YOUTUBE PLAYLIST
Tuesday, August 31, 2010
The Upanga Story
Upanga ni eneo muhimu sana katika historia ya muziki Tanzania. Hata katika miaka ya karibuni kulizuka kilichoitwa East Coast, muungano fulani wa wasanii wa Bongoflava toka maeneo ya Upanga, hii haikuwa mara ya kwanza kwa Upanga kuwa na wanamuziki waliotingisha mji. Enzi hizo za muziki wa soul, vijana wa Upanga walilipa eneo hili la mji jina la Soulville.Kwenye kona ya barabara ya Mindu na United Nations, nyumbani kwa familia ya Jengo, hapo ndipo palikuwa mahala pa mazoezi pa kundi lile la Groove Makers. Baadhi ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa Mohamed Maharage, Joseph Jengo, Emmanuel Jengo, Herbert Lukindo, Willy Makame, na mpiga Drums ambae mpaka leo yupo katika anga za muziki Jeff. Kipindi hiki kilikuwa ni wakati wa muziki wa soul na kundi hili lilikuwa kundi la ubora wa juu wakati huo. Upanga ilikuwa na kundi jingine The Strokers, hili lilikuwa na awamu mbili, awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo. Awamu ya pili ya kundi hili lilkuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Barlocks ni Bendi nyingine iliyochipukia Upanga, jina la Barlocks lilitokana na kuweko kwa kundi la Barkeys ambalo leo linaitwa Tanzanites. Barlocks walikuwa wakitumia vyombo vya Barkeys kwani kwa wakati huo bendi hizi zilikuwa kama mkubwa na mdogo. Barlocks hiyo ya awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Jimmy Jumba,Pimbi Sokoine, huyu alipewa jina la utani Pimbi kutokana na kuwa mrefu sana, Said Mbonde kaka yake Amina Mbonde mwanamuziki mwingine muimbaji,Sajula Lukindo, Abraham. Kulikuweko na makundi mengine mengi hapo Upanga, kama White Horse, Aquarius hapa walikuweko producer maarufu Hendrico Figueredo, Joe Ball,Joel De Souza, Mark De Souza,Roy Figueredo, Yustus Pereira,Mike De Souza. Baadhi ya wanamuziki wake walienda na kuungana na wengine Arusha na kuvuma sana na kundi la Crimson Rage, baadae wakarudi Dar na kujiita Strange. Baadhi ya kumbi walizokuwa wakipiga zilikuwa DI, Marine,Gymkhana,Maggot, St Joseph na kwenye shule mbalimbali.
(Picha ya juu-Emmanuel 'Emmy' Jengo, Joseph 'Joe' Jengo, Herbert 'Herby' Lukindo. Kati-Jeff 'Funky' nyuma yake ni Willy Makame. Picha ya chini Willy Makame)
Thursday, August 26, 2010
Marijani Rajabu
Wednesday, August 25, 2010
Blog Mpya ya haki za wasanii Tanzania
Saturday, August 21, 2010
Kinguti System
Ramadhan Maulid Kinguti maarufu kama Kinguti System ni mzaliwa Ujiji, Kigoma.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Super Kibissa ya Kigoma. Super kibissa ni bendi iliyoanziswa 1968 na Kinguti akajiunga nayo mwaka 1977. Wakati huo kiongozi wa bendi alikuwa Mlolwa Mussa Mahango ambaye alikuwa ni binamu yake Kinguti. Bendi ilikuwa mali ya watu watatu, Gollo Saidi, Haruna Mahepe, n Maulidi. Kinguti alitunga nyimbo kadhaa katika bendi hii kwa mfano-Kazi ni uhai, Mapenzi tabu,na Zaina. Mwaka 1979 alichukuliwa na Ahmed Sululu ambae alikua katibu wa Dodoma International na kuhamia Dodoma, ililazimika Dodoma International wamchukue kujaza nafasi ya Shaaban Dede ambaye alikuwa kahama Dodoma International na kuhamia JUWATA. Katika bendi hiyo alikutana kwa mara ya kwanza na mpiga gitaa mahiri Kassim Rashid. Baada ya hapo alihamia Orchestra Makassy ambapo wakati huo walikuweko wanamuziki akina Marehemu Masiya Raddi ambaye alifariki kwa kukanyagwa na daladala, Doctor Remmy, Andy Swebe, Keppy Kiombile, John Kitime, Issa Nundu, Kyanga Songa, Choyo Godjero na wengineo, pia alikuweko Mzee Aimala Mbutu kwenye solo, na Kassim Mganga kwenye rhythm. 1986 alijiunga Afrisso ngoma chini ya Lovy Longomba, hapa alitunga nyimbo sita, Pesa ni maua, Amana mpenzi, Estah Usituchonganishe, waimbaji wakati huo walikuwa Kinguti, Lovy na Anania Ngoliga,kwenye solo alikuweko mzee Kassim Mponda, na rhythm Maneno Uvuruge, Kwa muda mfupi alikuwa DDC Mlimani Park, na hapa akatunga kile kibao maarufu Visa vya mwenye nyumba, ambapo aliimba na Hassan Bitchuka, Francis Lubua,Hussein Jumbe na Benno Villa. Mwaka 1989 alikuwa moja ya wanamuziki waanzilishi wa Bicco Sound, wakiwa na Mafumu Bilali, Asia Darwesh, Andy Swebe, Mzee Aimala Mbutu, walitikisa na vibao kama Muuza chips, Leyla, Magreth maggie, Kitambaa cha kichwa, Nyumba ya kifahari, na nyingine nyingi tu. 1999 alijiunga na kilimanjaro Connection, alikaa bendi hii na Kanku Kelly kwa miaka miwili kisha kuanzisha bendi na akina Hassan Shaw The Jambo Survivors ambayo yupo mpaka leo
