukapanga mkakati, kwanza  wanamuziki wangegoma kushuka kwenye basi, na kwa kuwa mkataba ulimtaka wakala kuirudisha bendi Iringa baada ya ziara, bendi ilikuwa tayari kuachana na mkataba kama  wanamuziki wangepelekwa kwenye mgodi wa almasi wa Mwadui. Mgodi wa Mwadui ulikuwa chini ya shirika la STAMICO kama ilivyokuwa kampuni ya Diamond Cutting Company, tulijua kuwa kama tungefika kule ingekuwa kama kufika nyumbani.

Mimi nikaambiwa nishuke pale Mwanza kutafuta mfadhili ambaye angeweza kutukopesha shilingi alfu arobaini, fedha hizi ingekuwa ni mtaji tosha wa bendi kuweza kurudi Iringa kama mambo yasingefana Mwadui. Kweli tulipofika stendi Mwanza,  wakala akatangaza kuwa watu wote na vifaa vyote vishushwe ili basi liende service tayari kwa safari ya kurudi Iringa. Akajibiwa kuwa hakuna haja ya kushusha vyombo kwani havitaingilia service, ugomvi mkubwa ukazuka, hatimae ndipo wakala akaambiwa akitaka aachane nasi basi basi lituache Mwadui, alikubali na basi likaelekea Mwadui……Itaendelea,

Friday, January 13, 2023

MAMBO MOTOOO...MAQUIS ORIGINAL WARUDI JUKWAANI

MAMBO MATAMU YAJA
BENDI kongwe iliyokuwa maarufu sana, Maquis Original itauanza mwaka huu kwa kufanya maonyesho mawili makubwa ya kumbukizi ya enzi zake. Maquis Original awali ilikuwa ikiitwa Maquis du Zaire wakati ikiingia nchini Tanzania kwa mara ya kwanza, ilikuwa ikitokea  mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati huo nchi hiyo ikiitwa Zaire.
 Baada ya kuwasili Tanzania, haikupita muda mrefu bendi ikawa moja ya bendi tishio nchini. Nyimbo za bendi hii hata zile ilizo rekodi mwanzoni baada ya kuingia nchini bado ni nyimbo pendwa kwa waliokuweko enzi hizo na hata ambao wamezaliwa miaka mingi baada ya bendi kuwa imepotea katika ulimwengu wa muziki. Uamuzi wa wanamuziki wa bendi hii kujikusanya na kufanya maonyesho yao hakika ni faraja kubwa kwa wapenzi wa bendi hii. Bendi itafanya maonyesho mawili. Onyesho la kwanza litakuwa tarehe 21 Januari 2023 katika ukumbi wa Break Point Makumbusho na tarehe 27 January katika ukumbi wa Royal Village Dodoma

Hebu tukumbuke enzi hizo kwa kuangalia tangazo la dansi la Orchestra Maquis miaka hiyo ambalo nina uhakika litaleta kumbukumbu kwa wapenzi wa Maquis wa enzi hizo za Mtindo wa Telemka Chekecha Scania LBT III, wakati huo gari za Scania ndizo zilikuwa maarufu nchini na Scania LBT III ilikuwa gari yenye saiz kubwa kuliko zote, na ndio yenye kusifika zaidi. Maquis walikuwa na ufadhili wa kampuni hiyo ya magari, ukumbi wa nyumbani wa bendi hii wakati huo ulikuwa ukumbi wa White House uliokuwa Ubungo. Karibuni tena wapenzi wa White House mchangie, mambo yalikuwa mazito chini ya uongozi wa Chinyama Chiyaza ambae alikuwa mpiga Saxophone katika bendi. Wakati huu Maquis ilikuwa na maendeleo makubwa sana ya kuwa na mashamba, magari, matrekta na hata kuwa na Kota zake pale Sinza Palestina. Hebu angalia majina ya wanamuziki waliokuwa kwenye bendi hiyo, wote walikuwa miamba ya muziki.

Saturday, November 5, 2022

HISTORIA FUPI YA TAARAB YA TANGA

Marehemu Waziri Ally akiwa mdogo akiwa anapiga kinanda katika bendi ya Lucky star

