Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Monday, February 1, 2010


Wasanii ni kioo cha jamii, huu ni usemi ambao umezoeleka sana siku hizi katika vyombo vya habari na hata baina ya wasanii wenyewe. Usemi huu niliusikia kwa mara ya kwanza kutoka katika kinywa cha moja ya wasanii mahili nchini marehemu Mzee Godfrey Kaduma, ambaye pamoja na kuwa msanii mahiri ambaye kumbukumbu za usanii wake zinapatikana katika maandishi mengi na filamu kama vile Harusi ya Mariamu. Mzee Kaduma alieleza wazi kuwa usemi huo ni tafsiri ya usemi wa kiingereza ,”Artists are the mirror of the society”. Mirror ni kile kioo ambacho unajitizama ujione ukoje. Hivyo basi jamii ya Kitanzania ikitaka ijijue ikoje iwaangalie wasanii na kazi zao na ijue inajiangalia yenyewe. Msanii asie itafsiri jamii yake hujikuta yuko peke yake hana wapenzi.

Katika miezi miwili iliyopita kumejirudia jambo ambalo kila mara mimi huliona la ajabu sana. Na hii ni tabia ya viongozi kupiga marufuku shughuli fulani za kisanii. Nimesoma katika mikoa miwili wakuu wa mikoa wamepiga marufuku shughuli za kisanii. Kupiga marufuku ni jambo rahisi sana, tena rahisi zaidi katika sanaa kwani wasanii hawajawa na tabia ya kudai haki zao kisheria zinapopigwa marufuku, hivyo viongozi hutoa matamko ya namna hiyo bila woga wa kupata athari za matokeo ya matamko yao.

Tasisi moja imetangaza iko katika mchakato wa kutunga sheria ya kuwabana watunzi wa filamu kuhakikisha wanapeleka tungo zao kuhakikiwa kabla ya kuzitoa hadharani kwani nyingine zinakiuka maadili yetu.

Ningependa kuwakumbusha viongozi wanaopiga marufuku na hawa wanaotunga sheria za kubana watunzi kuwa wakumbuke, wasanii ni kioo cha jamii kwa hiyo yote yanayoendelea katika sanaa yanaonyesha jamii ilivyo. Hivyo basi kuvunja kioo, au kukataa kutumia kioo si njia ya kubadili ubaya wa sura yako.

Tatizo si wasanii, kwani wao ni sehemu tu ya jamii, tatizo ni mmomonyoko wa maadili katika jamii. Wakati unaruhusu vyombo vingine vionyeshe filamu zenye maadili ya kimagharibi masaa ishirini na nne na hivyo kutengeneza jamii inayokubali hayo, halafu kumkataza msanii wa Kitanzania asitunge hadithi ikiwa na maadili hayo mapya, atapata wapi wateja wa kazi zake? Atakachotengeza ataambiwa kazi zako zimepitwa na wakati.

Hata katika nchi ambazo zimeendelea kuna mfumo ambao hutengenezwa kulinda na kuendeleza maadili ya nchi hivyo wananchi kuishi wakiwa wana aina ya maadili ya nchi husika. Vyombo vya kurusha matangazo katika nchi nyingi huwa na asilimia iliyopangwa ya matangazo ambayo huitwa local content. Mfano kama mtu anataka kuendesha Radio au TV anajua kuwa asilimia sitini ya matangazo yake lazima yawe ni kutoka nchini, filamu, muziki na kadhalika, muziki hapa si bongo fleva na muziki wa dansi tu bali hata ngoma za kiasili. Jambo hili ni muhimu sana katika kujenga uzalendo lakini linajenga upenzi wa soko la kazi za sanaa za nchini, na hii inatengeneza ubunifu zaidi katika kazi za sanaa za nchi.

Wakati Balozi wa Japan anaweza akatoa DVD za bure zirushwe katika vituo vya TV nchini ambazo zinaonyesha utamaduni na maadili asili ya Japan, nabaki nawaza Balozi wetu yoyote yule atatoa nini kwenye nchi aliyoko akiambiwa nae atoe filamu toka kwao.

Serikali imeachia utamaduni unaendeshwa na wafanya biashara, matamasha mashindano , kutafuta vipaji na kadhalika kwa misingi ya biashara unafanya kitu kinacholipa. Serikali iwekeze tena kama zamani katika sekata hii ili kuweza kufufua na kukuza utamaduni wa Mtanzania ambao sasa unakokwenda ndio tunaonyeshwa na wasanii ambao kwa kuwazuia haisaidii kubadili mwelekeo wa maadili ya watu.

1 comment:

Mzee wa Changamoto said...

"Serikali imeachia utamaduni unaendeshwa na wafanya biashara, matamasha mashindano , kutafuta vipaji na kadhalika kwa misingi ya biashara unafanya kitu kinacholipa. Serikali iwekeze tena kama zamani katika sekata hii ili kuweza kufufua na kukuza utamaduni wa Mtanzania ambao sasa unakokwenda ndio tunaonyeshwa na wasanii ambao kwa kuwazuia haisaidii kubadili mwelekeo wa maadili ya watu."
What a CLOSING STATEMENT.
Truth, just truth and call it NAKED TRUTH.
Kwa kuongeza nguvu hapa, TUTAFIKA TUUUU

Adbox