Katika aina ya muziki ambao ulisababisha bendi kuanza katika mashule, ilikuwa ni aina ya muziki na kucheza ulioitwa 'jiving'. Shule nyingi zilikuwa na vikundi hivi, sekondari za kike na kiume zilishindana katika jiving. Muziki huu ulikuwa umetoka haswa Afrika ya Kusini. Siasa zikaingilia kati katika miaka ya mwishoni ya sabini na kuuwa jiving katika mashule mengi. Jiving ilikuwa inaambatana mara nyingine na filimbi kama alivyokuwa anapiga Spokes Mashiyane. Mbaraka Mwinyshehe ni matokeo ya muziki huu alikuwa bingwa wa kupiga filimbi. Pichani ni kikundi cha jiving cha Mkwawa High School The Skylarks Jiving Group, akiwemo mwandishi maarufu Danford Mpumilwa (watano toka kushoto) ambaye pamoja na kuwa mwimbaji wa Bendi ya shule hiyo Mkwawa Orchestra, aliendelea mpaka kufikia kuwa na bendi yake mwenyewe pale Arusha.
Katika miaka ya sitini na sabini shule nyingi za sekondari zilikuwa na Bendi (bendi ya magitaa), hata pale Chuo Kikuu Mlimani palikuwa na Bendi nzuri tu katika kipindi hicho, Kuna Bendi za shule nyingine zilipata umaarufu wa Kitaifa kama vile Bendi ya Shule ya Sekondari Kwiro ambayo iliweza kurekodi nyimbo zake Radio Tanzania. Niongelee shule moja nadhani itatoa changamoto ya kupata habari za bendi za namna hiyo katika shule nyingine. Pale Mkwawa high School Iringa ,kulikuwa na bendi mbili. Moja ilikuwa ikipiga muziki wa kiswahili ambayo ilikuwa na wanamuziki kama Sewando kwenye solo, Masanja kwenye rythm, John Mkama Bass,Manji,Danford Mpumilwa mwimbaji, mpiga tumba kwa sasa ni Askofu moja mashuhuri, wakati huo huo bendi ya pili ilikuwa na mwimbaji machachari Deo Ishengoma akiimba nyimbo za James Brown. Bendi hii ilikweza kurekodi RTD pia vibao kama Wikiendi Iringa na Ulijifanya lulu na kadhalika.
Dar Es Salaam pia palijaa bendi nyingi za shule na mitaani. Azania, Tambaza ni kati ya shule zilizokuwa na bendi za vijana katika enzi hizo, wakipiga muziki Jumapili mchana ukiitwa bugi. Bahati mbaya bugi lilipigwa marufuku na kuharibu mfumo mzima wa muziki wa vijana katika historia ya muziki Tanzania. (Pichani ni shule ya Mkwawa wakati huo.)
Tangazo jingine la dansi la miaka hiyo ambalo nina uhakika litaleta kumbukumbu kwa wapenzi wa Maquis wa enzi hizo za Mtindo wa Telemka Chekecha Scania LBT III, wakati huo gari za Scania ndizo zilikuwa maarufu nchini na Scania LBT III ilikuwa gari yenye saiz kubwa kuliko zote, na ndio yenye kusifika zaidi, karibuni tena wapenzi wa White House mchangie, mambo yalikuwa mazito chini ya uongozi wa Chinyama Chiyaza ambae alikuwa mpiga Saxophone katika bendi. Wakati huu Maquis ilikuwa na maendeleo makubwa sana ya kuwa na mashamba, magari, matrekta na hata kuwa na Kota zake pale Sinza Palestina. Hebu angalia majina yaliyopo katika bendi.
Mzee Hamisi Kitambi hatunae tena. Amefariki tarehe 26 Feruary 2010, na kuzikwa tarehe 27 February 2010. Mzee Hamisi Kitambi kwa mara ya mwisho alikuwa bendi ya Msondo Group. Mungu Amlaze pema peponi.(Picha kwa hisani ya ya www.issamichuzi.blogspot.com)