Katika miaka ya 50 wanawake tisa wa Tanga walijikusanya na kuanzisha  kikundi cha kuimba walichokiita Raha til Fuad maana yake Raha ya Moyo. Akina mama hawa chini ya bibie aliyeitwa Mama Akida au aka Mama Lodi, waliendesha kikundi chao wakiwa wanaimba nyimbo za Siti Binti Sadi na tungo zao ambazo waliimba katika melody ya nyimbo za kihindi zilizotamba wakati huo. Kundi hili liliendelea na kuanza kuruhusu wanaume kujiunga hasa wakiwa wapiga vyombo. Hata mtoto wa Mama Akida, Akida Jumbe hatimaye alijiunga na kundi hili kama mpiga accordion kwenye mwaka 1962. Kundi hili ambalo baadae lilikuja kuitwa Young Noverty, liliendelea mpaka kukaweko na mgawanyiko uliozaa kundi la Shaabab Al Waatan ambalo lilitawaliwa zaidi na wanaume.
 Hapo ndipo kukaanza mtindo wa kuweko kundi pinzani katika muziki wa taarab wa Tanga. Jambo ambalo kwa njia ya ajabu sana kwa kipindi kirefu likawa  linadumu kiasi cha miaka kumi kumi. Miaka ya 60, Young Noverty na Shabaab al Waatan, Miaka ya 70 Lucky Star Musical Club na Black Star Musical Club, miaka ya 80 Golden Star Taarab na White Star Taarab, miaka ya 90, Babloom Modern Taarab na Freedom Modern Taarab. Taarab ya Tanga kwa kweli ndio  haswa inastahili kuitwa Modern Taarab, kwani wao hawakufuata Taarab ile iliyoletwa Zanzibar enzi ya Sultan Seyyid Barghash.
Taarab ya Tanga ilikuwa ni ya makundi  yenye wanamuziki wachache kuliko makundi ya Taarab ile ya Zanzibar.
Vyombo vya vikundi vya Taarab ya Tanga
vilikuwa ni pamoja na Gitaa la besi, gitaa la solo, drums bongos ,akodion au kinanda. Nyimbo zao zilikuwa fupi na si ndefu kama zaTaarab ya Zanzibar au ambayo huitwa Taarab asili. Nyimbo za Taarab ya Tanga zilitegemea mipigo ya ngoma za asili za kumbwaya na chakacha na hata baadaye mitindo kama rumba,bossa nova. Na Taarab ya Tanga ndio iliyoanzisha moto wa vikundi vya taarab Tanzania Bara. Moshi kulikuwa na New Alwatan, AzimioTaarab, na Blue Star Taarab , Arusha kulikuweko na Blue Star Taarab, Dodoma ilikuwepo Dodoma Stars, Kondoa  kulikuwa na Blue Stars, Mbeya kulikuweko na Magereza Kiwira, Mwanza kulikuwa na Ujamaa Taarab, Bukoba  walikuwa na Bukoba Stars, na muendelezo huu uliingia mpaka Burundi kutokana na mwana muziki mmoja alie julikana kama Athmani Mkongo, alitoka Burundi na bendi yake kufika Tanga akahama kutoka muziki wa dansi na kuwa mwanamuziki mahiri wa Taarab na baadae kuipeleka kwao Burundi kukazaliwa kundi maarufu la Jasmine Taarab.


Thursday, November 3, 2022

MKOANI PIA KUNA WANAMUZIKI WAKALI, KWANINI WANATENGWA?

 

Kila jamii ina muziki, kuna aina mbalimbali za muziki na zenye matumizi mbalimbali, kadri ya utamaduni wa jamii husika.
Katika zama hizi hasa mijini, muziki huonekana hasa kazi yake ni kwa kuleta burudani. Lakini kwa asili katika jamii zetu mbalimbali muziki ulikuwa na matumizi ya aina nyingi na hata kupewa majina kutokana na shughuli husika.
Kati ya shughuli ambazo muziki ulitumika na sehemu  nyingine bado unatumika ni kwenye  matambiko, tiba,  misiba, sherehe mbalimbali kama mavuno, harusi na kadhalika.
Leo niongelee muziki na siasa za nchi yetu.
Kabla ya Uhuru, katika maeneo mbalimbali nchini, wanamuziki kama marehemu Mzee Moses Nnauye walianzisha vikundi vya muziki kuhamasisha kudai Uhuru, vikundi vya kwaya, ngoma za asili, na muziki wa taarab na muziki wa dansi, vilitunga nyimbo zenye ujumbe  ambao uliwafikia vizuri wananchi wengi na hivyo  kuwahamasisha kuwa wana haki ya kujitawala na kuanza kudai Uhuru.
Mara baada ya kupata Uhuru,Disemba 9 1961, vikundi vya muziki  vilitunga nyimbo zilizoongelea furaha ya kupata Uhuru na pia kuanza kuelezea ndoto za  wananchi baada ya uhuru. Mahusiano ya muziki na siasa yaliongezeka sana, na baada ya Tanzania kuamua kuwa nchi ya Kijamaa, serikali iliwekeza sana katika sanaa, kwani ilitambua kuwa hiyo ilikuwa njia muhimu ya kufikisha taarifa ya malengo ya serikali. Pamoja na kuweko majengo yalikuwa maalumu kwa ajili ya maonyesho ya muziki, pia yalihamasishwa mashindano, matamasha na maonyesho ya aina mbalimbali ya muziki kila kona ya nchi.

