YOUTUBE PLAYLIST

Wednesday, May 19, 2010

Magwiji wa kweli

Hawa wanamuziki kama unavyowaona wanapiga saxophone , walikuwa na mengi zaidi wanafanana walikuwa pia wanaweza kupiga vizuri vyombo vingine, japo hawakuwahi kuwa bendi moja lakini wote waliwahi kuwa katika bendi zilizorekodi muziki ambao unapendwa mpaka leo ni akina nani na walipiga vyombo gani na walipitia bendi gani?

Simba wa Nyika

Tanga ni mji ambao umekuwa chimbuko la mambo mengi katika ulimwengu wa muziki. Hata muziki wa dansi uliingia nchini kupitia Tanga. Kilimo cha katani chini ya mpango wake wa SILABU (Sisal Labourers Beureau) iliwezesha watu kutoka sehemu mbalimbali kukutana Tanga kwa ajili ya ajira ya kukata mkonge, na hivyo mchanganyiko huo wa makabila ulileta uchangamfu wa kimuziki katika jiji la Tanga mapema sana kuliko miji mingine. Kati ya mazao ya Tanga ni bendi maarufu ya Simba wa Nyika ambayo wanamuziki wake walitoka Tanga na kuweka makao yao kwa muda Arusha wakiitwa Arusha Jazz na mtindo wao Wanyika. Vijana hawa walipohamia Kenya wakajiita Simba wa Nyika na waliwasha moto wa nyika kimuziki na nyimbo zao tamu. Hapa ni picha yao mojawapo.

Kitendawili tena

Naleta picha nyingine ya wanamuziki wa zamani, bahati mbaya kuna mmoja katika picha hii amekwisha tangulia mbele ya haki, wa kwanza kushoto ni Salim Willis, drummer, na baadae mpiga gitaa wa Afro70, wa kwanza kulia ni mwanamuziki wa toka enzi hizo na mpaka leo bado yuko jukwaani je unamfahamu ameshiriki katika miziki mingi inayopendwa sana. Unakumbuka bendi alizopitia?

Tuesday, May 18, 2010

Afro 70

Afro 70 wakati wako juu. Waimbaji Monte Gomes na Steven Balisdya (alikuwa pia anapiga drums), Dick Unga,Shabby Mbotoni(alikuwa pia anapiga saxophone na bass). Magitaa Patrick balisdya, Owen Liganga(second solo), Salim Willis(second solo), Jack Matte (rythm guitar),Charle Matonya(Bass guitar), Paul Mdasias (drums), Didi Musekeni(Hayuko pichani mwimbaji).

Taarab ya Tanga


Katika miaka ya 50 wanawake tisa wa Tanga walijikusanya na kuanzisha wakaanzisha kikundi cha kuimba walichokiita Raha til Fuad maana yake Raha ya Moyo. Akina mama hawa chini ya bibie aliyeitwa Mama Akida au aka Mama Lodi, waliendesha kikundi chao wakiwa wanaimba nyimbo za Siti Binti Sadi na tungo zao ambazo waliimba katika melody ya nyimbo za kihindi zilizotamba wakati huo. Kundi hili liliendelea na kuanza kuruhusu wanaume kujiunga hasa wakiwa wapiga vyombo. Hata mtoto wa Mama Akida, Akida Jumbe hatimaye alijiunga na kundi hili kama mpiga accordion kwenye mwaka 1962. Kundi hili ambalo baadae lilikuja kuitwa Young Noverty,liliendelea mpaka kukaweko na mgawanyiko uliozaa kundi la Shaabab Al Waatan. Hapa ndipo kukaanza mtindo wa kuweko kundi pinzani jambo ambalo kwa njia ya ajabu sana limekuwa linadumu kiasi cha miaka kumi kumi. Miaka ya 1960s Young Noverty na Shabaab al Waatan, 1970s Lucky Star Musical Club na Black Star Musical Club, 1980 Golden Star Taarab na White Star Taarab, 1990, Babloom Modern Taarab na Freedom Modern Taarab. Taarab ya Tanga ndo haswa inastahili kuitwa modern Taarab, kwani wao hawkufuata taarab ile iliyoletwa Zanzibar enzi ya Sultan Seyyid Barghash, kundi la taarab hii lilikuwa dogo na vyombo vyake vilikuwa pamoja na Gitaa la besi, gitaa la solo, drums bongos ,akodion au kinanda. Nyimbo zao zilikuwa fupi na si ndefu kama za Kizanzibari., nyimbo zilitegemea mipigo ya ngoma za asili za kumbwaya na chakacha na hata baadaye mitindo kama rumba,bossa nova ilitumika kama mapigo. Na Taarab ya Tanga ndio iliyoanzisha moto wa vikundi vya taarab Tanzania Bara. Moshi kulikuwa na New Alwatan,AzimioTaarab, na Blue Star Taarab , Arusha-Blue Star Taarab,Dodoma-Dodoma Stars,Kondoa –Blue Stars,Mbeya-Magereza Kiwira, Mwanza-ujamaa Taarab, Bukoba –Bukoba Stars, na muendelezo huu uliingia mpaka Burundi kutokana na mwana muziki mmoja alie julikana kama Athmani Mkongo, alitoka Burundi na bendi yake kufika Tanga akawa mwanamuziki mahiri wa Taarab na hata kuipeleka kwao Burundi.(Pichani Waziri Ally wa Kilimanjaro Band, wakati huo akiwa Lucky Star akipiga kinanda)

Monday, May 17, 2010

Orchestra Lombelombe

Niliahidi kuwa nitaweka kipande cha gazeti chenye habari ya Orchestra Lombelombe, bendi ambayo wanamuziki wake walitoka katika bendi ya Morogoro Jazz. Bendi hii ilikuja baadae kuitwa Kurugenzi Jazz baada ya kuwa chini ya Ukurugenzi wa Mkoa wa Arusha, pichani ni Gumbo ambae alikuwa mpiga Bass, miaka ya sabini alihamia Iringa ambako alikuwa mfanya biashara.

Friday, May 14, 2010

Lady JD na Gadna Habash

Lady JD na Gadna G. Habash hongera kwa kutimiza miaka mitano ya ndoa.
Lady JD ni mwanamuziki ambaye amekuwa akiongeza kiwango cha ufanisi kwa wanamuziki siku hadi siku, na kila nyuma ya mwanamuziki mwanamke aliyeolewa, na mwenye mafanikio lazma kuna mume anaeungana nae kwa kila hatua. Shukrani kwako Gadna, wanamuziki wazuri wa kike wengi wamepotea katika fani kutokana na waume zao kuwazuia kuendeleza kipaji. Tunawatakia miaka mingi mingine ya furaha

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...