YOUTUBE PLAYLIST

Friday, June 2, 2017

MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA ANAUMWA ANAHITAJI MSAADA WA HARAKA WA KUSAFIRISHWA KUTOKA NDANDA HOSPITAL KUJA MUHIMBILI


MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA MTUNZI WA WIMBO MAARUFU WA KILA MUNU AVE NA KWAO, AMEUGUA GHAFLA AKIWA KATIKA ZIARA YA MUZIKI MIKOA YA KUSINI. ANATAKIWA KURUDISHWA DAR ES SALAAM MAPEMA APATE MATIBABU YA HARAKA MUHIMBILI. KWA SASA AMELAZWA KATIKA HOSPITALI YA NDANDA. ANAE ONA AMEGUSWA NA ANAWEZA KUTOA USAFIRI AU MSAADA WOWOTE  APIGE SIMU 0713644439 ILI KUWASILIANA NA KATIBU MTENDAJI WA BARAZA LA SANAA LA TAIFA.

NI MIAKA 27 TOKA KIFO CHA HEMEDI MANETI ULAYA

Picha niliyoipiga tukiwa chumba cha maiti Muhimbili, mbele yetu ulikuwa mwili wa Hemedi Maneti. Kati ya waliopo kwenye picha ni marehemu Mzee jacob John, mwenye shati jeusi na marehemu Salum Faya mwenye jaketi jekundu
Mara ya kwanza kukutana uso kwa uso na Hemedi Maneti ilikuwa ni wakati Vijana Jazz band ilipita Iringa  ikielekea Songea mwaka 1989. Wakti huo nilikuwa mwanamuziki wa Tancut Almasi Orchestra, na kama ilivyokuwa ada miaka ile, bendi ikipita katika mji ambao kuna bendi wanamuziki walikuwa wakipiga muziki pamoja. Tuliongea nae machache lakini aliongea kuhusu kufurahishwa na setting ya vyombo vyetu, alisema inafanya vyombo vyote visikike. Wakati huo hatukujua lakini kumbe alikuwa kishaongea na Shaaban Wanted, Mohamed Gotagota na Mohamed Shaweji ili wajiunge na Vijana Jazz band, na hakika walihamia bendi hiyo wiki chache zilizofuata.
Katika mlolongo huohuo nilijikuta nikiitwa kujiunga na Vijana Jazz Band mwezi wa September mwaka huohuo na kufikia Oktober 1989 niliwasili Dar es Salaam kujiunga na Vijana Jazz Band. Siku ya kwanza nilipofika Vijana maneti alinipa shilingi 300 za kuanza maisha. Nitafute guest house ya kuishi na chakula kwa wiki moja. Hiyo ndiyo kumbukumbu yangu ya kwanza ya Maneti ambaye miezi michache baadae, tarehe 31 May 1990 siku ya Alhamisi majira ya saa kumi na moja jioni, Hemed Maneti alifariki katika hospitali ya Mwananyamala.  Alikuwa ameanza kuwa na matatizo ya afya miezi kadhaa kabla ya hapo na  hatimae kupelekwa Tanga kwa ajili ya matibabu. Hali yake ilipozidi kuwa mbaya alirudishwa kwa ndege  kuwasili Dar Jumatano 30 May na kupelekwa moja kwa moja hospitali ya Mwananyamala ambapo alilala na kufariki kesho yake. Marehemu alisafirishwa kwenda kuzikwa Tanga siku moja baadae.
Wimbo wa mwisho kurekodi ulikuwa wimbo Nelson Mandela uliotungwa nami, ukiwa wimbo uliokuwa matayarisho ya ziara ya Nelson Mandela.

