YOUTUBE PLAYLIST

Monday, April 19, 2010

Dar Es Salaam Jazz-majini wa bahari

Dar Jazz ndiyo kati ya bendi za kwanza nchini. Bado kuna utata wa kumbukumbu kwani katika kipindi cha mwanzo kulikuwekona Coast Social Orchestra inayosemekana ilikuja kuwa Dar Jazz. Wakati huohuo kulikuweko na YMCA Social Orchestra, hivyo ipi ya mwanzo ni kitendawili bado. Pichani ni Dar Jazz 1968. King Michael Enoch akiwa na kofia na nadhani hatupati taabu kumtambua Patrick Balisidya.Kama unavyoona amlifier ya magitaa ilikuwa moja tu, na chini kwenye kiti, kuna amlifier ambayo iliunganishwa kwenye cone spikas, zile spika za chuma tunazoziona kwenye sehemu za ibada na hizo ndizo zilikuwa kwa ajili ya waimbaji.

Tanzania All Stars


Ukitaka kujua umahiri wa wanamuziki enzi hizo ni vizuri ukazisikiliza nyimbo za Tanzania All Stars. Karibuni nitazitundika wote tuzisikilize, katika wimbo wa Samora, Zahir Ally Zoro aliimba Kireno, Jabali aliimba Kiarabu, Aziz Varda Kihindi we bwana wee. Haya tujikumbushe kwa kuwataja majina wote unaowaona hapo juu.

Usimkwae mtu likwae chua


Chakachua ndio ulikuwa mtindo wao, walikuwa na mpiga solo ambae wapiga magitaa wote waliomjua wanamheshimu kwa upigaji wake. Kuna mwanamuziki Mtanzania aliyeko Japan aliwahi kunambia kuna siku aliwahi kumsikilizisha muziki wa Chakachua mpiga gitaa mahiri George Benson, George Benson alisikitika sana kusikia aliepiga gitaa vile ameshafariki kwani alitaka wakutane watengeneza kitu cha pamoja, huyu si mwingine bali ni Michael Vicent. Na bendi ilikuwa Urafiki Jazz iliyokuwa chini ya Kiwanda cha nguo cha Urafiki Dar Es Salaam

Sunday, April 18, 2010

TP OK Jazz Dar es Salaam 1974

Mwaka 1974, TP OK Jazz chini ya Lwambo Lwanzo Makiadi walitembelea Tanzania, na kupiga show tatu. Moja National Stadium, Diamond na Bahari Beach. Onyesho la Bahari Beach walishirikiana na Afro 70. Matokeo ya ushirikiano huo yalijitokeza kwa nyimbo kadhaa zilizopigwa na Afro 70 kuwa na solo lilifuata mipigo ya Franco. Nyimbo kama Dada Rida, Umoja wa wakina Mama, ni baadhi ya nyimbo hizo,tena hii nyimbo ya pili ilikuwa kama kopi ya wimbo Georgette wa Franco. Ujio huo ulianzisha utamaduni uliodumu kwa muda mrefu wa bendi kupenda kutumia vifaa vya aina ya Ranger FBT.
















Hunaaaaaaa mwana hunaaaaaa

Baada ya Marijan na Safari Trippers kuimba kibao Hanifa, na katika chorus kuimba neno 'huna'. Liligeuka kuwa neno ambalo lilitumika kama vile leo neno 'kufulia' linavyotumika. Ungemsikia binti akimwambia mwanaume 'Hunaaa" na liliweza kuleta ngumi neno hilo. Haya picha ya hali wakati huo kwa wasomaji wa Kiingereza
.

Enzi za Buggy


Leo ni Jumapili ngoja nilete picha ambayo kwa vyovyote ilipigwa Jumapili , maana ndio ilikuwa siku ya Buggy, lile dansi la mchana lililokuwa linaanza saa 7 au nane na kuisha saa kumi na mbili jioni. Unaona mavazi ya siku hizo?, si muda mrefu baada yalipigwa marufuku , na kukaweko na posters kila mahala zikionyesha nguo gani za kuvaa. Vijana wa TANU Youth League walikuwa wakitembea na mikasi na kuchana nguo zilizoonekana hazifai. Loh, Hawa Rifters walikuwa kati ya makundi mengi ya wanamuziki vijana waliokuwa wakipiga muziki wa soul, hapa bwana nyimbo za Otis Redding, Kipofu Clarence Carter, Wilson Pickett , James Brown,Sam and Dave, Isaac Hayes ilikuwa mwendo mdundo

Saturday, April 17, 2010

Msondo Ngoma


Msondo ngoma wana kila haki ya kujiiita Baba ya muziki. Bendi hii ilianza mwaka 1964,kama NUTA Jazz na imekuwa na mtindo wa Msondo miaka yote na imekuwa juu miaka yote. Nani anaweza kujipima na Msondo. Pichani Mzee Abel Balthazal akiwa anapiga gitaa, Mzee Mnenge kwenye saxaphone, jamani majina ya wengine tafadhali.

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...