YOUTUBE PLAYLIST

Wednesday, April 14, 2010

Orchestra Santa Fe

Kati ya maswali amabayo yamewahi kuulizwa humu ni kuhusu bendi hii Orchestra Santa Fe. Hii ilikuwa mwanzo ni bendi yenye asilimia kubwa ya wanamuziki Wakongo. Mkuu wa 'Libeneke' aliwahi kuuliza kama ndio ilikuwa Bendi ya kwanza ya Kikongo, ninauhakika haikuwa bendi ya kwanza ya Kikongo. Wenye taarifa zaidi kuhusu Bendi hii karibuni. Bendi hii ilikuwa ikipiga pale Gateways Mnazi Mmoja maeneo ambayo kuna wakati yalikuwa maeneo muhimu katika shughuli za starehe jijini Dar es Salaam.

Tuesday, April 13, 2010

Sokomokoooooooooo


Leo nimeona nianze kuanika picha nilizonazo hadharani , tukumbuke yalivyokuwa. Pichani ni Safari Trippers. Wapenzi wa Sokomoko mnakumbuka kipindi hiki. Hebu tupeane kumbukumbu

Thursday, April 8, 2010

Muziki wa staili moja

Miaka michache iliyopita kulianza hadithi moja ambayo vyombo vya habari vikaishikia bango, na baadae wanamuziki kadhaa nao wakashika bango nakutoa ushauri nasaha wa tatizo hilo. Tatizo hilo lililkuwa kwanini muziki wa bendi Tanzania hauwi maarufu. Kwa utafiti ambao washika bango waliufanya wakatangaza kuwa Tanzania tuna tatizo la kuwa tunapiga aina nyingi mno za muziki ndio maana haujulikani. Kwa hiyo wataalamu hawa wakiwa wanalinganisha na muziki wa Kikongo wakasema Mkongo mmoja akianzisha Kwasakwasa wote wanapiga Kwasakwasa , ikija Kibinda Nkoy wote wanapiga hivyo hivyo , kwa hiyo nasi tuwe na staili moja, tena ikapewa jina Achimenengule. Utafiti huu ni wa ajabu sana, tuanze na nchi yetu ina makabila zaidi ya 110,yenye mila mbalimbali na muziki mbalimbali, inashangaza kujaribu kufikiri wote hawa wapende aina moja tu ya muziki. Huko Kongo ambako kulitolewa mfano hata wakati wa kile kipindi kinachoitwa the Golden Age of Congolese Music, ndipo haswa upigaji wa aina mbalimbali ulipokuwepo. Huku kulikuwa na Dr Nico, Franco, John Bokello,African Fiesta, bendi za vijana kama Lipualipua , Belabela, Orchestra Kiam, Empire Bakuba, Veve, kila moja ilikuwa na aina yake ya muziki,wapi ilikuja kupatikana hiyo theory ya kupiga staili moja ni kitendawili. Tatizo la kudumaa kwa muziki wa Tanzania si kutokupiga staili moja.

Wednesday, April 7, 2010

Kwaya

Kwaya, kama neno lenyewe linavyoonekana ni neno la mapokeo likimaananisha aina ya utamaduni wa mapokeo. Ni neno lililotokana na neno 'choir'. Uimbaji wa kikundi cha watu. Muziki huu umepitia mabadiliko mengi yakitokana na sababu mbalimbali. Kwaya ilikuweko mwanzoni katika mashule na katika makanisa, baadae ikawa sehemu ya burudani hasa ikipata msukumo kutoka kwaya za Kusini mwa Afrika. Kwa wale waliokuwa maskauti wanakumbuka kuwa kwaya kilikuwa kipengele muhimu katika route march. Katika harakati za kutafuta uhuru kwaya zilichukua umuhimu sana katika kuhamasisha jamii. Lakini kama ilivyo kwenye muziki wa aina nyingine, muziki huu ulitokea kuwa na mabingwa wake. Si rahisi kumsahau Mzee Makongoro kama uliwahi kumsikia. Alikuwa na nini cha ziada? Mzee huyu alianzisha staili yake mwenyewe ya kwaya. Wakati kwaya nyingi zikiiga muziki wa Jiving wa South Africa yeye alikuja na kitu kipya ambacho bahati mbaya kimekosa mrithi. Karibuni tuliangalie hili swala la kwaya. Je tunaelekea wapi?

Taarab inakwenda wapi?



