YOUTUBE PLAYLIST

Wednesday, March 17, 2010

The Tanzanites


Kabla ya kuwa na jina hili waliitwa the Barkeys, moja ya bendi za zamani sana Tanzania picha hii ya siku ya mwaka mpya 1991 itawapa watu kumbukumbu za kutosha. Bibie hapo mbele ni Juliet Seganga

Saturday, March 13, 2010

Wanamuziki ndugu 1



Katika historia ya muziki kumekuweko na familia kadhaa ambazo zimekuwa zikitoa wanamuziki zaidi ya mmoja. Moja ya familia iliyokuwa maarufu ilikuwa ni familia ya akina Sabuni. Unawakumbuka? Niko katika mawasiliano na mwanamuziki mmoja aliyepiga na ndugu watatu kati ya hao na tutapata kumbukumbu nyingi karibuni

Kushoto Cuthbert Sabuni, chini ni Raphael Sabuni akiwa na mwimbaji wa kike ambaye bado natafuta jina lake lakini alijulikana kama 'Lady Soul'

The Comets


Hawa ni wanamuziki wa The Comets kabla hawajawa the Sparks. Haya wadau nani unamfahamu hapa? Una stories za wakati huo. Nilipata bahati ya kuwasikia 1969 pale ambapo iko shule ya Forodhani wakipiga bugy, na ilikuwa mara yangu ya kwanza kusikia wimbo Mammy Blue, haujanitoka kichwani mpaka leo. Nakumbuka pamoja na nyimbo kama Direct Me, Hard to Handle, walipiga nyimbo za Isaac Hayes (Black Moses) ambazo zilikuwa top kwa wakati huo, unaukumbuka Move on?

Thursday, March 11, 2010

Nawaachia wananchi waseme 2




Mitindo ya Bendi Zetu

Kuwa na mitindo au staili ya muziki limekuwa jambo la kawaida kwa bendi zetu hapa Tanzania. Zamani mtindo mpya ulikuwa ni mapigo mapya ya muziki au hata uchezaji mpya. Hata bendi ikiwa mpya ulitegemea iwe na mapigo mapya na hivyo kuwa na maana ya kuwa na mtindo mpya. Hii ilifanya upenzi au unazi wa bendi kama ilivyojulikana wakati huo kuwa mkali na unaweza kuelezeka. Ilikuwa hata mwanamuziki akiwa mzuri vipi akiingia kwenye bendi alilazimika kujifunza kwanza mapigo ya bendi yake mpya kabla hajaruhusiwa kutoa nyimbo mpya, hii ilikuwa ni kuratibu mtindo wa bendi.

Mitindo ilikuwa tofauti hata uchezaji wake. Wakati nikiwa Vijana Jazz tuliwahi kupiga pamoja na Msondo Ngoma, wakati huo OTTU. Wapenzi wa pande zote mbili walikuwa wanasema wanashindwa kucheza staili ya bendi pinzani. Utakubaliana na mimi kuwa wakati Vijana ikipiga mtindo wa Takatuka ni muziki tofauti na Pambamoto ya Mary Maria au Bujumbura, na ni tofauti na Saga Rhumba ya enzi ya VIP, kwa hiyo majina hayo hayakuja tu , kulikuwa na sababu ya kuyatafuta kuonyesha aina mpya ya mapigo. Majina ya mitindo hii, na uchezaji wake, ulitokana na mambo mbalimbali , mengine yalitungwa na wanamuziki au mengine wapenzi, na mengine vituko mbalimbali vilivyotokea wakati huo. Kwa mfano Bomoa Tutajenga Kesho ya Mambo Bado, ilitokana na sentensi ya tajiri mwenye baa ya Lango la Chuma kutamka sentensi hiyo, wakati wa matayarisho ya uzinduzi wa bendi ya Mambo Bado. hilo. Fimbo Lugoda ilitokana na mwanamuziki mmoja kutandikwa viboko na bibi yake baada ya kukutwa na picha ya mwanamke mzungu. Washawasha ya Maquis ni baada ya steji shoo mmoja aliyekaa chini ya mti kuangukiwa na mawashwasha na kuanza kujikuna. Wadau mna vyanzio vingine vya mitindo ya bendi zenu watu tujikumbushe?

Tuesday, March 9, 2010

Nawaachia wananchi waseme








Vijana Jazz Baada ya Maneti

Ushindani uliokuwepo kati ya Maquis Original na Vijana Jazz ulikuwa mkali sana mwanzoni mwa miaka ya tisini hasa kwa ajili ya siku ya Jumapili ambapo Vijana walikuwa Vijana Kinondoni, wakati Maquis wakiwa kwenye ukumbi wao wa Lang’ata Kinondoni. Muda wa maonyesho yote mawili ulikuwa uleule hivyo kila kundi lilikuwa linatafuta kila njia ya kumpiku mwenziwe.

Vijana Jazz iliamua kupata wanamuziki wengine wapya. Hapo akaingia Suleiman Mbwebwe toka Sikinde,Jerry Nashon toka BIMA, Benno Villa kutoka Sikinde lakini wakati huo akitokea Nairobi, Rahma Shally kutoka Sambulumaa, wote hao waimbaji. Shaaban Dogodogo akitokea Nairobi (solo gitaa), Mhando (keyboards), Ally Jamwaka toka Sikinde (tumba).

Hapo ndipo ilipoanza Pambamoto Saga Rhumba.

Ujio wa TP Ok jazz ulibadilisha sana mtizamo wa bendi kimziki. Ok Jazz , wakiwemo wakongwe wote kasoro Franco, maana hii ilikuwa baada ya kifo chake. Ingawaje walikuja na kijana mmoja ambae alikuwa anaimba kama Franco pia alikuwa anapiga gittaa kama Franco , walikuja na mtindo wa kuweko kwa magitaa mawili ya solo, tofauti na kawaida iliyokuweko ya kuweko second solo. Tofauti yake ni kuwa katika mfumo wa OK jazz, wapiga solo wote wawili walikuwa mahiri na magitaa yalipewa uzito sawa. Katika mfumo wa second solo, gitaa hili huwa linasindikiza tu solo gitaa. Kwa kutumia mfumo huu, recording maarufu ya VIP ilirekodiwa katika studio za TFC. Mzee John Ndumbalo fundi mitambo mwenye uwezo mkubwa ambao bahati mbaya kama yalivyo mambo mengi mazuri ya zamani ya Tanzania umetupwa na kusahaulika. Aliirekodi album hiyo. Iliyojaa nyimbo ambazo zina kumbukwa mpaka leo, Thereza (Jerry Nashon), VIP (Jerry Nashon), Bahari imechafuka (Benno Villa), Mfitini (John Kitime). Sauti za waimbaji humo akiwemo Jerry Nashon , Benno Villa Anthony, Said Hamisi, Freddy Benjamin,Abdallah Mgonahazelu, Mohammed Gotagota Suleiman Mbwebwe zilileta burudani kubwa wakati huo.

Wapiga magitaa wa Vijana Jazz chini ya Shaaban Yohana (Wanted), walikuwa Shaaban Dogodogo Solo,Agrey Ndumbalo Rhythm, Bakari Semhando na Manitu Musa Bass, hapo ilikuwa utamu kolea………………



Picha ya juu Madiluu System kushoto kwake Baker Semhando mpiga Bass wa Vijana Jazz. Chini kushoto Mohamed Gota gota, chini Agrey Ndumbalo

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...