YOUTUBE PLAYLIST

Wednesday, April 28, 2010

DJ wa kwanza

Katika kuzungumza na watu kupata mambo kwa ajili ya blog hii, nimepata hili ambalo naomba maoni. Kijana wa zamani mmoja kaniambia DJ wa kwanza anaemkumbuka alikuwa akikaa maeneo ya Keko Cocacola, alikuwa Mkongo fulani ambae jina kamsahau. Je, kuna mwenye kumbukumbu kuhusu hilo?

The Dynamites

Kikundi kingine toka enzi za miaka ya 69/70 hawa waliitwa The Dynamites. Hapa kwa kweli namtambua Salim Willis tu ambaye baadae alikuja kuwa mpiga second solo wa Afro70.

Midomo ya Bata

Upigaji wa vyombo vya kupuliza umepungua sana katika bendi zetu hapa Tanzania. Kumekuwa na maelezo kuwa tatizo hili limetokana na kuanza kutumika kwa Keyboards au vinanda aina ya synthesizer. Vinanda hivi vina uwezo wa kutoa milio mbalimbali ikiwemo ya vyombo vya kupuliza kama trumpet na saxophone. Lakini mi nadhani ni maendeleo ya mtiririko wa uigaji wa nini kinachotokea Kongo. Ni jambo lisilopingika kuwa kwa miaka mingi sana bendi nyingi zimekuwa zikiiga kile kinachotokea Kongo. Mara nyingine hata kufikia kuiga nyimbo nzima kutoka kwa bendi za Kongo. Na mara nyingine kuiga mfumo wa muziki kutoka huko. Kwa misingi hiyo, bendi zetu nyingi ziliamua kuacha kupiga vyombo vya kupuliza mara baada ya kuona bendi nyingi za Kongo zikiacha kutumia vyombo hivyo.
Lakini kwa ukweli kabisa vyombo vya upulizaji vina raha yake na utamu wake. Wapigaji wake hutengeneza step zao za kucheza na hupanga sauti za kupishana kati ya trumpet na saxaphone na huongeza raha sana katika muziki. Kwa sasa ni bendi chache kama vile DDC Mlimani Park, OTTU, Vijana Jazz, MAK Band, African Beat ndio wanaendeleza upigaji wa vyombo vya kupuliza.

Sunday, April 25, 2010

Akina mama nao- Asia Darwesh


Asia Darwesh ni miongoni mwa wanamuziki wanaoheshimika sana katika jamii ya wanamuziki na wapenzi wa muziki waliowahi kusikia au kufurahia kazi zake. Katika picha hapo juu Asia ambae alikuwa mpiga Keyboards wa kutumainiwa anaoneka picha ya juu akiwa na King Kiki enzi za Double O, na chini akiwa Mk Sound. Asia aliwahi pia kupigia Bicco Stars ambapo yeye pamoja na Andy Swebe na Mafumu Bilali na wenzao (waliihama MK sound), waliweza kuipandisha sana chati bendi hii. Hatimae Asia aliweza kumiliki bendi yake na alipatwa na umauti akiwa na bendi yake ambayo ilifanya vizuri sana huko Uarabuni.

Mzee Joseph Nyerere


Mzee Joseph Nyerere alikuwa mpenzi sana wa Vijana Jazz Band. Nakumbuka siku za Jumapili ambapo Bendi ilikuwa na onyesho lake lililoitwa Vijana Day mara nyingi ungemkuta pembeni akisikiliza muziki na pengine akiomba special request. Ilikuwa ni burudani pale ambapo aliamua siku hiyo kucheza maana alikuwa na staili ya peke yake iliyofanya mtu apende kumuangalia. Historia inasema alisoma Tabora Boys na alikuwa Band Master wa bendi ya shule na alipendwa sana kutokana na mbwembwe zake alipokuwa akiongoza na kifimbo cha Band Leader. Mzee Joseph aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa TANU Youth League. Pichani akiwa jukwaani na Marehemu Hemedi Maneti katika Ukumbi wa Vijana Kinondoni, kwa mbali nyuma anaonekana Aggrey Ndumbalo akiwa ameshika gitaa na Said Hamisi muimbaji wa Vijana akiwa napiga makofi, wote wamekwisha tangulia mbele ya haki.

Libeneke 2

Katika blog hii tuliwahi kuzungumzia chanzo halisi cha neno LIBENEKE. Nilieleza kuwa neno hili na hasa linapounganishwa na kusema 'endeleza libeneke', lilitokana na wimbo wa Butiama Jazz Band uliokuwa ukitaja majina ya wanamuziki wa bendi hiyo na kila mmoja akiambiwa aendeleze libeneke. Nimepata bahati ya kuongea na aliyekuwa Kiongozi na mpiga solo wa Butiama Jazz Band. Alikuwa na haya ya kusema. Butiama Jazz Band ilianzishwa mwaka 1971, makao yake makuu yalikuwa mtaa wa Kongo maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam, jirani kabisa na DDC. Ilianzishwa na asilimia kubwa ya wanamuziki kutoka Ifakara na ndio maana waliamua kuchukua jina la ngoma ya kwao na kuuita mtindo wa bendi yao Libeneke. Kiongozi wa bendi alikuwa Mzee Makelo na Katibu wa Bendi Mzee Mustafa Mkwega. Mzee Mkwega aliwahi kufanya kazi kwa Hayati Mwalimu Julius K Nyerere na hivyo alikuwa anawasiliana nae kwa karibu. Alikwenda kwa niaba ya wenzie na kumuomba Mwalimu awasaidie vyombo vya muziki, na aliwatuma wakalete Profoma invoice ya vyombo, walipoleta Mwalimu aliitia saini na ilitosha kwenda kupewa vyombo vipya dukani. Kama shukrani kwa Mwalimu waliita bendi yao Butiama Jazz Band. Na kuanzia hapo kila mwalimu alipoenda likizo ya mwaka Butiama bendi ilikwenda huko kutumbuiza wageni mbalimbali waliokuwa wanamfuata Mwalimu huko.

Saturday, April 24, 2010

Maquis Original


Maquis Original wakiwa katika uwanja wa Jamhuri Dodoma. Mwenye nyeusi tupu akiwa na gitaa ni Dekula Kahanga Vumbi, wa pili toka kushoto na suruali nyeusi ni Issa Nundu haya tuwataje wengine hapa.

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...