Nikisema tuanze kutaja mitindo ya bendi ni mingi sana maana kila bendi imekuwa inakuja na mtindo wake. Majina mengine ya mitindo yana historia na maana na mengine yana kuwa yakutunga na kwa kweli hata waliokuwa wanayatumia hawana maelezo ya maana ya maneno hayo. Mundo,Msondo, sokomoko, dondola, kiweke, segere matata,super mnyanyuo, vangavanga, chikwalachikwala, libeneke na kadhalika ilikuwa mitindo ya bendi mbalimbali, na muziki wa bendi ulikuwa ndiyo unaonyesha utofauti huo. Kwa mfano katika mji wa Tanga ulikuwa na bendi kubwa mbili, Jamuhuri Jazz na Atomic Jazz. Jamhuri ilikuwa na mtindo wa Toyota, na baadae Dondola, hata muziki katika awamu hizi mbili katika bendi hiyohiyo ulikuwa tofauti. Atomic walikuwa na mtindo wa Kiweke. Muziki wao ulikuwa tofauti na ule wa Jamhuri. Na wapenzi wa Jamhuri hata wakizeeka husifu mtindo wa upigaji wa Jamhuri na rythm la Harrison Siwale(Satchmo). Kadhalika wapenzi wa Atomic watakwambia hakuna kama Kiweke, upigaji solo wa John Kijiko, bass la Mwanyiro na kadhalika. Mtu ambae kisha sikia muziki katika mtindo wa Ambianse wa Cuban Marimba, hawezi kuchanganya na Likembe wa Moro Jazz. Nimeanza kwanza kwa kutaja bendi zilizokuwa katika mji mmoja tena huko mikoani ambapo watu walikuwa wachache na wanamuziki wanajuana na kuishi jirani. Hali hiyo ndio iliyokuwa Tabora, ambako pamoja na Tabora Jazz, kulikuweko na Nyanyembe Jazz, Kiko Kids, muziki wa kila bendi ulikuwa tofauti na mwingine. Dar es salaam kulikuwa na bendi nyingi na hivyo mitindo mingi. Hakuna aliyeweza kuchanganya Maquis na OSS, wala Sikinde na msondo, Sokomoko, afrosa, Katakata vumbi nyuma ya Kyauri voice havikuwa na mpka wa kulinganishwa. Kikubwa ninachotaka kueleza ni kuwa bendi kuwa na mtindo ilikuwa si jina tu bali kulikuweko na kazi ilifanyika ili kupata kulinda na kuendeleza mtindo ambao bendi iliamua kuwa nao. Nakumbuka wakati wa mazoezi enzi hizo unaweza ukatunga wimbo ukianza kuimba wenzio watakwambia mbona unafanana na bendi fulani na hapo utakarabatiwa mpaka uwe katika mtindo wa bendi husika.