Watu waliokuwa vijana na watoto katika miaka ya 60, 70, na 80 wanaweza kukueleza hadithi ndefu jinsi walivyokuwa wakishiriki kwa namna moja au nyingine katika nyimbo mbalimbali zilizohusu mambo ya nchi yao. Kulikuwa na shughuli za muziki kuanzia ngazi ya vijiji, mada mbalimbali zilitungiwa muziki kwa kutumia muziki wa asili, kwaya na muziki wa kisasa. Kwa njia hiyo taarifa za mambo mbalimbali zilieneka kila kona ya nchi japokuwa mawasiliano ya umma  yalikuwa hafifu mno kulinganisha na zama hizi.
 Kulikuweko na Maafisa Utamaduni wa Wilaya na Mkoa nchi nzima, na maafisa hawa wakahamasisha kuanzishwa vikundi vya muziki wa aina mbalimbali kwenye sehemu za kazi, shuleni, vijijini na kadhalika.  Taasisi za serikali na mashirika ya umma vilihamasishwa kuanzisha vikundi vya sanaa, na ndipo kukawepo kundi la sanaa la Taifa, vikundi vya sanaa majeshini ambapo huko pia kukawa na vikundi vya taarab na dansi, mashirika kama Bima, DDC, URAFIKI, TANCUT na mengine mengi yakawa na vikundi vya sanaa vizuri sana, Kurugenzi za mikoa Dodoma na Arusha nazo zikaanzisha vikundi, Umoja wa Vijana wa TANU nao ukawa na vikundi ikiwemo bendi yake maarufu Vijana Jazz band. Vikundi vyote hivyo vilishiriki sana katika kuimba nyimbo mbalimbali za maisha katika jamii na pia siasa, na maendeleo na nchi. Katika mfumo huo walikuja kupatikana akina Mzee makongoro , Mzee Mwinamila, John Komba na kadhalika.  
Viongozi wa ngazi mbalimbali walivitembelea vikundi vilivyo chini ya himaya yao kuvikagua navyo viljitayarisha kuonyesha umahiri wao, hivyo nchi nzima ilichangamka kwa ubunifu katika muziki wake.

Katika ziara ambazo zilichukuliwa kwa uzito mkubwa na  vikundi vyote, zilikuwa ziara za viongozi wakuu wa  nchi. Mazoezi yalikuwa makubwa, kwaya zilitunga nyimbo mpya, ngoma zilitunga nyimbo mpya, bendi na vikundi vya taarab vilitunga nyimbo mpya, kila moja ilijitahidi kwa umahiri ili tu kupata nafasi kuonyesha kazi mbele ya umma na viongozi hao wakuu. Na hakika kabla ya kiongozi kuanza shughuli au  hotuba, wanamuziki waliburudisha umma kwa kazi zao. Ni katika mfumo huo ambapo wanamuziki kama Bi Shakila walipogunduliwa. Ilikuwa ni siku Mwalimu Nyerere alipotembelea Pangani na Shakila akawa mmoja wa wanamuziki wa pale Pangani walioweza kutumbuiza mbele ya Mwalimu Nyerere, na umahiri wake kugunduliwa. Na hali kadhalika wasanii wengi waliokuja kuwa maarufu walionekana kwanza katika maonyesho mbele ya viongozi wakuu.
Machifu wengi wa zamani walitumia wasanii kupata taarifa za hali ya utawala wao. Wasanii wachekeshaji na wanamuziki waliweza kutunga vichekesho au nyimbo zilizokuwa zikielezea ukweli wa jinsi wananchi walivyokuwa wakijihisi wakiwa chini ya Chifu wao, nae alichukua ujumbe huo uliokuwa ukionekana kama utani au wimbo mzuri na kuufanyia kazi.
Zama hizi za dot com mambo ni tofauti sana, ni jambo la kawaida kabisa viongozi wa juu wakiwa katika ziara zao nchini,  kusindikizana na wanamuziki ‘maarufu’ Kitaifa.  Hali hii ya kuletewa msanii ‘maarufu’ kutumbuiza ‘nyumbani kwao’  na kuwadharau wasanii wenyeji ina waacha wasanii wenyeji wakijiuliza maswali kuhusu thamani yao mbele ya kiongozi huyo mkuu. Taratibu hii mpya pia inamyima kiongozi mkuu fursa ya kuona sura nyingine ya sanaa za wananchi anaowaongoza,  na muhimu zaidi anakosa kusikia ujumbe mpya kutoka kwa wananchi wa sehemu anayozuru.
Nina imani kabisa kabisa kuwa wasanii wote wana haki sawa mbele ya viongozi wakuu, hivyo si haki kudharauliwa kwa kipimo cha umaarufu wa kibiashara.

 

 

 

 

 

Monday, October 3, 2022

USHIRIKINA KATIKA MUZIKI HISTORIA NI NDEFUUUU


Imani ya uchawi ni utamaduni ambao umekuweko katika historia ya jamii zote za binadamu. Maandiko ya dini mbalimbali yanatuhakikishia kuwa jambo hilo lipo na hulilaani. Mara nyingi hudhaniwa kuwa kadri maendeleo na elimu yanavyoongezeka ndio imani ya ushirikina inavyopungua na kupotea, lakini ni wazi dhana hiyo si ya kweli, safari ya kuachana na uchawi bado ni ndefu sana, kwani ukipita katika mitaa mingi utaona vibao vikiashiria waganga wanaoweza kutibu matatizo  mbalimbali kama ‘kusafisha nyota’, ‘kuondoa majini’, ‘kurudisha mpenzi aliyekimbia’ na kadhalika, wasomi wenye milolongo ya shahada na stashahada si ajabu kabisa nao kuwakuta kwenye vibanda vya waganga wakitafuta kusaidiwa kwenye mambo ambayo  mtu mwingine ungetegemea yanawezekana kwa juhudi tu za kibinadamu.

Muziki haujakwepa kuguswa na dhana ya ushirikina. Muziki unatumika unatumika katika kufanikisha dhana ya uchawi na wanamuziki wengi wanaamini na kushiriki katika shughuli mbalimbali za uchawi.

