Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Thursday, August 26, 2010

Marijani Rajabu

Marijani Rajabu kwa vyovyote ni mmoja wa wanamuziki ambao wametoa mchango mkubwa katika ulimwengu huu wa muziki. Japo ni miaka mingi toka mauti yake yalipomfika, bado nyimbo zake zinapigwa na wanamuziki mbalimbali majukwaani na hata kurudiwa kurekodiwa tena. Marijani alizaliwa maeneo ya Kariakoo mwaka 1954. Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia. Alilelewa vizuri kwa misingi ya dini ya Kiislam kwa hivyo alihudhuria mafunzo ya dini utotoni kama inavyotakiwa. Akiwa na umri wa miaka 18 hivi, alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips. Mwaka 1972 Marijani alihamia bendi ya Safari Trippers. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Safari Trippers kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo. Miezi michache baadae Marijani na wenzie waliibukia Dar International. Pia huku kulikuwa na wanamuziki wazuri na haraka bendi ilipata umaarufu wa hali ya juu kwa vibao vyake kama Zuena na Mwanameka. kutokana na hali wakati huo bendi ilirekodi vibao hivi RTD na kuambulia sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao. Kati ya mwaka 1979 na 1986 bendi ilipiga karibu kila wilaya nchi hii na kufurahisha sana watu na mtindo wao wa Super Bomboka. Uchakavu wa vyombo hatimae mwaka huo 1986, ukamaliza mbio za bendi hii. Kwa miezi michache Marijani akashiriki katika lile kundi kubwa la wanamuziki 57 waliotengeneza Tanzania All Stars, kundi hili lilirekodi vibao vinne ambavyo si rahisi kwa bendi zilizopo sasa kufikia ubora wake kimuziki. Marijani alipitia Mwenge Jazz kw muda mfupi, na kukaa kama mwaka mmoja Kurugenzi Jazz ya Arusha, kisha akajaribu kuanzisha kundi lake la Africulture na mtindo wa Mahepe lakini kwa ukosefu wa vyombo mambo hayakuwa mazuri. Kufiki1992 hali ya Marijani ilikuwa ngumu akiishi kwa kuuza kanda zake ili aweze kuishi.Pamoja na nyimbo nyingi, za kuimbia Chama tawala na serikali, na hata tungo yake Mwanameka kutumiwa katika mtihani wa kidato cha Nne. Rajabu Marijani hajawahi kukumbukwa rasmi kama mmoja wa wasanii bora Afrika ya Mashariki

20 comments:

Anonymous said...

Kitime!
Ninatamani sana mtu kama Bwana George Kavishe meneja wa Kinywaji cha kilimanjaro beer angesoam makala hizi ama hii, na iwe kama changamoto kwake kwa tuzo zinazoandaliwa na kampuni ya TBL. Inashangaza sana na hainiingii akilini kuona wanamiziki wanao jiita wakongwe kama bwana muhina wa Tanzanite bend akiweza kumsahau mtukama marijani. Hata wanamuziki wa kizazi hiki cha dansi wanadiriki kuzirudia nyimbo za marijani kwa kejeli kwa maana ya kutozipa kiwango ni upuuzi na bora wangeachana na jambo hili. Hapa sasa napata kuamini kauli ya mwanamuziki mmojangili alipotoa maoni ya tuzo za kili mwaka huu kwamba ni TUZO DHAIFU ambazo hazikuzingatia viwango.
Nataraji hii itakuwa wake up call kwa wahusika ili wajipange vinginevyo Tuanzishe Tuzo ya Morris Nyunyusa ambayo itakuwa maalum kwa wanamuziki wakongwe kama wakina marijani na wengine wa daraja lile.

emu-three said...

Najaribu kutafakari hawa wakongwe kama bado wangekuwepo, hapa Marijan Rajab, Chiriku Maneti, Mbaraka Mwishehe....

Kitime J said...

Mara nyingine ngumu kuingia kichwani mambo yanayofanyika

Kitime J said...