Vijana Jazz enzi za Ngapulila
Kati ya awamu nyingi za Vijana Jazz Band moja iliyoleta changamoto na furaha ni ile awamu ya nyimbo , Ngapulila, Ogopa Tapeli, Adza. Pichani baadhi wa wanamuziki wa wakati huo. Picha ya kwanz a juu- Mzee Joseph Nyerere akiwa na Kulwa Milonge na Hamis Mnyupe, picha ya pili wapiga trumpet marehemu Chondoma, Hamis Mnyupe, na Kulwa Milonge. Picha ya chini ni kundi zima la Vijana Jazz wakiwa na Mheshmiwa Seif Khatib, hapa wanaonekana akina Shaaban Dogodogo, Hemed Maneti,Shaaban Wanted, Abou Semhando na wengine wengi.Kama unavyoona alama za x wengi hawapo tena nasi duniani.
Wednesday, August 18, 2010
Shaw Hassan Shaw
Kwa wapenzi wa Vijana Jazz wanakumbuka vile vipande vya keyboards vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni, mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu alizaliwa
tarehe 25/sept/1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi. Aliporudi Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.
Ni chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda). Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College. Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana na wanamuziki wengi lakini wengi pia wametangulia mbele ya haki. Waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Abuu Semhando, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Mirambo, Hassan Dalali, Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA), na Marehemu Abel Baltazar , hapa alikutana na wanamuziki kama Benno Villa Anthony na Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu, mwenyewe anasema, ‘….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…’. Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa akakutana na Zahir Ally, Ally Choki Rwambow, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani, pili hii bendi ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel mbalimbali Malaysia,Singapore, Indonesia,Thailand na Japan jambo ambalo lilifanya aone kila kitu ni kigeni. Katika bendi hiyo alishirikiana na akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy,Delphin Mununga na Kinguti System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hiyo ilijiita Jambo Survivors Band, itakumbukwa kwa ule wimbo Maprosoo uliokuwa katika album ya MAPROSOO. Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Wameshapita Oman , Fujairah, U.A.E, Singapore, Malaysia na sasa wapo Thailand. Shaw anasema wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia akiwa na Kanku Kelly kwa mara ya kwanza kupiga muziki akiwa amezungukwa na watu weupe Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja.
(Picha ya juu Burhan Muba, Kinguti System ,Hassan Shaw, ya chini ni Vijana Jazz, Hassan Shaw wa mwisho kulia)
Tuesday, August 3, 2010
Lister Elia
Huyu ni mwanamuziki mpiga keyboards, zao la Dodoma, kule alikotoka Patrick Balisdya, Anania Ngoliga, Rahma Shally na wengi wengine. Lister mtoto wa mchungaji atakumbukwa sana kwa kazi yake katika bendi ya Sambulumaa lakini baada ya hapo alipitia Afriso Ngoma ya Lovy Longomba na Orchestra Safari Sound wale vijana wa Kimara, na hatimae akatua MK Sound(Ngoma za Magorofani). Hiyo ilikuwa baada ya wanamuziki akina Andy Swebe, Mafumu Bilali, na Asia Darwesh kuhamia Bicco Sound, alitua huko wakati mmoja na Ally Makunguru, Rahma Shally na hivyo kujiunga na Joseph Mulenga , Makuka, Matei Joseph na wengineo. Lister pia ni mtunzi wa vitabu na mwanamuziki ambae amesoma vizuri muziki kwa sasa yuko Japan habari zake za sasa zinapatikana kwenye website yake http://www.listerelia.com/
(Pichani Sambulumaa katika picha kabla tu ya uzinduzi wa bendi hiyo, picha ya pili Lista akiwa OSS)
SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.
TANCUT ALMASI ORCHESTRA wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...
-
Hawa ndio The Jets (1972), ambao baadae walikuja kuwa STC Jazz, ambayo ndio chanzo cha Biashara Jazz. Waliopo hapa wa kwanza Belino, Raphael...
-
Mara baada ya kutoa ule wimbo maarufu wa Kisambaa Shakaza, Eddy Sheggy mwenyewe na Wasambaa wengine wakaanza kuitwa Shakaza. Eddy Sheggy ali...
-
Suleiman Mbwembwe, aliyekuwa anajulikana pia kwa jina la Electronic Voice, alikuwa mwimbaji na mtunzi aliyeng'ara katika enzi zake. Aki...