Tuanze na dhana ya muziki iliyopewa jina la Kiingereza ‘ healing music’. Duniani kote waganga na wachawi hutumia muziki wa aina yake kupandisha mashetani au kuita mizimu na kadhalika, muziki huu ndio huitwa healing music, huku kwetu mara nyingine huitwa muziki wa kupandisha mashetani. 

Katika maisha yangu ya muziki niliona na kusikia vituko vingi vilivyohusishwa na imani ya uchawi. Mara ya kwanza kuanza kuona vitimbi hivi ‘live’ ni nilipojiunga bado mdogo na kuwa mwanamuziki katika bendi yetu ndogo huko Iringa. Tualianza kupiga muziki wenyewe wachache bila kuwa na wazo lolote la kuhusisha muziki wetu na imani yoyote ya kishirikina. Siku moja akaja mzee mmoja akatukaribisha kufanya mazoezi kwenye sehemu yake ya biashara, na kwa vile tulikuwa hatuna sehemu maalumu tuliona huu ni ufadhili mkubwa.  Tulihamishia vyombo vyetu vichache kwake, na haikuchukua muda mrefu tukagundua kuwa biashara yake ni uganga wa kienyeji. 
Siku moja akatueleza kuwa hatutaweza weza kuwa bendui kubwa bila ‘kusafishwa nyota’. Tulipewa dawa za kuoga na tukaendelea na mazoezi makali tukijua muda wetu wa kuwa bendi kubwa umewadia. Tulikubaliana kuwa tungepunguza deni la kazi yake ya kutusafisha nyota kwa kumlipa kidogo kidogo kila tulipofanya onyesho, kweli tukaanza kumlipa kila tulipopiga. Sikumbuki ni muda gani tuliendelea kumlipa yule mganga, japo kuwa hakuna chochote kilichobadilika katika hadhi ya bendi yetu.
Siku moja mganga yule alienda disco na akamtishia msichana mmoja kwa nyoka aliyekuwa nae mfukoni, hapo ndipo alipokamatwa na polisi na hatukumuona tena deni likayeyuka.
 Miaka mingi baadae nilikuja kujiunga na bendi moja kubwa jijini Dar es Salaam, hapo ndipo nilipoona tena shughuli za ushirikina. Ilikuwa ni siku chache baada ya kurekodi nyimbo mpya za bendi yetu katika studio za Radio Tanzania. Kulikuwa na kipindi kilichoitwa Misakato , kipindi ambacho kilitambulisha nyimbo mpya zilizorekodiwa na studio za redio hiyo, tulikuwa tumekubaliana kuwa wanamuziki wote tukusanyike nyumbani kwa kiongozi wetu ili wote tuzisikilize nyimbo zetu zikirushwa kwa mara ya kwanza hewani.  Zilipoanza kupigwa nyimbo zetu nikashuhudia mmoja wa viongozi wetu akiwa anaifukiza redio kwa moshi kutoka dawa zilizokuwa zimechomwa kwenye kifuu cha nazi,  hii ilikuwa kwa imani kuwa kwa kufanya hivyo, vibaovyetu vipya vikisikika vitatikisa roho za wasikilizaji wake. Katika kundi hili vituko vingi viliendelea hatimae tulizoea kuwa uongozi wa bendi yetu unaamini sana uchawi. Kuna wakati aliletwa mganga ambaye alidaiwa aliwahi kuifanya timu moja maarufu ya soka, ishinde kombe  na kuwa bingwa wa Taifa, hata jina lake aliitwa Bingwa, kutokana na sifa hizo bendi ilimchukua kwa mkataba na kazi yake ikawa ni kukaa mlangoni akijifanya ni muuza machungwa, hapo alitakiwa afanye vimbwanga vyake ili wateja wengi waingie kwenye muziki. Yeye alidai kila anapomenya chungwa kwa kuunganisha maganda kama mkanda, basi na wateja nao wataingia katika ukumbi kwa kuunganika kwa foleni ndefu, huyu alikaa nasi kiasi cha kuweza kuwa  katika misafara mbalimbali ya bendi tulipoenda ziara za mikoani. Harakati za bendi kutafuta umaarufu kwa uchawi ilifikia mpaka bendi ikasafiri hadi kwenda Mpanda, ambako viongozi wa bendi walikwenda kwa mganga na kufanya mambo yao ambayo yalihusisha na hata kumchinja mbuzi. Baadae walirudi na nyama ya mbuzi huyu mpaka tulipokuwa tumefikia, nadhani masharti yalikuwa ni sisi wanamuziki wote tule kipande cha mbuzi yule wa kafala. Sijajua mpaka leo viongozi walifanya nini na nyama ya mbuzi yule maana wanamuziki walifanya mgomo wa kumla yule mbuzi.
 Ushirikina una matatizo ya kufanya watu wasiaminiane hata kwenye bendi yenyewe, haikuchukua muda mrefu bendi ilipoanza kupoteza umaarufu, Kiongozi wa bendi akaaitisha mkutano na kutuambia kuwa kuanguka kwa bendi kunatokana na mmoja wetu kuiloga bendi, hapo ikatolewa tishio kuwa mtuhumiwa asipojitaja mwenyewe na kuomba msamaha mganga aliyeagua hilo aliahidi atamfanya awe kichaa. Jambo ambalo liliungwa mkono na wote kuwa kama ni kweli kuna mtu namna hiyo basi apate uchizi. Hakuna aliyekumbwa na tatizo hilo mpaka leo.
Miezi michache baadae, wanamuziki wawili walioamua kuacha bendi walirudisha sare za bendi kama ilivyokuwa kawaida zama zile. Shati zilikuwa zimechanywa kwenye kwapa na suruali kuchanywa kwenye maungio ya miguu kwa imani kuwa hizo ndizo sehemu zenye jasho kwa hiyo kama wangerudisha sare zao bila kuondoa sehemu hizo wangeweza kurogwa kirahisi na kuharibiwa maisha.

