YOUTUBE PLAYLIST

Saturday, March 6, 2010

Mlimani Park Orchestra

Mlimani Park ilianzishwa mwaka 1978,ikiwa na wanamuziki kama Abel Balthazar (solo na second solo), Muhiddin Maalim Gurumo(muimbaji), Cosmas Thobias Chidumule (muimbaji), Joseph Mulenga(Bass), Abdallah Gama (rhythm), Michael Enoch (Saxophone), Hamisi Juma(mwimbaji), George Kessy(kinanda), Haruna Lwali(Tumba), ikiwa chini ya TTTS (Tanzania Transport and Taxi Services).

Mwaka 1983 shirika hilo lilipopiga mueleka kifedha kama mashirika mengi wakati huo bendi ikawekwa chini ya himaya ya Dar es Salaam Development Corporation (DDC). Chini ya uangalizi wa mwanamuziki mkongwe king Michael Enoch ambaye atakumbukwa kuwa alikuwa mpiga solo hatari sana wa Dar Jazz enzi za mtindo wao Mundo (mpaka akapewa sifa ya King), bendi ilinyanyuka ikiwa na sauti ya kipekee na mpangilio wa vyombo uliofanya bendi ilitikise jiji. Michael Enoch ambaye mpaka mauti yake alijulikana pia kwa sifa ya Ticha kutokana na kufundisha wanamuziki wengi na pia kuweza kupiga vyombo vingi, alikuwa ndie kiongozi wa Bendi kwa miaka mingi baadae. Umahiri wa King au Ticha (mwite upendavyo sifa zote anastahili), utaweza kuusikia katika nyimbo Tucheze Sikinde na Nalala kwa taabu alipiga alto saxophone (saksafon ndogo yenye sauti za juu), kwenye nyimbo nyingine alikuw anapiga tenor saxophone (saks kubwa yenye sauti za chini)

Mlimani Park Orchestra na mtindo wao wa Sikinde uliotokana na ngoma ya Kizaramo. Na ukaongezwa kibwagizo Ngoma ya Ukae, yaani Sikinde ngoma ya nyumbani, umekuwa ndo nembo ya bendi hii iliyojiwekea nafasi katika historia ya muziki wa Tanzania. Ni vigumu kutaja wanamuziki wote waliopitia DDC Mlimani Park lakini najua kwa msaada wa wadau tutapata majina mengi kadri itakavyowezekana. Lakini nianze na listi ifuatayo lakini pengine nigusie jambo ambalo watu wengi hawalijui, wimbo maarufu wa Gama ulitungwa na Tchimanga Assossa katika kipindi kifupi alichopitia bendi hii. Haya baadhi ya wanamuziki ni:

Hassani Rehani Bitchuka, Muhiddin Maalim Gurumo, Cosmas Tobias Chidumule, Hamisi Juma, Benno Villa, Francis Lubua, Max Bushoke ,Shaaban Dede ,Tino Masinge, Hussein Jumbe, Fresh Jumbe, Hussein Mwinyikondo vocals; Joseph Mulenga, Abel Balthazar, Henry Mkanyia, Michael Bilali, solo guitar; Abdallah Gama, Muharami Saidi, Mohamed Iddi, Huruka Uvuruge 2nd solo and rhythm guitars;

Suleiman Mwanyiro, Julius Mzeru bass guitar; Habibu Abbas, Chipembere Saidi, Juma Choka drums;Haruna Lwali, Ally Omari Jamwaka, Mashaka Shaban tumba; George Kessy Omojo organ; Boniface Kachale, Ibrahim Mwinchande, Machaku Salum, Hamisi Mirambo, Ally Yahya trumpets; "King" Michael Enoch, Juma Hassan, Joseph Bernard, Shaban Lendi saxophones karibuni wadau kuongeza utamu.


