YOUTUBE PLAYLIST

Thursday, April 15, 2010

Vijana Jazz ilikotokea





Mwaka 1971 Umoja wa Vijana wa TANU uliamua kuanzisha Bendi na kumpa jukumu hilo mwanamuziki John Ondolo Chacha. Ili kutaengeneza bendi, Marehemu Mzee Ondolo aliweza kuwashawishi vijana wa bendi ya Zezemba wakajiunga nae lakini hawakukaa nae muda mrefu kwani walikuwa ni waajiriwa wa kiwanda cha nguo cha Urafiki, hivyo akalazimika kujenga tena Bendi na kwenda hadi Bagamoyo alipoikuta bendi ya Kizibo na akapata wapigaji kumi. 1972 wapigaji wengine tena wakaacha bendi, hivyo akalazimika kutafuta wengine na kikubwa ni kuwa alimpata mpiga solo Hassani Dalali ambaye aliweza kuwatafuta wenzie. Bendi ilipelekwa JKT mwaka 1973, wakati huu tayari ilishampata mtunzi na mwimbaji kutoka TK Limpopo ya Juma Kilaza, kwa jina Hemed Maneti, na baada ya muda kidogo iliweza kumpata Hamis Fadhili kutoka Jamhuri Jazz.
1974 walienda Nairobi na kurekodi nyimbo ambazo ziliaweka msingi wa bendi hiyo. Baadhi ya nyimbo hizo ni Magdalena, Niliruka Ukuta. Mtindo wa bendi wakati huo ulikuwa Kokakoka Balaa

Belesa Kakere

Salehe Kakere, maarufu kama Belesa Kakere, hapa akitangaza kuhamia Orchestra Bima Lee. Hebu soma maelezo katika habari yake unapata picha kamili ya mwanamuziki huyu na kazi zake na historia yake kwa ufupi

Wednesday, April 14, 2010

Vyombo vya habari

Katika kusoma magazeti ya zamani,(nitazitoa baadhi ya makala hapa), imeniijia kuwa tunatatizo kubwa la uandishi na utoaji wa habari za shughuli za muziki. Makala za muziki za siku hizi, nyingi ni kuhusu nani kapagawisha wapi au mcheza show gani alikaa vibaya au ana uhusiano na nani. Kimsingi ni kama vile taarifa kuhusu muziki ni gossips zinazoendelea katika uwanda wa wanamuziki. Hakuna taarifa ya taaluma katika muziki huo. Unaweza kupata taarifa nzuri kuhusu Beyonce lakini ukakosa taarifa kuhusu Anna Mwaole ambaye yuko jijini Dar es Salaam. hili liko hata kwenye vituo vya redio vya wilayani, ambako huko nako watangazaji wengi wanaiga kuanzia uongeaji, mpangilio wa vipindi, maadili na kadhalika kutoka redio maarufu za Dar es Salaam.
Huko wilayani nako wanadai hawana taarifa za wasanii wa hapo wilayani kwa kuwa wasanii hawaleti taarifa zao, lakini mtu huyohuyo atakaa masaa kadhaa kwenye internet akitafuta taarifa zote kuhusu msanii wa nje. Napata taabu kujua aina ya mafunzo wanayopata waandishi katika vyuo vya uandishi siku hizi. Na tena nakumbuka kuwa wandishi wengi wa zamani hawakupitia vyuo kama vilivyo siku hizi kwanini hakuna ubora wa uandishi sasa? Kwanini tunakosa ufanisi zaidi siku hizi ? au ni mimi ndio mwenye kuona kuna tatizo ambalo halipo? katika makala nitakazoziposti hapa ambazo ni za miaka ya sabini naona kuna maelezo ambayo nayakosa katika uandishi wa siku hizi.

