Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Saturday, February 13, 2010

Historia za mfumo wa Bendi

Utaratibu wa bendi hapa nchini ulifuata sana utaratibu wa bendi za nje kutokana na muziki wa bendi kuwa ni wa mapokeo. Hapa naongelea aina ya vyombo vilivyotumika stejini. Katika rekodi za kwanza zaidi za bendi kama vile zile za Cuban Marimba bendi zilipiga bila chombo chochote kilichotumia umeme kwa kuiga staili ya Cuba, na pia teknolojiaa ya vifaa vya umeme ilikuwa bado kuingia. Hivyo kulikuwa na gitaa moja na ngoma za kizungu (drums), bongoz, na vyombo vya kupuliza, filimbi, trumpet, saxaphone. Nyimbo za zamani za Salum Abdallah na Dar es Salaam Jazz Band zinatoa picha za vyombo hivyo. Mwanzoni mwa miaka ya 60, vifaa vya umeme vilianza kutumika na bendi kwa kawaida zilikuwa na Gitaa la bezi, rithim na solo,tarumbeta na saksafon. Halafu kulikuwa na bongoz. Baadae tumba zilichukua nafasi ya bongoz. Baadae bendi ziliingiza gitaa jingine ambalo liliitwa second solo. Hili lilikuwa gitaa ambalo lilipigwa katikati ya rithm na solo. Cuban Marimba katika kipindi fulani cha Mzee Kilaza aliweza kuongeza gitaa jingine waliloliita chord gitaa.
Kuingia kwa vinanda kuliliondoa gitaa la second solo katika bendi, japo kwenye bendi kama Tancut almasi na Vijana Jazz gitaa hilo liliendelea sambamba na kinanda. Kinanda pia kikachukua nafasi ya tarumbeta na saxaphone katika bendi nyingi. Kwa bendi zile ambazo zilikuwa zikifuata muziki wa magharibi mpangilio wao haukuwa na mfumo maalumu kutokana nani aina gani ya muziki wanafuatia. Mpaka sasa bendi kama The Kilimanjaro kwa kawaida hupiga gitaa moja,vinanda vitatu, gitaa la bezi, drums na conga au maarufu tumba. Wakati bendi kama Shada ni wana kinanda magitaa mawili na ngoma ya kiasili. Tatizo kubwa sana sasa ni bendi zinaigana katika mfumo katika kila kitu ubunifu ziro. Franko Makiadi aliondoka kwenye mfumo wa second solo akawa na solo gitaa 2, yeye mwenyewe akipiga solo na akawa na mpiga solo mwingine katika wimbo uleule. Ni wakati sasa wanamuziki kuangalia nyuma na kuona ni nini wanaweza kujifunza kitakachofanya muziki wao uwe tofauti na wa wengine.

2 comments:

Baraka Mfunguo said...

Safi sana mkuu. Ninajifunza mengi sana kupitia blogu hii. Napongeza sana uamuzi wa kuianzisha kwani ni fursa nzuri kwa kizazi chetu cha sasa nami nikiwa mmojawao kujua ni wapi tulipotoka. Ni lazima nipite hapa walau mara tatu kwa siku.

SIMON KITURURU said...

Ubunifu kwa wengi ni kitu kigumu na utashuhudia hilo kuanzia mtaani. Ukianzisha kufuga kuku watu wakaona kama unafanikiwa utakuta mtaa mzima una banda la kuku pia.

Na naamini kwa kufuata hata mfumo/ arrangements za miziki mingi ya asili Tanzania naamini kuna utajiri mkubwa ambao bado hatujauona katika tika steji za muziki wa sasa ambazo huweza kuzaliwa.

Nami kama Mkuu Baraka Mfunguo, nakiri pia na kaugonjwa kakupita katika blogu hii mara kedekede.

Adbox