Kumbuka kuwa marijan,Maneti, na Mbaraka wangekuwa hai, wangekuwa wazee, na kwa hali ya vyombo vya habari vilivyo sasa wangeambiwa wamepitwa na wakati, nahata heshima ya interview sidhani kama wangepata

Anonymous said...

Hii makala yako Bwana Kitime imenitia uchungu sana. Inaonyesha ni jinsi gani viongozi wetu walivyo wanafiki na wabinafsi. Wanachotaka wao ni kuimbiwa nyimbo za kuwasifu na kuwatukuza tu. Sishangai Marijani kutelekezwa na wakubwa toka alipokumbwa na hali ngumu kimaisha hadi mauti yalipomfika. Hii pia ilimtokea Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alipofariki katika ajali ya gari nchini Kenya mwaka 1979. Viongozi wa chama na serikali tukufu, ambao Mbaraka aliwaimbia nyimbo nyingi tu za kuwatukuza, walimtelekeza na kumsahau katika mauti. Mbaraka alionekana kama msaliti kwa kuwa tu alifia nchini Kenya ambayo kwa wakati huo ilikuwa imetengwa na Tanzania kwa sababu ambazo mpaka sasa sijazielewa. Hivi ni kiongozi gani wa chama au serikali anayekumbuka tarehe walizofariki watu kama Mbaraka, Marijani na Hemed Maneti achilia mbali mchango wao mkubwa kwa Tanzania na Watanzania kwa ujumla? Hivi wanamuziki hawa na wengine waliotoa mchango mkubwa ambao wametangulia mbele ya haki wanakumbukwa nchini Tanzania kama serikali na wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanavyomkumbuka Luambo Luanzo Makiadi? Mimi nadhani tusiwalaumu sana hawa vijana wanaokimbilia Bongo Fleva kwa kuwa wanaelewa itawalipa japo kwa muda mfupi kuliko kumenyeka miaka nenda rudi bila kuwa na mafanikio yoyote au japo kupata shukurani ya maneno kutoka kwa watawala.

Perez said...

"...sauti yako nyororoo naipenda unapoimba,
inanikumbusha mbali sana, hebu we kaka imbaaa,
We hapo uliye mbele..."

Yaani! We acha tu

Kitime J said...

Mwaka 1972 STC Jazz walikuja Iringa wakafikia Kilimanjaro Guest House. Nakumbuka kuwa pale nikiwashangaa Raphael Sabuni na gitaa lake lenye rangi nyekundu na nyeusi, lakini ninachokumbuka zaidi ni kuwa walikuwa na record player ya Siera, mimi nilikuja pale na santuri ya bendi ya Kongo inaitwa Vox Africa, nyimbo ilikuwa Magie. Maneno yake yalikuwa ya kiswahili,
.....Nakupenda sana Mgie
Unisikize mpenzi wangu
Magie nakubembeleza, oh Magie wangu usikie mpaka huruma.
Magie, Magie kuya twende.
Baada ya kusikiliza wimbo huu, Marijani aliwauliza wenzie , 'Hivi sisi tutakuja kuimba vizuri kama hawa?'Ukweli ni kuwa nikisikiliza leo nyimbo hiyo, na nikilinganisha na nyimbo za Marijani za Safari Trippers na Dar International,ni kuwa kawaacha mbaaaaaaaaaaaaali kiuimbaji. Huyo ndiyo Marijani.

MICHUZI JR said...

Da naisoma habari hii huku nikijaribu kupiga picha ya uhalisia kabisa ya maisha ya Mzee Marijani,namna alivyokuwa akihangaika kifamilia,kijamii na hata kitaifa kama sio kimataifa.Kwa kazi alizofanya alipaswa kuwa mwenye urithi wa kutosha wa kazi yake na hata familia yake kuendelea kuneemeka kwa namna moja ama nyingi,lakini waaapi masikini marijani kafariki akiwa hajafaidi kabisa matunda ya kazi yake ambayo mpaka sasa ni dhahabu.Watu wa hakimiliki nao hao ndio kwanza wanasua tu.R.I.P Marijabu Rajabu

Kitime J said...