Sunday, April 2, 2017

TUMETIMIZA MIAKA 11 TOKA KUONDOKEWA NA TX MOSHI WILLIAM


Mazoezini katika ukumbi wa Amana katika uhai wake
Moshi William alizaliwa mwaka 1958 hale Mwakinyumbi Korogwe. Pale palikuwa na Mzee mwanamuziki maarufu aliyekuwa akiitwa Mzee Masongi na bendi yake ilikuwa chnzo cha wanamuziki wengi maarufu akiwemo Moshi William. Jina halisi la Moshi William lilikuwa Shaaban Ally Mhoja lakini alikuja kubadili na kuitwa Moshi William kutokana na kuja kulelewa na baba mwingine. Alipewa kisifa cha TX, na Julius Nyaisanga.

Moshi alifariki siku ya tarehe 29 March 2006 katika wodi ya Sewa Haji baada ya operesheni ya kuondoa chuma katika mguu wake uliovunjika kwenye ajali. Alifariki saa tatu kasoro robo asubuhi na kuzikwa siku hiyohiyo katika makaburi ya Keko Machungwa. Moshi lipitia bendi kadhaa baada ya kutoka Hale zikiwemo UDA Jazz, Safari Trippers, Polisi Jazz na hatimae kutua JUWATA 1982. Ambapo aliweza kutuacha na album 13. Na pia alishinda tuzo la mtunzi bora kuanzia mwaka 2003 hadi 2005.
Kaburi la Moshi William

Mungu amlaze pema Shaaban Ally Manongi, TX Moshi William

Sunday, February 23, 2014

MAPENDEKEZO YA WASANII KATIKA RASIMU YA KATIBA MPYA.



