YOUTUBE PLAYLIST

Friday, March 19, 2010

Cuban Marimba


Kuanzia miaka ya 1920 mpaka 1940 Tanzania, hususani Tanzania bara, wanamuziki na wapenzi wa muziki walifuatilia sana muziki kutoka Cuba kupitia sahani za santuri za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Trio Matamoros and Sexteto Habanero, ambao walitoa santuri zikiwa na namba zinazoanzia GV1, GV2 na kuendelea na kupata upenzi mkubwa katika ukanda huu wa Afrika. Ni vikundi hivi ambavyo viliingiza mitindo kama rhumba, Bolelo, Chacha na kadhalika. Kwa kweli bendi za muziki wa dansi zingepata mengi ya kimapinduzi kama zingeweza kusikiliza na kuelewa muziki wanaoupiga kiini chake ni nini.

Kutokana na hamu hiyo ya kuujua na kuupiga muziki wa kicuba kisawasawa Marehemu Salum Abdallah aliwahi kutoroka kwao Morogoro akakimbilia Mombasa ili apande meli aende Cuba, bahati mbaya safari yake iliishia Mombasa kwa kuishiwa fedha, ambako alianza kupata shida lakini kwa kuwa baba yake alikuwa mwarabu, Ushirika wa waarabu wa Mombasa walimtaarifu mzee huyo kuhusu alipo mwanae na alimfuata na kumrudisha Morogoro. Salum Abdallah Yazidu aliyefahamika sana kama SAY, mwaka 1948 alianzisha bendi yake akaiita La Paloma, ambalo ni jina la wimbo maarufu ambao uliotoka Cuba ukiwa na maana Njiwa, wimbo huu unaendelea kupigwa hadi leo ukiimbwa na kurekodiwa kwa lugha mbalimbali, hata hapa Tanzania bendi nyingi huzisikia zikipiga wimbo huu na kuweka maneno yake ya papo kwa papo hasa kabla dansi rasmi halijaanza. Bendi ya La Paloma ndio ilikuja kuwa Cuban Marimba Band, Salum Abdallah aliiongoza bendi hiyo mpaka kifo chake 1965. Aliyeichukua na kuiendeleza alikuwa Juma Kilaza. Kilaza aliiendeleza vizuri kwa kutunga mamia ya nyimbo yaliyofurahisha sana watu miaka ya 60 na 70. Morogoro ulikuwa mji uliosifika kwa muziki, huku kukiwa na Mbaraka Mwinshehe na Morogoro Jazz, na huku Juma Kilaza na Cuban Marimba. Kuna watu walikuwa wakihamia Morogoro wikiendi na kurudi Dar siku ya Jumatatu asubuhi. Kati ya nyimbo maarufu za Cuban Marimba zinazodumu kwenye kumbukumbu ni wimbo Ee Mola Wangu, ambao Salum Abdallah awali aliutunga kwa mashahiri marefu lakini akachukua beti chache kutengenezea muziki akilalamika kuwa kuna walimwengu wanamtakia mabaya, lakini siku ya kufa atawashitakia maiti wenzake kuhusu ubaya huo.

Pichani ni Cuban Marimba baada ya Salum Abdallah, wa kwanza kulia Juma Kilaza, mwenye mawani Ufuta mpiga solo. Wadau malizieni majina ya hawa wanamuziki wengine. Mheshmiwa Tsere uliishi sana Morogoro tusaidie

Mheshimiwa mchango wako ni muhimu

Nimekuwa najaribu kumshawishi Mheshimiwa mmoja ambaye alikuwa Waziri kwa muda mrefu na sasa ni Mbunge atoe mchango katika blog hii, Mheshimiwa huyo katika miaka ya sitini alirekodi nyimbo moja nzuri sana ya kumsifu Mwalimu Nyerere. Mheshimiwa huyo alirekodi kibao hicho wakati akisoma Uholanzi.
Pia Balozi mmoja maarufu aliyekuwa akiimba nyimbo za James Brown miaka hiyo najaribu kumwomba ruksa atusaidie experience zake.
Mzee moja marehemu sasa lakini ana watoto wengi wanamuziki, japo yeye alikuwa mwalimu Tabora school alinieleza kisa cha Mheshimiwa mmoja (Mbunge muhimu), ambaye nitamwomba ruksa yake nitaje jina lake baadae, ambaye alilazimika kuwa anamlimia kajibustani kake ili afundishwe gitaa. Nashukuru kuwa mheshmiwa huyo mpaka sasa ni msaada mkubwa sana katika fani ya muziki hasa wa dini

Thursday, March 18, 2010

LIBENEKE

Mheshimiwa mmoja kaniomba niweke mwanga kwenye hili neno ambalo limetajwa hapo juu. Katika kumbukumbu zangu, Libeneke ulikuwa mtindo wa Butiama Jazz Band, bendi iliyokuwa chini ya uongozi wa marehemu mzee Mkwega, ikiwa na mpiga solo mzee Makelo ambae yuko Shikamoo Jazz, baadhi ya waimbaji akiwemo Saidi Hamisi ambaye kwa miaka mingi mpaka kifo chake alikuwa Vijana Jazz. Kulikuweko na wimbo ambao ulikuwa maarufu ukiwataja wanamuziki wa bendi hiyo na kibwagizo chake kilikuwa ....waache waseme, watachoka wao mtindo libeneke utatia fora...... Mkuu wa libeneke upo? Karibu wapenzi wa Butiama Jazz

Wednesday, March 17, 2010

The Tanzanites


Kabla ya kuwa na jina hili waliitwa the Barkeys, moja ya bendi za zamani sana Tanzania picha hii ya siku ya mwaka mpya 1991 itawapa watu kumbukumbu za kutosha. Bibie hapo mbele ni Juliet Seganga

Saturday, March 13, 2010

Wanamuziki ndugu 1



Katika historia ya muziki kumekuweko na familia kadhaa ambazo zimekuwa zikitoa wanamuziki zaidi ya mmoja. Moja ya familia iliyokuwa maarufu ilikuwa ni familia ya akina Sabuni. Unawakumbuka? Niko katika mawasiliano na mwanamuziki mmoja aliyepiga na ndugu watatu kati ya hao na tutapata kumbukumbu nyingi karibuni

Kushoto Cuthbert Sabuni, chini ni Raphael Sabuni akiwa na mwimbaji wa kike ambaye bado natafuta jina lake lakini alijulikana kama 'Lady Soul'

The Comets


Hawa ni wanamuziki wa The Comets kabla hawajawa the Sparks. Haya wadau nani unamfahamu hapa? Una stories za wakati huo. Nilipata bahati ya kuwasikia 1969 pale ambapo iko shule ya Forodhani wakipiga bugy, na ilikuwa mara yangu ya kwanza kusikia wimbo Mammy Blue, haujanitoka kichwani mpaka leo. Nakumbuka pamoja na nyimbo kama Direct Me, Hard to Handle, walipiga nyimbo za Isaac Hayes (Black Moses) ambazo zilikuwa top kwa wakati huo, unaukumbuka Move on?

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...