YOUTUBE PLAYLIST

Saturday, April 24, 2010

Baziano na Kasheba


Kwa wapenzi wa Fauvette na baadae Kasheba Group na Zaita Muzika, sauti ya Baziano si rahisi kusahaulika. Lakini kwa mapenzi yake Mungu, Baziano(wa kwanza kushoto) na mpiga gitaa wake Ndala Kasheba (wa pili kutoka kulia) hatunao tena duniani Mungu awalaze pema peponi. Pichani pia yupo Kasongo Mpinda (mwimbaji) wa pili kushoto, na Matei Joseph (mpiga drums).

Akina mama nao


Ni jambo lisilopingika kuwa akina mama wamekuwa sambamba na wanaume katika kuendeleza gurudumu la muziki wa nchi hii. Kumekuwa na tatizo la mtizamo na hivyo kufanya akina mama kutokuonekana sana katika fani hii kwa vile siyo siri imekua ikipigwa vita katika miaka yote. Pamoja na kuwa hakuna anaetamka hadharani kuwa wanamuziki ni wahuni, lakini taratibu na sheria zinaongea lugha ya kimya kuwa hivyo ndivyo. Nitoe mifano
1. Pamoja na kuwa kuna syllabus ya muziki kuanzia darasa la kwanza, kumekua hakuna jitihada kubwa ya kuhakikisha waalimu wanapatikana. Chuo cha Butimba ndio kimekua chanzo cha waalimu wa muziki lakini akishafika mashuleni hupangiwa vipindi vingine, na muziki huacha kama ulivyo.
2. Leo hii akiingia mwanamuziki kutoka nje ya nchi huhitajika kuwa na work permit, lakini kwa wanamuziki wa nyumbani hakuna taratibu zozote za ajira inayotambulika, hata wahudumu wa ndani wanatetewa bungeni lakini si wanamuziki. Angalia hata Waziri anaeshughulika na Vijana wa Tanzania na Kazi haoni soni kutoa ajira kwa vijana kutoka nje ya nchi yake katika fani ya muziki. Idadi ya wanawake katika muziki imekua kubwa sana kwa sasa ikilinganishwa na zamani lakini bado kuna wanawake wengi waliotikisa anga hizi zamani. Pichani ni muimbaji wa kike wa Afro 70 kutoka South Africa ambaye alisaidia sana kufanya muziki wa Afro kuwa na vionjo tofauti na bendi nyingine. Muimbaji huyu aliitwa Nini, na alirekodi nyimbo moja na Afro70, Mayele. Nini alikua na kaka yake aliyeitwa Vuli ambaye alipiga pia muziki hapa Tanzania na kutunga nyimbo ambayo bado inapiga na bendi kadhaa Tanzania'Lonely Child'. Vuli aliendelea na hatimaye kuwa manamuziki wa Lucky Dube.

Friday, April 23, 2010

Kilimanjaro Band 1




Kilimanjaro Band ni kati ya bendi kongwe hapa Tanzania. Ilianza mwanzoni mwa miaka ya sabini. Imewahi kutokea bendi ikapiga katika harusi ya mzazi na pia mtoto. Generation nzima ya familia. Maelfu ya watu wamekwisha hudhuria maonyesho ya Kilimanjaro Band hebu hapa tuone kati ya picha zao za zamani.

Bendi za Mkoa wa Morogoro

Kati ya mikoa iliyokuwa na Bendi nyingi, sijui kama ulikuweko ulioushinda mkoa wa Morogoro. Ilikuwa kila wilaya ina bendi. Baadhi ya bendi ninazozikumbuka ni Morogoro Jazz, Super Volcano, Cuban Marimba Band, Les Cuban, TK Limpopo, Kilosa Jazz (alikotokea Abel Balthazar), Ifakara Jazz, Sukari Jazz, Imalinyi Jazz, Mahenge Jazz, Kwiro Jazz., Mzinga Troupe. Na hata wale wakali wa wakati huo na ule wimbo wao enye maneno,

Waache waseme watachoka wao,

Mzee Makelo endeleza libeneke,

Waache waseme watachoka wao,

mtindo libeneke unatia fora

Hapa naongelea Butiama Jazz Band, iliyokuwa inapiga muziki kwa mtindo wao uliotokana na ngoma ya kwao Libeneke,wao ni wa Ifakara hivyo nao ni bendi ya mkoa wa Morogoro japo jina lilitokana na mahala alipozaliwa Baba wa Taifa.(Mzee Mkwega aliyekuwa mwenye bendi alikuwa kada mzuri sana wa CCM, hata kifo chake kilimkuta akiwa mtumishi wa CCM ofisi ndogo Dar es Salaam).

Mpaka leo ukienda Ifakara wakati wa msimu wa mavuno ikiwa kuna sherehe za jumla kama vile kipaimara, ndo utajua wanavyopenda ngoma. Kuna vikundi vingi vya ngoma ya Sangula na kila kikundi kimejipa jina la Bendi, hivyo utakuta mabango yakitangaza Tancut Almasi, Msondo, Super Volcano, na kila nyumba yenye sherehe huandaa kundi lake ni raha tupu hapo

Tuesday, April 20, 2010

Those were the days


Those were the days my friend,
We thought they would never end,
We would sing and dance for ever and a day.
We'd live the life we chose,
We'd fight and never loose ,
Cause we were young O yes we were young. Katika picha.. Patrick Balisidya na Salim Willis enzi za Afro 70

The Rifters 2


Kuna mara nyingine nakosa la kusema nikifikiria hali iliyopo katika ulimwengu wa muziki leo hapa Tanzania. Akina Raphael walikuwa wanawaza nini wakati wanapiga hapa? na ilikuwa nyimbo gani? wanaonekana wana mawazo hawa ni The Rifters

Shaaban Yohana Wanted


Nilikutana na Shaaban Yohana kwa mara ya kwanza katika bendi ya Tancut, ambapo gitaa lake la solo husikika katika nyimbo zote zilizokuwemo katika album za kwanza za bendi ile. Alipiga gitaa katika nyimbo zifuatazo:-
Nimemkaribisha nyoka
Kashasha
Tutasele
Mtaulage
Masafa Marefu
Butinini. Lakini aliniacha Tancut na kwenda Vijana Jazz huko tukakutana tena ambako solo lake linakumbukwa katika nyimbo nyingi kama vile Aza, Ogopa Tapeli,Thereza, Shoga, Malaine nk. Aliacha bendi ya Vijana na kujiunga na Ngorongoro Heroes akatesa sana huko, kisha akatimkia Botswana ambako yuko mpaka leo, muda mwingi akiutumia kama mwanamuziki wa studio.

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...