Muziki wa Taarab umekuwa na historia ya kukua na kubadilika kama muziki wa aina nyingine. Lakini nimejitahidi kusikiliza muziki huu wa sasa ambao bado unatangazwa kama muziki wa Taarabu naanza kupata taabu kukubali kama kweli kinachoendelea sasa ni Taarab. Upigaji wake sasa unaanza kusisitiza sana uchezaji, ni ukweli usiopingika kuwa sasa sebene ya Kikongo imeanza kutawala katika tungo mpya za taarabu. Uchezaji wake ambao unaleta utata katika maadili ya Watanzania wengi. Naomba wapenzi wa Taarab na wanaoona wanaifahamu Taarab hii ya sasa ya Alamba alamba watumegee nini hasa kinachoendelea? Juzi nimepata barua pepe kutoka Mtanzania mwenzangu mmoja alioko USA, akilalamika kuwa walitangaziwa kuwa kuna onyesho la Taarab na alipofika huko akakuta mwimbaji mmoja maarufu wa Taarab akiwa na CD yake na kufanya play back ta Taarab, kwa kifupi hakustahimili maana aliona kapunjwa mno. Haya ndugu zangu ukumbi ni wenu

Sunday, April 4, 2010

Hayawi hayawi.........





Hatimae inataka kuwa. Kama ambavyo wapenzi wengi wa Blog hii wamekuwa wanaomba,mwanga umeanza kuonekana kuwa itawezekana. Wenye afro zao wazitimue au wakachome tena nywele hahahaha, wenye raizon zao, wenye slimfit zao,(kama zitawatosha na hivyo vitambi), wenye superfly, pekos, maxi, midi, mini wazitoe vumbi maana wanamuziki wa zamani wameamua kuwa watafanya show moja kubwa ambapo wanamuziki wa toka enzi za buggy watapanda tena stejeni na kujikumbusha yalivyokuwa. Onyesho hilo ambalo pia litahusisha Madjs wa enzi hizo linategemea kufanyika mwezi July. Tayari Kilimanjaro bendi wametoa vyombo na eneo la mazoezi na wanamuziki kadhaa wamekwisha jitokeza kukubali kushiriki. Fuatilia katika blog hii upate kujua nani na nani watakuwepo. Mapato ya onyesho hilo yataenda kwenye huduma ambayo itatajwa baada ya siku chache.

Saturday, April 3, 2010

Teknolojia na ubora wa muziki

Nadhani kuna haja ya kuongelea swala la teknolojia katika muziki na hapa nitazungumzia teknoljia ya kurekodi. Nyimbo karibu zote ambazo husifika kama zilipendwa zilirekodiwa wakati wa kutumia kanda(tape), kwa teknolojia iliyoitwa 'two track recording' (pichani juu). Kwa teknolojia hii ilihitaji wanamuziki kuwa wazuri sana na fundi nae kuwa mzuri, kwani kama unarekodi wimbo bendi nzima lazima ipige kwa pamoja na akikosea mtu lazima kurudia wimbo wote tena kwa pamoja. Kwa bendi zilizorekodi RTD miaka hiyo zilipewa siku mbili za kurekodi kinachoitwa album siku hizi, yaani nyimbo sita au zaidi kwa kipindi cha siku mbili. Siku ya kwanza Bendi ilitakiwa kufika asubuhi kwenye studio za RTD, ambapo ilifanyika kazi ya kufunga vyombo vyote na kuvijaribu hapo fundi mitambo ndipo alipokuwa na kazi kubalance vyombo vyote viwe vinasikika inavyostahili. Mchana wa siku hiyo ililazimika bendi kurekodi nyimbo zote bila kukosea hata kama ni kumi. Siku ya pili ilitumika kurekodi kipindi cha klab raha leo show. Mwanamuziki yoyote wa siku hizi atakwambia haiwezekani kurekodi nyimbo sita kwa siku moja. Teknolojia ya sasa hutumia njia inayoitwa 'multi track recording', ilianza kwa kurekodi kwenye kanda maalumu tack 4,kisha zikawezekana 8,16,32 na kuendelea. Siku hizi kwa kutumia program za kompyuta ktu una uwezo wa kuwa na mamia ya tracks, hivyo basi hata bendi ya watu mia kila mtu akaweza kuja siku yake na kurekodi kipande chake , akakakirudia mpaka kikawa sawa, na ndio maana siku hizi kurekodi wimbo mmoja inaweza ikachukua hata mwezi na zaidi , kwa kurudia sehemu zenye makosa, kuzibadili kabisa na kadhalika, na siku hizi kuna hata teknolojia inayoweza kurekobisha sauti iliyoimbwa vibaya kwa maana hata kama hujui kuimba unaweza ukatengezwa mpaka uonekane unajua kuimba. Kama kawaida teknolojia mpya ina faida nyingi sana lakini mwisho wa yote faida hizi huonekana pale akiwepo fundi mitambo mzuri na msanii mzuri. Waliorekodi enzi za two track duniani kote husifia ule utamu ambao hupatikana wakipiga pamoja, ambao hupotea kama kazi itarekodiwa kila msanii akija kwa wakati wake.

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...