Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Friday, March 5, 2010

Mlimani Park Orchestra

Mlimani Park ilianzishwa mwaka 1978,ikiwa na wanamuziki kama Abel Balthazar (solo na second solo), Muhiddin Maalim Gurumo(muimbaji), Cosmas Thobias Chidumule (muimbaji), Joseph Mulenga(Bass), Abdallah Gama (rhythm), Michael Enoch (Saxophone), Hamisi Juma(mwimbaji), George Kessy(kinanda), Haruna Lwali(Tumba), ikiwa chini ya TTTS (Tanzania Transport and Taxi Services).

Mwaka 1983 shirika hilo lilipopiga mueleka kifedha kama mashirika mengi wakati huo bendi ikawekwa chini ya himaya ya Dar es Salaam Development Corporation (DDC). Chini ya uangalizi wa mwanamuziki mkongwe king Michael Enoch ambaye atakumbukwa kuwa alikuwa mpiga solo hatari sana wa Dar Jazz enzi za mtindo wao Mundo (mpaka akapewa sifa ya King), bendi ilinyanyuka ikiwa na sauti ya kipekee na mpangilio wa vyombo uliofanya bendi ilitikise jiji. Michael Enoch ambaye mpaka mauti yake alijulikana pia kwa sifa ya Ticha kutokana na kufundisha wanamuziki wengi na pia kuweza kupiga vyombo vingi, alikuwa ndie kiongozi wa Bendi kwa miaka mingi baadae. Umahiri wa King au Ticha (mwite upendavyo sifa zote anastahili), utaweza kuusikia katika nyimbo Tucheze Sikinde na Nalala kwa taabu alipiga alto saxophone (saksafon ndogo yenye sauti za juu), kwenye nyimbo nyingine alikuw anapiga tenor saxophone (saks kubwa yenye sauti za chini)

Mlimani Park Orchestra na mtindo wao wa Sikinde uliotokana na ngoma ya Kizaramo. Na ukaongezwa kibwagizo Ngoma ya Ukae, yaani Sikinde ngoma ya nyumbani, umekuwa ndo nembo ya bendi hii iliyojiwekea nafasi katika historia ya muziki wa Tanzania. Ni vigumu kutaja wanamuziki wote waliopitia DDC Mlimani Park lakini najua kwa msaada wa wadau tutapata majina mengi kadri itakavyowezekana. Lakini nianze na listi ifuatayo lakini pengine nigusie jambo ambalo watu wengi hawalijui, wimbo maarufu wa Gama ulitungwa na Tchimanga Assossa katika kipindi kifupi alichopitia bendi hii. Haya baadhi ya wanamuziki ni:

Hassani Rehani Bitchuka, Muhiddin Maalim Gurumo, Cosmas Tobias Chidumule, Hamisi Juma, Benno Villa, Francis Lubua, Max Bushoke ,Shaaban Dede ,Tino Masinge, Hussein Jumbe, Fresh Jumbe, Hussein Mwinyikondo vocals; Joseph Mulenga, Abel Balthazar, Henry Mkanyia, Michael Bilali, solo guitar; Abdallah Gama, Muharami Saidi, Mohamed Iddi, Huruka Uvuruge 2nd solo and rhythm guitars;

Suleiman Mwanyiro, Julius Mzeru bass guitar; Habibu Abbas, Chipembere Saidi, Juma Choka drums;Haruna Lwali, Ally Omari Jamwaka, Mashaka Shaban tumba; George Kessy Omojo organ; Boniface Kachale, Ibrahim Mwinchande, Machaku Salum, Hamisi Mirambo, Ally Yahya trumpets; "King" Michael Enoch, Juma Hassan, Joseph Bernard, Shaban Lendi saxophones karibuni wadau kuongeza utamu.


5 comments:

Anonymous said...

Mkuu,

Kwenye Bass guitar tusimsahau Marehemu Dogodogo!

Pia tusisahau kwamba nyimbo ya Neema ambayo ilikuwa ni utunzi wa Cosmas Chidumule ilishinda tuzo ya nyimbo bora kwa miaka miwili mfululizo mwaka '85 na '86. Hii nyimbo hata leo ni moja ya classic compositions za muziki wa dansi wa Tanzania.

Mghh, katika watunzi na waimbaji wa muziki wa dansi Tanzania Cosmas Chidumule yumo katika kama siyo 5 basi 10 bora! Cosmas ni mtunzi wa nyimbo zenye maudhui ya hali ya juu na muziki wenye mwafaka na maudhui. Uimbaji wake Cosmas ni wa asili ya Kingoni halafu akauinterweave katika muziki wa dansi. Ukimsikiliza anavyoimba utasikia vionjo kama vya waimbaji wa ngoma za asili za Wangoni na Wandendeule kwa mfano Lizombe, Kitoto au Todi. Pia utasikia vionjo kama vya uimbaji wa Muheshimiwa John Komba au yule aliyekuwa kiongozi wa kikundi cha sanaa JKT jina lake limenitoka alikuwa anaitwa Kapteni Mpandanchi kama sikosei.

Hakuna ubishi Sikinde ilitikisa na kutingisha muziki wa dansi Tanzania.

Anonymous said...

Sioni jina la Joseph Benard na Kassim Rashid.....nadhani ni watu waliochangia kwenye kazi za bendi hii au?

John F Kitime said...

Joseph Bernard nimemtaja , lakini kama nilivyosema tushirikiane kuwakumbuka wengine , angalia nimesahau jina la Machaku

PEAF said...

John, Hata Ramadhani Challenge (bassist) sioni jina lake vipi?

Kisondella, A.A said...

Ramadahani Kinguti - Mwimbaji (sijui yuko wapi kwa sasa), Adamu Bakari "sauti ya Zege) - Mwimbaji (marehemu), John Malyanga - bass (nasikia yuko Tabora Jazz), Shaban Mabuyu -bass (amehama inasemekana yup kwenye bendi ya Hussein Jumbe), Muhidini Kisukari - bass (marehemu) Mabesi - bass(yeye hakudumu sana), Lazaro Lenny - trumpet (marehemu), Kalamazoo Nyembo - sax (sijui alipo kwa sasa), Herman Gervas - rythim/solo (marehemu), Fadhili Uvuruge - rythim (sijui alipo kwa sasa), Gasper Kanuti - rythim (marehemu), Joseph Kanuti - rythim/solo (sijui alipo kwa sasa), Mhina Panduka "Toto tundu" - mwimbaji (sijua alipo kwa sasa, Saad Ally - drums (sasa yupo Msondo), Kang'ombe - drum (alikwenda msondo sijui kwa sasa yupo wapi).

Mkuu Kitime nafikiri mpaka hapo nimejaribu kuziba mapengo ya wanamuziki ambao aidha wapo sikinde au waliwahi kupitia sikinde.

Kisondella - Mafinga (Iringa)

Adbox