Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Wednesday, September 8, 2010

Kuanzishwa kwa Mlimani Park Orchestra

Sababu ya Mlimani Park kuzaliwa ikiwa imeundwa na kundi kubwa la wanamuziki kutoka Dar International ilitokea kwa bahati sana. Kwa maelezo ya mwanamuziki aliyekuwepo wakati huo, hadithi nzima ilitokana na bendi ya Dar International kukodishwa na Chuo Cha Ardhi katika sherehe yao ya kuwaaga wanachuo wazamani na kukaribisha wapya. Chuo cha Ardhi kilikodi ukumbi wa Mlimani Park kwa ajili ya shughuli hiyo. Wakati huohuo utawala wa Mlimani Park ulikuwa mbioni kutengeneza bendi baada ya kumalizika mkataba wa Orchestra Fukafuka katika ukumbi huo. Tchimanga Assossa ambaye alikuwa amekuja na Bendi ya Fukafuka alibaki nchini na alikuwa katika hatua za mwisho za kwenda kufuata wanamuziki wengine kutoka Kongo kwa ajili ya ukumbi huo. Hivyo basi Dar International wakati huo ndio wakivuma na nyimbo kama Magreti walianza kuporomosha muziki chini ya kiongozi wao Abel Balthazal. Uongozi wa Mlimani Park ulipigwa butwaa na muziki wa hawa jamaa, Abel aliitwa pembeni na kuulizwa bendi iko chini ya mkataba wa nani? Na je, wanamuziki wangeweza kukubali kuajiriwa na na Mlimani Park wakati huo ikiendeshwa na TTTS? Kwa vile Dar International ilikuwa ya mtu binafsi na hawakuwa na ajira yoyote ya kudumu katika bendi hiyo, haraka sana wanamuziki walikubali wazo hilo. Kesho yake viongozi wa Dar International walienda kukutana na viongozi wa ukumbi wa Mlimani Park, na wakakubaliana kuazisha kambi ya bendi mpya palepale katika ukumbi wa Mlimani. Haikuwa taabu maana vyombo vilivyonunuliwa wakati wa mkataba wa Orchestra Fukafuka vilikuwa mali ya Mlimani Park kwa hiyo bendi ilianza kwa Abel kusisitiza kupata wanamuziki kama Muhidin Gurumo,ikumbukwe kuwa ni huyu Abel ndiye aliyeisuka Dar International baada ya kuwachukua wanamuziki wote wa Safari Trippers kundi zima wakati huo, Kassim mponda, Joseph Bernard, Marijan Rajabu, Ben Peti, Zito Mbunda,Bito Elias na wengine kasoro Christian Kazinduki na kutoka Tanzania Stars ya Maggot walitoka Joseph Mulenga, George Kessy , Haruna Lwali na wengineo. Na kwa staili hiyohiyo skwadi nzima ya Dar International ikageuka kuwa Mlimani Park. Muda mfupi kabla la hili ugomvi mkubwa ulikuwa umetokea Dar International kati ya Marijani Rajabu na Abel Balthazar katika ubishi kuhusu tungo aliyoleta Marijani ambayo Balthazar alidai kuwa ni ya Tabu Ley kwa hiyo akatunge tena, jambo lililoleta kushikana mashati, na kusababisha Marijani kusimamishwa kazi. Wakati yuko benchi ndipo mpango mzima wa kuhamia Mlimani ulifanyika hivyo mwenye vyombo alilazimika kumfwata tena Marijani na kumwomba aunde bendi upya, na ndipo Super Bomboka ikaundwa.

Mlimani Park ikaanza ikiwa na Tchimanga Assossa ambaye safari ya kwenda kutafuta wanamuziki Kongo ikawa imekwisha. Na mchango wa kudumu wa Assossa wakati huo ni utunzi wa ule wimbo Gama.