Hawa wanamuziki wa zamani, kazi zao chache huwa zinaibiwa kutokana na kuuzwa katika CD na DVD, wao hupata mafao kutokana na kazi zao kutumika katika radio TV, sherehe mbalimbali, kupigwa hadharani na wanamuziki wengine katika kumbi mbalimbali,kupigwa kwenye vyombo kama jukeboxes, au kwenye mabaa nadhalika. Wenye majuke box Tanzania wanalipa kwa matumizi ya kazi hizi, watumiaji wengine imekuwa ngumu japo taratibu wenye kumbi na bar na mahoteli wameanza kulipa. Watumiaji wakubwa Radio na TV hawajaonyesha nia ya kulipa na kuwa wanatoa kila kisingizio, japo watangazaji wao huwa watu wa kwanza kupiga kelele kuwa wasanii wanaibiwa. Radio na TV hupata mamilioni ya fedha toka makampuni mbalimbali ambayo yanadhamini vipindi , vipindi hivyo vinatumia muziki lakini hawataki kulipa , hata wale wenye sifa za kusaidia vijana katika kutengeneza maisha yao hawalipi. Hata vyombo vya serikali pia havilipi. Hebu fikiria matumizi ya wimbo kama Rangi ya Chungwa na Georgina, ingekuwa warithi wanapata mafao inavyostahili, ni wazi maisha ya warithi wa wanamuziki hawa yangekuwa na unafuu.

Anonymous said...

nimekuwa shabiki wa Marijani tokea akiwa STC, safari Trippers hadi Dar International ninacheza nyimbo zake nyingi tu ninazo isipokuwa kuna nyimbo mbili nimezimiss muda mrefu nazo ni :
1. Mwanangu shida - STC Band
2. jua laniangazia akiwa na safari Trippers
nitashukuru kaka Kitime kama kutakuwa na uwezekano wa kuziweka katika Media player yako nipate kuburudika. nimejaribu kusearch katika mitandao mbalimbali sijazipata hizo nyimbo.
please kakata kitime
kila la heri

Kitime J said...

Sina huo wimbo wa STC kwa wakati huu lakini Jua laniangazia ninao. Natatizo la media player ntakapokuwa tayari kwa vyovyote nitahakikisha ninazitundika

Anonymous said...

naona JK ulisahau kidogo kuongeza Mahepe ngoma ya wajanja.

Anonymous said...

Mzee Kitime hii habari ya Hayati Marijan Rajab imenipa mchanganyiko wa huzuni na hasira kali. Hivi tunayo serikali kweli? Na ndio nakumbuka kwamba wimbo wake wa Mwanameka ulitumika na Baraza la Mitihani mbona hawakumlipa mzee wa watu? Hivi kama serikali nayo ni wezi wa sanaa nani atawasaidia wasanii wa kweli? Yani nakaribia kutoa mchozi huku nina hasira kali.

Kama Marijani Rajabu angekuwa mmarekani au kutoka nchi yoyote yenye maana (narudia tena nchi yenye maana na sio Banana Republic kama yetu) angekuwa multi-billioner. Tena billioner in terms of US Dollars sio madafu yetu. Ilikuwaje afe maskini? Hivi bila watu kama Marijani RTD wangepiga miziki gani redioni miaka ya nyuma?

Nasema tuna serikali ya kihuni. Majuzi mheshimiwa alikuwa anatamba kusaidia "wasanii" kwa kuwanunulia mtambo wa kurekodi. Hivi bongo fleva ni usanii? Hata kama wangekuwa wasanii kwanini serikali isiwakabidhi wasanii wenyewe kupitia chama chao halali huo mtambo badala ya kuwapa wahuni wa Clouds FM wautumie kwa manufaa yao? Hivi wanajua ni mabinti wangapi wamepata mimba kwa kupitia wahuni wa THT na Clouds? Hivi ninani katuroga watanzania?

