YOUTUBE PLAYLIST

Saturday, February 13, 2010

Historia za mfumo wa Bendi

Utaratibu wa bendi hapa nchini ulifuata sana utaratibu wa bendi za nje kutokana na muziki wa bendi kuwa ni wa mapokeo. Hapa naongelea aina ya vyombo vilivyotumika stejini. Katika rekodi za kwanza zaidi za bendi kama vile zile za Cuban Marimba bendi zilipiga bila chombo chochote kilichotumia umeme kwa kuiga staili ya Cuba, na pia teknolojiaa ya vifaa vya umeme ilikuwa bado kuingia. Hivyo kulikuwa na gitaa moja na ngoma za kizungu (drums), bongoz, na vyombo vya kupuliza, filimbi, trumpet, saxaphone. Nyimbo za zamani za Salum Abdallah na Dar es Salaam Jazz Band zinatoa picha za vyombo hivyo. Mwanzoni mwa miaka ya 60, vifaa vya umeme vilianza kutumika na bendi kwa kawaida zilikuwa na Gitaa la bezi, rithim na solo,tarumbeta na saksafon. Halafu kulikuwa na bongoz. Baadae tumba zilichukua nafasi ya bongoz. Baadae bendi ziliingiza gitaa jingine ambalo liliitwa second solo. Hili lilikuwa gitaa ambalo lilipigwa katikati ya rithm na solo. Cuban Marimba katika kipindi fulani cha Mzee Kilaza aliweza kuongeza gitaa jingine waliloliita chord gitaa.
Kuingia kwa vinanda kuliliondoa gitaa la second solo katika bendi, japo kwenye bendi kama Tancut almasi na Vijana Jazz gitaa hilo liliendelea sambamba na kinanda. Kinanda pia kikachukua nafasi ya tarumbeta na saxaphone katika bendi nyingi. Kwa bendi zile ambazo zilikuwa zikifuata muziki wa magharibi mpangilio wao haukuwa na mfumo maalumu kutokana nani aina gani ya muziki wanafuatia. Mpaka sasa bendi kama The Kilimanjaro kwa kawaida hupiga gitaa moja,vinanda vitatu, gitaa la bezi, drums na conga au maarufu tumba. Wakati bendi kama Shada ni wana kinanda magitaa mawili na ngoma ya kiasili. Tatizo kubwa sana sasa ni bendi zinaigana katika mfumo katika kila kitu ubunifu ziro. Franko Makiadi aliondoka kwenye mfumo wa second solo akawa na solo gitaa 2, yeye mwenyewe akipiga solo na akawa na mpiga solo mwingine katika wimbo uleule. Ni wakati sasa wanamuziki kuangalia nyuma na kuona ni nini wanaweza kujifunza kitakachofanya muziki wao uwe tofauti na wa wengine.

Friday, February 12, 2010


Mwaka 1982/83 Tchimanga Kalala Assossa alianzisha na kuongoza bendi iliyoweza kutia changa moto katika ulimwengu wa muziki wakati huo. Bendi hiyo iliitwa Orchestra Mambo Bado na mtindo wake wa Bomoa Tutajenga Kesho. Wanamuziki katika bendi hiyo walikuwa Tchimanga Assossa, Kiongozi na muimbaji, Kazembe wa Kazembe mpiga solo (pamoja na jina hilo alikuwa Msukuma), William Maselenge, rythm guitar, Huluka Uvuruge second solo guitar, Sadi Mnala drums, Mzee Albert Milonge second solo, Lucas Faustin muimbaji, John Kitime muimbaji na rythm guitar, George Mzee muimbaji, Athuman Cholilo muimbaji, Likisi Matola Bass na keyboards, Jenipher Ndesile muimbaji, selemani Nyanga Drums. Album ya kwanza ya bendi hii ilikuwa na nyimbo zilizotamba kama vile Kutokuelewana, Bomoa Tutajenga Kesho , hii ilipigwa marufuku. Picha ya Assossa iliyotoka kwenye tangazo la kwanza la bendi, hapa akiwa amevaa shati la ndege ambalo kwa siku hizo walikuwa wanavaa wajanja tu.

Thursday, February 11, 2010

Hemed Maneti


Hemed Maneti mwanamuziki muimbaji aliyetokea Cuban Marimba na kutua Vijana Jazz mpaka kifo chake. Wimbo wa mwisho aliyorekodi uliitwa Nelson Mandela uliyotungwa na John Kitime. Wimbo huo ulitungwa ili kupigwa radioni wakati Mzee Mandela alipokuwa anatembelea Tanzania mara baada ya kuachiwa toka gerezani. Hakupanda tena jukwaani baada ya kurekodi wimbo huo.

Tuesday, February 9, 2010

Muziki wa soul

Kila zama na vitabu vyake ni msemo unaoeleza kuhusu mambo ambayo hutokea katika kipindi fulani. Kila wakati kuna kizazi kipya, jambo ambalo kila kiza kipya kilichopo hudhani wao ndo wa kwanza. Katika miaka ya sitini kulikuwa na kizazi kipya cha wakati huo na moja ya muziki uliopendwa na kupigwa na vijana wakati huo ni muziki aina ya soul. Vijana walivaa kama wanamuziki wa soul wa wakati huo, walipiga muziki wao na bendi zilijipa majina ya bendi za soul. Ntataja baadhi ya wanamuziki ambao walipendwa na vijana wakati huo, najua kizazi kipya wa enzi hizo watakuwa na mengi ya kusema.

