YOUTUBE PLAYLIST

Sunday, February 28, 2010

Kina nani hawa?


Leo natoa picha 3 za wanamuziki maarufu wakati wakiwa bado makinda, swali ni akina nani hawa?


Saturday, February 27, 2010

Mzee Hamisi Kitambi Hatunae Tena


Mzee Hamisi Kitambi hatunae tena. Amefariki tarehe 26 Feruary 2010, na kuzikwa tarehe 27 February 2010. Mzee Hamisi Kitambi kwa mara ya mwisho alikuwa bendi ya Msondo Group. Mungu Amlaze pema peponi.(Picha kwa hisani ya ya www.issamichuzi.blogspot.com)

Friday, February 26, 2010

Wana Bantu Ngoma wanakula miziki

Bantu Group chini ya Komandoo Hamza Kalala imekwisha toa wakali wengi katika anga la muziki hapa Tanzania. Komandoo mwenyewe ana historia ndefu ikiwemo ya kuwa moja wa waanzilishi wa Bendi ya Vijana chini ya mkongwe John Ondolo Chacha. Amekwishapitia bendi kama Matimila na kushiriki vibao vikali kama Alimasi, amepitia UDA na ikawa katika anga za juu kimuziki Tanzania wakati wake. Komandoo hatasahauliwa na vibao alivyopiga Vijana kama Mary Maria , mpini wake wakati wa Pambamoto Awamu ya pili haujarudiwa tena. Kibao chake Nimekusamehe lakini sitakusahau cha Washirika Stars ni picha tosha ya kazi za Hamza. Pichani ni Juni 1, mwaka 1996. Kwenye onyesho kubwa la Siku ya Mazingira ambalo ndilo lilikuwa onyesho la kwanza la muziki 'live' kuonyeshwa na ITV. Na lilirushwa kwa muda wa masaa kama 6 wananchi wakipiga simu lilendelee hewani!!!!. Wasanii kama MR2 walipata umaarufu mkubwa baada ya tamasha hili pale Mnazi Mmoja. Tamasha liliendeshwa na CHAMUDATA chini ya Mwenyekiti John Kitime.
Picha ya chini tunamwona watatu toka kushoto Eddy Sheggy, na mwishoni ni Rogart Hegga ambaye kwa sasa yuko Twanga Pepeta.

Vumbi





Kwa wapenzi wa Maquis Original jina la "Vumbi" ni la kutia kumbukumbu nyingi sana, na kwa wale ambao wamekuwa wakiusikia ule wimbo wa Chatanda Ngalula walisikia tena na tena Tchimanga Assossa akilitaja jina hilo wakati Vumbi anacharaza gitaa tamu la solo kwenye wimbo huo. Vumbi kwa sasa anaendelea na muziki huko Sweden na maelezo ya maisha yake kimuziki ni haya. Jina lake kamili ni Alain Kahanga Dekula , alizaliwa katika jimbo la Kivu katika Jamhuri ya Kongo. Baada ya kumaliza High School alianza kupiga gitaa katika bendi ya Bavy National iliyokuweko Uvira Kusini mwa Kivu. Baadae akiwa na kaka yake Rachid King wakajiunga katika bendi ya Grand's Mike Jazz Band wakati huo ikiwa na wanamuziki kama Remmy Ongala,Kasaloo Kyanga,na Kawele Mutimanwa. Akaja Tanzania na kujiunga na Orch.Maquis Original na kati ya nyimbo ambazo anajulikana nazo sana ni Ngalula and Makumbele.Wakiwa na mtindo wa Zembwela-Sendema,alikuwa jukwaa moja na miamba wa magitaa wakati huo akina Nguza Viking "Big Sound" na marehemu Ilunga Lubaba. Vumbi kwa sasa yuko Sweden akiwa na yule mwanamuziki maarufu toka Uganda Sammy Kasule wakiwa na bendi ya Ba makonde wamekwisha toa album CD mbili- Bamakonde na Asante. Akiwa na bendi ya kaka yake Rachid King Orch Grand’s Mike wametoa album ya CD Bolingo Ekeseni