Orchestra Santa Fe

Kati ya maswali amabayo yamewahi kuulizwa humu ni kuhusu bendi hii Orchestra Santa Fe. Hii ilikuwa mwanzo ni bendi yenye asilimia kubwa ya wanamuziki Wakongo. Mkuu wa 'Libeneke' aliwahi kuuliza kama ndio ilikuwa Bendi ya kwanza ya Kikongo, ninauhakika haikuwa bendi ya kwanza ya Kikongo. Wenye taarifa zaidi kuhusu Bendi hii karibuni. Bendi hii ilikuwa ikipiga pale Gateways Mnazi Mmoja maeneo ambayo kuna wakati yalikuwa maeneo muhimu katika shughuli za starehe jijini Dar es Salaam.

Tuesday, April 13, 2010

Sokomokoooooooooo


Leo nimeona nianze kuanika picha nilizonazo hadharani , tukumbuke yalivyokuwa. Pichani ni Safari Trippers. Wapenzi wa Sokomoko mnakumbuka kipindi hiki. Hebu tupeane kumbukumbu

Thursday, April 8, 2010

Muziki wa staili moja

Miaka michache iliyopita kulianza hadithi moja ambayo vyombo vya habari vikaishikia bango, na baadae wanamuziki kadhaa nao wakashika bango nakutoa ushauri nasaha wa tatizo hilo. Tatizo hilo lililkuwa kwanini muziki wa bendi Tanzania hauwi maarufu. Kwa utafiti ambao washika bango waliufanya wakatangaza kuwa Tanzania tuna tatizo la kuwa tunapiga aina nyingi mno za muziki ndio maana haujulikani. Kwa hiyo wataalamu hawa wakiwa wanalinganisha na muziki wa Kikongo wakasema Mkongo mmoja akianzisha Kwasakwasa wote wanapiga Kwasakwasa , ikija Kibinda Nkoy wote wanapiga hivyo hivyo , kwa hiyo nasi tuwe na staili moja, tena ikapewa jina Achimenengule. Utafiti huu ni wa ajabu sana, tuanze na nchi yetu ina makabila zaidi ya 110,yenye mila mbalimbali na muziki mbalimbali, inashangaza kujaribu kufikiri wote hawa wapende aina moja tu ya muziki. Huko Kongo ambako kulitolewa mfano hata wakati wa kile kipindi kinachoitwa the Golden Age of Congolese Music, ndipo haswa upigaji wa aina mbalimbali ulipokuwepo. Huku kulikuwa na Dr Nico, Franco, John Bokello,African Fiesta, bendi za vijana kama Lipualipua , Belabela, Orchestra Kiam, Empire Bakuba, Veve, kila moja ilikuwa na aina yake ya muziki,wapi ilikuja kupatikana hiyo theory ya kupiga staili moja ni kitendawili. Tatizo la kudumaa kwa muziki wa Tanzania si kutokupiga staili moja.

Wednesday, April 7, 2010

Kwaya

Kwaya, kama neno lenyewe linavyoonekana ni neno la mapokeo likimaananisha aina ya utamaduni wa mapokeo. Ni neno lililotokana na neno 'choir'. Uimbaji wa kikundi cha watu. Muziki huu umepitia mabadiliko mengi yakitokana na sababu mbalimbali. Kwaya ilikuweko mwanzoni katika mashule na katika makanisa, baadae ikawa sehemu ya burudani hasa ikipata msukumo kutoka kwaya za Kusini mwa Afrika. Kwa wale waliokuwa maskauti wanakumbuka kuwa kwaya kilikuwa kipengele muhimu katika route march. Katika harakati za kutafuta uhuru kwaya zilichukua umuhimu sana katika kuhamasisha jamii. Lakini kama ilivyo kwenye muziki wa aina nyingine, muziki huu ulitokea kuwa na mabingwa wake. Si rahisi kumsahau Mzee Makongoro kama uliwahi kumsikia. Alikuwa na nini cha ziada? Mzee huyu alianzisha staili yake mwenyewe ya kwaya. Wakati kwaya nyingi zikiiga muziki wa Jiving wa South Africa yeye alikuja na kitu kipya ambacho bahati mbaya kimekosa mrithi. Karibuni tuliangalie hili swala la kwaya. Je tunaelekea wapi?

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...