Saturday, July 31, 2010

Mbaraka Mwinyshehe Mwaluka 1Ukikaa na kusikiliza muziki wa Mbaraka kwa makini unajifunza mengi sana, kwa mashahiri ya nyimbo hizo unapata picha ya maisha yalikuwaje enzi hizo. Furaha, machungu, vicheko, vilio na kadhalika. Upigaji wake wa gitaa, ni somo zuri sana kwa mpigaji anaetaka kujiendeleza katika upigaji wa solo. Katika vipindi vyake vya kuanzia Morogoro Jazz hadi Super Volcano alipitia staili nyingi za muziki, baadhi kama Sululu, Likembe, Masika Zolezole na kadhalika. Tofauti na bendi nyingi ambazo hubadili majina ya mitindo bila kubadili muziki wenyewe, staili za Mbaraka zilionyesha mabadiliko. Nyimbo katika staili ya Likembe zilikuwa tofauti na zile za Masika Zolezole. Kipindi hicho wapenzi wa muziki waliweza kuondoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro kufaidi wiki endi ya muziki aidha wa Cuban Marimba, au Morogoro Jazz. Picha ya juu Mbaraka Mwinyshehe, ya chini toka kushoto Sulpis Bonzo, Mlinzi Mustafa(huyu baadae alipigia Urafiki Jazz), Shaaban Nyamwela, Abdul Mketema (mwenye Saxaphone),Samson Gumbo,Mbaraka Mwinyshehe.Hapa wakiwa Morogoro Jazz Band

Friday, July 30, 2010

Mwanamuziki Mheshimiwa Paul Kimiti


Kwa muda mrefu nilikuwa na nia ya kuweka taarifa kuhusu wimbo wa kumsifu Nyerere ambao uliimbwa na Mheshmiwa Paul Kimiti. Nilijitahidi kutaka kupata taarifa kutoka kwake ikawa haikuwezekana lakini karibuni nilisoma maelezo ya Mheshmiwa mwenyewe kuhusu kazi hiyo, ambayo alisema walifanya akiwa Mwenyekiti wa wanafunzi kutoka Tanganyika katika chuo kikuu cha Netherlands kati ya mwaka 1962 na 1965. Akiwa na wanamuziki wenzake wakiwa na kundi waliloliita Safari Brothers walirekodi nyimbo hii nzuri sana kuhusu Mwalimu Nyerere. Mheshimiwa alisema walitoa dola 20,000 walizozipata kutoka Philips records kwa Mwalimu alipotembelea Netherlands April 1965, pesa hizo walitoa ili kuchangia maendeleo ya nchi yetu, na huo ndio ulikuwa mwanzao wa uhusiano wake na Mwalimu.

Wednesday, July 28, 2010

Kida Waziri arudi ulingoni

Kida waziri miaka ya 90.

Kida Waziri au kama alivyokuwa akiitwa enzi zake Vijana Jazz Stone Lady amerudi na album yake yenye nyimbo 6 ikiwa na nyimbo kama Wifi zangu, Shingo Feni, Penzi haligawanyiki na nyinginezo, pia ameimba wimbo wa Mary Maria akishirikiana na mwanae Waziri, ambae kajitahidi kuimba zile sehemu za uimbaji wa marehemu babake.

Kida Waziri alivyo sasa.