Mpiga tumba mmoja tuliyekuwa nae bendi moja alinichekesha aliponihadithia kuwa kiongozi wa bendi yao moja aliyopitia, aliwahi kuwapeleka kwa mganga aliyewataka waende na vyombo vyao vya muziki. Kisha akawa ana chanja chombo na kukipaka dawa,na baada ya hapo kumchanja mwenye chombo matakoni na kumpaka dawa!!!!
Katika mizunguko kwenye bendi mbalimbali, siku moja bendi yetu ilikuwa na mpambano wa kupiga bendi zaidi ya moja katika ukumbi mmoja. Hili lilichukuliwa kuwa ni jambo kubwa na la hatari linalohitaji matayarisho,  mganga maalumu lazima atafutwe ili kuilinda bendi isimalizwe na wapinzani. Ilikuwa inaaminika kuwa katika mpambano wa bendi, uchawi hutumika kuimaliza bendi ambayo itakuwa haina kinga, siku moja kabla ya pambano, maboksi ya spika yalifunguliwa na ndani yake  kuliwekwa tunguli na hirizi mbalimbali tayari kwa mpambano. Nakumbuka siku hiyo bendi pinzani nayo iligoma kupanga vyombo kwenye jukwaa kuu kwa madai kuwa kuna mbuzi alifukiwa katika jukwaa lile.

Kwa ukweli kabisa hata wanamuziki kutembeleana mara nyingine ilikuwa ni vigumu, kwani ukionekana mwanamuziki wa bendi nyingine katika ukumbi, basi bendi iliyo jukwaani haina raha, anaweza hata akatumwa mtu kufuatilia kila utakachofanya. Na ilikuwa vigumu kuruhusiwa kugusa vyombo vya bendi nyingine kwa wasiwasi wa kuwa unaweza ukaloga kile chombo. Niliwahi kuona bendi ikisimamisha muziki katikati ya onyesho na kudai shabiki mmoja wa bendi pinzani, tena alikuwa mwanamke, atolewe ukumbini kwani alikuwa ametumwa kufanya ushirikina, na hakika alitolewa nje.

Kulikuwa na hadithi nyingi zilizoonyesha ni kiasi gani cha ushirikina bendi ziliweza kufanya ili kupata wateja. Kuna bendi ambayo ilisifika kuwa kila wakimaliza kupiga muziki walipita katika kumbi mzima  na kuokota vizibo vya chupa za bia na soda, mifupa na mabaki ya nyama zilizotupwa na wateja, na hata kupata maji toka vyoo vya ukumbi na kwenda kuloga ili wale walioingia wasiingie bendi nyingine yoyote kasoro yao. Bendi nyingine zilidaiwa kuwa ziliweka mkataba ambapo zililazimika kutoa kafala ya mtu mmoja kila mwaka, hivyo viongozi wa bendi kufiwa na watoto, ndugu na hata wanamuziki wageni waliojiunga katika bendi hizo kukutwa na mauti ambayo habari za chini chini zilidai ni katika kutoa kafala.

 

Bendi mbili ambazo zilikuwa na upinzani mkubwa katika jiji la Dar es Salaam zilidaiwa hata kutaka kuweka uchawi katika chanzo cha maji Dar es Salaam , na kujikuta wakitaka kuumbuana hadharani kuhusu hilo.
Kuna wanamuziki wapiga magitaa wa zamani waliowahi kupatwa na matatizo ya akili na wazee wengi mpaka leo hudai matatizo yao yalitokana na ushindani wa uchawi katika bendi zao. Kama nilivyosema imani ya uchawi huleta kutokuaminiana na hata madhara makubwa ya kutuhumiana mambo ambayo mara nyingi hayana ukweli wowote. Kuna mwanamuziki niliyejaribu kumshawishi aingie katika bendi niliyokuwa nikipigia , alikataa katakata kwa kuwa alidai mmoja wa wanamuziki katika bendi hiyo ni mchawi.
Mwanamuziki mmoja mpiga gitaa mahiri aliwahi kunihadithia jinsi alivyopita uchochoro wa nyumba ya mwanamuziki mwenzake akashangaa kusikia jina lake likitajwa na mwenzie aliyekuwa chumbani kwake na kusema,’ Nyota ya …….(jina la mwanamuziki huyo) izimike kama kaa hili’, akadai alichungulia katika ufa na akakuta mwenzie anatumbukiza kaa la moto kwenye maji.
Ugonjwa wa ukimwi ulipoanza kuuwa wanamuziki kwa mara ya kwanza mara nyingi ulihusishwa na uchawi. Rafiki yangu mmoja nilipomtembelea wakati akiwa hoi kitandani akanambia,’Nikupe siri? Mi ntakufa lakini nauawa na wanamuziki wenzangu kwenye bendi. Nimepata mganga kanitajia na majina kabisa’. Miezi michache baadae mwanamuziki huyu kabla hajafariki alinambia,’Mjomba sijalogwa wala nini, udude huu, unaniua udude’. Alifariki siku chache baada ya kunambia haya.
Kama nilivyosema awali, elimu na teknolojia hazijaondoa kabisa dhana ya uchawi. Siku moja nilimsikia producer maarufu akiwakanya wasanii wa muziki wa Bongofleva wanaoingia studioni mwake, wasifanye mambo ya ushirikina kwenye studio yake.

