YOUTUBE PLAYLIST

Wednesday, February 17, 2010

Vijana Jazz Vs Maquis

Katika kipindi cha mwisho cha miaka ya 80, Kinondoni ilkuwa inawaka moto kwa Vijana siku ya Jumapili. Lang'ata ambayo baadae ilikuja kuwa Club ASET na sasa kanisa, palikuwa ndo ukumbi wa Dansi za kuanzia mchana kwa Bendi ya Maquis. Ukija hapa mbele Vijana Jazz Pambamoto awamu ya pili chini ya uongozi wa Hemed Maneti walikuwa nao kila Jumapili mchana wanaporomosha Dansi, na siku hiyo ilipewa jina Vijana Day. Kwa kweli Maquis walikuwa wanajaa watu na Vijana wanajaa watu. Kulikuweko na wapenzi wa kudumu wa Vijana kama ilivyokuwa Maquis. Wakati huo nyimbo kama Ngalula, Makumbele zilikuwa zinalia Lang'ata huku Vijana wanateremsha Shingo feni, Ngapulila, Azda. Ushindani huu ulilazimisha bendi kujitahidi kupiga vizuri na kwa displine au la wapenzi wanahamia bendi jirani. Kuna wakati Vijana Jazz walikuwa wanaanza muziki saa kumi na moja jioni na kupumzika saa tatu na nusu usiku kisha kumaliza dansi saa nne. Maquis wakawa wanaanza saa kumi na kumaliza saa tano usiku. Na wakaanza kuruhusu mtu yeyote atakayekuwa kapigwa muhuri wa kuruhusu kutoka nje ya ukumbi Vijana Jazz,aliruhusiwa kuingia Maquis bure. Vijana wakabadili ratiba na kuanza kupiga saa 9 mchana, kwa mtindo wa bandika bandua, yaani muziki nonstop. Na kufuta kupumzika hadi saa tano. Hiyo ndo ilikuwa raha kwa wapenzi. Vijana haikuwa na show wakati wa Maneti, Lakini show ilikuja baadae katika kukabili show ya Maquis ambayo ilikuwq nzuri sana chini ya mwalimu wao Wabangoi. Majina makubwa yalitawala madansi hayo Maquis kulikuwa na Dekula Vumbi kwenye solo,second solo Mbwana Cox (aliyetoka Vijana Jazz), banza Mchafu Bass, Nguza Viking, Adios, Tshimanga Assossa,Parashi Lukumbule Vijana Jazz kulikwa Shaaban Wanted, Hemed Maneti, Eddy Sheggy, Adam Bakari, Kida Waziri, Abou Semhando, Rashid Pembe na wengine wengi, basi raha kila jumapili ilikuwa kama tamasha

Kati ya Bendi ambazo Mzee J Mwendapole aliziendesha kwa muda mrefu ni Afriso ngoma. Hiyo ilikuwa bendi yake, ikawa na wanamuziki kama Maida na Belly Kankonde, iliweza kurekodi nyimbo kadhaa, lakini bendi hii iliongezeka umaarufu alipoingia marehemu Lovy Longomba, wakati huo akiwa na akina Kinguti system, Anania Ngoliga, Toffy Mvambe, Salim Shaaban Malik Nduka Masengo(Maliky Star) hao wakiwa waimbaji, Solo Gitaa- John Maida, Peter Kazadi, Robert Tumaini Mabrish, Rythm- Mjusi Shemboza, Bass-George na Kasongo, Drum -Ayub Karume, Abdul, Tumba- Magoma Sony, Trumpet-Juma Urungu, Ramadhani, Mbaraka Othman. wengi kati niliowataja wametangulia mbele ya haki. Baada ya hapo aliwahi pia kuwa na bendi ambayo ilikuwa na wanamuziki kadhaa kutoka sikinde ikawa inaitwa Sikinde Academia, ambayo haikudumu sana. Baada ya hapo amekuwa msaada mkubwa wa kuwasaidia wanamuziki wengi vyombo wakati wananzisha bendi zao.
Pichani ni Marehemu Lovy Longomba