Monday, February 22, 2010

Historia fupi ya muziki wa dansi

Ukitaka kuongea muziki wa dansi uliingiaje nchini ni muhimu kujua historia ya mji wa Tanga. Tanga ndipo muziki wa dansi ulipoingilia nchini. Wajerumani waliusambaratisha mji wa Tanga kwa mizinga kati mwaka 1888 na 89. Na baada ya hapo kuujenga upya kwa kufuata mpangilio uliosababisha Tanga kuwa na mitaa maarufu kama barabara ya kwanza ya pili na kuendelea. Wajerumani walianzisha shule ya kwanza ya serikali Tanga 1892 na hapohapo wakanzisha bendi ya shule ya kwanza, pamoja na kuwa Wajerumani hawakutawala muda mrefu baada ya hapo lakini Waingereza waliiendeleza sana bendi hiyo iliyokuwa ikipiga aina mbalimbali za muziki wa kigeni. Dansi ilianza kwanza kama klabu ambapo watu walialikana kuja kucheza aina mbalimbali za muziki wa kizungu mtindo maarufu unaojulikana kama ballroom dancing. Aina hizi za klabu zilianzia Mombasa na kuingia nchini kupitia Tanga na kisha kuletwa Dar Es Salaam na klab iliyokuwa maarufu Tanga iliyoitwa Tanga Young Comrades Club, klabu nyingine ilianzishwa ikaitwa New Generation Club ambayo ilianzisha matawi miji mbalimbali. Klabu hizi ndizo zilizozaa bendi za dansi. Inaonekana Dar Es Salaam ndio ilikuwa ya kwanza kuwa na bendi yake African Association Jazz Band, ambapo wanamuziki wengine waliihama na kuanzisha Dar Es Salaam Jazz Band, hiki kilikuwa kipindi kati ya miaka 1930 na 1940, kwenye 1950 kulikuwa na bendi maarufu Bagamoyo iliyoitwa Lucky Star jazz band ambayo ilikuwa na urafiki na Dar Jazz. Baada ya hapo kulianza bendi ambazo wanamuziki na wanachama wake walipatikana kutokana na wanakotoka, kulikuweko na Ulanga Jazz band ya Wapogolo, Rufiji Jazz Band iliyoanzishwa na Wandengeleko, Western Jazz iliyoanzishwa kwanza na Wanyamwezi. Bendi zote hizi baadae zilikuja kuwa na wanachama mchanganyiko bila kujali uzawa. Na kulikuweko na Skokian Jazz Band hii ilikuwa ni bendi na klabu ya watu mchanganyiko. Mwaka 1958 wanamuziki kutoka Kilwa walianzisha Kilwa Jazz Band wanamuziki hawa walitoka bendi iliyoitwa Tanganyika Jazz. Ilipofika 1966 bendi ilikuwa na wanamuziki takribani 26, 15 wakiwa Kilwa A na 11 Kilwa B. Zamani bendi zilikuwa na mtindo wa kuwa na bendi B ambayo ni ya Vijana. Patrick Balisdya aliwahi kuwa Dar Jazz B. Kilwa Jazz ilikuwa na wanachama kama 50 wengine wakiwa viongozi wa juu serikalini. Waliolipa ada ya uanachama na hivyo kuweza kuingia madansi ya bendi bila kulipa. Wakati huo makao makuu ya Kilwa Jazz yalikuwa katika ukumbi ambao kwa sasa unaitwa Kwa Madobi maeneo yaa Jangwani…itaendelea.

Friday, February 19, 2010

Jerry Nashon aka Dudumizi


Nimeweza kumpata mtu ambae ndiye aliyemlea Jerry Nashon kimuziki na haya ndo aliyoniambia kuhusu Jerry. Nae si mwingine bali ni Bwana Ruyembe ambae kwa sasa ni kiongozi pale Baraza la Sanaa la Taifa

Jerry alikulia Musoma Mjini kijiji kiitwacho Kigera kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Musoma jirani na shule ya Sekondari Mara. Nilikutana naye mara ya kwanza akiwa Musoma Catholic Mission club ambayo leo ni Mwembeni secondary School akiwa anajifunza kupiga gitaa. Alikuwa ana mazoea ya kwenda kwenye hiyo social club ya kanisa iliyowaunganisha vijana wanamichezo mbalimbali. Nilimchukua katika Bendi yangu niliyokuwa nimeiunda muda huo 1980s ikiitwa Special Baruti Band. Nilimuunganisha na Mpiga rhythm wangu akiitwa Charles Koya ambaye hivi sasa anapiga na Bendi ya Mwanza Hotel (solo guitar), ili amwendeleze na akiwa pia mwana Bendi wetu. Alikuwa mwanafunzi mzuri alikuwa na bidii na akaweza baada ya muda mfupi kupiga programu yetu kubwa! Mimi nilikuwa mtunzi na mwimbaji licha ya kumiliki Bendi hiyo. Tulirekodi naye mara ya kwanza TFC pia RTD na baadaye tulirekodi Kenya katika studios mbalimbali na producers mbalimbali na tumepiga muziki clubs mbalimbali Nairobi ikiwa kama vile Bombax Hotel, Kaka Night Club, Rwadhia Night Club na nje ya Jiji katika mikoa takribani yote ya Kenya kasoro Mombasa na Kisumu! Hapa tulishirikiana na mwanamuziki hodari Joseph Kamaru. Muda huo yeye akipiga gitaa la rythm na Bendi yetu wakisaidiana na Koya. Jerry alivutiwa na uimbaji pia utunzi baada ya kuona nafasi niliyokuwa nayo na umaarufu nilioupata enzi hizo Nairobi. Alijifunza nikampa mwanga na kipaji chake kikajitokeza katika kuimba na utunzi pia!.Hatimaye Jeshi la Magereza Musoma walimchukua kwa nia ya kumleta Dar ajiunge na Bendi yao ya Magereza. Alipitia mafunzo na aliondoka baada ya kuwa na Special Baruti kwa miaka miwili na nusu hivi au mitatu. Muda huo Musoma kulikuwa na Musoma Jazz Band(segese) ambayo mimi na wanamuziki wengi wa Special Baruti tulipigia baadaye tukahama na kuiacha hali mbaya! Ilikuwepo pia Mara Jazz Band(Sensera) hizi ndizo zilikuwa Band maarufu mjini hapo wakati huo. Aidha ilikuwapo bendi iliyomilikiwa na Parokia ya Catholic Mission Makoko Seminary ikiitwa Juja Jazz Band lakini ilikuwa ndogo sana na haikuwa kwa misingi ya kibiashara zaidi!. jerry Baadae alijiunga na Bima Orchestra na kisha Vijana Jazz mpaka mauti yake.


SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...