Na siku chache baada ya hapo tena mwanamuziki mwingine wa muziki huo kawataja ambao aliwaita wabaya wake wanaomloga.!!!!!!! Nikaona loh kumbe shughuli bado inaendelea, wanamuziki hawa wenye umri mdogo tayari wamekwisha jenga imani ya kulogana katika enzi hizi za dijitali, safari bado ndefu sana, USHIRIKAINA BADO UKO HAI KATIKA SANAA YA MUZIKI

Monday, September 12, 2022

MITINDO ILITAMBULISHA BENDI NA MUZIKI WAKE

 



Katika miaka ya karibuni, utamaduni wa kila bendi kuwa na mtindo wake umefifia sana. Lakini ulikuwa utamaduni uliokuwa maarufu sana kuanzia miaka ya sitini. Kila bendi ilipoanza, ilijinasibu kwa kuja na mtindo wake, ingekuwa siku hizi ingetambulika kama kuji ‘brand’.
Ni vigumu kutaja mitindo yote iliyowahi kugunduliwa kwani kuna mingi ambayo haikuwahi kupata nafasi kutambuliwa katika vyombo vya utangazaji au kuwekwa  katika kumbukumbu za aina yoyote. Majina ya mitindo mingine ilikuwa na sababu au historia na maana maalumu, lakini majina mengine yalikuwa ya kutunga tu na kwa kweli hata waliokuwa waliokuwa wakiyatumia hawakuwa na maelezo ya maana ya maneno hayo. Nakumbuka nikiwa bado mwanamuziki mdogo huko Iringa tulikuwa na bendi ambayo mtindo wake ulikuwa ni Chikwala chikwala, namkumbuka aliyetunga jina hili, alikuwa mpiga gitaa la rhythm ambaye pia alikuwa fundi saa. Hata yeye hakuwa na maelezo ya maana kuhusu jina lile, ila kwa wakati ule, ilikuwa ni staili kwa majina ya mitindo  ya bendi kuwa na jina linalojirudia rudia, hii ilitokana na bendi kadhaa Kongo kuwa na majina yaliyojirudia rudia mfano Orchestra Lipua Lipua, Orchestra Bella Bella na Orchestra Shama Shama.
Baadhi ya majina ya mitindo ya bendi yalikuwa Mundo, Saboso,  Msondo, Sokomoko, Dondola, Toyota, Kiweke, Segere matata, Super mnyanyuo, Vangavanga, Libeneke, Chakachua, Sululu, Ambianse, Takatuka, Afrosa na majina mengineyo mengi. Bendi nyingi zilibuni hata aina ya uchezaji wa mitindo yao, na uchezaji mwingine ulibuniwa hata na wapenzi wa bendi hizi. Kila bendi ilikuwa ikijitahidi kuwa tofauti na bendi nyingine. Kwa mfano katika mji wa Tanga ulikuwa na bendi kubwa mbili, Jamhuri Jazz Band na Atomic Jazz Band, kuna wakati bendi ya Jamhuri ilikuwa na mtindo wa Toyota, na baadae Dondola, wakati  Atomic walikuwa na mtindo wa Kiweke, muziki wao ulikuwa tofauti, hivyo Jamhuri ikawa na wapenzi wake na Atomic ikawa na wapenzi wake, na mpaka leo, wazee waliokuwa wapenzi wa bendi hizi mbili hubaki kusifia ubora wa bendi zao, wazee wa Jamhuri husifu mtindo wa upigaji wa gitaa la rythm la Harrison Siwale(Satchmo), huku wapenzi wa Atomic watakwambia hakuna kama Kiweke, kwani upigaji wa gitaa la solo wa John Kijiko, au bass la Mwanyiro haukuwa na mpinzani. Kule Morogoro kulikuwa na Morogoro Jazz Band na Cuban Marimba, bendi hizi zilikuwa na mitindo mbalimbali kwa nyakati mbalimbali, na wapenzi wao walikuwa tayari kutetea ubora wa mitindo ya bendi zao. Cuban Marimba wakisifia mtindo wa Ambianse, Morogoro wakisifia Likembe, au sululu. Na hakika kulikuwa na tofauti kubwa ya mitindo hii miwili japo ilipigwa na bendi zilizotoka mji mmoja.
Nimeanza kwanza kwa kutaja bendi zilizokuwa katika mji mmoja, tena huko mikoani ambako kwanza miji ilikuwa bado na watu wachache kulinganisha na sasa, wanamuziki walikuwa wanajuana na kuishi jirani, hali hiyo ndio iliyokuwa Tabora, ambako pamoja na Tabora Jazz, kulikuweko na Nyanyembe Jazz, Kiko Kids, lakini muziki wa kila bendi ulikuwa tofauti na mwingine. Dar es salaam kulikuwa na bendi nyingi na hivyo mitindo mingi, na pia kulikuwa na bendi za watu wa mataifa kutoka nje ya Tanzania. Kulikuwa na bendi za Magoa, kulikuwa na bendi za Wakongo, nao pia wakawa na mitindo yao.  Hakuna aliyeweza kuchanganya mtindo wa Ogelea piga mbizi ya  Maquis na mtindo wa Chunusi wa  Orchestra Safari Sound, hata pale ambapo wanamuziki wa kutoka bendi moja walipohamia bendi pinzani kila bendi ilibaki na staili yake na kuilinda kwa kuongeza ubora kila mara. Hivyo haikuwezekana ukasema  Sikinde na Msondo zilipiga muziki uliofanana au mitindo ya Sokomoko na Afrosa ilikuwa na ukaribu. Kikubwa ninachotaka kueleza ni kuwa bendi kuwa na mtindo ilikuwa si jina tu bali kulikuweko na kazi ilifanyika ili kupata, kulinda na kuendeleza mtindo ambao bendi iliamua kuwa nao. Nakumbuka wakati wa mazoezi enzi hizo unaweza ukatunga wimbo ukianza kuimba wenzio watakwambia mbona unafanana na bendi fulani na hapo utakarabatiwa mpaka uwe katika mtindo wa bendi husika.