Tuesday, February 16, 2010

Kwa heri Juma Mwendapole

Kwa masikitiko makubwa nimepata taarifa ya kifo cha mdau muhimu wa muziki wa dansi Juma Mwendapole. Amefariki Ijumaa tarehe 12 February 2010 na kuzikwa kesho yake. Mwendapole ndiye aliyekuwa mmiliki wa Bendi ya Afriso Ngoma iliyokuwa na wanamuziki maarufu kama Lovy Longomba. Kwa miaka ya karibuni wanamuziki wengi wamekuwa wakimtegemea kwa kukodi vyombo vya muziki toka kwake. Bendi nyingi zisingekuweko kama si msaada wa Juma Mwendapole.
Mungu Amlaze pema peponi Amin

Saturday, February 13, 2010

Historia za mfumo wa Bendi

Utaratibu wa bendi hapa nchini ulifuata sana utaratibu wa bendi za nje kutokana na muziki wa bendi kuwa ni wa mapokeo. Hapa naongelea aina ya vyombo vilivyotumika stejini. Katika rekodi za kwanza zaidi za bendi kama vile zile za Cuban Marimba bendi zilipiga bila chombo chochote kilichotumia umeme kwa kuiga staili ya Cuba, na pia teknolojiaa ya vifaa vya umeme ilikuwa bado kuingia. Hivyo kulikuwa na gitaa moja na ngoma za kizungu (drums), bongoz, na vyombo vya kupuliza, filimbi, trumpet, saxaphone. Nyimbo za zamani za Salum Abdallah na Dar es Salaam Jazz Band zinatoa picha za vyombo hivyo. Mwanzoni mwa miaka ya 60, vifaa vya umeme vilianza kutumika na bendi kwa kawaida zilikuwa na Gitaa la bezi, rithim na solo,tarumbeta na saksafon. Halafu kulikuwa na bongoz. Baadae tumba zilichukua nafasi ya bongoz. Baadae bendi ziliingiza gitaa jingine ambalo liliitwa second solo. Hili lilikuwa gitaa ambalo lilipigwa katikati ya rithm na solo. Cuban Marimba katika kipindi fulani cha Mzee Kilaza aliweza kuongeza gitaa jingine waliloliita chord gitaa.
Kuingia kwa vinanda kuliliondoa gitaa la second solo katika bendi, japo kwenye bendi kama Tancut almasi na Vijana Jazz gitaa hilo liliendelea sambamba na kinanda. Kinanda pia kikachukua nafasi ya tarumbeta na saxaphone katika bendi nyingi. Kwa bendi zile ambazo zilikuwa zikifuata muziki wa magharibi mpangilio wao haukuwa na mfumo maalumu kutokana nani aina gani ya muziki wanafuatia. Mpaka sasa bendi kama The Kilimanjaro kwa kawaida hupiga gitaa moja,vinanda vitatu, gitaa la bezi, drums na conga au maarufu tumba. Wakati bendi kama Shada ni wana kinanda magitaa mawili na ngoma ya kiasili. Tatizo kubwa sana sasa ni bendi zinaigana katika mfumo katika kila kitu ubunifu ziro. Franko Makiadi aliondoka kwenye mfumo wa second solo akawa na solo gitaa 2, yeye mwenyewe akipiga solo na akawa na mpiga solo mwingine katika wimbo uleule. Ni wakati sasa wanamuziki kuangalia nyuma na kuona ni nini wanaweza kujifunza kitakachofanya muziki wao uwe tofauti na wa wengine.

