Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Saturday, April 24, 2010

Libeneke 2

Katika blog hii tuliwahi kuzungumzia chanzo halisi cha neno LIBENEKE. Nilieleza kuwa neno hili na hasa linapounganishwa na kusema 'endeleza libeneke', lilitokana na wimbo wa Butiama Jazz Band uliokuwa ukitaja majina ya wanamuziki wa bendi hiyo na kila mmoja akiambiwa aendeleze libeneke. Nimepata bahati ya kuongea na aliyekuwa Kiongozi na mpiga solo wa Butiama Jazz Band. Alikuwa na haya ya kusema. Butiama Jazz Band ilianzishwa mwaka 1971, makao yake makuu yalikuwa mtaa wa Kongo maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam, jirani kabisa na DDC. Ilianzishwa na asilimia kubwa ya wanamuziki kutoka Ifakara na ndio maana waliamua kuchukua jina la ngoma ya kwao na kuuita mtindo wa bendi yao Libeneke. Kiongozi wa bendi alikuwa Mzee Makelo na Katibu wa Bendi Mzee Mustafa Mkwega. Mzee Mkwega aliwahi kufanya kazi kwa Hayati Mwalimu Julius K Nyerere na hivyo alikuwa anawasiliana nae kwa karibu. Alikwenda kwa niaba ya wenzie na kumuomba Mwalimu awasaidie vyombo vya muziki, na aliwatuma wakalete Profoma invoice ya vyombo, walipoleta Mwalimu aliitia saini na ilitosha kwenda kupewa vyombo vipya dukani. Kama shukrani kwa Mwalimu waliita bendi yao Butiama Jazz Band. Na kuanzia hapo kila mwalimu alipoenda likizo ya mwaka Butiama bendi ilikwenda huko kutumbuiza wageni mbalimbali waliokuwa wanamfuata Mwalimu huko.

1 comment:

Anonymous said...

Namkumbuka mzee Alphonse Makello,alitoka Kilombero Jazz na kwenda Dar miaka ya 1971,na wakaanzisha hiyo Butiama Jazz,na kweli mtindo wao wa dansi ulikuwa unaitwa Libeneke,na kulikwa na wimbo wao kabisa wakitaja majina yao na kusema ENDELEZA LIBENEKE,nadhani kuanzia hapo watu wakaushika msemo huo wa kuendeleza libeneke.Kwa upande mwingine huyu mzee Makello ndiye alinifanya hata
mimi nikawa na hamu zaidi ya kuweza kujifunza kupiga gitaa,Pia alikuwa anafanya kazi pamoja na baba yangu na baba ya mpiga besi wa wana Njenje Keppy Kiombile.katika kiwanda cha sukari cha Kilombero, mimi ni mwanamuziki wa ki Tanzania niishie nchini Japan,Tuko pamoja na bwana Fresh Jumbe na Lster Elia
kabla ya kuja Japan nilikuwa napigia
bendi ya Simba Wanyika kwa takriban miaka 10 hivi.
Abbu Omar,Prof.Junior,Tokyo Japan.

Adbox