 Utangulizi
Baada ya maagizo kutoka Tume ya Katiba ya kuwa kila kundi kutayarisha mapendekezo ya rasimu ya Katiba, wasanii nao chini ya mashirikisho yao manne Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Muziki, Shirikisho la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za ufundi  waliweza kuja na mapendekezo kadhaa ambayo waliyawasilisha katika Tume, kwa bahati mbaya hakuna kipengele chochote cha mapendekezo hayo kilicho ingizwa katika Rasimu ya Katiba. Kwa ushirikiano, Mashirikisho haya ya sanaa yameamua kufikisha mapendekezo yao moja kwa moja kwa Wabunge wa Bunge la Katiba ili kuwezesha vipengele hivyo kuweko katika Katiba yetu mpya.
 Mapendekezo
1.    Kutambuliwa kwa wasanii kama kundi maalumu katika Katiba.
Katika Rasimu ya Katika kuna makundi maalumu kadhaa ambayo yametajwa, kama vile wakulima, wavuvi, wafugaji, na kadhalika  na hivyo kutambuliwa kikatiba. Wasanii ni kundi kubwa katika jamii ya Kitanzania. Wasanii wapo karibu katika kila kaya Tanzania. Wafinyanzi, wasusi, wapambaji, wanamuziki waigizaji, mafundi mbalimbali wa ushonaji ujenzi na kadhalika, wako wengi wala hata wao hawajitambui kama ni wasnii kutokana na mazingira waliyomo. Katika ripoti mojawapo ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati huo ilikuwa ni milioni 6, ni wazi kuwa idadi hiyo kwa sasa itakuwa imepanda.  Katika miaka ya karibuni vijana wengi wamekuwa wanaongezeka kujiunga na kundi hili kwani katika sanaa kumekuwa na uwezekano wa kujipatia ajira, tena isiyokuwa na ukomo. Na hivyo sanaa kwa sasa si utamaduni peke yake bali ni sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania. Wasanii ni sehemu muhimu katika sekta ya Hakimiliki, takwimu za ripoti ya WIPO(World Intellectual Property Organisation) ya mwaka 2010, kuhusu mchango wa sekta ya hakimiliki katika uchumi wa Tanzania, inaonaonyesha  kuwa sekta hii, kati ya 2007-2010 ilichangia kati ya asilimia 3-4.6% ya gross domestic product(GDP). Na kiasi cha kati ya TSH 38.930 bilioni na 86.686 billion kilipatikana kama kipato cha walioajiriwa katika sekta hiyo. Kati ya watu 28, 202 na 44, 331 waliajiriwa rasmi, na hiyo ilikuwa kati ya asilimia 4.5 na 5.2% ya kundi zima la waajiriwa wa Taifa hili. Kwa kipimo cha GDP, sekta hii ilikuwa zaidi ya sekta ya madini, ambayo wote ni mashahidi imekuwa katika mazungumzo kila kona ya nchi. Na katika ajira sekta hii ilikuwa juu zaidi ya sekta nyingi zikiwemo madini, usafirishaji, mawasiliano, afya na ustawi wa jamii, maji, gesi, na hata ujenzi. Kwa mchango wa sekta hii wa 3.2% katika GDP kwa mwaka 2009 , umeweka sekta hii kuwa bora kuliko sekta za aina yake katika nchi  kama Croatia 3%, Singapore 2.9%, Latvia 2.9%, Lebanon 2.5%, Kenya 2.3%. Na katika mchango wa ajira sekta hii ilikuwa juu ya Romania, Bulgaria, Lebanon, Jamaica, Colombia, Kenya na Ukraine. Takwimu hizi hazijionyeshi katika takwimu za serikali kwa kuwa sanaa bado inaonekana ni utamaduni tu, na thamani yake katika uchumi haitiliwi uzito. Kutambuliwa kwa kundi hili kutawezesha kutungwa sheria na taratibu za kuwezesha Wasanii kuongeza ajira na mapato, na Taifa kufaidika na uchumi wa  raslimali hii.
2.     Kutajwa kwa  MilikiBunifu Intellectual Property ) katika Katiba.
Mali ziko za aina 3. Kuna mali zinazohamishika, mali zisizohamishika na mali zitokanazo na ubunifu. Aina mbili za kwanza zimetajwa katika katiba na ulinzi wake hujulikana na ni wa jadi. Lakini hii aina ya tatu ya mali huwa ni ngumu kuilinda kutokana na mfumo wake kuwa haushikiki hivyo sheria maalumu hutungwa kulinda aina hii ya mali (IP Laws). Mali zitokanazo na ubunifu kwa sasa ndio mali zenye kipa umbele duniani. Uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali, ugunduzi wa njia mbalimbali za kuboresha maisha, sanaa na mengi yanayolindwa na milikibunifu, vimeweza kutoa ajira kubwa na kutoa mchango mkubwa wa kipato kwa wagunduzi na nchi ambazo wagunduzi hao wamekuwa wakiishi au kuzisajili kazi zao. Kama wasanii, haki zetu katika milikibunifu zinajulikana kama Hakimiliki, lakini kama Watanzania tunaona ni muhimu kulinda haki zote za Milikibunifu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nchi zote ambazo zimeweka taratibu imara za kulinda Milikibunifu duniani, zimewezesha wabunifu wake kubuni mambo ambayo yameweza kubadilisha maisha ya binadamu wengine duniani kote. Marikani iliweka kipengele cha Ulinzi wa hakimiliki katika katiba yake tangu mwaka  Agosti 1787, na kazi za wagunduzi wa Marekani tunaziona kila wakati katika kazi za sanaa na teknolojia. Korea kusini ilinakiri sehemu ya katiba ya Marekani kuhusu ulinzi wa Milikibunifu kuanzia mwaka 1948, kwa wakati huu wote ni mashahidi wa bidhaa kama Samsung, Ld Daewoo, Hyundai na kadhalika.
Milikibunifu pamoja na kulinda haki katika kazi za sanaa ambazo picha ndogo ya mapato yake zimetajwa hapo juu, Milikibunifu italinda haki za wabunifu wetu, tafiti za wasomi wetu, ugunduzi mbalimbali, taratibu mbalimbali za mambo yetu ya kiasili, dawa za asili za miti yetu, na taratibu za matumizi ya dawa hizo, na mali asili zetu nyingine nyingi tunazozifahamu na ambazo bado hatujazifahamu .
Kuna hasara nyingi ambazo hupatikana kama nchi haina ulinzi wa Milikibunifu, mifano michache hapa Tanzania, ni kupoteza kwa Milikibunifu ya jina Tanzanite, ambayo licha ya kuwa inachimbwa Tanzania tu lakini jina linamilikiwa na kampuni ya Afrika ya Kusini. Vazi la kikoi, pamoja kuwa ni la asili ya Tanzania, milikibunifu imesajiliwa Kenya, staili ya michoro maarufu ya Tingatinga milikibunifu yake iko Japan. Na haya ni machache ambayo yameshitukiwa Milikibunifu ikifuatiwa vizuri ndipo haswa ukubwa wa tatizo utakapojulikana. Kuna ulazima mkubwa wa kutaja Milikibunifu katika katiba na kuanisha ulazima wa kulinda kuendeleza na kwezesha wabunifu wan chi kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo








