YOUTUBE PLAYLIST

Wednesday, March 3, 2010

Bendi za wanafunzi mashuleni


Katika miaka ya sitini na sabini shule nyingi za sekondari zilikuwa na Bendi (bendi ya magitaa), hata pale Chuo Kikuu Mlimani palikuwa na Bendi nzuri tu katika kipindi hicho, Kuna Bendi za shule nyingine zilipata umaarufu wa Kitaifa kama vile Bendi ya Shule ya Sekondari Kwiro ambayo iliweza kurekodi nyimbo zake Radio Tanzania. Niongelee shule moja nadhani itatoa changamoto ya kupata habari za bendi za namna hiyo katika shule nyingine. Pale Mkwawa high School Iringa ,kulikuwa na bendi mbili. Moja ilikuwa ikipiga muziki wa kiswahili ambayo ilikuwa na wanamuziki kama Sewando kwenye solo, Masanja kwenye rythm, John Mkama Bass,Manji,Danford Mpumilwa mwimbaji, mpiga tumba kwa sasa ni Askofu moja mashuhuri, wakati huo huo bendi ya pili ilikuwa na mwimbaji machachari Deo Ishengoma akiimba nyimbo za James Brown. Bendi hii ilikweza kurekodi RTD pia vibao kama Wikiendi Iringa na Ulijifanya lulu na kadhalika.

Dar Es Salaam pia palijaa bendi nyingi za shule na mitaani. Azania, Tambaza ni kati ya shule zilizokuwa na bendi za vijana katika enzi hizo, wakipiga muziki Jumapili mchana ukiitwa bugi. Bahati mbaya bugi lilipigwa marufuku na kuharibu mfumo mzima wa muziki wa vijana katika historia ya muziki Tanzania. (Pichani ni shule ya Mkwawa wakati huo.)


Tuesday, March 2, 2010

Swali la Leo

Bendi gani iliimba wimbo- Mali ya mwenzio sio mali yako? Na dongo lilikuwa likielekezwa kwa nani?

Chinyama Chiyaza

Tangazo jingine la dansi la miaka hiyo ambalo nina uhakika litaleta kumbukumbu kwa wapenzi wa Maquis wa enzi hizo za Mtindo wa Telemka Chekecha Scania LBT III, wakati huo gari za Scania ndizo zilikuwa maarufu nchini na Scania LBT III ilikuwa gari yenye saiz kubwa kuliko zote, na ndio yenye kusifika zaidi, karibuni tena wapenzi wa White House mchangie, mambo yalikuwa mazito chini ya uongozi wa Chinyama Chiyaza ambae alikuwa mpiga Saxophone katika bendi. Wakati huu Maquis ilikuwa na maendeleo makubwa sana ya kuwa na mashamba, magari, matrekta na hata kuwa na Kota zake pale Sinza Palestina. Hebu angalia majina yaliyopo katika bendi.

Monday, March 1, 2010

Swali la Leo

Swali la leo......... Bendi gani ilipiga wimbo wa Banchikicha? Kwa msaada tu bendi hiyo ilishinda mashindano ya Bendi Bora Tanzania 1973

Sunday, February 28, 2010

Kina nani hawa?


Leo natoa picha 3 za wanamuziki maarufu wakati wakiwa bado makinda, swali ni akina nani hawa?


Saturday, February 27, 2010

Mzee Hamisi Kitambi Hatunae Tena


Mzee Hamisi Kitambi hatunae tena. Amefariki tarehe 26 Feruary 2010, na kuzikwa tarehe 27 February 2010. Mzee Hamisi Kitambi kwa mara ya mwisho alikuwa bendi ya Msondo Group. Mungu Amlaze pema peponi.(Picha kwa hisani ya ya www.issamichuzi.blogspot.com)

Friday, February 26, 2010

Wana Bantu Ngoma wanakula miziki

Bantu Group chini ya Komandoo Hamza Kalala imekwisha toa wakali wengi katika anga la muziki hapa Tanzania. Komandoo mwenyewe ana historia ndefu ikiwemo ya kuwa moja wa waanzilishi wa Bendi ya Vijana chini ya mkongwe John Ondolo Chacha. Amekwishapitia bendi kama Matimila na kushiriki vibao vikali kama Alimasi, amepitia UDA na ikawa katika anga za juu kimuziki Tanzania wakati wake. Komandoo hatasahauliwa na vibao alivyopiga Vijana kama Mary Maria , mpini wake wakati wa Pambamoto Awamu ya pili haujarudiwa tena. Kibao chake Nimekusamehe lakini sitakusahau cha Washirika Stars ni picha tosha ya kazi za Hamza. Pichani ni Juni 1, mwaka 1996. Kwenye onyesho kubwa la Siku ya Mazingira ambalo ndilo lilikuwa onyesho la kwanza la muziki 'live' kuonyeshwa na ITV. Na lilirushwa kwa muda wa masaa kama 6 wananchi wakipiga simu lilendelee hewani!!!!. Wasanii kama MR2 walipata umaarufu mkubwa baada ya tamasha hili pale Mnazi Mmoja. Tamasha liliendeshwa na CHAMUDATA chini ya Mwenyekiti John Kitime.
Picha ya chini tunamwona watatu toka kushoto Eddy Sheggy, na mwishoni ni Rogart Hegga ambaye kwa sasa yuko Twanga Pepeta.

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...