YOUTUBE PLAYLIST

Thursday, February 4, 2010


Kati ya mwanamuziki Mtanzania ambae historia hajamtendewa haki kutokana na kutothaminiwa kwa kazi zake ni marehemu Mzee Frank Humprik. Mzee Humprik anaeonekana hapa katika picha ya rangi ameishi kwa miaka mingi ya mwisho wa maisha yake Lushoto. Mzee huyu akiwa na dada zake wawili walitikisa anga za muziki wa Afrika ya Mashariki, na bado wanaendelea kufanya hivyo japo hawatambuliwi kabisa. Kundi lao lililoitwa Frank na dada zake waliuletea ulimwengu nyimbo kama Embe dodo imelala mchangani, Kolokolola, Chaupele Mpenzi na nyingine nyingi ambazo bendi bado zinapiga nyimbo hizo mpaka leo na baadhi ya wanamuziki wamekuwa wanazirekodi bila hata kutaja mtunzi wa nyimbo hizo. Mbaya zaidi mara nyingi nyimbo hizo zimekuwa zikitambulishwa kama nyimbo za mwanamuziki mwingine kutoka Kenya marehemu Fundi Konde.
Mzee Fundi Konde ambae hapa chini yuko na mwanamuziki mwingine maarufu wa Kenya Fadhili William aliyeimba Malaika, ndiye aliyetuachia nyimbo kama Ajali haikingi, Mama Leli, Wekundu si hoja, Mombasa siendi tena na kadhalika

Mzee Frank Humprick


Kati ya mwanamuziki ambae hajatendewa haki kutokana na kutothaminiwa kwa kazi zake ni marehemu Mzee Frank Humprick. Mzee huyu akiwa na dada zake walitunga nyimbo nyingi sana ambazo mpaka leo zinapigwa majukwaani na karibu kila bendi Afrika mashariki. Bendi nyingine zimediriki kurekodi upya nyimbo hizo tena bila hata kumtaarifu Mzee huyu au nduguze. Baya zaidi ni nyimbo zake nyingi kutambulishwa kuwa ni za Fundi Konde. Nyimbo zake kama Embe dodo imelala mchangani, Chaupele mpenzi,I am a democrat(uliopigwa marufuku wakati wa mkoloni),Kolokolola na nyingine nyingi. Mzee huyu Mtanzania aliyekuwa akiishi Lushoto mpaka kifo chake anastahili kuenziwa na wapenzi wote wa muziki Tanzania.

John Mwenda Bosco,ni kati ya wanamuziki ambao w alileta mabadiliko mengi katika muziki wa Afrika ya Mashariki. Muziki wake unapendwa sana mpaka leo. Je unajua alikuwa nani?

Peter Colmore ambaye alifanya kazi kwa karibu sana na Mzee Ally Sykes ambaye kwa bahati mbaya hajatunukiwa nafasi anayostahili katika historia ya muziki wa Tanzania ndie aliye mleta John Mwenda Bosco Afrika ya Mashariki. Bosco alitambulishwa kwa Colmore kupitia Edward Masengo,mwanamuziki mwingine toka Kongo ambae alikuwa maarufu sana na hasa kutokana na matangazo ya biashara yaliyokuwa yanafanywa na kampuni ya Colmore na Mzee Sykes, Colmore akalazimika kumfuata Bosco hadi Congo ambapo serikali ya Kibergiji wakati huo ilimlazimisha alipe Faranga 30,000 kama pesa ya kuhakikisha atamrudisha Bosco kwao. Bosco alikuwa tayari anajulikana sana Afrika ya Mashariki kupitia santuri zake. Kati ya nyimbo maarufu za Bosco ni ule wimbo wa ala tupu ambao hutumika na Radio Tanzania kuashiria kuanza kwa kipindi cha zilipendwa.

Taarab
Muziki wa Taarab unautata wa vyanzo viwili. Kuna wanaosema taarab iliingia nchini mwetu kupitia ikitokea Mombasa. Kuna tafiti nyingine ambazo zinaonyesha Sultan Barghash wa Zanzibar aliwapeleka wanamuzikiwawili Misri kujifunza upigaji wa Taarab,na hao waliporudi ndo walipanda mbegu ya Taarab nchini mwetu. Taarab imekuwa nahistoria ambayo ya kuwa na aina nyingi za taarab, na mpaka leo mabadiliko ya taarab yanaendelea. Imefikia sasa kuna hata vikundi vya taarab vina wacheza show. Taarab imekuwa pia ni ya kucheza na si kusikiliza ujumbe tu kama ilivyokuwa zamani

Wednesday, February 3, 2010

Extra Bongo ya Ally Choky kazini







Vijana Jazz Band wakisubiri kupiga muziki katika siku ya kumpokea Mzee Nelson Mandela mara baada ya kuachiwa kifungoni, hapa wakiwa stadium Morogoro. Toka kushoto waliosimama John Kitime kwa sasa yupo Kilimanjaro Band, Marehemu Agrey Ndumbalo, Mhasibu wa Bendi, Abou Semhando yupo African Stars (Twanga Pepeta),Marehemu Fred Benjamin, Said Mnyupe yuko Msondo,Said Mohamed Ndula, Rashid Pembe anendelea na muziki Mak Band, Hassan Show yupo Malasyia na Kinguti System wakipiga muziki huko. Waliokaa mpenzi wa bendi, marehemu Bakari Semhando, Juma Choka yupo sikinde.

Picha ya chini, Mohammed Gotagota, Freddy Benjamin,Mhando,Said Mohamed 'Ndula',Rashid Pembe,Aggrey Ndumbalo, hiyo ndo Vijana Jazz Saga Rhumba


Tancut Almasi Orchestra, bendi iliyokuwa namakazi yake Iringa kuanzia 1987, ilikuwa chini ya Kiwanda cha kuchonga almasi cha hapo Iringa, Diamond Cutting Company. Bahati mbaya wengi ni marehemu. Kutoka kushoto Buhero Bakari inasemekana ni mganga wa dawa za asili kwa sasa,marehemu Kyanga Songa, Kasaloo Kyanga yupo Dar anaendelea na muziki,Kabeya Badu, yuko na King Kiki na wazee sugu, Marehemu Kalala Mbwebwe, Abdul Mngatwa, yuko Iringa ameacha muziki, Akuliake Salehe aka King Maluu yupo Dar anaendelea na muziki

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...