Miezi
chache zilizopita rafiki yangu mmoja alinambia ameamua kuunda bendi mpya kabisa,
alikuwa na lengo la kuleta muziki mpya kabisa katika anga ya muziki Tanzania. Aliongea
kwa furaha na ni wazi alikuwa ana nia ya kufanya kitu kikubwa, maana alikuwa
amegharamia fedha nyingi kununua vifaa vipya kabisa vya kuanzisha bendi. Mwezi
mmoja baada ya mazoezi kuanza alinitafuta na kunambia ameamua kuvunja bendi na
vyombo anauza. Nilipomuuliza kwanini kabadili mawazo katika kipindi kifupi
vile, hata onyesho moja halijafanyika? Akanijibu. ’Wanamuziki wamenishinda, wana
matatizo makubwa ya ndhamu’. Kiukweli sikushangaa sana kwani jambo hili si geni
kabisa kwenye tasnia ya muziki kwa siku hizi. Mfumo wa uendeshaji bendi siku
hizi ni tofauti sana na miaka ya nyuma.
Nichukue
mfano wa bendi Vijana jazz Band, bendi ambayo nilijiunga mwaka 1989. Kujiunga
na bendi hii kulitokana na mwaliko niliyoupata kupitia kwa muimbaji rafiki
yangu Marehemu Mohamed Shaweji. Shaweji tulikuwa wote Tancut Almasi Orchestra kisha
yeye akaniacha kule na na kujiunga na Vijana Jazz Band, yeye na muimbaji
mwingine Marehemu Gota gota wakiwa wamemfuata mpiga gitaa Shaaban ‘Wanted’
Yohana, aliyetoka Tancut pia na kuhamia Vijana Jazz Band miezi michache kabla.
Hivyo siku moja nikiwa na bendi ya Tancut Almasi kwenye onyesho kwenye ukumbi
wa CCM kata ya 14 Temeke, Shaweji alikuja na kunambia kuwa Hemed Maneti,
kiongozi wa Vijana Jazz Band alikuwa anataka nijiunge na bendi yake. Nilikubali
na mwezi Oktoba 1989 nilijiunga na Vijana Jazz. Kufikia mwezi wa Desemba mwaka
huohuo nikawa nimepewa wadhifa wa kuwa Band Master, kazi za Band Master ni
kuangalia nidhamu ya jumla ya wanamuziki, ikiwemo mahudhurio mazoezini na kazini,
uchelewaji, ulevi, usafi binafsi wa mwanamuziki na pia kupanga ratiba ya nyimbo
ambazo zinatakiwa kupigwa katika onyesho.
Kwa mfumo uliokuweko, Band Master aliweza kumsimamisha mwanamuziki
yoyote aliyekiuka sheria za bendi, au kutoa adhabu ya kukatwa fedha kutoka
kwenye mafao yake ya kila wiki ikiwa ni adhabu kwa makosa mbalimbali. Nguvu
hizi zilifanya wanamuziki kuwa na nidhamu wakati wote wawapo kwenye shughuli za
bendi. Ikumbukwe kuwa katika bendi kulikuweko na kiongozi mkuu Band Leader.
Huyu alikuwa na mamlaka ya kufukuza mtu kazi na pia kuajiri na ndie anaepanga
hata ukubwa wa mshahara, lakini alikuwa haingilii madaraka ya Stage Master. Kwa
kawaida wanamuziki waliona ni heri matatizo yao yaishie kwa Band Master kwani
yakifika kwa Band Leader yanakuwa ndio yamefika hatua ya mwisho isiyo na rufaa
na inaweza kuwa hasara kubwa. Ili kuonyesha Band Master alivyokuwa na nafasi ya
pekee, siku moja wakati niko Vijana jazz band, ilikuwa twende kwenye moja ya
maonesho na kuna gari ilikuwa inatupitia wote majumbani kwetu, tulipofika
nyumbani kwa Band Leader Hemed Maneti, alitoka nje akiwa na karatasi kutoka
hospitali akaja kunitaarifu kama Band Master, kuwa hataweza kuja kazini kwani
anaumwa, Maneti alikuwa Band Leader lakini alikuwa akiheshimu nafasi ya Band
Master, tena nilikuwa bado mgeni katika bendi. Hii ilikuwa ni ishara wazi kwa
wanamuziki wengine kuwa Band Master lazima aheshimiwe na wote.
Hali
si hivi katika bendi nyingi siku hizi. Ngumu kujua nani mwenye madaraka gani
kwani bendi zinakuwa na mwenye bendi, mkurugenzi wa bendi, meneja, maseneta,
kiongozi wa bendi, wadau wa bendi. Wote hawa wana mamlaka zisizo na mipaka,
wanaweza kuamua wimbo gani upigwe, wanaweza kuamua nani atimuliwe au nani
aingizwe kwenye bendi, mmoja akimsimamisha mwanamuziki kwa utovu wa nidhamu
mwingine anaweza akamrudisha, hakuna mtu mwenye amri ya mwisho kuhusu lolote
lile, hivyo nidhamu imeshuka sana, na pasipo na nidhamu si rahisi kuweko na
maendeleo yoyote yenye tija.
Sasa
nizungumzie kosa la rafiki yangu aliyetaka kuanzisha bendi na ikamshinda,
kwanza baada ya kununua vyombo, aliaanza kutafuta wanamuziki akisaidiana na
watu wake wa karibu, kisha akamteua kiongozi wa bendi, ambae kimsingi kilikuwa
kilemba cha ukoka kwani rafiki yangu ndie aliyekuwa na amri ya mwisho kuhusu
lolote katika bendi. Na kwa kuwa hakuwa na muda wa kushinda kila mahala na
bendi, kundi likawa halina kiongozi mwenye mamalaka na mwisho kila mtu akawa anafanya lake, walevi wakalewa
sana, wachelewaji wakendelea na uchelewaji wao, hakukuwa na mtu aliyekuwa na
uwezo wa kutoa mwelekeo wa bendi kinidhamu wala kimuziki. Muziki wa bendi kwa
ujumla umekumbwa na tatizo hili la kukosa uongozi, maamuzi mengi yanafanyika
kwa vikao, hata maamuzi yale ambayo ni ya kitaaluma yanangoja makubaliano ya
wengi, na kwa mtindo huu bendi zitachelewa sana kujikwamua kwenye tope ambalo
zimenasa. Ushauri kwa wanaotaka
kufungua bendi, ni bora kumtafuta mwanamuziki mmoja ambaye unaamini anaweza
kutengeneza muziki unaoutaka au unaodhani utakuletea biashara kisha umwachie
aijege hiyo bendi na wanamuziki anaoona yeye wanafaa, hapa tayari utakuwa
umejenga utawala unaoeleweka. Mwenye vyombo usiingilie moja kwa moja mambo ya
bendi, wanamuziki wakishajua kuwa kiongozi wa bendi hana mamlaka kamili,
nidhamu inavunjika.
No comments:
Post a Comment