YOUTUBE PLAYLIST

Monday, July 25, 2022

MWAKA MMOJA BILA MPIGA KINANDA WAZIRI ALLY SEIF

 
















Ni mwaka mmoja toka mwanamuziki Waziri Ally Seif alipotutoka ghafla., naikumbuka vyema siku ili, ilikuwa siku ya Ijumaa tarehe 23 July 2021 , kama saa nne usiku hivi nilipoamshwa na mlio wa simu yangu, nilikuwa tayari usingizini kwani mchana ule nilikuwa nimefanya mizunguko mingi sana katika eneo la Ngome Kongwe Zanzibar, nikiwa katika harakati za Tamasha la filamu la ZIFF, kwani kulikuwa na filamu ambayo niliiweka muziki nayo ilikuwa ikishindana katika matuzo mbalimbali ya tamasha lile. Nilishangaa kona namba iliyokuwa ikiita, ilikuwa ya Lulu, binti wa marehemu mwanamuziki mwenzangu Mabruk Omari  maarufu kwa jina la Babu Njenje, binti huyu  makazi yake ni Uingereza. Nikapokea simu ile, cha kushangaza alikuwa analia, nikamuuliza vipi? Akanijibu ‘ Anko kwani we hujui? Kuna mtu kanipigia simu kuwa Anko Waziri  amefariki, hebu nihakikishie maana siamini’. Nikamwambia subiri kwani habari za uzushi wa vifo vya watu katika siku hizi za teknolojia rahisi za mawasiliano ni jambo la kawaida sana. Niliwapigia wanamuziki wawili wa bendi ya Kilimanjaro nao wakanambia hawana taarifa ya kifo, ila walikuwa na taarifa kuwa Waziri alikuwa kapelekwa hospitali nikapewa namba ya mmoja wa waliompeleka Waziri hospitali namba hiyo ikawa haipatikani. Hatimae ukaja ujumbe wa Whatsapp ukionyesha kuwa rafiki na ndugu mkubwa wa Waziri Ally, bwana Aboubakary Liongo alikuwa katoa taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa Waziri Ally hatunae tena. Nikampigia Aboubakary akanihakikishia kuwa Waziri Ally hatunae tena. Hatimae nilimtumia Lulu ujumbe  wa maandishi kuwa kweli Anko wake hatunae tena. Na ghafla simu nyingi zikaanza kupigwa nyingine za pole na nyingine za waandishi wakitaka taarifa na nyingine za wapenzi na mashabiki wa bendi ya Kilimanjaro wakitaka kujua kama walichokisikia ni kweli. Na hilo liliendelea usiku mzima.

Nilianza kukumbuka historia yangu na Waziri Ally, nilimuona kwa mara ya kwanza mwaka kati ya mwaka 1984 na 1985 wakati huo, bendi ya Kilimanjaro ilipokuwa ikiitwa The Revolutions na ikiwa na makazi yake Kilimanjaro Hotel Dar es Salaam. Bendi hiyo ilikuwa imetoa tangazo gazetini  ikataka watu wanaotaka kushindana kuimba wimbo wa ABBA wa I have a dream wafike katika ukumbi wa Simba Grill wa hoteli ya Kilimanjaro, kwa kuwa nilikuwa najua kuimba wimbo huo nikawa mmoja ya washiriki.  Baadae nikaja sasa kuongea nae binafsi baada ya bendi hiyo kuhamia hoteli iliyokuwa inaitwa Bushtrekker, na alikuwa akiuuza kinanda chake wakati huo nilikuwa katika bendi iliyokuwa ikihitaji kinanda, hapo tukaongea na kujadili kile kinanda, japo tulishindwa kukinunua. Tuliendelea kukutana hapa na pale katika shughuli mbalimbali za kimuziki kama vile semina na mikutano mbalimbali au hata matamasha kama vile mashindano ya bendi ya Top Ten Show.  Mwaka 1999 nikiwa Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Waziri Ally alikuwa mmoja ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, katika mwaka huu juhudi za CHAMUDATA kupata studio yake ya kisasa ya kurekodi, gazeti lake na kituo chake cha redio zikafikia kileleni, tukaweza kuanzisha taasisi ya habari ya CHAMUDATA iliyoitwa Asilia News Agency, ambamo Waziri Ally alikuwa mmoja ya wajumbe wa bodi wa taasisi hiyo ambayo ingeendesha redio na gazeti la CHAMUDATA kwa msaada wa taasisi ya Norway iliyoitwa Stromme Foundation. Bahati mbaya sana sana  viongozi wa Halmshauri Kuu na Kamati kuu ya CHAMUDATA walikuja kuukataa mradi huo wote kwa kuwa walielezwa kuwa Katiba ya CHAMUDATA ilikuwa na mapungufu na ilitakiwa irekibishwe kabla ya kuendelea na mradi. Jambo ambalo viongozi hao waliliita kuiingiliwa kwa chama chao na kuukata mradi, jambo lililotulazimu baadhi ya viongozi  kuamua kujiuzuru uongozi wa CHAMUDATA, akiwemo Waziri Ally na Abdul Salvador na mimi ambaye nilikuwa mwenyekiti wakati huo.