OTIS REDDING alileta raha kwa vibao kama Mr Pitiful, Fa-fa-fa-fa ambao Papa Wemba aliuimba tena miaka michache iliyopita. Sitting on the dock of the Bay, Respect, na wimbo ambao kila bendi ya soul iliupiga Direct Me. Otis alifariki katika ajali ya ndege ya kukodi na wanamuziki wenzake wane wa kundi lake la Barkays


Wilson Pickett alizaliwa March 18 1941, na kufariki kwa ugonjwa wa moyo Alhamisi 19 January 2006 alipendwa na nyimbo zake kama In the Midnight Hour, Don’t Fight It, Ninety-Nine and a Half (Won’t Do), She’s So Good to Me, Land of a 1,000 Dances,
Mustang Sally, na Funky Broadway nakuigwa sana na bendi za vijana wakati ule

James Brown huyu alikuwa ni mzee wao, alipewa majina mbalimbali kama Soul Brother Number One, the Godfather of Soul, the Hardest Working Man in Show Business, Mr. Dynamite, the Original Disco Man. Na mzee huyu ndo alikuwa kinara wa soul music miaka ya sitini, alikuwa mwanzilishi wa funk katika miaka ya 70, na alitoa mchango katika rap music miaka ya themanini. Pia alijua kucheza, Michael Jackson alikiri kuwa ile moonwalk aliipata toka kwa James Brown. JB alikuwa na nyimbo nyingi sana nitaje chache tu, The Popcorn, Mother Popcorn, Papas got a brand new bag, I am black and proud, Sex machine, James alifariki 25 Disemba 2006. Muhimu kutaja kundi lake the Famous Flames aliloanza nalo toka 1955.

Clarence Carter mwimbaji kipofu ambaye aliwakamata vijana kwa nyimbo kama too weak to fight, getting the bills ,slip away, patches

Aretha Franklin- mwanamke wa shoka huyu alipendwa sana kwa nyimbo zake kama respect, save me na think,

Sunday, February 7, 2010

Wanamuziki kutoka Kongo


Huwezi kuongea kuhusu muziki wa bendi Tanzania bila kutaja wanamuziki kutoka Kongo. Kuna sababu kadha wa kadha. Kwanza historia. 1945 kwa sababu za kipropaganda Wamarikani walianzisha kituo cha radio kikubwa katika mji unaoitwa sasa Kinshasa hii iliwezesha muziki wa Wakongo kusikika katika eneo kubwa la Afrika ya kati na mashariki, 1947 ndugu wawili wa Kigiriki walianzisha record company katika mji unaoitwa sasa Kinshasa na santuri za wanamuziki kama Wendo Kolosay na nyimbo kama Akili ya bibi sawasawa mtoto mdogo zilisambazwa chini ya label ya Ngoma na Loningisa na kusambaa sana nchini kwetu, mambo haya mawili yaliweza kuusambaza muziki wa Kikongo katika maeneo yaliyoizunguka na kufanya wanamuziki kuanza kuiga mipigo ya Wakongo. Vita ya wenyewe kwa wenyewe ilianzisha kuhama kwa wanamuziki kutoka Kongo na kuja Afrika Mashariki. Kati ya wanamuziki wa kwanza kuja huku ni Paschal Onema. Lakini baada ya hapo zilikuja Bendi nyingi. Nakumbuka Super Bocca na wimbo wao Suzana mwana Tanzanie, Maquiz du Zaire, Fauvette haya jamani karibu tuendelee .........Pichani ni Mzee Makassy mara tu baada ya kuingia nchini kutoka Uganda

Enzi za Buggy

Katika miaka ya 60 hadi katikati ya 70 kulikuwa na bendi nyingi za vijana ambazo unaweza kulinganisha na wanamuziki wa sasa wanaojulikana kama kizazi kipya. Katika jiji la Dar es Salaam, kulikuweko na bendi nyingi kama vile The Sparks, The Comets, The Flames, The Jets, Crimson Rage, The Lovebugs, Trippers Imagination, Safari Trippers, Afro 70. je unakumbuka nyingine ?

Bendi Zetu

Tanzania tuna bahati mbaya ya kutokuweka kumbukumbu nyingi sana. Kati ya hizo ni kumbukumbu za bendi gani au vikundi gani vya muziki viliwahi kuweko. Labda tusaidiane kila mmoja wetu ajaribu kukumbuka ni kikundi gani kilikuweko wilayani kwake nianzae na mifano michache
******
Iringa-
Highland Stars
Tancut Almasi Orchestra
Chikwala chikwala
Ruaha International
Vico Stars
Mkwawa Orchestra
******

Morogoro
La Paloma Jazz
Cuban Marimba
Morogoro Jazz
Les Cubano
Vina vina Orchestra
******

Ifakara
Sukari Jazz
Kilombelo Jazz
Malinyi Jazz
Kwiro Jazz
Mahenge Jazz
******

Tanga
New Star Jazz
Jamuhuri Jazz
Atomic Jazz
Tanga International
Amboni Jazz
******

Tabora
Tabora Jazz
Nyanyembe Jazz
Kiko Kids haya tuendelee
******

Mwanza
Orchestra Super Veya
******

Moshi
Orchestra Zaire Success
Bana Africa Kituli
********

Mpwapwa
Mpwapwa Jazz
******

Dodoma Jazz
Dodoma International
Materu Stars
Saki Band
Super Melody
*****

Songea
Tembo Jazz
Orchestra Sere sere
******

Lindi
Mitonga Jazz
******

Masasi
Kochoko Jazz

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...