37 comments:

Anonymous said...

kwa mara nyingine tena John mwakitime AKA mzee nyongise kwa sisi wa zamani wachache tunakutambua hivyo , umeweza kukonga nyoyo za wasomaji wa blog hii. Nimefurahi sana kuipata kwa undani story nzima ya mlimani park. Nimemkumbuka marehemu Haruna Luwali na tungo yake ya " mama naomba ruhusa leo wiki endieee" sidhani kama alipata kufaidika na utunzi wake japo mkono wake katika tumba unasikika vizuri sana. Kadhalika utunzi wa assosa wa Gama wimbo ambao mpaka leo sidhani kama hata hawo waliobakia mlimani wana ubavu wa kulirudia solo la introduction na madoido yake kama ilivyo kuwa. Sina hakika kama Geoge Kessy Omondi yuko wapo na kama yupo hai na anafanya mamabo ya miziki?
Ulikuwa ni wakati wa kupendeza na wakukumbukwa sana sana . Sijui wewe ulikuwa wapi nyakati hizo na ulikuwa unajishughulisha na nini?

Anonymous said...

Nikiwa kama mpenzi wa sikinde nimefurahi sana kupata habari hii ya mwanzo wa Mlimani Park, kwa sababu habari nilizosikia mimi ni kwamba sikinde walichota wanamuziki kutoka msondo na ndipo bifu kali zilipoanza baina ya hizi bendi mbili,na hatimaye mashabiki wa msondo walidiriki hata kuwavizia sikinde katika show yao moja na kuwamwagia choo (MAVI).Msondo katika miaka ya nyuma ilikuwa na ubabe kutoka mashabiki mpaka uongozi. Kuna wakati inasemekana walimfukuza Shaaban Dede na kumvua sare zao hadharani, na ndio ukawa chanzo cha wimbo wa talaka rejea punde alipohamia sikinde na msondo kumuomba arudi na kujiunga nao tena lakini alikataa katakata. Bado tunasubiri story nyingi kutoka good old days. Big up Kitime.

Webmaster Kalley A.P said...

Kaka john kitime, naomba kujua jina la mwanamuziki aliyekuwa akiimba wimbo wa Gama katika squad ya sikinde.

Anonymous said...

Mzee Kitime, mimi sio mzee ila nakushauri jambo mzee wangu niwie radhi maana kijana kama mimi sina hadhi ya kukushauri. Hivi kwanini usitunge kitabu kutumia hizi data unazomwaga humu mtandaoni? Naamini kama ni costs unaweza kupitisha kikapu humu mtandaoni ukapewa. Pia kama ni utaalamu watu kama sie tunao. Nipo hapa Australia kuna opportunities nyingi za kibunifu kama unataka. Ni wazo tu lakini ungeweza kabisa kutengeneza kitabu ambacho mpaka sasa nadhani ninacho kichwa cha habari au jina lake. "THE RISE AND FALL OF MUSIC IN TANZANIAN" Yaani kwa maneno butu, "Kuibuka na Kuanguka kwa Muziki Tanzania. Hiki kitabu kitakupa utajiri wa kutisha mzee wangu sio siri. Kwa sisi tunaoishi kwenye nchi za magharibi tunajua kuwa takwimu kama izi unazomwaga humu mtandaoni ni dhahabu zinazoweza kukufikisha mbali. Ni hayo tu mzee wangu.

Anonymous said...

Ni historia nzuri ambayo wengi hatukuijua.

Wimbo wa Gama intro yake imepigwa kwa gitaa la rythm, ambalo kama sikosei alipiga Abdalah Gama au Muharami Said. Hali kadhalika sauti inasikika ikiongoza wimbo inafanana na Cosmas Chidumule, kama nimekosea atatusahihisha kaka Kitime.

Hongera tena kwa habari hizi moto mot za muziki wa Tanzania

Kisondella, A.A said...

John mwakitime AKA mzee nyongise napenda nikutanbue kihivyo.

