Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Tuesday, September 14, 2010

Maneno Uvuruge 2


Katika kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi hii kwa ajili ya ule wimbo Milima Ya Kwetu, pia nae Banza Tax akajiunga kipindi hiki. Na kule Mabibo bendi ya Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige pia wakajiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi. Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Marehemu Mzee Juma Mrisho, Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waliingia Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba.

Mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.

Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa (itaendelea………) (Pichani...Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo....)

7 comments:

Kisondella, A.A said...

Mzee Kitime, Historia nzuri sana ya kuruka huku na kule kwa Maneno Uruvuge. Hii inanipa nafasi kuwataja baadhi ya wanamuziki ambao walikuwa au wanaongoza kwa kuhama hama bendi.

1) Marehemu Eddy Sheggy
2) Marehemu Adam Bakari
3) Banza Stone
4) Mhina Panduka
5) Hussein Jumbe
6) Ally Choki

Ni wachache sana ambao wanadai kutafuta maendeleo lakini ukweli dhahiri ni masilahi

Kisondella - from Mafinga (Iringa)

Kitime J said...

Hawa uliowataja wana sababu mbalimbali za kuhamahama, wengine ni mabingwa wa kufukuzwa kutokana na tabia zao. Kwa hiyo kila mmoja ana hadithi yake. Hata Maneno alijikuta anafanya kazi sana lakini malipo kidogo,hivyo kuhama hapo ni lazima.

Kisondella, A.A said...

Mzee Kitime ni kweli kabisa zama za kupiga muziki wa sifa zimepitwa na wakati, sasa ni muziki kibiashara;

Sidhani kama mwanamuziki anaweza kuvumilia kukaa kwenye bendi moja kama mambo yake hayaendi sawia, hata hivyo wengine ni tooooo much.

Tusema wanamuziki kama Said Mabera (tangu aipoingia Msondo sijawahi kusikia amechomoka na kurudi), Joseph Bernado (tangu aipoingia Sikinde sijawahi kusikia amechomoka na kurudi), na wengineo; tuseme hawa wameridhika kimaisha au wameamua tu kukubali matokeo

Kisondella

Anonymous said...

Dah! Huyu jamaa kumbe ana historia ndefu saaaana katika muziki. Kumbe nilichokuwa nakifahamu kuhusu maisha ya muziki ya Maneno Uvuruge ni sawa na tone la maji katika bahari. Shukrani nyingi Bwana Kitime.

Anonymous said...

John!
Hivi zama zile kuhamia bend kwa ushawishi kulifuatiwa na mikataba ya kimaandishi? ama ni mdomotu! ama pengine kuaminiana?
Nimefurahi pia kuliona jina la Kalamazoo Nyembo mmoja kati ya wapulizaji wazuri wa sax wa enzi hizo. Je waweza kujuwa yuko wapi nyakati hizi na anashiriki muziki ama ni mstaafu?
Pia kama utapata nafasi hebu siku moja utuletee historia ya OMACO maana kuna weza kuwa na lakujifunza hapo kwa wadau wa muziki.
Kila la kheri katika kuendeleza blog hii makini. Vipi Blog ya njenje itakuwa hewani liniii

Anonymous said...

Mwakitime naomba ukipata profile ya Shabani Yohana Wanted alipokuwa Vijana Jazz utuwekee humu, nadhani katika wapiga magita ya kuongoza alikuwa balaa. Na ule wimbo wa Top Queen na Zaituni za Saga Rhumba alipiga solo nani?

Anonymous said...

Kama sikosei taarifa za Shaaban Yohana 'Wanted' zimo humu na nakumbuka post hiyo ilikuwa na wachangiaji wengi sana na iliibua mjadala mzito. Namshauri Anonymous 00:51 aangalie katika older posts.

Adbox