Friday, February 12, 2010


Mwaka 1982/83 Tchimanga Kalala Assossa alianzisha na kuongoza bendi iliyoweza kutia changa moto katika ulimwengu wa muziki wakati huo. Bendi hiyo iliitwa Orchestra Mambo Bado na mtindo wake wa Bomoa Tutajenga Kesho. Wanamuziki katika bendi hiyo walikuwa Tchimanga Assossa, Kiongozi na muimbaji, Kazembe wa Kazembe mpiga solo (pamoja na jina hilo alikuwa Msukuma), William Maselenge, rythm guitar, Huluka Uvuruge second solo guitar, Sadi Mnala drums, Mzee Albert Milonge second solo, Lucas Faustin muimbaji, John Kitime muimbaji na rythm guitar, George Mzee muimbaji, Athuman Cholilo muimbaji, Likisi Matola Bass na keyboards, Jenipher Ndesile muimbaji, selemani Nyanga Drums. Album ya kwanza ya bendi hii ilikuwa na nyimbo zilizotamba kama vile Kutokuelewana, Bomoa Tutajenga Kesho , hii ilipigwa marufuku. Picha ya Assossa iliyotoka kwenye tangazo la kwanza la bendi, hapa akiwa amevaa shati la ndege ambalo kwa siku hizo walikuwa wanavaa wajanja tu.

Thursday, February 11, 2010

Hemed Maneti


Hemed Maneti mwanamuziki muimbaji aliyetokea Cuban Marimba na kutua Vijana Jazz mpaka kifo chake. Wimbo wa mwisho aliyorekodi uliitwa Nelson Mandela uliyotungwa na John Kitime. Wimbo huo ulitungwa ili kupigwa radioni wakati Mzee Mandela alipokuwa anatembelea Tanzania mara baada ya kuachiwa toka gerezani. Hakupanda tena jukwaani baada ya kurekodi wimbo huo.

Tuesday, February 9, 2010

Muziki wa soul

Kila zama na vitabu vyake ni msemo unaoeleza kuhusu mambo ambayo hutokea katika kipindi fulani. Kila wakati kuna kizazi kipya, jambo ambalo kila kiza kipya kilichopo hudhani wao ndo wa kwanza. Katika miaka ya sitini kulikuwa na kizazi kipya cha wakati huo na moja ya muziki uliopendwa na kupigwa na vijana wakati huo ni muziki aina ya soul. Vijana walivaa kama wanamuziki wa soul wa wakati huo, walipiga muziki wao na bendi zilijipa majina ya bendi za soul. Ntataja baadhi ya wanamuziki ambao walipendwa na vijana wakati huo, najua kizazi kipya wa enzi hizo watakuwa na mengi ya kusema.

OTIS REDDING alileta raha kwa vibao kama Mr Pitiful, Fa-fa-fa-fa ambao Papa Wemba aliuimba tena miaka michache iliyopita. Sitting on the dock of the Bay, Respect, na wimbo ambao kila bendi ya soul iliupiga Direct Me. Otis alifariki katika ajali ya ndege ya kukodi na wanamuziki wenzake wane wa kundi lake la Barkays


Wilson Pickett alizaliwa March 18 1941, na kufariki kwa ugonjwa wa moyo Alhamisi 19 January 2006 alipendwa na nyimbo zake kama In the Midnight Hour, Don’t Fight It, Ninety-Nine and a Half (Won’t Do), She’s So Good to Me, Land of a 1,000 Dances,
Mustang Sally, na Funky Broadway nakuigwa sana na bendi za vijana wakati ule

James Brown huyu alikuwa ni mzee wao, alipewa majina mbalimbali kama Soul Brother Number One, the Godfather of Soul, the Hardest Working Man in Show Business, Mr. Dynamite, the Original Disco Man. Na mzee huyu ndo alikuwa kinara wa soul music miaka ya sitini, alikuwa mwanzilishi wa funk katika miaka ya 70, na alitoa mchango katika rap music miaka ya themanini. Pia alijua kucheza, Michael Jackson alikiri kuwa ile moonwalk aliipata toka kwa James Brown. JB alikuwa na nyimbo nyingi sana nitaje chache tu, The Popcorn, Mother Popcorn, Papas got a brand new bag, I am black and proud, Sex machine, James alifariki 25 Disemba 2006. Muhimu kutaja kundi lake the Famous Flames aliloanza nalo toka 1955.

Clarence Carter mwimbaji kipofu ambaye aliwakamata vijana kwa nyimbo kama too weak to fight, getting the bills ,slip away, patches

Aretha Franklin- mwanamke wa shoka huyu alipendwa sana kwa nyimbo zake kama respect, save me na think,

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...