YOUTUBE PLAYLIST

Sunday, March 28, 2010


Unamkumbuka msanii huyu?

Katika makala za hapo nyuma tulitaja kundi la Barlocks lililokuwa na makao yao pale juu ya Patel Stores , jengo linaloangaliana na Printpak, Barlocks lilikuja badilika na kuwa Mionzi. Kundi hili la Mionzi lilikuwa likipiga mara nyingi New Afica Hotel katika ukumbi wa Bandari Grill na Kilimanjaro Hotel pale Simba Grill. Habari zaidi kuhusu kundi hili zinafuata lakini hapa kuna picha ya kundi hili wakati huo akiwemo Innocent Galinoma, Martin Ubwe, na Frank

Wednesday, March 24, 2010

Dr Ufuta enzi hizo na sasa



John,

Mimi ni mmjoja kati wa fans wa blog yako. Nilikuwa Morogoro mjini na kwa bahati nzuri wakati napata chai ya jioni pale B1 restaurant akapita mwanamuziki mkongwe DOKTA UFUTA Nilifanya nae maongezi mafupi maana alikuwa na haraka kidogo akiwahi kazini, kwa sasa ni mlinzi wa usiku" babu mlinzi" katika moja ya makampuni ya ulinzi pale Morogoro. Tuliongea sana na nikakumbuka last article uliyotoa ya Cuban Marimba na jinsi alivyokuwa akionenaka kijana very hundsome. sasa kupitia taswira hizi chache hivi ndivyo alivyo.

Louie
(Dr Ufuta ndiye mwenye miwani katika hili ganda la santuri enzi hizo)

Sunday, March 21, 2010

Bendi za Wilayani nje ya Dar Es Salaam



Nimeona nirudie tena posting hii pengine iliwahii mno, miaka iliyopita karibu kila wilaya ilikuwa na bendi, naomba tusaidiane kukusanya kumbukumbu hizi muhimu kwa historia ya muziki wa Taifa letu. Kwa mfano pale Same niliwahi kukuta band ya Tanu Youth League siikumbuki jina lake, pia nimeshakuta bendi pale Igunga, Mwadui, Sumbawanga, Makambako, kule Mbeya, nakumbuka ilikuweko bendi ya Bwana Remmy, hebu tuchangie tuone tutafika wapi. Bendi hizi ziliwahi kutoa vibao vingi vilivyotingisha anga za muziki wakati huo. Kwa mfano Shinyanga Jazz na kibao chao Tenda wema uende zako kilichotungwa na kuimbwa pia na Mzee Zacharia Daniel, ambae mpaka kifo chake aliitwa Mzee Tenda wema, au vibao vya Mzee Zahir Ally Zorro akiwa na Kimulimuli, Kabwe,Tausi na vingi vingine , waliopitia JKT Mafinga wakati huo wanakumbuka raha ya bendi hii. Unajua kwanini Bendi iliitwa Kimulimuli? Bendi ilipata taa za stage zinazowakawaka zilizokuwepo pamoja na bendi kwa hiyo taa hizo kumulikamulika ndo kukatoa jina la Kimulimuli kuna kitu kingine muhimu, kwa kuwa bendi zilitoka sehemu mbalimbali kila moja ilikuwa na staili yake na hivyo kuleta utamu katika anga za muziki. Kila mtu atakubali hakuna kitu kinakosesha raha kama kusikiliza muziki unaofanana kila kukicha,

(Pichani ni John Kitime na Kasaloo Kyanga wakiimba wimbo wa Masafa Marefu na kukumbuka walipokuwa wanaitwa Bush Stars)

Iringa-
Highland Stars
Tancut Almasi Orchestra
Chikwala chikwala
Ruaha International
Vico Stars
Mkwawa Orchestra

Kimulimuli JKT

TX Seleleka

Bose Ngoma
******
Morogoro
La Paloma Jazz
Cuban Marimba
Morogoro Jazz
Les Cubano
Vina vina Orchestra
Sukari JazzKilombelo Jazz
Malinyi Jazz
Kwiro Jazz
Mahenge Jazz

Kilosa Jazz

Les Cuban
******

Tanga

Atomic Jazz

Jamuhuri Jazz
Tanga International
Amboni Jazz

Bandari Jazz

Watangatanga

Lucky Star

Black Star
******
Tabora
Tabora Jazz
Nyanyembe Jazz
Kiko Kids

Usoke Jazz

******

Kigoma

Super Kibisa Orchestra

Mwanza
Orchestra Super Veya

******
Moshi
Orchestra Zaire Success
Bana Africa Kituli
********
Dodoma
Dodoma Jazz
Dodoma International
Materu Stars
Saki Band
Super Melody

Mpwapwa Jazz

(Pichani Kibonge, mwanamuziki mkongwe wa Super Melody ya Dodoma)