Umenifichua nilikujificha na umenichokoza. Mimi ni kati ya wale wapenzi wa sikinde damu damu. Nashukuru sana kwa historia hiyo ya Sikinde, ni wachache sana wanaojua kuwa muanzilishi hasa wa Mlimani Park (Sikinde) alikuwa Marehemu Abel Barthazar, wengi wanafikiri ni Mjomba Maalim Muhidin Gurumo. Kwa Nyongeza tu ni kwamba Marehemu Abel Barthazar ndiye chachu ya kuhamisha wanamuziki kimbali (niki maanisha kundi kubwa), Kama alivyotuelezea Mzee wa Nyongise alivyoweza kulivuta kundi kubwa Safari Trippers kutengeneza Dar International, hivyo hivyo ndivyo alivyofanya kwa kutoa wanamuziki wengi toka Dar International na kutengeneza Mlimani Park, Na hivyo hivyo kama alivyoweza kutoa ushawishi wa Hugo Kisima (wakati huo Mkurugenzi wa Orchesta Safari Sound), kuchukiua kundi kubwa la wanamuziki wa DDC Mlimani Park (Mwaka 1985) na kusuka upya upya bendi ya Orchestra Safari Sound chini ya mtindo wa Ndekule, Pia ni huyu huyu Abel Barthazar ambaye muda mfupi kabla hayakutana na mauti alisuka vyema bendi ya Magereza Jazz, itakumbukwa kuwa kwa mapenzi aliyokuwa nayo kama muasisi wa Mlimani Park alitoa ushawishi kwa wanamuziki Hassan Kunyata (mwimbaji) na Gervas Herman (solo gita)(Marehemu) wajiunge na DDC Mlimani Park.

Mzee Nyongise tupo pamoja; nilikuongezea listi ya wanamuziki wa Mlimani Park aidha ambao bado wapo Sikinde and waliwahi kupitia Sikinde kwenye post yako ya mwezi wa tatu (link:http://mwakitime.blogspot.com/2010/03/mlimani-park-orchestra.html.

Nafikiria kuandika chochote "kwanini Marehemu Joseph Batholonew Mulenga "King Spoiler" alipewa jukumu la kupiga gita la solo kwa nyimbo nyingi badala ya Marehemu Abel barthazar. Kimsingi wakati Joseph Batholonew Mulenga anajiunga na Mlimani Park alikuwa anapiga gita la bass. Mpaka hapo nitakapo pata wasaa nitapost hii information.

Kisondella ,A.A - From Mafinga (Iringa)

Kisondella, A.A said...

Hi Webmaster Kalley A.P!
Kwa niaba ya Mzee John Kitime, ningependa kukujibu kuwa katika wimbo "Gama" kama ulivyotungwa na Tchimanga Assossa, John Kitime amelielezea vizuri uliimbwa na Cosmas Chidumule mpaka pake Chorus inapoanza Marehemu Hamis Juma 'Maalim Kinyasi' anaungana naye halafu Hamis Juma akiendelea kuimbisha.

Mzee John Kitime nimeona nikusaidie kujibu hili, ili uendelee na majukumu mengine ya kutafuta habari muziki hasa ambao sisi vijana wa zamani ndio hazina yetu

Kisondella, A,A - From Mafinga - Iringa

Kisondella, A.A said...

Hi Webmaster Kalley A.P!
Kwa niaba ya Mzee John Kitime, ningependa kukujibu kuwa katika wimbo "Gama" kama ulivyotungwa na Tchimanga Assossa, John Kitime amelielezea vizuri uliimbwa na Cosmas Chidumule mpaka pake Chorus inapoanza Marehemu Hamis Juma 'Maalim Kinyasi' anaungana naye halafu Hamis Juma akiendelea kuimbisha.

Mzee John Kitime nimeona nikusaidie kujibu hili, ili uendelee na majukumu mengine ya kutafuta habari muziki hasa ambao sisi vijana wa zamani ndio hazina yetu

Kisondella, A,A - From Mafinga - Iringa

Anonymous said...

Kudadeki wallahi...Hii Mzee Mwakitime kwa post hii kama kungekuwa na tuzo ningekutunukia. Kisa hiki cha Mlimani Park kimenisisimua sana na kunipa fikra ndefu sana. Hilo squad la Baltazar, Mponda na Mulenga sijui mtu atasemaje hapo? Mola awalaze pema wazee wetu hao Marijani, Mulenga, Mponda na Abel, mchango wao hautasahaulika daima.