Sunday, July 18, 2010

Drums

Ukisema drums katika anga za muziki utakuwa umeeleweka kuwa unaongelea zile ngoma za kizungu ambazo hupigwa kwa kutumia miguu na mikono. Uwingi wa drums huanzia ngoma kubwa moja na ndogo moja (snare), na tasa moja (Hi hat), na kuendelea kwa uwingi kadri ya utajiri na uwezo wa mpiga drum. Katika nyimbo za Dar es Salaam Jazz ambazo zilirekodiwa kwenye miaka ya 30, drums zilitumika hivyo si chombo kigeni katika muziki wa Tanzania. Katika miaka ya sitin chombo hiki kilitoweka katika bendi nyingi za muziki wa rumba, lakini kikarudi tena kwa nguvu baada ya kuingia kwa staili ya kavacha kutoka Kongo. Bendi ambazo zilikuwa zikipiga muziki wenye mahadhi ya kimagharibi ziliendelea na drums katika kipindi chote na kuweza kuunganisha na tungo za zao za rumba kwa ufanisi mkubwa kama ilivyotokea kwa bendi kama Afro70. Drum huwa chombo kinacholinda spidi ya wimbo, na staili ya wimbo, kama ni chacha, tango, waltz au ngoma ya Kimakonde au Kipogoro. Drums huweza kuleta utamu sana kama zikimpata mpigaji.
Siku hizi kuna drums za umeme, hizi huwa na uwezo wa kuongeza au kupunguza sauti, na kuzibadili zikalia milio mbalimbali, kwa mfano kulia kama ngoma za kihindi au kulia kama tumba au hata nyingine zinaweza zikipigwa zikawa zinatoa milio ya ndege!!!.Bendi ya kwanza kuwa na electronic drums ilikuwa Chezimba, wakati huo drums zikipigwa na Charles Mhuto, Tanzanite nao wakanunua zao, na kwa upande wa bendi za rumba MK Group, ikifuatiwa na Vijana Jazz na Bima Lee walikuwa wa mwanzo kuwa na drums hizi

Friday, July 16, 2010

Gitaa la rythm
Katika mfumo wa awali bendi zilikuwa zikitumia magitaa matatu, Solo, rythm na Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble kiasi na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine. Inasemekana kaka yake Dr Nico, ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa la nne lililoitwa second solo. Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm. Bendi ya Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita chord guitar. Lakini leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umaaarufu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe. Kati ya wapiga rythm maarufu namkumbuka Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale mpiga rythm wa Jamhuri Jazz. Yeye alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo. Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri wakati huo. Kumbuka wimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Marehemu Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha. Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu. Katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne na kuweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Leo vionjo vya upigaji huo vinarudi kwa njia ya ajabu sana. Vikundi vya taarab vimeanza 'kuachia rythm' gitaa moja kubaki linapiga peke yake, japo wao hupiga gitaa la solo lakini staili ni ile ya enzi. Siku hizi kelele huwa nyingi kiasi unaweza ukatembelea bendi 3 ukaona mtu anapiga gitaa la rythm lakini husikii anapiga nini.

Thursday, July 15, 2010

Uliwafahamu Hot 5 wa Magomeni Kota?

Kuna swali nimeulizwa sina jibu,na kila ninae muuliza hana kumbukumbu nalo. Nimeulizwa kama nilikuwa nalifahamu kundi lililoitwa Hot 5 ambalo masikani yake yalikuwa Magomeni Kota, kundi hili lilikuwepo kabla ya Flaming Stars kuhamia Mombasa.....kuna mwenye taarifa?

Atomic Jazz Band


Atomic ilikuwa moja kati ya bendi zilizowika sana nchi hii. Bendi iliyokuwa na makazi yake Tanga, Tanga wakati huo ikiwa na vikundi vingi maarufu vya muziki, kama vile Jamhuri, White Star, Amboni, Lucky Star, Black Star. Bass katika bendi hii kwa kweli lilikuwa likiingiza upigaji wa bezi katika kiwango kipya,wapigaji wake walileta changamoto hata walipokuja hamia katika bendi mpya. Pichani toka kushoto John Mbula -Saxophone,Rodgers- mwimbaji, John Kilua-Thumba(huyu alikuwa ni ndugu ya Julius Kiluwa ambaye ndiye alikuwa mwenye bendi),John Kijiko-Solo gitaa, Hemed Mganga-rythm gitaa (niliwahi kupiga bedni moja na mzee Mganga kwa wakati fulani. Tulikuwa wote Orchestra Makassy na ndie baba mzazi wa mwimbaji wa kizazi kipya Kassim Mganga),Mohamed Mzee-Bass.
Picha hii ilikuwa ni jarada la santuri iliyokuwa na wimbo maarufu Mado Mpenzi Wangu. Wimbo ulikuwa ni ujumbe wa kweli kutoka kwa mwanamuziki mmoja kwenda kwa mpenzi wake ambae jina kidogo linafanana na Mado ili kuficha ukweli. Mtunzi wa wimbo huu alikuwa mpenzi sana wa bendi hii na bado kwa rafiki zake anajulikana kwa jina la Mado. Siku hizi amekuwa mpenzi tu wa kawaida wa muziki.