 Kwa kuwa vifaa vya studio vilikuwa tayari vimeshaingia nchini, Abdul Salvador, Waziri Ally, mimi na bendi nzima ya Kilimanjaro, tulishirikiana kuhakikisha studio inatengenezwa na kuanza kufanya kazi kama ilivyopangwa katika maombi ya mradi, studio iliwekwa chini ya Bodi ya muda ikitegemewa kuwa viongozi wa CHAMUDATA wangeona kosa lao na kurudi kuja kuchukua na  kuendesha mradi wao,  jambo hilo hakilikutokea, Ubalozi wa Norway hatimae baada ya kutangaza gazetini ukaikabidhi studio hiyo kwa KIlimanjaro Band. Na ilikuwa katika kipindi hiki nilipojiunga na Kilimanjaro Band kama mwanamuziki na kuanza kufanya kazi kwa karibu na Waziri. Kwanza alikuwa makini sana kila kitu  alichokuwa akikifuatilia. Tulikuwa na ratiba nzuri sana ya mazoezi makali yaliyobebwa na upigaji wake mahiri wa kinandana upangaji wa sauti za waimbaji. Mwaka 2000 tukaweza kurekodi katika studio yetu album ya Kinyaunyau, na Waziri Ally alienda na ‘tracks’ Uingereza kufanya ‘mastering’ ya album  hiyo ambayo inatamba mpaka sasa na hata wanamuziki wa Bongofleva wameweza kurekodi tena na tena wimbo wa tupendane na vibwagizo vingi kutoka album hiyo bado vinaendelea kutumika katika nyimbo mpya zinazorekodiwa na wanamuziki wapya. Tuliweza kuchapisha CD, kanda za video na kanda za kaseti za album ya Kinyaunyau hukohuko UIngereza na hatimae kuziingiza nchini. Tulihakikisha tunalipa kodi zote vizuri na kuweka mahesabu yetu sawa, nia ilikuwa kuionyesha TRA makusanyo ambayo ingeweza kuyapata kutokana na biashara ya muziki, lakini pamoja na jitihada hizi TRA hawakuonyesha kujali au kuelewa nia yetu mara zote tulizojaribu kuwaona. Waziri Ally aliingiza Kilimanjaro Band LTD kuwa mmoja wa wanachama wa Chamber of Commerce ili kuonyesha kuwa muziki nayo ni biashara na alikuwa muwakilishi kwa muda mrefu wa bendi na wasanii kwa ujumla katika taasisi hiyo.  Busara za Waziri Ally zilimfanya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Bodi wa Tamasha la muziki la Sauti za Busara linalofanyika kila mwaka Zanzibar, na akawa mjumbe aliyetegemewa kwa muda mrefu.  Historia yake kimuziki ya Waziri  ilianzia Tanga ambako ndiko alikozaliwa. Akajiunga na kundi maarufu la Lucky Star kama mpiga kinanda wakati akiwa bado mtoto mdogo. Mzee Moses Nnauye alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida akaanzisha bendi iliyoitwa Ujamaa Jazz Band  na kuwakusanya wanamuziki mahiri akiwemo Waziri Ally na marehemu  Suleiman Mwanyiro, bendi hiyo ilikuwa ikipiga muziki kwa mtindo waliouita King’ita.  Waziri alirudi tena Tanga na kujiunga na kundi lililokuwa limeanzishwa na vijana wa Kigoa waliokuwa hapo Tanga, na kukutana huko na Marehemu Mabruki Omary maarufu kwa jina la Babu Njenje na Mohamed Mrisho  maarufu kwa jina la Moddy. Kundi hilo lilikuwa likiitwa Love Bugs. Baadae jina lilibadilika na kundi kuitwa The Revolutions. Kundi hili lilitoka Tanga na kuanza kuwa maarufu katika hoteli kubwa za Dar es Salaam na Arusha. Na ni wakati huu Waziri Ally aliondoka Revolutions na kujiunga na kundi la JUWATA. Katika kundi hili Waziri aliweza kushiriki katika nyimbo ambazo zilikuja kuleta mapinduzi katika umuhimu wa kinanda kwenye bendi za ‘rhumba’. Wimbo wa Beresa Kakere unaojulikana kama Sogea Karibu ulimpa nafasi Waziri kupiga kinanda ambacho kimeufanywa wimbo huo upendwe mpaka leo, na pia kukipa heshima kinanda katika muziki wa rhumba la Tanzania, katika zama hizo kinanda kilidharauliwa sana katika muziki wa rhumba na kuitwa chombo cha muziki wa Taarab au muziki wa hotelini. Waziri hakukaa sana JUWATA na baada ya miezi michache akarudi Revolutions, kuhama huku kukampatia jina la utani la Kissinger. Henry Kissinger alikuwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani kati ya mwaka 1973 hadi 1977 na alijukana sana kwa kusafiri kwake nchi mbalimbali, na kuhama kwa Waziri kutoka Revolutions na kwenda JUWATA kukafananishwa na Kissinger na akapewa jina hilo la utani mpaka umauti wake. Waziri hakuwahi kuhama tena Revolutions, mwaka 1997 bendi hii ikabadili jina na kujiita Kilimanjaro Band baada ya kuweka maskani ya muda katika jiji la London na kurekodi album ya kwanza iliyoitwa Katakata,  hivyo kuona bendi ingetambulika ya Kiafrika zaidi kwa jina la Kiafrika.  Waziri Ally ambaye amezaliwa mwezi Novemba mwaka 1954, aliwahi kunambia alipokuwa mdogo alikuwa akitaka kuwa hakimu, akawa anatoroka hata shule kwenda mahakamani na kusikiliza kesi zinavyoendelea. Mama yake alikuwa askari magereza, na baba yake Mzee Ally Seif yu hai. Kwa miaka kadhaa ya karibuni,  Waziri alikuwa na tatizo kubwa la moyo, na amewahi kwenda India mara mbili kwa ajili ya matibabu, alikuwa akitumia dawa kila siku ili kuwa katika hali ya unafuu. Ucheshi wake na utani wake ulificha maumivu aliyokuwa nayo moyoni mpaka kifo kilipomkuta. Nimalizie kusema Mungu amlaze pema peponi ndugu yetu na rafiki yetu Waziri Ally Seif.      


No comments:

Post a Comment

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...