Mara

Mara Jazz

Musoma Jazz


Ruvuma
Tembo Jazz
Orchestra Sere sere

Super Matimila

******

Lindi
Mitonga Jazz
******
Masasi
Kochoko Jazz


Mtwara

Bandari Jazz


Shinyanga

Shinyanga Jazz

Friday, March 19, 2010

Cuban Marimba


Kuanzia miaka ya 1920 mpaka 1940 Tanzania, hususani Tanzania bara, wanamuziki na wapenzi wa muziki walifuatilia sana muziki kutoka Cuba kupitia sahani za santuri za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Trio Matamoros and Sexteto Habanero, ambao walitoa santuri zikiwa na namba zinazoanzia GV1, GV2 na kuendelea na kupata upenzi mkubwa katika ukanda huu wa Afrika. Ni vikundi hivi ambavyo viliingiza mitindo kama rhumba, Bolelo, Chacha na kadhalika. Kwa kweli bendi za muziki wa dansi zingepata mengi ya kimapinduzi kama zingeweza kusikiliza na kuelewa muziki wanaoupiga kiini chake ni nini.

Kutokana na hamu hiyo ya kuujua na kuupiga muziki wa kicuba kisawasawa Marehemu Salum Abdallah aliwahi kutoroka kwao Morogoro akakimbilia Mombasa ili apande meli aende Cuba, bahati mbaya safari yake iliishia Mombasa kwa kuishiwa fedha, ambako alianza kupata shida lakini kwa kuwa baba yake alikuwa mwarabu, Ushirika wa waarabu wa Mombasa walimtaarifu mzee huyo kuhusu alipo mwanae na alimfuata na kumrudisha Morogoro. Salum Abdallah Yazidu aliyefahamika sana kama SAY, mwaka 1948 alianzisha bendi yake akaiita La Paloma, ambalo ni jina la wimbo maarufu ambao uliotoka Cuba ukiwa na maana Njiwa, wimbo huu unaendelea kupigwa hadi leo ukiimbwa na kurekodiwa kwa lugha mbalimbali, hata hapa Tanzania bendi nyingi huzisikia zikipiga wimbo huu na kuweka maneno yake ya papo kwa papo hasa kabla dansi rasmi halijaanza. Bendi ya La Paloma ndio ilikuja kuwa Cuban Marimba Band, Salum Abdallah aliiongoza bendi hiyo mpaka kifo chake 1965. Aliyeichukua na kuiendeleza alikuwa Juma Kilaza. Kilaza aliiendeleza vizuri kwa kutunga mamia ya nyimbo yaliyofurahisha sana watu miaka ya 60 na 70. Morogoro ulikuwa mji uliosifika kwa muziki, huku kukiwa na Mbaraka Mwinshehe na Morogoro Jazz, na huku Juma Kilaza na Cuban Marimba. Kuna watu walikuwa wakihamia Morogoro wikiendi na kurudi Dar siku ya Jumatatu asubuhi. Kati ya nyimbo maarufu za Cuban Marimba zinazodumu kwenye kumbukumbu ni wimbo Ee Mola Wangu, ambao Salum Abdallah awali aliutunga kwa mashahiri marefu lakini akachukua beti chache kutengenezea muziki akilalamika kuwa kuna walimwengu wanamtakia mabaya, lakini siku ya kufa atawashitakia maiti wenzake kuhusu ubaya huo.

Pichani ni Cuban Marimba baada ya Salum Abdallah, wa kwanza kulia Juma Kilaza, mwenye mawani Ufuta mpiga solo. Wadau malizieni majina ya hawa wanamuziki wengine. Mheshmiwa Tsere uliishi sana Morogoro tusaidie

Mheshimiwa mchango wako ni muhimu

Nimekuwa najaribu kumshawishi Mheshimiwa mmoja ambaye alikuwa Waziri kwa muda mrefu na sasa ni Mbunge atoe mchango katika blog hii, Mheshimiwa huyo katika miaka ya sitini alirekodi nyimbo moja nzuri sana ya kumsifu Mwalimu Nyerere. Mheshimiwa huyo alirekodi kibao hicho wakati akisoma Uholanzi.
Pia Balozi mmoja maarufu aliyekuwa akiimba nyimbo za James Brown miaka hiyo najaribu kumwomba ruksa atusaidie experience zake.
Mzee moja marehemu sasa lakini ana watoto wengi wanamuziki, japo yeye alikuwa mwalimu Tabora school alinieleza kisa cha Mheshimiwa mmoja (Mbunge muhimu), ambaye nitamwomba ruksa yake nitaje jina lake baadae, ambaye alilazimika kuwa anamlimia kajibustani kake ili afundishwe gitaa. Nashukuru kuwa mheshmiwa huyo mpaka sasa ni msaada mkubwa sana katika fani ya muziki hasa wa dini

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...