Kilimanjaro awards ni upuuzi mwingine nisiotaka kuusikia. Tangu yaanze hayo mashindano si Mbaraka Mwinshehe, Marijan Rajabu wala Maneti waliotajwa kuwa washindani achilia mbali kushinda tuzo. Wanafikiri kutengeneza kilevi kunawawezesha kujua nani ni mwanamuziki bora? TAnzania imeoza kila sekta si bure.

Nikirudi kwa MArijani mimi naamini serikali inawajibika kuitunza familia yake tena bila masharti. Nasema hivi kwasababu imetumia kazi yake kutunga mtihani wa sekondari. Pia kwa miaka nenda rudi wamepiga muziki wake bure kwenye redio yake. Ni dhambi kama hizi za unyonyaji ndizo zinazofanya Tanzania nchi yenye utajiri wa madini na mafuta kuwa maskini wa pili toka mwisho duniani. EHE MUNGU HEBU TUMA TUFANI IWAMALIZE MAFISADI WOTE WANAONYONYA WATANZANIA NA FAMILIA ZAO. HATA KAMA NI KWA KUANGUKA KWENYE KAMPENI I DON'T CARE WEWE MALIZA WOTE. AMEN!!!

Anonymous said...

Kilio Cha Samaki:katika mfumo wa "Haki Miliki" Serikali ya Tanganyika ao Tanzania toka zamani haijawahi kutunga mfumo wakulinda haki za Wanamziki wake kama Nchi zingine Duniani.Bendi zilikua za Shirika;Bima Lee,Juwata Jazz,Uda Jazz...Bendi binafsi;Maquis Original,Safari Sound...hali ya Wasanii katika maslahi ilikua duni inaishia kwenye Mishahara...Wasanii wamehamasisha na kuelemisha sana Jamii kwa tungo zao,Wasanii wametoa mchango mkubwa katika Serikali za Tanganyika na Tanzania...Wasanii walilazimika kutoka Nje ili ku Rekodi kama Nairobi ili wapate kipato kikubwa...mfano Mbaraka Mwishehe Mauti yalimkuta Kenya alikua akitafuta riziki.RTD Chombo cha Serikali kilikua cha kwanza kuhujumu Wasanii,wakirekodi katika Studio za Pugu Road(Nyerere Road),kesho unasikia Nyimbo ziko katika Santuri Kenya...!!! Msanii hapati haki yake...katika Miaka ya 80 kulizuka uhasama baini Mlimani Park na RTD, sababu Mlimani ilitamka katika Vyombo vya habari RTD inahujumu Nyimbo zao,ikabidi wapigwe marufuku RTD.Tanzania haina mfumo wa kuenzi Wasanii wake,Marijan Rajabu mimi na mwiita OPERA ya TANZANIA nani ameisha enzi sauti yake?leo hii twaita Muziki wa Kizazi Kipya kesho itakua Kizazi cha Zamani...Dr.Remmy Ongala ameitangaza Muziki wa Tanzania kimataifa,leo hii hakuna Mjumbe wa Serikali katika Sanaa wa kwenda kwa Remmy kumpa hata wazo lakufanya Fondation(Dr.Remmy)hata kama ni MLOKOLE ili kusaidia Vijana wa fwate Nyayo ya Remmy...hata Kilimanjaro Awards haijawahi kutafakari wanani kama akina Ray Charles,Steve Wonder,Muhammed Ali,James Brown wa Tanzania?tuwaenzi katika Awards zetu.Jirani zetu DRCongo ni mfano wa kuiga,Mwaka jana walisherekea miaka 20 ya kifo cha Franco...BBC ilikua na Kipindi ikitangaza,mbona Tanzania haitaki kukumbuka Wasanii wake kama Salumu Abdalah,Mbaraka Mwishehe,Marijan Rajabu,Patric Balisidya,Abeli Baltazar,Joseph Mulenga,Michael Enock,Ndala Kasheba,Ilunga Lubaba...n.k
Miaka ya 80 Wasanii waliunda Chombo chao CHAMUDATA,ndio kulikua uhasama kati yao wenyewe ila ilikua ni kutokana na Kazi zao kunyonywa na Wahindi... mpaka leo Serikali haipendi kuwanasa hao MAFISADI sugu,ambao wana kula NAO,Msanii anakufa Msasikini... Mlala Hoi...