Huku nilipo wanasema "Urakoze Chane Mwakitime"!

Maselepa "Mzee wa Zamani"
Dans Republique Du Burundi

Kisondella, A.A said...

Anonymous 2:37 amenistua sana, anapomwomba mola awalaze pema Marijani, Mulenga, Mponda na Abel; Hivi Mzee Kasim Mponda,alifariki??. Naomba Mzee Kitime thibitisha hilo kabla sijaanza kumuenzi kwa kusikiliza nyimbo ambazo aidha alizitunga au alipiga solo, wakati akiwa na Juwata Jazz Band (Msondo Ngoma) au alipochepuka kidogo na kupiga na DDC Mlimani Park (Sikinde)

Kisondella - From Mafinga (Iringa)

Anonymous said...

Anony wa 15:06. Pamoja na Dede kutunga wimbo wa Talaka Rejea, alirudi Msondo akitokea Bima Lee mwaka 1987, japo hakukaa sana. Nakumbua alirekodi nyimbo kadhaa katika ujio wake wa pili Msondo, lakini sizikumbuki majina.

Anonymous said...

Bwana Kitime, Anony wa 02:37 hapo juu kanistua kidogo. Hivi Kassim Mponda kafariki? Itakuwa ajabu mwanamuziki mahiri kama yeye afariki halafu nisijue. Tafadhali litolee ufafanuzi hili.

Anonymous said...

JK,

Umemtaja Beni Peti, je yuko wapi kwa sasa? na ni kweli ndiye mtunzi wa wimbo wa Margret wa Dar International?

-Muarubaini

Anonymous said...

Kwako Anon 06:28. Moja ya nyimbo Dede alizorekodi katika ujio wake wa pili Msondo ni 'Ajuza'. Nadhani hiyo ilikuwa ni 1986 mwishoni au 1987 mwanzoni.

Anonymous said...

Kwako Anon 06:28. Moja ya nyimbo Dede alizorekodi katika ujio wake wa pili Msondo ni 'Ajuza'. Nadhani hiyo ilikuwa ni 1986 mwishoni au 1987 mwanzoni.

Bana said...

Mdau Kisondella asante sana kwa kutuchimbulia data zingine muhimu umenikuna sana hasa ulipomgusa Mulenga. Nina hamu sana ndugu yangu hebu tudokezee kidogo kwanini Mulenga alipiga badala ya Mponda,ndio tunakumbushana tulipotoka. Halafu mdau 00:00 wa kitabu, hiyo title ingebadilika - afadhali kuita : "Historia ya Muziki wa Dansi Tanzania - Tulikotoka na Tuendako" au kwa kiingereza butu "The history of Music in Tanzania: A Glance on the Past and its Future".

Bana
USA

Kisondella, A.A said...

Naomba samahani kwa Mzee Kitime kuchukua nafasi katina blog yako kumzungumzia kidogo Marehemu Joseph Batholomew Mulenga ("King Spoiler)na uhusani kwanini alipewa Jukumu la soloist one kulinganisha na Marehemu Abel Barthazal.

Kwanza ifahamike kuwa Marehemu Abel alikuwa mmoja ya wapigaji hodari sana wa gita la kuongoza (solo, lakini kilichokuwa kinawaudhi wenzie ni "KUTOJIBIDIISHA" au kwa ufupi alikuwa na kauzembe fulani fulani. Pamoja na kwamba alikuwa muasisi wa Mlimani Park lakini tabia yake ya kuchelewa kufika dansini, kutojizuia hasira pale yanapotokea makosa katika upigaji wa muziki ni baadhi ya mambo ambayo yalimpelekea wenzake kutomuona "serious man".

