Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Sunday, March 7, 2010

Tancut Almasi awamu ya kwanza

Mwaka 1986 wafanyakazi wa Kiwanda cha kuchonga Almasi cha Iringa chini ya Jumuiya yao ya Wafanyakazi (JUWATA), waliamua kukubaliana na mzungu mmoja tajiri wa almasi kuwa wao wamchongee almasi katika kipindi kifupi hivyo kufanya overtime na ile pesa ya overtime awaletee vyombo vya muziki. Kwa msaada wa wanamuziki waliokuweko pale Iringa, akina Mamado Kanjanika, Juma Msosi, Saidi Kananji waliweza kuchagua kupitia catalogues walizopata vyombo aina ya Yamaha. Ninauhakika bendi ingekuwa Dar es Salaam ingechagua Ranger FBT, kwani kilikuwa kipindi cha ukichaa wa Ranger hasa baada ya Mzee Makassy kupata vyombo hivyo.

Vyombo vilifika na kuanza kutumiwa na wanamuziki waliokuwepo wakati ule. Uongozi wa Bendi ulimuita Ndala Kasheba kuja kuzindua vyombo hivyo na ikiwezekana kuiongoza bendi, Kasheba alifika Iringa lakini wakashindana masharti na uongozi wa kiwanda cha Tancut.

Pamoja na kuwa alikuwa mwenyeji wa Iringa John Kitime alikuwa anapiga muziki Dar es Salaam ndipo alipoitwa nyumbani kujiunga na bendi hiyo. Kundi la wanamuziki toka Dodoma lilioitwa Super Melody likiwa na mtindo wao wa Zunguluke,nalo lilikuja ili kuteka kabisa bendi, lakini uongozi wa Bendi uliokuwepo uliwachukua wanamuziki wanne tu wa Bendi hiyo. Waimbaji wawili akiwemo Saburi Athuman (kiongozi wa sasa Vijana Jazz), mpiga gitaa Mohamed Ikunji, na mpiga saxophone ambae hakukugusa saxophone hilo hata siku moja. Baada ya hapa kulianza wimbi la wanamuziki kujiunga na bendi hii wakiwemo Shaaban Wanted, Abdul Salvador, Mohamed Shaweji, Banza Tax na wengineo.

Pamoja na kutokukubaliana na Tancut, Ndala Kasheba aliwataarifu mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa kuhusu bendi, wao nao walikuja Iringa na kujiunga wakifuatana na Mafumu Bilali Bombenga. Hapa ndipo awamu ya kwanza ya Tancut ilipoanza kuwika na vibao kama Kashasha, Nimemkaribisha Nyoka, Tutasele, Mtaulage, The Big Four. Wanamuziki wa wakati huu walikuwa , Shaaban Wanted Solo, John Kitime Mamado Kanjanika Rhythm, Mohammed Ikunji Second Solo, Amani Ngenzi Bass, Saidi Kananji Tumba, Ray Mlangwa na Buhero Bakari Trumpet, Mafumu Bilali na Abdul Mngatwa Saxophone, Abdul Salvador Keyboards. Kasaloo Kyanga, Kyanga Songa, Hashim Kasanga, Mohammed Shaweji, Banza Tax alikaa muda mfupi akatoka kabla ya kurekodi awamu ya kwanza lakini alirudi awamu ya pili na kuweza kurekodi .


Picha ya juu Kasaloo na Marehemu Kyanga Songa.Picha ya chini toka kushoto Buhero Bakari,Abdul Salvador,Kasaloo Kyanga, Asha Salvador(mke wa Abdul), na Kyanga Songa Miembeni Bar Ilala

9 comments:

Baraka Mfunguo said...

Safari sio kifo Mama yeye ! Subiri nitarudii Mama watoto.

Nyongiseee nigenenene nyongise


TANCUT hao baba

Faustine said...

.....Hivi wapi naweza kupata au kununua albums za bei hii? Nina collection ya bendi nyingine lakini sina za Tancut, UDA jazz band, Panasonic na baadhi ya nyimbo za Vijana "wana pamba moto."

Kwa nyie mnaoshughulika na mambo ya muziki Tanzania. Ni vyema nyimbo za bendi za zamani na hata za sasa zikahifadhiwa kwa faida za vizazi vijavyo. Je kwa kupitia CHAMUDATA au BASATA kuna mkakati kama huu?

Mdau wa nyimbo za zama hizo>
Faustine
drfaustine.blogspot.com

Anonymous said...

Ninakwenda safari, safari yenyewe ya masafa marefu
Najua nyuma utabaki, watasema mengi.
Hao wabaya wetu mama, watafurahi ...............
.........
Nikirudi mama nitakuletea zawadi
zawadi nono mama watoto........