Wiki chache zilizopita nilipata bahati ya kuhudhuria onyesho moja la bendi iliyoko Mbeya, baridi ndio ilinilazimisha kukumbuka kuwa niko Mbeya, upigaji, uchezaji, uimbaji wa bendi hii ulikuwa kama bendi nyingi zilizopo Dar es Salaam. Bendi zimekuwa kama vile zimepewa amri kuwa lazima zipige muziki unaofanana. Toka umeingia mtindo wa ‘sebene’ mwanzoni mwaka 2000, basi ni kama kila ubunifu umesimamishwa. Hata zile bendi ambazo hupiga nyimbo za bendi ya zamani, hulazimisha kuingiza sebene, kwenye nyimbo hizo. Juzijuzi kwenye onyesho moja kubwa la muziki, bendi moja ilikuwa ikipiga wimbo wa Super Volcano unaoitwa Shida, ghafla ukabadilika kwa kuongezewa sebene.  Kipindi aina ya muziki wa sebene ulipokuwa ukiingia nchini, kulikuwa na aina ya muziki wa hapa nyumbani uliokuwa unaitwa Mchiriku. Sasa toka wakati huo,Mchiriku umeweza kujiongeza na kubadilika mpaka sasa unaitwa singeli, tena hata hiyo singeli imeanza kuota matawi, lakini wanamuziki wa dansi wamekwama palepale kwenye sebene. Hili linanikumbusha enzi za teknolojia ya santuri, santuri zilikuwa zinaweza kupata mchubuko na hivyo sindano ikakwama sehemu moja, ikawa inarudia kupiga muziki sehemu ileile haiendi mbele wala hairudi nyuma mpaka betri itakapoisha.

Wednesday, August 31, 2022

USUPA STAA NI DHANA YA ZAMANI INAYOBORESHWA NA TEKNOLOJIA

 




Ma ‘superstar’ ni watu ambao wametokea kujizolea umaarufu mkubwa katika jamii. Superstar anaweza kuwa ametokea katika nafasi mbalimbali katika jamii, anaweza akawa mwanasiasa, mwalimu, mkulima au mtu yeyote katika jamii, hapa kwetu sifa hii zaidi huhusiana na wasanii. Sifa ya ‘usupastaa’ imejitokeza zaidi baada ya tasnia ya filamu kukua, jambo ambalo limeenda sambamba na kuongezeka kwa vyombo vya utangazaji.  Na kwa kweli katika zama hizi tunao watu wengi ambao wanapewa sifa  ya ‘u superstar’ katika jamii. Hakuna chuo maalumu cha kufundisha usupastaa kwani umaarufu wa mtu huweza kutokana na sababu mbalimbali. 