Hali iliyopelekea Maalim Muhidini Gurumo kupewa uongozi wa bendi huku Abel akiachwa mwanamuziki wa kawaida; Kwa uzoefu wa muziki wa muda mrefu Gurumo akishirikiana na Marehemu Michael Enock "King" (ambaye asili yake hasa ni mzambia, walikutana na kumtumia zaidi Mulenga kupiga gita la solo kuliko bass (ambayo aliachiwa kwa asilmia kubwa likipigwa na Julius Mzeru. Habari za ndani ni kwamba huyu Mulenga alikuwa mpwa wa King Enock, lakini hili halikutakiwa kukuzwa sana kuepuka usumbufu wa kupendelewa na mambo mengine ya kiuamiaji.

Mulenga kimsingi alikuwa kinyume kabisa na Abel, yaani alikuwa mbunifu katika upigaji solo, mwenye kujibidiisha, na pia mtunzi mzuri sana. hali iliyompelekea si tu kupendwa na wanamuziki wenziwe bali kwa asilimia kubwa kupiga nyimbo zote za Sikinde kwa gita la kuongoza yaani "Solo". Hii ilimfanya Mulenga mwenyewe kuachana na gita la bass na kujikita kwenye gita la kwanza yaani solo.

Ubunifu, kujibidihisna na utunzi unajidhihirisha hata pale alipoama sikinde mwaka 1984 na kujiunga na Bendi ya Bima (Bima lee, ambapo alileta mageuzi makubwa katika muziki wa Bima Lee enzi hizo, wakibadilisha bendi na kuita Bima Lee 84 "Magnet Tingisha".

Kutokana kwamba Abel hakuridhika na hatua ya Mulenga kupewa uzito zaidi na pia msuguano wa uongozi kati yake na Gurumo aliamua kuhama bendi na kujiunga na Orchestra Safari Sound ambako pia hakukaa sana kabla ya kuelekea Magereza Jazz Band ambako maisha yake duniani ndipo yalipohitimishwa.

Kwa ufupi ni hitoria fupi ya hawa wanamuziki wawili mahiri kwa upigaji wa gita la solo ambao hatunao tena katika ulimwengu huu lakini mchango wao katika mageuzi na mapinduzi ya muziki wa dansi hayatosalulika.

Mzee Kitime kwa kuwa wewe ni mwanamuziki mkongwe wa dansi na mimi binafsi nakusheshimu sana kwa kujibidihisha si kimuziki tu, hata katika masuala mbali mbali, (umewahi kuwa jaji katika kutathimini vipaji vya uimbaji wa vijana katika kipindi cha Bongo Search), na pia ni mwanamuziki pekee wa Tanzania ambaye ameamua kwenda na wakati na kutumia technologia ya compututer ki-internet katika kuelezea masuala mbali mbali ya muziki wetu wa dansi na mwanamuziki wake); kama kuna lolote ambalo aidha nimeliacha au sikuliweka vyema kuhusiana na wanamuziki hawa wawili basi naomba ongeza ili mdau BANA pamoja na wengine waweze fahamu na kuelimika

Kisondella - from Mafinga (Iringa)

Kitime J said...

Aksante sana kwa mchango wako Kisondella, teknolojia hii inatuwezesha kupata michango toka kila pande ya dunia kwa kweli inaleta faraja, na kutuwezesha kujua mengi. Naomba unitafutie taarifa za Mohamed Sululu, huyu alianzia Kibisa huko Kigoma, akawa Super Melody Dodoma na staili yao ya Zunguluke, akahamia Tancut Almasi na kisha JKT Kimulimuli, ambapo alifanya masikani yake hapo Mafinga, yeye ndo aliyemtoa Kinguti System Kigoma, ana historia nyingi tafadhali kama ukimpata nitaarifu ntafunga safari kuja kumuona rafiki yangu huyo. E mail yangu jkitime@gmail.com. Kuhusu hilo tatizo la Mulenga na Balthazal, pia kuna maelezo mengine toka kwa mwanamuziki aliyekuweko wakati huo. Upigaji wa Balthazal na Mulenga ni tofauti, hivyo wakawa wamegawana nyimbo ili kuondoa monotony katika nyimbo, nitapeleza tena kujua hiyo taarifa uliotupatia.