Wednesday, March 6, 2013

KABEYA BADU HATUNAE TENA

MWANAMUZIKI WA SIKU NYINGI AMBAYE ALIKUWA ANAIMBA KATIKA BENDI YA WAZEE SUGU- KABEYA BADU -AMEFARIKI LEO ASUBUHI KATIKA HOSPITALI YA MUHIMBILI BAADA YAKUPATA MATATIZO YA FIGO KUSHINDWA KUFANYA KAZI. KABEYA ALIPITIA BENDI NYINGI IKIWEMO, ORCHESTRA FAUVETTE, ORCHESTRA SAFARI SOUND, MAQUIS, INTIMATE RHUMBA, TANCUT ALMASI, NA WAZEE SUGU
MSIBA UTAKUWA KWAKE TANDIKA MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI

Friday, February 18, 2011

Super Kamanyola ya Mwanza


Beno Villa Anthony

Beno

Mukumbule Parash

Super Kamanyola


Ally Yahaya na Roy Mukuna

Beno na Parash



Anna Mwaole

John Hamisi




Mwaka 2006,wanamauziki kadhaa wa zamani walijikusanya na kuanzisha bendi ambayo ilijulikana kama Tanza Muzika, bendi hii ilikuwa na wanamuziki kama akina Kasongo Mpinda Clayton, Issa Nundu, Mukumbule Parashi na wengine wengi wazuri. Pamoja na kuwa bendi nzuri walikosa vyombo na hivyo kuwa chini ya himaya ya jamaa walioweza kuwa na vyombo, ambao nao mwaka 2007 wakajitoa na hivyo kundi hilo kuvunjika. Wanamuziki wachache wakahamia Mwanza na kuungana na  kundi la Mwanza Carnival, hao walikuwa Roy Mukuna, Seseme Omary,Mukumbula Parashi,Issa Nundu, Bonny Chande . Miezi michache baada ya kuanza kwa kundi hili mfadhili wa kikundi akaanza kuugua na hivyo kundi hilo kusambaratika tena.. Wanamuziki wakaamua kurudi Dar Es Salaam na huko Ally Yahaya, ambaye ni mpiga trumpet nae akajiunga nao na wakajipa jina jipya Super Kamanyola. Na ni wakati huu wakaalikwa kwenye bonanza la Villa Park Mwanza, si muda mrefu baada ya hapo uongozi wa Mwanza Villa Park ukaingia katika makubaliano ya  kuifanya Super Kamanyola kuwa resident Band. May 2010 bendi ikahamia rasmi Mwanza. Kundi hili lina wanamuziki wafuatao.Roy Mukuna, Saxophonist na Kiongozi wa Bendi, Ally Yahaya Trumpetist Katibu wa bendi, Seseme Omary Solo guitar na uimbaji, Beno Villa Anthony mwimbaji na mpiga Keyboards, na pia mshauri wa bendi, Mukumbule Parashi muimbaji, Rashid Mwezigo mwimbaji, Anna Mwaole muimbaji, Bonny Chande Bass guitar, John Hamisi rhythm guitar, na Duncan Matembe Drums. Kwa kweli ni burudani kuisikiliza bendi hii ambayo ikiwa inapiga nyimbo za zamani za Maquis, OSS, Tancut Almasi, TP OK Jazz, African Fiesta, utadhani unazisikia bendi zenyewe.



SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...