Wasanii huingia katika sanaa kwa njia na sababu mbalimbali, wengine huzaliwa na kipaji, wengine huingia katika fani hiyo kama njia ya kutafuta maisha, wengine huingia kwa kuiga wenzao waliomo katika sanaa, kuna hata waliolazimishwa na ndugu na jamaa kuingia katika fani ya sanaa, na kadhalika. Kutokana na sababu hizi mbalimbali za kujiingiza kwenye sanaa, waliomo humu nao wanakuwa na mategemeo mbalimbali yatakayopatikana katika fani hiyo. Wengine nia yao ni kutengeneza sanaa nzuri, bila kujali sifa wala malipo, wengine wanafanya sanaa ili wapate kipato kizuri na wengine wakitegemea sifa tu kutokana na ubora wa kazi yao. Na wengine kutumia sanaa kama jukwaa la kufanyia shughuli nyingine kabisa ambazo hazihusiani na sanaa. Wasanii waliomo katika sanaa kutafuta kipato, hulazimika kutafuta mbinu mbalimbali ili sanaa yao iuzike, na moja ya njia kubwa ya kuhakikisha sanaa inauzika ni kwa wao kuwa maarufu. Watu wengi wanatabia ya kufuatilia maisha na kununua kazi za sanaa za watu maarufu. Kutokana na sababu hii, msanii huanza mbinu mbalimbali za kupata umaarufu. Msanii atajitokeza kwenye vyombo vya habari kutangaza kazi zake na hata kuelezea maisha yake, picha zake nzuri kusambazwa,na hata kazi hizo kusambazwa ili watu wengi wazifahamu.

Katika nchi ambazo tasnia imejengeneka vizuri, kuna makampuni maalumu ambayo hutumia mamilioni ya fedha kujenga sifa za msanii husika na kazi zake, kwa kutegemea faida kubwa baadae. Msanii huingia katika mikataba ya muda mrefu na kampuni huwekeza katika kujenga sifa ya msanii ili kupata wateja wengi wa kazi za msanii huyo.

Je unapataje ‘u super star’ hapa Tanzania? Kama ilivyo duniani kote kuna wasanii ambao kazi zao zimepokelewa vizuri na jamii na kuwafanya wasanii mbalimbali kuwa maarufu kwa urahisi sana. Lakini kuna mambo mengi ambayo yanapita nyuma ya pazia katika kupata ‘u superstar’ hapa kwetu. Rushwa ni moja ya jambo kubwa katika kujenga ‘ma superstar’ wa hapa kwetu. Na hili halikuanza karibuni, kwa wanamuziki wa zamani wanaelewa hali ilivyokuwa enzi kulipokuwa na redio moja tu, ilivyolazimika kutoa rushwa ili mashahiri ya nyimbo walizotaka kurekodi yakubalike na nyimbo zirekodiwe, kisha kutoa rushwa ili nyimbo zilizorekodiwa zipigwe kwenye vipindi mbalimbali huku sifa za kujenga usupastar wa wasanii hao zikimiminika, hali hii haiko tofauti sana na sasa japo kwa sasa kuna utititiri wa redio na luninga. Watangazaji wengi wamefaidika na rushwa kutoka kwa wasanii waliokuwa na hamu ya ‘kutoka’. Kuna wakati watangazi wa redio mbalimbali walitengeneza umoja, ambapo mwanamuziki alikuwa akilipia ili kazi zake zirushwe hewani. Watangazaji wa vipindi vya redio wengi waligeuka kuwa mameneja wa wasanii na hivyo kuhakikisha wanawatangaza wasanii wao ili wawezekuwa ‘ma supersta’. Rushwa ya ngono sio siri katika tasnia ya sanaa katika kutafuta ‘u superstar’ . Wasanii wa kike wengi wana hadithi ya kupitia katika mtihani huu katika kutafuta ‘kutoka’. Kuna wakati wasanii  wawili wakubwa wa kike, walitangaza mpango wa kuanza kuwajenga wenzao ili wasipitie adha ya kudaiwa rushwa hii. Jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa rushwa hii bado iko hai.

Katika kutafuta ‘U superstar’, kuna wasanii ambao wamefanya mambo mengi ya ajabu ikiwemo kutunga visa ambavyo vingewaweka katika vichwa vya habari. Habari za msanii kufumaniwa, kupigwa, kulewa, kulazwa hospitali, kupendana, kuachana na kadhalika vimekuwa vikitungwa na wasanii mbalimbali ili kujiweka katika nafasi ya kutengeneza hadithi kwenye vyombo vya habari kujiongezea umaarufu. Ujio wa mitandao ya kijamii umekuwa tena nafasi nzuri za kutengeneza ‘U superstar’ wasichana ambao wamekuwa wanatumia sanaa kama daraja la kupata ‘U superstar’, wamekuwa wakitumia kurasa zao kwa kutundika picha wakiwa nusu utupu ili mradi kutafuta kujulikana na kupata wateja wa shughuli isiyohusiana na sanaa.

Matokeo ya vurugu hizo zote ni kuwa msanii kuwa ‘superstar’ si lazima awe msanii bora. Wako wasanii wa aina hiyo wengi na ukiulizia kazi zao za sanaa, hazionekani au hazijulikani. Na kwa kazi zao za kisanii ambazo hutolewa hadharani, huishia kupotea baada ya muda mfupi, lakini sifa za ‘u supersta’ zinaendelea kujengwa kwa namna moja au nyingine. Jambo ambalo ni bahati mbaya kwa tasnia nzima ya sanaa, nikuwa masupastaa hawa wajanja wajanja huaminiwa sana hata na viongozi wa ngazi za juu nchini,  na hutumika kama vigezo vya kukua kwa tasnia. Na mara nyingine huombwa hata kutoa ushauri wa namna ya kuboresha tasnia ya sanaa. Mungu isaidie tasnia ya sanaa Tanzania.

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...