Kisondella, A.A said...

Mzee Kitime hakuna wasi wasi Mimi mwenyewe nimepiga ile miezi yangu 12 ya mujibu wa sheria, pale JKT Mafinga, na kwa sabau nilikuwa mpenzi sana wa muziki wa dansi nilikuwa nao karibu wale wana muziki, nitachomoka nifike pale Jeshini ili nijue wapi huyu jamaa yupo na nini kinaendelea;

Japokuwa habari za kusikitisha ni kuwa wanamuziki wengi walitangulia mbele ya haki kwa sababu moja ama nyingine, lakini ngoja tuanze na hili la Mohamed Sululu

Kisondella

Anonymous said...

Ningeomba mdau Kisondella uangalie upya hii sera ya Abel,Mulenga na Gurumo, kwa sababu wakati Abel&co. wanaihama Sikinde kwenda Safari Sound,huyu Mulenga alikuwa tayari yuko Bima Lee kitambo, na Abel alihama wakati mmoja na Gurumo kwenda Safari Sound.

Kisondella, A.A said...

Anonymous 12.04 ni kweli usemavyo kipindi ambacho Abel Barthazar alipohama kwenda Orchestra Safari Sound (OSS)walipishana kidogo na Mulenga ambaye pia alikuwa amekwenda Bima Lee.

Ninavyojua ni kwamba mwaka 1984 muda mfupi baada ya Mulenga, Mwanyiro, Gama na Dede kuamia Bima, tayari Abel alikuwa hayupo, ndipo Mlimani walikuwa wanamtumia zaidi Marehemu Michael Bilal na Hennry Mkanyia kwenye solo; huku second Solo akiwepo Marehemu Muharami Saidi "Golden Finger".

Katika kipindi cha miezi Michache ndani ya mwaka 1985 baada ya Abel Barthazar kuondoka, kundi la wanamuziki 7 wa Sikinde (Muhidihi Gurumo, Hassan Bitchuka, Kassim Rashid, Ally Makunguru, Charles John Ngosha, Ally Jamwaka, Beno Villa (japokuwa Beno hakukaa sana alirudi Sikinde. kwa hiyo walimkuta Abel Barthazar tayari akiwa yupo kule OSS, kwa hiyo Abel hakuhama pamoja na akiwa Gurumo.

Pia kumbuka hiko lilikuwa kundi la kwanza kwenda Orchestra Safari Sound ambapo ndani ya muda mfupi sina kumbu kumbu vizuri ilikuwa baada ya mwaka au vipi kundi la pili likiongozwa na Maxillian Bushoke, Fresh Jumbe, Hamis Juma,Cosmas Chidumule waliamia pia OSS; Kitendo ambacho Sikinde walimulaumu sana Hugo Kisima (Mmiliki na Mkurugenzi wa bendi ya OSS wakati huo)kutaka kuiua Sikinde

Kisondella - From Mafinga (Iringa)

Anonymous said...

Asante Kisondella kwa mara nyingine kwa kunisahihisha, kwa sababu kipindi kile kilikuwa ni taabu tupu kwa wanamuziki kuhama kila siku hivyo ni rahisi kusahau kidogo.Lakini Bitchuka alirudi tena DDC na kutoa vile vibao kama kuku na ni nani aliyemdanganya mpenzi wangu, wakati huo huo alifanya kazi pembeni na Juma Ubao katika kundi lililojulikana kama THE SIX MANYARA, wakatoa vibao safi sana, kimojawapo ni TAABU.Dooo jamani haya mambo yananikumbusha mbaali sana,shukran zimwendee Kitime kwa kazi nzuri, nikiwa kama mpenzi wa sikinde najifunza mengi ambayo sikuyafahamu, kwa hiyo wadau tuendelee kupeana habari motomoto,kwani hatupo sehemu moja lakini mtu unaanza kupata zile feeling za kijiweni.

Kisondella, A.A said...