Anonymous said...

Nimejaribu kutafuta tarehe aliyofariki Marijani Rajab sijapata. Nimetafuta katika mtandao sijaona kitu. Hata vyombo vya habari vinapomtaja Marijani havisemi ni lini alifariki kwa kuwa havifahamu.Hii inaonyesha ni jinsi gani tunavyopoteza kumbukumbu za wanamuziki wetu waliotutoka.

Anonymous said...

Loh nimepata huzuni sana kusikia mazingira aliyofia Jabali la Muziki. Marijani ni Franco wa Tanzania, nyimbo alizotunga zilikua na falsafa nzito sana kuhusu maisha. Nyimbo zake, kama ilivyo kwa Franco alikuwa akiongelea maisha sio kama leo watu wanatunga bila falsafa. Mwanameka aliyemtoa Musa pangoni niliwahi kumuona Mtoni kwa Azizi Ali bado alikuwa pande la mama ilikua ni kisa cha kweli. Zile nyimbo za NDOA YA MATESO na BABA ANNA zilikuwa zikimliza jirani yangu pale Magomeni Kota kila siku.

Wanamuziki wa leo wajifunze nyimbo za Marijani kwamaana ya kuchambua fani na maudhui ili wawe na tungo za kifalsafa. Ukimuangalia Franco ilikuwa hivyo hivyo kwa Mario No. 1 na 2, Makambo Ezali Burreau, Pesa Position, nk.

RIP Jabali.

Maselepa "mzee wa zamani"
Dans Republique Du Burundi.

Abbu Omar,Prof Jnr/Tokyo said...

Mkuu Kitime,
asaaante sana kwa juhudi zako za kendelea kuielimisha jamii kuhusu habari za wanamuziki na muziki wa miaka iliyopita kwa ujumla,nataka kuchangia tu kusahihisha kuwa baada ya Safari Trippers kufa Dar International ikaundwa,na nyimbo zake za kwanza kabisa siyo kundi la mwanameka,Walianza na nyimbo kama Vipi mwana,Hongera mwalimu Nyerere,Hayati Karume nk.wanamuziki
walioanzisha hii Dar International
ni pamoja na mwenyewe Marijani,King Enock,Cosmas Thobias,na baadhi ya wanamuziki wengine mashuhuri ambapo hawakukaa sana ndipo wakaenda kuunda DDC Mlimani park Orch.Ikumbukwe tu kuwa mwanzo wa Sikinde ulitokana na kundi kubwa kutoka ile Dar International ya kwanza na pia baadhi kutoka Nuta Jazz(Ottu ),hata hivyo
Marijani hakukata tamaa aliweza kukaza mkanda na kuendelea mbele.mimi binafsi kama mwanamuziki nina kumbukumbu kubwa ya kuhusu wanamuziki na bendi za miaka hiyo maana nilikuwa nafuatilia kwa karibu sana mambo ya mabendi.nitajitahidi kuwa natoa mchango wangu pindi niwapo na nafasi,kazi nzuri bwana Kitime.
Abbu Omar,Prof.Jnr(The Tazanite Band (Tokyo)Japan.

Kitime J said...

Loh bahati gani hii kupata ujumbe toka kwa mwanamuziki wa miaka mingi Abbu Omar. Abbu tuwasiliane kupitia jkitime@gmail.com kuna mengi wadau wablog hii watapata toka kwako. Historia kubwa ya Simba Nyika na hasa Les Wanyika tuwasiliane. Ben anapiga wapi siku hizi?

Kisondella, A.A said...

Mzee Kitime huyu Mdau wa Abbu Omary ni yule tuliyezoea kumwita Proffessal Omary mpiga bass wa Less Wanyika/Simba wa Nyika??, au nimechanganya maji na mafuta?

Kisondella

Kitime J said...

Haswa kwa sasa yuko Japan akiendeleza shughuli za muziki

Adbox