Wednesday, July 14, 2010

Lutumba Simaro wa Ok Jazz


BANNING EYRE ni mwandishi Mmarekani aliyefanya mazungumzo na mwanamuziki Lutumba Simaro mpiga gitaa wa kundi la OK Jazz, kuna mengi ya kujifunza kwa wanamuziki wa Tanzania
SWALI: Nini kinaendelea katika muziki wa Kongo siku hizi?
SIMARO: Kinachoendelea sasa sikipingi, mi ndio baba yao, hawa vijana kuna kitu walichoingiza katika muziki. Wameleta damu mpya na ujana kweli lakini,kuna monotony mno, Huwezi kutofautisha bendi moja na nyingine. Wanavyoimba, wanavyocheza na wanavyopiga mgitaa katika kile wanachoita seben. Kuna mtangazaji mmoja anaitwa Gaspar wa Studio Maximum, ana kipindi kimoja ambapo nilikuwa nasikia wimbo wa Werrason lakini alikuwa JB anecheza na wimbo wa JB ukichezwa show na Werra, kwa kweli huwezi kuona tofauti ya muziki wa hawa wawili.
Enzi za OK Jazz, Franco alikuwa mtunzi mzuri sana, mimi nikajiunga nikaleta style yangu, Josky alipokuja nae akaleta staili yake. Ndombe nae pia akaja na staili yake. Wote tulikuwa OK Jazz, gitaa la Franco ndilo lilitawala na kuweka nembo ya staili zetu mbalimbali. Papa Wemba akiimba najua ni Papa Wemba ana staili yake. Mdogo wangu Kofi nae anastaili yake, Zaiko ya Nyoka Longo pia wana staili yao
Kama wangeweza kunisikiliza ningewaambia hivi hawa vijana wanajitoa Wenge na kuanzisha makundi yao, ni muhimu kuja na utofauti, wana waimbaji wazuri sana, watunzi wazuri na wamepata bahati kuweza kurekodi katika studio za kisasa wana jukumu la kuendeleza ubunifu. Wakati wetu wa enzi za Vicky Longomba, Mujos na Kabasele, kama we ni mwimbaji ulilazimika kuimba aina mbalimbali za muziki. Muziki wa Ulaya au Marekan na kwa staili mbalimbali. Mtu akiomba Tango, unapiga Tango , ukitakiwa kuimba Waltz uliimba style hiyo, lakini waimbaji wetu wa sasa, hakuna kitu. Na wapiga magitaa pia, tulikuwa na wapiga magitaa wakali kama Papa Noel, na Tino Baroza, na hata Franco. Wapiga magitaa siku hizi ukiwauliza unamfahamu Nico Kasanda? Tuno Baroza? Kimya kinatawala. Muhimu kujua staili zao ili kujitafutia stail mpya. Nina mpiga gitaa ana miaka 20, wiki iliyopita nilimpa sanduku zima la santuri akafanye mazoezi, nashukuru ameanza kuniuliza maswali mengi kuhusu upigaji mbalimbali. Utunzi nao unapwaya pia utakuta wimbo unataja majina ya watu 200, wanaita “mabanga”, nawauliza majina mengi ya nini wananiambia hawa huwa wanawalipa vizuri.
Vijana wana bahati wana teknolojia nzuri, wana TV nyingi na nzuri za kuweza kuwafanyia promotion, Wakati wetu tulikuwa na radio moja tu, hivyo ililazimu kufanya kazi nzuri ili ujulikane. Nawakumbuka Soki Dianzenza na Soki Vangu walikuja na kitu kipya, Nyboma, Pepe Kalle wote watakumbukwa kwa aina yao ya uimbaji.
Nimeitafsiri kwa ruksa ya Banning Eyre. Kwa habari nyingi zaidi angalia www.afropop.org