Nashukuru sana anonymous 02:02; Ni kweli Bitchula alirudi baadaye sana. Ni historia ya kusikitisha jinsi Sikinde walivyovurugwa na kuamwa na wanamuziki wengi kwa wakati mmoja. Labda nikipata utulivu ningelipenda kwa ruksa ya Mzee Kitime kuelezea japo kwa ufupi jinsi gani Sikinde walikabiliana na suala hili.

Kumbuka vijembe ya M.V Mapenzi no.2 (Sikinde) dhidi ya Usimchezee Chatu OSS - Ndekule)

Kisondella

Kisondella, A.A said...

Nashukuru sana anonymous 02:02; Ni kweli Bitchula alirudi baadaye sana. Ni historia ya kusikitisha jinsi Sikinde walivyovurugwa na kuamwa na wanamuziki wengi kwa wakati mmoja. Labda nikipata utulivu ningelipenda kwa ruksa ya Mzee Kitime kuelezea japo kwa ufupi jinsi gani Sikinde walikabiliana na suala hili.

Kumbuka vijembe ya M.V Mapenzi no.2 (Sikinde) dhidi ya Usimchezee Chatu OSS - Ndekule)

Kisondella

Anonymous said...

Mdau Kisondella nakushukuru sana kwa ufafanuzi wako mzuri sana. Isingekuwa wote hawa wameshatangulia mbele ya haki ningekuomba unisaidie tena kufahamu nani alikuwa zaidi kwa maana ya tofauti za ufundi wao wa upigaji ili vijana wa leo wajifunze.Kila nisikilizapo solo la Mulenga na la Abel huwa nakosa mshindi. Wenzetu hawa wameondoka na ufundi wao, sijui kwa sasa tunaweza kusema nani kavaa kofia zao.At least Mzee Mabera ndo amebaki. Pangamawe angetulia ni mpigaji mzuri sana tatizo ujana mwingi.

Shukrani sana mzee Mwakitime.

Bana

Anonymous said...

Ndio Kisondella, hizo bifu nazikumbuka ile MV Mapenzi II lilikuwa ni dongo la moja kwa moja kwa OSS,Pia yale madongo ambayo DDC alikuwa akitupiana na Msondo mpaka Marijani Raajab kuingilia kati na kuwasema kwa kibao KAZI YENU WOTE NI WAHUNZI KWA NINI HAMUELEWANI KILA MTU ATIE FITINA KWA MWENZIWE WATU TUNATAKA VITENDO WALA HATUTAKI MIZENGWE MIZENGWEEEE.Namuomba Kitime akupe ruksa tu,sio mbaya kuelimishana fani ambayo ni moja ya mfumo wa maisha ya binadamu.

Kisondella, A.A said...

Anoynymous 11:18 Shukurani, wakati mwingine madongo yalisaidia sana kukuza muziki nasisitiza "wakati mwingine". Wanamuziki walikaa chini na kuumiza vichwa vyao kuhakikisha wanafanya kazi bora zaidi kuliko wenzao; Unapozungumuzia Msondo na Sikinde nafikiri vijembe vile havitakuja tokea tena katika ulimwengu wa muziki wa dansi, (it was toooo much,ilikuwa katika kila album (au mkupua wa muziki lazima kuwe na wimbo mmoja ambalo ni kombora kwa bendi hasimu.

Japokuwa madongo pia yalianza mbali, Kilwa Jazz, ??,??. (Nafikiri Mzee Kitime anaweza kuwa na kumbukumbu nzuri zaidi)

Tukumbuke pia kuwa si Msondo na Sikinde bali angalia Maquiz (ogelea piga mbizi) na Orchestra Safari Sound (Chunisi)

Anonymous said...

Hiyo ni kweli kabisa, bila kusahau bendi za mji kasoro bahari nazo zilikuwa na bifu zao.....

Anonymous said...

JK,Bado naililia blog ya njenje. Je yaweza kuwa tayari lini?

Anonymous said...

