Nadhani kuna haja ya kuongelea swala la teknolojia katika muziki na hapa nitazungumzia teknoljia ya kurekodi. Nyimbo karibu zote ambazo husifika kama zilipendwa zilirekodiwa wakati wa kutumia kanda(tape), kwa teknolojia iliyoitwa 'two track recording' (pichani juu).

Kwa teknolojia hii ilihitaji wanamuziki kuwa wazuri sana na fundi nae kuwa mzuri, kwani kama unarekodi wimbo bendi nzima lazima ipige kwa pamoja na akikosea mtu lazima kurudia wimbo wote tena kwa pamoja. Kwa bendi zilizorekodi RTD miaka hiyo zilipewa siku mbili za kurekodi kinachoitwa album siku hizi, yaani nyimbo sita au zaidi kwa kipindi cha siku mbili. Siku ya kwanza Bendi ilitakiwa kufika asubuhi kwenye studio za RTD, ambapo ilifanyika kazi ya kufunga vyombo vyote na kuvijaribu hapo fundi mitambo ndipo alipokuwa na kazi kubalance vyombo vyote viwe vinasikika inavyostahili. Mchana wa siku hiyo ililazimika bendi kurekodi nyimbo zote bila kukosea hata kama ni kumi. Siku ya pili ilitumika kurekodi kipindi cha klab raha leo show. Mwanamuziki yoyote wa siku hizi atakwambia haiwezekani kurekodi nyimbo sita kwa siku moja. Teknolojia ya sasa hutumia njia inayoitwa 'multi track recording', ilianza kwa kurekodi kwenye kanda maalumu tack 4,kisha zikawezekana 8,16,32 na kuendelea. Siku hizi kwa kutumia program za kompyuta ktu una uwezo wa kuwa na mamia ya tracks, hivyo basi hata bendi ya watu mia kila mtu akaweza kuja siku yake na kurekodi kipande chake , akakakirudia mpaka kikawa sawa, na ndio maana siku hizi kurekodi wimbo mmoja inaweza ikachukua hata mwezi na zaidi , kwa kurudia sehemu zenye makosa, kuzibadili kabisa na kadhalika, na siku hizi kuna hata teknolojia inayoweza kurekobisha sauti iliyoimbwa vibaya kwa maana hata kama hujui kuimba unaweza ukatengezwa mpaka uonekane unajua kuimba. Kama kawaida teknolojia mpya ina faida nyingi sana lakini mwisho wa yote faida hizi huonekana pale akiwepo fundi mitambo mzuri na msanii mzuri. Waliorekodi enzi za two track duniani kote husifia ule utamu ambao hupatikana wakipiga pamoja, ambao hupotea kama kazi itarekodiwa kila msanii akija kwa wakati wake.