Saturday, July 10, 2010

SITI BINTI SAAD


Kwa kila hali Siti Binti Sadi anastahili kuenziwa. Kwa akina mama, mwanamke huyu shujaa aliyetoka katika familia maskini ya kijijini, ataenziwa kwa kuwa aliweza kushinda mfumo uliokuwa ukizuia wanawake kujichagulia mfumo wa maisha yao, na kuweza kujitokeza kufanya yale ambayo hayakuwezekana kwa mwanamke wa aina yake kabla. Alijitokeza na kuwa mwanamke mwimbaji mwenye nguvu za kuendesha shughuli za muziki katika mfumo uliotawaliwa na wanaume.

Kwa akina mama wanamuziki katika Taarabu, alikuwa ndio ufunguo ya mfumo uliopo ambao taarab inaongozwa na waimbaji wa kike.

Alikuwa ndie mwasisi wa kuimba taarab kwa Kiswahili.

Kwa wanamuziki wote kwa ujumla Siti Binti Sadi ni super star wa kweli.

- Alirekodi santuri zaidi ya 150

- Alikuwa wa kwanza kwenda kurekodi nyimbo zake India May 1928

- Umaarufu wake ulisababisha Columbia Records kujenga studio Zanzibar katika enzi yake ili tu kumrekodi.

Oktoba 1936 aliwahi kufanya onyesho moja huko Pangani na kupata shilingi 1200. Kwa thamani ya pesa wakati ule, mtu aliweza kupanga chumba kwa shilingi 1 kwa mwezi. Na Pangani ilikuwa na wastani wa watu 1500. Si rahisi msanii yoyote wa leo hapa nchini kuweza kufikia Usuper Star huo.

Siti alizaliwa mnamo mwaka 1880 na kufariki 1950.

Wednesday, July 7, 2010

Live photoz Wakongwe concert

We made it pamoja na very strange things happening on the way

Sabasaba........

Hayawi hayawi leo yatakuwa , Wanamuziki na Djs wakongwe leo watakuwepo Karimjee Hall kwa masaa 6 mfululizo,Nimemuona DJ Cedou, DJ John Peter wakiwa na Lps na turntables tayari kuonyesha walichokuwa wakikifanya enzi zao. Maelezo zaidi baadae.

Monday, July 5, 2010

Orchestra Mambo Bado

Orchestra Mambo Bado ilikuwa bendi ambayo haikukaa kwa muda mrefu katika anga za muziki. Bendi hii ilianza mwaka 1981, ikiwa chini ya 'Mtoto Mzuri' Tchimanga Assossa ikajulikana sana kwa ajili na mtindo wake ulioitwa Bomoa Tutajenga kesho. Pichani Sadi Mnala Drums (yuko Msondo), William Maselenge rythm guitar(marehemu), Andre Milongo(?), Bass na Second Solo, Kazembe wa Kazembe(marehemu) Solo guitar. Pamoja nao walikuweko John Kitime(Njenje), Jenipher Ndesile (?), George Mzee(Marehemu), Likisi Matola(Moonlight Band),Lucas Faustin(Police Brass Band) na Huluka Uvuruge(Msondo), baadae Athumani Cholilo(Marehemu) na Banza Tax(Marehemu), Selemani Nyanga(Uholanzi), Nana Njige(Marehemu). Wimbo wao Bomoa Tutajenga Kesho ulipigwa marufuku.

Saturday, July 3, 2010

The Djs

Hii picha ni kumbukumbu kubwa katika ulimwengu wa Disco Tanzania. Pichani ni kati ya the most bfamous Djs Tanzania wakati huo. Najua wadau mtawataja wote hapa, Meb, Masoud Masoud, John Peter, .................

Mwanzo