Mdau 01:19, umegusia mji kasoro bahari, vile vitisho vya Mbaraka vya Jogoo la Shamba hawiki mjini sijui alilengwa nani, mnaweza kunisaidia nina hamu na hucheka kila nisikilizapo..."ungepigana nami aibu ingekukuta...kipigo ungekipata..." Mbaraka alipiga mkwara sana hapa na Sululu lake!

Anonymous said...

JK,

Sina ufahamu wa muziki kabisa, lakini hivi kuna kundi lolote hapa Tanzania lililofikia kiwango cha DDC mlimani park? naona kama bendi hii ilikuwa highest point ya muziki.

-Muarubaini

kitime said...

Muarubaini unasema hivyo kwa kigezo gani?

Anonymous said...

Mlimani ilifikia highest peak nyimbo zile za Kata ya Maji ukweni, Siwalaumu Enyi wakwe nk ilikuwa hatari sana hii bendi...huku Bushoke...huku Cosmas...balaa tupu!

Anonymous said...

Hi JK,

Sina ufahamu sana wa muziki, lakini kila ninaposikiliza nyimbo kama Barua kwa mama, Celina, Gama, Pesa, Taxi driver, Linda,Mfaume, Nawasukuru wazazi, Fikirini, Mume wangu Jerry, Christina Bundala n.k.

Nashawishika kusema hapa Tanzania ilikuwa katika kiwango cha juu sana kimuziki..je kwa upeo wako kuna kundi lingine lililowahi kupiga muziki wa nyumbani kufikia katika kiwango hiki?

-Muarubaini

Anonymous said...

Mdau 02:490 na Muarobaini mmenikuna sana kukumbushia hizo nyimbo za Nginde. Mimi nilikua mpenzi wa Maquis lakini Nginde ya kipindi cha Bushoke, Bitchuka na Cosmas ilikuwa balaa sana.Sijui mpiga solo lile alikuwa nani katika nyimbo za Clara,Siwalaumu Enyi Wakwe,Kata ya Maji na Christina Bundala. Hivi kwanini huyu Bushoke harudi kuja kurudisha enzi zile? Oh masikini zamani!

Maselepa "Kama Zamani"
Zamani Sports Club
Kimara Suka - DAR

Anonymous said...

Nakubaliana na wadau kwamba Nginde ilitoa vibao vingi vizuri mno kuliko bendi nyingine hapa TZ, na hiyo uliyotoa ni baadhi tu ya listi,hebu niongeze na Khadija,Kupenda sio ndoto,Pole Mkuu mwenzangu,Halima,Clara,...listi ni ndefu, na ndio maana walitwaa ubingwa wa muziki Tanzania kihalali kabisa!!! Upande wa solo alikuwa Abel Balthazar pamoja na Mulenga,sikiliza vizuri rythm,nina uhakika ni Muharami Saidi.Lile squad lilikuwa ni moto wa kuotea mbali!!Kama nimesahau kitu mdau Kisondella atanisahihisha au vipi?

Anonymous said...

Tangu naaza kusoma hii "thread" pamoja na "comments" zake nimeshindwa kuzuia machozi,masikini mziki wa Tanzania.Hawa watu walikuwa na uwezo wa asili wa kufahamu jambo husika (genius) na hilo limedhihirika katika mziki wao. kwa dhati kabisa mimi naamini kuwa Bitchuka ni namba 3 kwa ubora wa kuimba Duniani, chini ya Michael Jackson na Gregory Isaacs, ni maoni yangu tu.Nyindo alizoimba Bitchuka zilikuwa tamu sana,bila kujali ni bendi gani aliimba nyimbo husika. Nadhani utamu wa nyimbo za Sikinde zilizopelekea wao kuwa Mabingwa wa Mziki Tanzania zilichochewa na ile "rising and falling of the Pitch sound" ya Bitchuka.nakubaliana na mdau kuwa Sikinde ya Bitchuka,Cosmas na Bushoke ndiyo iliyokuwa Tamu Zaidi sababu viwango vya vipaji vya hawa watu vilikuwa vya kipekee.

Adbox