YOUTUBE PLAYLIST

Wednesday, August 18, 2010

Shaw Hassan Shaw


Kwa wapenzi wa Vijana Jazz wanakumbuka vile vipande vya keyboards vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni, mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu alizaliwa

tarehe 25/sept/1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi. Aliporudi Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.

Ni chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda). Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College. Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana na wanamuziki wengi lakini wengi pia wametangulia mbele ya haki. Waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Abuu Semhando, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Mirambo, Hassan Dalali, Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA), na Marehemu Abel Baltazar , hapa alikutana na wanamuziki kama Benno Villa Anthony na Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu, mwenyewe anasema, ‘….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…’. Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa akakutana na Zahir Ally, Ally Choki Rwambow, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani, pili hii bendi ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel mbalimbali Malaysia,Singapore, Indonesia,Thailand na Japan jambo ambalo lilifanya aone kila kitu ni kigeni. Katika bendi hiyo alishirikiana na akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy,Delphin Mununga na Kinguti System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hiyo ilijiita Jambo Survivors Band, itakumbukwa kwa ule wimbo Maprosoo uliokuwa katika album ya MAPROSOO. Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Wameshapita Oman , Fujairah, U.A.E, Singapore, Malaysia na sasa wapo Thailand. Shaw anasema wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia akiwa na Kanku Kelly kwa mara ya kwanza kupiga muziki akiwa amezungukwa na watu weupe Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja.

(Picha ya juu Burhan Muba, Kinguti System ,Hassan Shaw, ya chini ni Vijana Jazz, Hassan Shaw wa mwisho kulia)



8 comments:

  1. Anonymous22:12

    John! Nimefurahi sana kupata habari za mtu wangu niliyepotezana nae sana kupitia makala yako hii. Burhani Muba aka Jazz man. Ninadiriki kusema ni mmoja kati ya wapigaji wa gitaa linalo ongoza (solo) aliyetulia sana. Anatone kwenye vidole vyake na mara nyingi yukomakini sana katika kuhakikisha hafanyi fyongo katika kazi zake.
    Asante sana kwa hili .

    ReplyDelete
  2. Anonymous11:09

    Naam kwa kweli huyu Bwana ndiye pekee aliweza kumtoa jasho Abdul Salvadol. Ki ukweli, ile keyboard aliyopiga kwenye "Penzi haligawanyiki" ni mwisho wa habari. Ufundi wa hali ya juu kuanzia kwenye intro hadi mwisho wa mziki. Ila na wimbo wenyewe ulikuwa mkali mno. Mzee kitime hebu katazeni hao wanaozirudia hizi nyimbo. Yaani wanaziaribu mno. KWanini wasiimbe zao hata kama wapo vijana jazz kwa sasa. Nasikiliza hizo nyimbo yaani zimechakachuliwa mno. Waambieni waache kuharibu utunzi wa watu jamani.

    ReplyDelete
  3. Anonymous13:31

    John,

    Ni Hassan Show aliyepiga kinanda kwenye wimbo wa 'Tereza' wa Vijana Jazz?

    Kama ni yeye alipiga vizuri mno..solo guitar nadhani alikuwa Shaban Yohana.

    -Marubaini

    ReplyDelete
  4. Wakati wa Thereza Shaw alikuwa keshahama Vijana, mpiga keyboard alikuwa kijana anaitwa Mhina Mhando, alienda Kenya miaka mingi iliyopita, nasikia yuko Nakuru anapiga piano katika hotel ya Intercontinental

    ReplyDelete
  5. Anonymous23:46

    Wapiga vinanda mahiri Waziri Ally - Njeje, Hasan Shaw - Jambo Survivors, Mhina Mhando - Kenya , Je Balozi Kitime huyu Richard Dyauli aliyewahi kupiga kinanda na chini ya Kundi la Maestro Ndala Kasheba kwa sasa (Richard Dyauli) yupo wapi na kundi gani?

    ReplyDelete
  6. Yeye hupendelea zaidi kuitwa Richy, anapiga peke yake kwa kutumia sequencer. Mara kadhaa amakuwa akienda mashariki ya kati kwa mikataba ya miezi mitatu mpaka 6

    ReplyDelete
  7. Anonymous17:39

    Namuunga mkono mtoa mada hapo juu aliyeeleza kukerwa kwake na mtindo wa wanamuziki kurekodi upya nyimbo za zamani. Ikumbukwe kuwa haiwezekani hata siku moja kupata kitu bora zaidi ya kile ambacho ni ‘original’. Cha kusikitisha hapa ni kwamba wanaorudia nyimbo za zamani si wanamuziki wa sasa tu, bali hata magwiji katika fani hiyo. Kwa mfano, hivi karibuni Sikinde walirekodi upya nyimbo zao za mwanzoni mwa miaka ya 1980 kama Hiba na Mwanetu. Ninachoweza kusema ni hizi nyimbo zilizorekodiwa kwa kutumia ma-synthesizer badala ya ala za upepo ni mbaya, mbaya, mbaya kabisa! Kingine ni kwamba baadhi na wanamuziki wa sasa wana uwezo mdogo mno ukilinganisha na wale waliopiga nyimbo ‘original’. Kwa mfano, Sikinde wameshindwa kabisa kurudufu utalaam wa marehemu Joseph Mulenga na Suleiman Mwanyiro katika nyimbo zao walizozirekodi upya. Ukija kwa Vijana Jazz ya sasa ndio balaa. Hao wanaopiga upya nyimbo za bendi hiyo sidhani kama waliwahi kuhudhuria maonyesho ya Pamba Moro na Saga Rumba hata siku moja pale Vijana Social Hall enzi hizo.

    ReplyDelete
  8. Anonymous13:09

    Safi sana mzee mwakitime, wallahi posts zako hizi zimenikumbusha mbali sana. Nilikuwa najiuliza mara kwa mara kati ya Father Kidevu na Hassan Show nani moto hadi leo sina jibu.

    Maselepa
    "Kama zamani"
    Safarini Bujumbura, Burundi

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...