YOUTUBE PLAYLIST

Monday, May 17, 2010

Orchestra Lombelombe

Niliahidi kuwa nitaweka kipande cha gazeti chenye habari ya Orchestra Lombelombe, bendi ambayo wanamuziki wake walitoka katika bendi ya Morogoro Jazz. Bendi hii ilikuja baadae kuitwa Kurugenzi Jazz baada ya kuwa chini ya Ukurugenzi wa Mkoa wa Arusha, pichani ni Gumbo ambae alikuwa mpiga Bass, miaka ya sabini alihamia Iringa ambako alikuwa mfanya biashara.

Friday, May 14, 2010

Lady JD na Gadna Habash

Lady JD na Gadna G. Habash hongera kwa kutimiza miaka mitano ya ndoa.
Lady JD ni mwanamuziki ambaye amekuwa akiongeza kiwango cha ufanisi kwa wanamuziki siku hadi siku, na kila nyuma ya mwanamuziki mwanamke aliyeolewa, na mwenye mafanikio lazma kuna mume anaeungana nae kwa kila hatua. Shukrani kwako Gadna, wanamuziki wazuri wa kike wengi wamepotea katika fani kutokana na waume zao kuwazuia kuendeleza kipaji. Tunawatakia miaka mingi mingine ya furaha

Wednesday, May 12, 2010

Nani hawa? Picha ilipigwa Dodoma 1961


Nimepigiwa simu leo na mzee mmoja akanambia amesikia kuhusu blog hii na ana kitu cha kuchangia. Kanipa picha hii ambayo pengine ni ya zamani kuliko nyingi humu ndani. Kanambia siku moja 1961 alitoroka shule ili aweze kumwona mwanamuziki ambaye alimpenda kuliko wote. Alikuwa anasoma Dodoma wakati huo, na aliweza kupata picha siku hiyo picha hii naiweka kwenu. Swali, nani anaweza kuwataja wanamuziki waliomo katika picha hii.? Wanaoimba hapo wote ni marehemu, anaepiga gitaa yu hai na picha yake ya sasa iko katika blog hii.

Tuesday, May 11, 2010

Zahir Ally Zorro


Muziki una mengi ya kushangaza, unaweza ukafika wakati ambapo mwanamuziki fulani kila akitoa nyimbo inatokea kupendwa. Hali hii inanikumbusha kipindi Zahir Ally Zorro alipokuwa JKT Kimulimuli Jazz , bendi iliyokuwa katika kambi ya Mafinga huko Iringa. Wakati huo ambapo JKT ilikuwa na makundi mawili ya askari kuna wale waliojitolea kwa ridhaa kujiunga na jeshi hilo na kulikuweko na wale waliolazimika kujiunga kwa mujibu wa sheria. JKT ilianzisha bendi mbili ambazo zote zilikuwa na muziki mkali. Dar es Salaam kulikuwa na JKT Kimbunga Stereo, jina lililotokana na staili yao ya Kimbunga, na Iringa kulikuwa na JKT Kimulimuli, hii ilitokana na kuwa na taa za steji zenye kuwakawaka. Bendi ya JKT Kimulimuli ilipata umaarufu sana baada ya mwanamuziki Zahir Ally Zorro kujiunga na bendi hii. Ilikuwa ni kama lazima usikie vibao vya bendi hii kila siku radioni. Kabwe..tungo kuhusu mtoto mtukutu alieanza uhuni toka mdogo na kulazimika kufungwa hata jela ya watoto. Kitu mapenzi kilianza zamani.....maneno ya kibao kingine kilichogusa sana hisia za watu, Tausi...wimbo unaohusu mwanamuziki aliyemtungia wimbo mpenzi wake. Ilikuwa kama vile kila kibao anachotunga Zahir kinakuwa hit.

Sunday, May 9, 2010

Mkongwe mwingine


Wengi tutakuwa tunamfahamu sana marehemu Ndala kasheba alieko kulia, je unamfahamu huyo anaesalimiana nae. Subiri usikie mchango wake katika muziki wa Tanzania

Abdalla Gama


Kwa wapenzi wa DDC Mlimani Park, jina la Abdallah Gama ni jina muhimu katika historia ya bendi hiyo. Mwanamuziki huyu mpigaji wa gitaa la rythm alipata umaarufu zaidi baada ya wimbo wa uliotungwa na Assossa -Gama, ambao mpaka leo bado unafurahisha sana. Gama na wenzie kama Joseph Mulenga, Abel Balthazar, Cosmas Chidumule chini ya King Michael Enoch waliweza kutunga na kutengeza nyimbo ambazo bado zinaleta burudani miaka thelathini baada ya kutungwa. Abdallah Gama tena atakumbukwa kwa kazi zake alipokuwa BimaLee wakiwa na watunzi kama Jerry Nashon, Shaaban Dede, solo la Mulenga , nba besi la Mwanyiro, hapo ilikuwa utamu kolea. Pichani Gama(mbele)akiwa na mpiga gitaa mwingine Huruka Uvuruge ambae sasa yuko Msondo, na mpiga drum Matei Joseph ambae kwa sasa anendesha bendi yake African Minofu

Friday, May 7, 2010

Wanamuziki ndugu 3


Kitendawili kingine. Picha hii ilipigwa Seaview 1974, kuna wanamuziki wa Afro70, na wanamuziki ndugu ambao nao wametoa mchango mkubwa katika fani ya muziki, unawatambua ni akina nani hapo?

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...