Friday, March 5, 2010

Patrick Pama Balisidya


Jina Patrick Balisdya halitakuwa geni kabisa kwa wadau wa blog hii,lazima roho zimeanza kuwadunda kama inavyokuwa kwangu kila nikimkumbuka Blai. Patrick Pama Balisidya alizaliwa Mvumi Dodoma tarehe 18 April 1946. Kabila lake alikuwa Mgogo , kabila ambalo lina wanamuziki wengi maarufu kutokana na muziki kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kabila hilo. Mama yake alikuwa anapiga kinanda kanisani na hivyo basi kutokana na asili ya kabila lake na pia kutokana na mama yake, hakika huyu angeweza kujisifu kuwa muziki uko katika damu yake.

Mdau mmoja alitutaarifu kuwa Balisidya alikuwa kiongozi wa Bendi ya shuleni kwake Dodoma secondary School. Ambapo kutoka hapo alijiunga na Chuo cha Ufundi , na baada ya kumaliza mafunzo alifanya kazi hiyo kwa muda na 1967 akawa tayari anapiga muziki Dar Es Salaam Jazz B. Kufikia mwaka 1970 Patrick alikuwa ameanzisha kikosi chake mwenyewe Afro70, kikiwa na mtindo wake Afrosa. Alikuwa mbunifu katika muziki wake, na kwa muda mrefu alikwepa sana kuingia katika wimbi la kufuata mapigo ya Kikongo kitu ambacho hata wakati huo bendi nyingi zilikifanya, japokuwa kukutana na Franco wakati alipofanya moja ya ziara zake nchini humu kulimfanya abadili mtindo kwa kipindi kifupi na katika nyimbo moja wapo aliiga kabisa solo la Franco alilolipiga kwenye wimbo wake Georgette.

Afro70 iliwakilisha wanamuziki wa Tanzania katika maonyesho ya mtu mweusi Lagos,Nigeria. (FESTAC festival 1977). Vyombo alivyotumia katika maonyesho haya vilimsumbua akili mpaka alipofariki, kwani muda mchache kabla ya Festac, wakati huo serikali ikiwa imeshamtaarifu kuwa ndie atakuwa mwakilishi wa Tanzania, vyombo vyake vyote vilihalibika katika ajali ya gari. Serikali ilinunua vyombo vipya ambavyo siku zote Balisdya alisema aliambiwa ni vyake baada ya maonyesho. Aliporudi kutoka Nigeria Kiongozi mwingine wa serikali aliamuru vyombo virudishwe serikalini na kwa kitendo kile kutangaza kifo cha Afro70. Vyombo hivyo vilitumika kuanzisha bendi ya Asilia Jazz ambayo ilikuwa Bendi ya Wizara ya Utamaduni na Vijana. Balisdya alitumia muda mwingi kujaribu kudai haki yake hiyo ambayo ilimkwepa mpaka mwisho wa maisha.

Mwaka 1979, Balisidya alikwenda Sweden na kushirikiana na kikundi cha Archimedes akatoa album nzuri sana iliyoitwa Bado Kidogo. Kuna wakati Patrick alijiunga na Orchestre Safari Sound, (masantula) na kupiga piano katika ule wimbo maarufu, ‘Unambie siri’, Patrick pia alikuwa mpigaji mahiri wa keyboards. Kwa kweli nyimbo za Patrick zilizokuwa juu katika chati ni nyingi. Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa, Nakupenda kama Lulu, Ni masahaka na mahangaiko, Afrika.

Patrick alifariki tarehe 7, Agosti 2004.