Umenikumbusha mbali sana John. nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 90 wakati nilipokuwa mbali na familia yangu kwa safari ya kikazi basi ukichezwa wimbo huo ulikuwa unaniliza.

Endeleza libeneke.

Anonymous said...

John!
Umenikumbusha Dodoma miaka mingi kidogo wakati huo studio za RTD kanda ya kati dodoma. mabush stars walizuka kuja kunasa sauti za tungo zao. Bendi mpya vyombo vipya na wanamuziki wakongwe.
Fundi mzowefu( Muhandisi ) wa sauti kwa sasa yuko TBC Chrispine Lugongo na msaidizi wake Ernest mwana wa rajabu wakati huo akiwa ni trainee.

Gilber Boma akiwa ni mkuu wa studio na Abdul Ngarawa mkurugenzi wa RTD dodoma na Mzee Ben Kiko mzee wa sensa maana nyimbo bila kupotiwa ni haitorekodiwa.

Hapa ninakumbuka baada ya kufanya setting ambayo ilikuwa siku nzima kesho yake walianza kurecod maana enzi ile trucking bado bendi inatinga studio na vyombo vyote na mnapiga dansi live.

Siku hiyo ulikuwa unarecodiwa winbo wa samahani ya uongo. Kilichonivutia ni umahiri wa mpiga tumba wa wakati huo marehemu Haruna Luwali ambaye yeye ndiye aliyekuwa kinara wa wimbo ule kwa maana ya kuuongoza kwa tumba zake.

Kwa mujibu wa kanuni za studio nyakati zile walitakiwa kupiga "soft" lakini kwa midadi tumba za haruna zilikuwa zikinaswa na microphne za waimbaji jambo lililopelekea kuviza ubora wa kibao kile.
Hivyo baada ya marudio ya takriban mara 4 iliamuliwa itolewe spika ndogo iwe kama monitor nje ya studio kwenye coridor ya kuingilia studio (kama ulifika dodoma), Haruna alilazimika kupigia tumba zake nje huku akifuatilia kupitia spika ndogo aliyo wekewa na kwa sauti ya chini.
kesho yake wanamuzi wote wakiwa na ari mpya na akili mpya waliuchagua wimbo ule kuwa ndio uchukuliwe kama kumbukumbu ya RTD.
Baada ya hapo ninamkumbuka Mohamed Tengeneza ambaye alipata kuwa mpiga drum wa tuncu sina hakika ni awamu gani kipindi hicho ndipo hata haji lizege alikuwa katika harakati zake za mweisho za kuhama bendi.

Anonymous said...

kaka Kitime !
Hapa umenimaliza. naikumbuka Tancut Almasi ya wakina kawelee mutimanwa,King maluu akulyaki salee, marehemu Dingi tuka moly tu!Marehem mzee kalala mbwembwe, Marehemu hashim kasanga, marehemu haruna lwali ambaye ndiye mwalimu wa marehemu Sidy morris Super conga.
napaona iringa paleeeeeeeeee! Kwakweli blog hii ni ya watu makini.
Hebu ukipata nafasi utukumbushe Bicco stars ya wakina Kinguti, Ray Thomas, mafumu bilali, Andy swebe, Ramadhani Zahoro(burungutu)Marehemu Aimalambutu Simaroo (baba mkwe wa Luiza Mbutu)Yahaya omar,Maneno cholilo, Fresh jumbe mkuu na wengine . haka kalikuwa kabendi maana waliweza kuwa na marehemu asia daruwesh na marehemu Sidy Moris.
Leo mbeba box niko Iringa Kiroho napaona ruaha international.
Siku njema kwako

Mija Shija Sayi said...

Kumbe umepigia Tancut almasi! Bendi gani tena umepigia Kitime?

halafu ule wimbo wa Milima ya kwetu umepigwa na bendi gani vile, nimesahau kidogo.

John F Kitime said...

Naamu miaka imepita sasa. Hiyo ilikuwa awamu ya mbele sana

John F Kitime said...

Kwa kweli sipajui mahala ambapo unaweza kupata album hizi ukosefu wa uelewa wa hakimiliki unaleta utata wa namna ya kuziuza tena album hizi.

John F Kitime said...

Nimebahatika kupigia The Oshekas, Biashara Jazz(kumbakisa) wiki moja, TX seleleka, Chikwalachikwala, Orchestra Makassy(disco agwaya),Orchestra Mambo Bado(Bomoa tutajenga kesho),Tancut Almasi(Fimbo Lugoda),Vijana Jazz, Magoma Moto Sound,Kilimanjaro Band.Milima ya kwetu ilipigwa na Super Rainbow

Adbox