Daima tutakukumbuka Patrick Pama Balisidya,

Mungu akulaze pema peponi

Jiving


Katika aina ya muziki ambao ulisababisha bendi kuanza katika mashule, ilikuwa ni aina ya muziki na kucheza ulioitwa 'jiving'. Shule nyingi zilikuwa na vikundi hivi, sekondari za kike na kiume zilishindana katika jiving. Muziki huu ulikuwa umetoka haswa Afrika ya Kusini. Siasa zikaingilia kati katika miaka ya mwishoni ya sabini na kuuwa jiving katika mashule mengi. Jiving ilikuwa inaambatana mara nyingine na filimbi kama alivyokuwa anapiga Spokes Mashiyane. Mbaraka Mwinyshehe ni matokeo ya muziki huu alikuwa bingwa wa kupiga filimbi. Pichani ni kikundi cha jiving cha Mkwawa High School The Skylarks Jiving Group, akiwemo mwandishi maarufu Danford Mpumilwa (watano toka kushoto) ambaye pamoja na kuwa mwimbaji wa Bendi ya shule hiyo Mkwawa Orchestra, aliendelea mpaka kufikia kuwa na bendi yake mwenyewe pale Arusha.

Wednesday, March 3, 2010

Bendi za wanafunzi mashuleni


Katika miaka ya sitini na sabini shule nyingi za sekondari zilikuwa na Bendi (bendi ya magitaa), hata pale Chuo Kikuu Mlimani palikuwa na Bendi nzuri tu katika kipindi hicho, Kuna Bendi za shule nyingine zilipata umaarufu wa Kitaifa kama vile Bendi ya Shule ya Sekondari Kwiro ambayo iliweza kurekodi nyimbo zake Radio Tanzania. Niongelee shule moja nadhani itatoa changamoto ya kupata habari za bendi za namna hiyo katika shule nyingine. Pale Mkwawa high School Iringa ,kulikuwa na bendi mbili. Moja ilikuwa ikipiga muziki wa kiswahili ambayo ilikuwa na wanamuziki kama Sewando kwenye solo, Masanja kwenye rythm, John Mkama Bass,Manji,Danford Mpumilwa mwimbaji, mpiga tumba kwa sasa ni Askofu moja mashuhuri, wakati huo huo bendi ya pili ilikuwa na mwimbaji machachari Deo Ishengoma akiimba nyimbo za James Brown. Bendi hii ilikweza kurekodi RTD pia vibao kama Wikiendi Iringa na Ulijifanya lulu na kadhalika.

Dar Es Salaam pia palijaa bendi nyingi za shule na mitaani. Azania, Tambaza ni kati ya shule zilizokuwa na bendi za vijana katika enzi hizo, wakipiga muziki Jumapili mchana ukiitwa bugi. Bahati mbaya bugi lilipigwa marufuku na kuharibu mfumo mzima wa muziki wa vijana katika historia ya muziki Tanzania. (Pichani ni shule ya Mkwawa wakati huo.)


Tuesday, March 2, 2010

Swali la Leo

Bendi gani iliimba wimbo- Mali ya mwenzio sio mali yako? Na dongo lilikuwa likielekezwa kwa nani?

Chinyama Chiyaza

Tangazo jingine la dansi la miaka hiyo ambalo nina uhakika litaleta kumbukumbu kwa wapenzi wa Maquis wa enzi hizo za Mtindo wa Telemka Chekecha Scania LBT III, wakati huo gari za Scania ndizo zilikuwa maarufu nchini na Scania LBT III ilikuwa gari yenye saiz kubwa kuliko zote, na ndio yenye kusifika zaidi, karibuni tena wapenzi wa White House mchangie, mambo yalikuwa mazito chini ya uongozi wa Chinyama Chiyaza ambae alikuwa mpiga Saxophone katika bendi. Wakati huu Maquis ilikuwa na maendeleo makubwa sana ya kuwa na mashamba, magari, matrekta na hata kuwa na Kota zake pale Sinza Palestina. Hebu angalia majina yaliyopo katika bendi.

Monday, March 1, 2010

Swali la Leo

Swali la leo......... Bendi gani ilipiga wimbo wa Banchikicha? Kwa msaada tu bendi hiyo ilishinda mashindano ya Bendi Bora Tanzania 1973

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...